Wasomi wanakimbia fani, ama wanakimbizwa?

Inasemekana wasomi wanakimbilia siasa.

Wanaowaunga mkono wanasema serikali haijali utaalam wao. Inawakejeli kwa malipo kiduchu. Wao, kwa kuona kuwa siasa zinalipa, wanaamua kuzitelekeza fani zao wanakimbilia majimboni kwa lengo la kupata maslahi manono.

Inasemwa pia kuwa siasa nayo inawahitaji wataalam kama Maprofesa, Madaktari wa Falsafa na watu kama hao. Kwamba ubobevu wao unatoa mchango mzuri likija suala la maamuzi. Je, ni kweli wanasaidia katika maamuzi? Je, si kweli kwamba kila aina ya ufisadi tunaousikia leo umefanyika mikononi mwa wasomi? Wamesaidia nini?

Wanaowapinga, wanasema kuwa elimu yao ilipaswa kujikita katika kuileta jamii maendeleo kupitia fani walizobobea bila kujali serikali inawajali ama la.

Kwamba wangejikita vema katika fani zao, ni lazima wangeyapata mafanikio hayo wanayoyafuata katika siasa.

Wanasema, kuna ulazima gani wa kila mtu kukimbilia siasa ili kufanikiwa? Je, siasa ndio kila kitu? Je, kukimbilia siasa si dalili ya ufinyu wa elimu yetu? Wanashindwaje 'kujifanikisha' katika fani zao?

Maoni

  1. Waacheni tu na uhuru wao wa kuchagua wanachotaka kufanya maishani. Ikiwa msomi ana takakuwa mwanasiasa basi na awe mwanasiasa na aifanye kazi hiyo kwa heshima ya kulinda maslahi ya wote. Na ikiwa mtu asiye msomi anataka kuwa mwanasiasa na awe, naye pia aifanye kazi hiyo kwa heshima ya klulinda maslahi ya wote.
    Ikiwa watu wote wanaokuwa wanasiasa bila kujali tabaka lolote la rangi, jinsi, jinsia, elimu, ukwasi nk watafanya mambo kinyume na inavyotarajiwa kwa mujibu wa sheria za wakati huo, basi wanastahili kupata hukumu na kuvuliwa vyeo vyao vya kisiasa.
    Uamuzi wa mwisho anao Mwananchi mpiga kura, hayo ya wizi na udanganyifu vile vile yanaweza kubadilika ikiwa wanannchi watatumia nguvu waliyonayo wao , kwa kuwa Wananchi ninaamini ndiyo Wenyenchi na wenye nchi ni wote viongozi na waliowapa dhamana za uongozi.
    Sidhani kama lipo kosa, waachieni tu uhuru walionao Kikatiba maadamu hawavunji sheria.

    JibuFuta
  2. Mie nadhani sio vibaya wakiwa wanasiasa maana nadhani elimu yao,upeo wao, na uelewa wa masuala mbalimbali kitaifa na kimataifa inasaidia, hasa wakiongoza sekta zinazohusiana na taaluma zao.Tatizo litakalojitokeza ni kuwa huko wanakotoka kutadidimia. Na kwa mtizamo wangu maendeleo,maamuzi mzuri na matokeo mazuri yanakuwepo iwapo tu watakakotoka kumeimarika maana wao watakuwa policy makers,watekeleza wengine.Sasa watekelezaji wakiwa hakuna ua hawana ujuzi wa kutosha hakuna matokeo mazuri tutakayoyaona. Pia mtu hufanya kazi vizuri afanyapo kazi aipendayo na nafikiri hawa wasomi wanazipenda fani zao ila nadhani maslahi kidogo ni moja ya sababu kubwa inayosababisha kutafuta uelekeo mwingine. Nafikiri hawa wasomi wakiridhika na wakipatacho huko kwenye fani zao sidhani kama wengi wao watakilimbilia siasa maana naamini wengi wao siasa sio chaguo lao la kwanza ila ndiko mara nyingi (kwa nchi zetu zinazoendelea )ukiweko huko mambo yanakunyokea kwa muda mfupi sielewi siri ni ipi labda hawa wasome wameijua ndio maana waikimbilia.

    JibuFuta
  3. Tazama hapa uone wanachokimbilia.

    http://matondo.blogspot.com/2009/03/mkiona-niko-kimya-mjue-kwamba.html

    Kuna wachache ambao nawafahamu ambao kweli wana uchungu na wanataka kuleta mabadiliko. Kuna wengine ambao pia wanafuata maslahi kwani hawaridhishwi na wanachokipata kwa sasa. Mambo yote haya mawili nadhani yanakwenda pamoja. Wengine wanatibukia ughaibuni - Botswana, Afrika Kusini, Ulaya na Marekani. Wasomi wanayo nafasi kubwa kama kweli wataheshimu usomi wao na kukoma kuwa "walamba viatu" na "wapigania matumbo" Hata hivyo, kama alivyosema Subi, wenye nchi hasa ni wananchi na hawa wakiwa na mwamko unaotakiwa basi...

