Hatua Tano za Kuandaa Wasifu Utakaokupa Ajira




Moja wapo ya sababu zinazochangia watu kukosa ajira wanazoomba ni uwezo mdogo wa kujenga wasifu wao katika maandishi.  Wasifu ni maelezo binafsi yanayolenga kumshawishi afisa mwajiri kuwa unazo sifa za kutosha kupata ajira unayoomba.

Vyuo vyetu, kwa bahati mbaya, haviweki msisitizo katika ‘mambo madogo’ kama haya. Matokeo yake watu wengi wazuri wenye ujuzi wanashindwa kuonekana kwa waajiri.


Katika makala haya tunaangazia maeneo matano unayohitaji kuyazingatia unapojenga wasifu utakaoutumia kuomba kazi.

Imarisha utambulisho wako

Maafisa waajiri makini wana tabia ya kwenda mbele ya kile kilichondikwa. Lengo ni kukufahamu vizuri. Swali kuu unalohitaji kulijibu kwa ufasaha kupitia wasifu wako ni, ‘Wewe ni nani hasa?’

Siku hizi teknolojia inawasaidia maafisa waajiri kukufahamu kirahisi sana. Mbali na maelezo mazuri unayoyaweka kwenye wasifu wako, mwajiri anaweza kukutafuta kwenye mitandao ya kijamii.

Kupitia taarifa unazoweka na kuzisambaza (share) kwenye kurasa zako za mitandao ya kijamii, afisa mwajiri makini anaweza kuamua mtazamo na uelewa wako ulivyo.

Maana yake ni kwamba yale unayoyafanya kwenye mitandao ya kijamii ni sehemu ya uandishi endelevu wa wasifu wako wa kazi. Hakikisha unapatikana mtandaoni na unaweka mambo yanayojenga utambulisho wako.

Lakini pia kuliko kuonekana wewe ni mpenzi wa masuala mepesi na mpiga porojo zisizo na tija mitandaoni ni bora kutokupatikana kabisa mitandaoni.
Mbali na mitandao ya kijamii, mtandao wa inteneti inafanya iwe rahisi kutuma maombi yako kupitia tovuti zinazosaidia kusambaza maombi ya kazi kama LinkedIn. 

Hata hivyo, iko hatari ya taarifa zako ulizowahi kuzituma kwingine kupatikana kirahisi na yeyote anayetafuta taarifa zako mtandaoni. Hakikisha taarifa unazotuma mitandaoni hazijichanganyi. Hata kama ni kweli kunaweza kuwa na tofauti ndogo ndogo, bado ni muhimu utambulisho wako ubaki kuwa ule ule.

Eleza uzoefu ulionao

Kwa kawaida, afisa mwajiri hutafuta mtu mwenye uzoefu unaokidhi nafasi ya kazi iliyotangazwa. Lazima ufanye kazi ya kumhakikishia kuwa wewe ni mtu sahihi.
Kazi kubwa unayohitaji kuifanya ni kuhusianisha sifa zilizotangazwa na mwajiri na uzoefu ulionao. Jiulize, ninakidhi vipi sifa zinazohitajika? Je, uzoefu wangu unatosha kuomba kazi ninayoitafuta?

Inawezekana uzoefu ulionao hauendani moja kwa moja na ule unaohitajika kwa kazi hiyo. Jambo la kukumbuka ni kwamba wakati mwingine, unaweza kuwa na uzoefu unaoweza kuhamishika kwenda kwenye eneo jingine.

Kwa mfano, kama ulifanya kazi ya kujitolea kama mchambuzi wa data (data analyst) na kazi unayoomba haijataja uzoefu huo, bado unayo fursa ya kuhusisha uzoefu huu na mahitaji ya kazi unayoomba.

Kama unavyoona, kujitolea kunaweza kukusaidia kupata uzoefu hata kama hujaajiriwa. Usiache kutafuta fursa ya kujitolea zikusaidie kupata ujuzi bila ajira.

Onyesha ujuzi wako

Sambamba na uzoefu wa kazi, mwajiri makini anahitaji kuona una ujuzi upi unaoweza kuwa na tija kwenye kazi atakayokupa. Ujuzi ni zaidi ya maarifa. Mtu mwenye ujuzi hutumia maarifa yake kufanya kitu kinachoonekana.

Hakikisha wasifu wako unasimulia hadithi ya ujuzi ulionao. Achana na porojo za kuorodhesha majukumu uliyowahi kuyafanya mahali fulani. Mfano, ‘Katika nafasi hiyo kazi yangu ilikuwa kuandaa taarifa ya fedha kwa kipindi cha kila robo mwaka.’ Maelezo kama haya ni mazuri lakini hayaonyeshi ujuzi.