    JibuFuta
  4. Duh!,sasa kama ulitaka uwe mwanasiasa ya nini ubobee kwenye fani ya kitabibu ambayo huifanyii kazi tena?

    JibuFuta
  5. Egidio,
    Mipango na Ratiba hubadilika kulingana na vichocheo katika mazingira.
    Bado nadhani uhuru huo wa mtu kufanya siasa bila kujali tabaka unastahili kuachwa na uendelee kuwepo na wenye kuweza kuutumia wautumie vyema kabisa.
    Tunahitaji wanasiasa wasomi ikiwa wasio wasomi hawajaweza kutufikisha tunakotaka kufika na hao wasomi pia wakishindwa kutufikisha tunakotaka bado tutaendelea kuwa na mchanganyiko wa waliosoma na wasiosoma hadi tuelewane tunakotaka kufika.
    Hiii habari ya kusoma hadi unamaliza majengo ya shule na kuwa na digrii sita sita wachilia mbali za kutunukiwa halafu unarudi katika eneo la kazi unaandika invoice ya kuomba sindano na bandeji za kisha majibu yanarudi baada ya wiki mbili kuwa sindano sita ulizoomba zimepatikana mbili tu wakati waliokujibu hazipatikani wanakwenda kutibiwa jibu Afrika Kusini, haufai.
    Mpanda ngazi mpandie huko huko aliko mtunguane huko huko kabla hajavunja ngazi. Ukicheka na nyani utaishia kuvuna mabua tu.

    JibuFuta
  6. kweli tunao wasomi, wameshazikacha fani,
    japo wao hawasemi, twaona wazi machoni,
    na wala hawajitumi, taaluma zi kapuni,
    nadhani siasa tamu!

    kwani wamesoma nini, mbona hakijawafaa,
    walikaa darasani, kumbe walijihadaa,
    vyeti wametupa chini, kwingine wamezagaa,
    nadhani siasa tamu!

    JibuFuta
  7. Kaka Bwaya, usiwe kipofu, hivi kuna fani inayolipa hapa nchini kama siasa?

    Juzi hapa tumefunuliwa na hao hao wanasiasa kuwa wanapokaa pale Dodoma wakisinzia wanalipwa mshahara wa mwalimu kwa siku moja, yaani mshahara ambao mwalimu anausotea mwezi mzima tena wakati mwingine unacheleweshwa, mwanasiasa anaupata kwa siku moja tu. sasa kuna kazi inayolipa kama hiyo, haya achana na vikao vya bunge maana sio wanasiasa wote ni wabunge, je wale walioteuliwa kwenye bodi za mashirika ya umma, mawaziri wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na wengine na wengine, idadi ni ndefu sana.

    Naamini itafikia mahali vyuo vyetu vitafungwa na mahospitali yatafungwa kwa kukosa wataalamu iwapo hatua hazitachukuliwa kuangalia upya sera zetu za ajira kwa wataalmu wetu.

    Serikali inasema kuwa haina uwezo wa kuwalipa watalamu wetu mishahara mizuri kulingana na taaluma zao lakini mbona fedha nyingi zinaelekezwa kwa wanasiasa tena wengine hawana taaluma inayolingana na malipo wanayoyapata, wizi mtupu......

    JibuFuta
  8. fred katawa31/3/09 3:21 PM

    Dada Subi,mwananchi hawezi kuwa mwenye nchi bali kila nchi ina wenye nchi na wananchi sio wenye nchi bali ni wananchi ambao ni sehemu ya wenye nchi.

    Kura haiwezi ikamuondoa mwenye nchi madarakani isipokuwa tu pale mwenye nchi anapoamua kutoka kwa hiari yake madarakani.Kura itamuondoa vipi wkt wanaohesabu kura ni wenye nchi,wanaoandaa makaratasi ya kupigia kura ni hao hao na wanaotangaza matokeo ni hao hao?

    Sehemu nzuri ya kuwa mmojawapo wa wenye nchi ni kuwa mwanasiasa.Ninaamini kuwa mwanasiasa yeyote ni mchoyo na mbinafsi na hayupo kwa ajili ya kutetea maslahi ya wananchi.Wanasiasa ni waigizaji wazuri sana,usipokuwa makini waweza kudhani wanawatetea wananchi.