Kadri inavyowezekana, fikiria namna ulivyoweza kutumia vipaji, uzoefu wako na ari ya kazi kuleta mabadiliko kupitia majukumu  uliyowahi kupewa.
Mfano, kama ulikuwa afisa masoko kwa mwajiri wako aliyepita, eleza ulivyofanikiwa kuongeza mauzo ya bidhaa. Mwajiri anapoona uwezo huu kwako, anakuwa na shauku ya kukuita kwa usaili.

Jambo la kuzingatia ni kwamba maelezo yako ni lazima yaonyeshe ushahidi kuwa una uwezo wa kupunguza matatizo na hivyo kuongeza tija kwa mwajiri.

Fupisha maelezo yako

Muhimu kukumbuka kuwa afisa mwajiri hana muda wa kusoma maelezo marefu yasiyo ya lazima. Wingi wa maombi yanayopitia mezani kwake hufanya achoshwe na aya ndefu zenye maelezo mengi.

Lazima kujifunza namna ya kumvutia bila kumchosha. Ili hilo liwezekane, jifunze kuchagua nini cha kusema na kipi uachane nacho na bado ujumbe wako ubaki na nguvu ile ile.

Inashauriwa utumie sentensi fupi fupi zisizotengeneza aya ndefu. Kama una maelezo ya ziada, tumia mtindo wa dondoo.

Pia hakuna kanuni ya upi ni urefu sahihi wa wasifu. Lakini kwa mtu ambaye ndiye kwanza amemaliza chuo na anatafuta ajira yake ya kwanza, kurasa mbili za karatasi ya A4 zinatosha.

Tengeneza mtandao wa ajira mapema

Vijana wengi hutumia muda mwingi kusoma lakini wanasahau ‘kujiongeza’ nje ya wigo wa darasa. Pamoja na kusoma, bado usisahau kazi kubwa na muhimu ya kutengeneza mtandao mzuri wa watu wanaokuamini sasa na baadae.
 
Usitarajie kuwa kazi zitakufuata kirahisi rahisi. Wakati mwingine waajiri hutafuta watu sahihi kupitia watu wanaowaamini. Unapokuwa na watu wengi wanaoufahamu uwezo wako inakuwa rahisi kupata taarifa zitakazokusaidia kupata kazi.

Mtaji wa kwanza wa watu ni makundi ya kijamii uliyonayo tayari. Kuna wanadarasa wenzako, watu mnaoabudu mahali pamoja na hata timu za michezo.
Lakini pia, unahitaji kukutana na watu wapya kadri inavyowezekana. Wasiliana na watu ambao tayari wanafanya kazi unayoitafuta. Kama unatafuta kazi ya karani wa benki, kutana na makarani wa benki. Kama unatafuta kazi ya uandishi wa habari, lazima kujenga mtandao wa watu ambao tayari wanafanya kazi hiyo.

Jambo la kuzingatia 

Unapowasiliana na watu hawa, onyesha uwezo wako badala ya kuwa ombaomba wa misaada. Thamani itakayoonekana kwako ndiyo itakayokuwekea mazingira ya kuaminika. Mtu anayekuamini atakukumbuka anapokutana na habari za kazi unayoihitaji.

Maoni

  1. Asante sana Mr. Bwaya. Ni kweli fact hii niliwahi kuipata mahali. Sio kwamba ajira hazipo, na tuna wasomi wengi wa darasani, ila wengi tunashindwa kubadili knowledge kuwa skills. na matokeo yake unabaki usomi wa vyeti yaani cheti, stashahada, shahada na shahada za juu. Wengi wanakosa hata mbinu za kuonyesha kuwa ni kweli wanajua hasa kwenye mahojiano, na kukosa uzoefu.





    JibuFuta
  2. Ni madokezo mazuri sana!!

    JibuFuta
    Majibu


    1. Jinsi ya Kujifunza

      Bila shaka, unaweza kunufaika kwa kujua kazi za mikono iwe unajifunza kazi hizo ili kujiruzuku au kutumia ustadi huo nyumbani. Unaweza kufunzwa kazi hizo shuleni. Au labda, unaweza kujifunza kazi hizo nyumbani. Jinsi gani? Kwa kufanya kazi za nyumbani. Dakt. Provenzano, aliyetajwa mapema, anaandika hivi: “Kazi za nyumbani huwafaidi hasa vijana kwa kuwapa ustadi muhimu sana ambao utawanufaisha watakapokuwa wakiishi mbali na wazazi.” Hivyo, uwe macho ili uone kazi zinazohitaji kufanywa. Je, kuna nyasi zinazohitaji kukatwa au kiti kinachohitaji kurekebishwa?

      Badala ya kukushushia heshima, kufanya kazi za mikono kutakunufaisha sana. Usiepuke kazi za mikono! Badala yake, jitahidi “kuona mema” kwa ajili ya kazi yako ngumu, kwani Mhubiri 3:13 husema kwamba “hiyo ndiyo zawadi ya Mungu.”(jw.org/sw)

      Futa

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?

Pay $900? I quit blogging