    Wasomi wamejiunga huko kwa sababu ya ubinafsi na uchoyo wao.Hata kama ni suala la maslahi daktari unaamua kuacha watu waliokusomesha wanakufa kisa unalipwa laki 5 badala ya milion 7 kwa mwezi?

    JibuFuta
  9. Wao kuingia kwenye siasa wala si kosa. Na nadhani tunahitaji wasomi kwenye utawala wa kisiasa. Lakini nia hasa ya kuingia kwenye siasa ndio iletayo utata. Ni kweli kuwa tunahitaji mwenye kujua utabibu kuongoza "siasa za afya" ama mwanasheria kutusaidia kwenye katiba, pengine mwanamazingira kwenye wizara ya mazingira chini ya Ofisi ya makamu wa rais, mtaalamu wa mipango miji kwenye wizara ihusuyo makazi, "mwanasayansi" kwenye wizara ya sayansi na teknolojia. Na kama alivyosema Da Subi kuwa ni haki pia kikatiba. Kwa hiyo licha ya kuwahitaji, bado wana haki ya kuwemo siasani. Tatizo ni kile wanachofanya wakishafika huko. Sio wote wafanyao lakini wafanyapo wanatesa wengi. Kwa hiyo haijalishi nani anatenda ubaya, bado ataendelea kuwa m'baya na muovu. Tatizo ni pale watendapo kwa kutumia ujuzi ambao walistahili kuutumia kuliletea taifa tija na kisha kutumia ujuzi na kipato chao kusimamisha taratibu za kisheria.
    Lakini wana haki na tunawahitaji. ILA TUNAHITAJI WAAMINIFU

    JibuFuta
  10. Nchi hii inahitaji wanasiasa, wahadhiri, madaktari wanasheria, wataalamu wa kilimo, wataalamu wa madini, mainjinia, mafundi sanifu wa majengo na kadhalika na kadhalika.
    Kwa hiyo sio vibaya mtu kuchagua kazi anayoipenda kwa hiyari yake bila kusukumwa na wala kushurutishwa.

    Nakubaliana na kaka Mubelwa kuwa hata katika siasa tunawahitaji hawa wataalamu ili watusaidie kutengeneza sera na mipango ya maendeleo.

    JibuFuta
  11. Nakubaliana na Subi.

    JibuFuta
  12. Nuru Shabani1/4/09 10:23 AM

    Jamani tuache utani,wanaojiita wasomi wanakimbia fani zao,wote wanataka kuwa wanasiasa.
    Mimi binafsi silipingi hilo kwani kila mtu anao uhuru wa kuchagua cha kufanya.
    Tatizo linakuja kuweka siasa hata kwenye mambo ambayo hajahitaji siasa,kama alivyosema da subi.
    Tunategemea msomi akipata nafasi katika siasa atautumia usomi wake ktk kuendeleza nchi yake lakini sivyo.Nijuavyo mimi kila fani ina miiko yake 'ETHICS'.
    Sasa ukitaka kujua wasomi wanakimbia fani zao ni pale wanapokimbia miiko ya usomi wao.
    Ni hayo tu

    JibuFuta
  13. Kwa mshahara huo wa Milioni Saba na ushee kwa mwezi na UHESHIMIWA juu kwa wabunge wetu,yayumkinika kusema kwamba siasa ni miongoni mwa shughuli chache kabisa halali nchini Tanzania inayolipa mithili ya biashara haramu.Kama anavyosema dada Subi,acha tu waende huko maana hizo mbinde za mishahara huko wanakokimbia si ndogo.Naafikiana pia na Da Koero kuwa siasa imekuwa mradi wa ulaji.

    JibuFuta
  14. Sio wasomi wote
    wazikimbiazo fani zao. Kuna wanaokimbia,na wanakimbia kweli kweli,sio wanakimbia kama vichaa yani pasipokutambua sababu hasa zinazowakimbiza, ,wanakimbizwa na maslahi duni ,na si vinginevyo. Kwa nini ni vigumu sana kusikia mwanasheria kaacha uanasheria na kaenda kuwa mwalimu wa sekondari?
    Umewahi kumsikia mwalimu aliyeacha kufundisha na akaenda kuwa mmachinga? Ukweli ni kwamba hujawahi na ni vizuri ukijiuliza kwa nini.
    Umewahi kusikia mwasibu kakimbilia kwenye ualimu? Lakini ni zaidi ya mara zisizo hesabika umesikia walimu wanakuwa wahasibu,wahandisi, madaktari,wanasheria n.k.
    Kwa hiyo tatizo ni maslahi.

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?

Pay $900? I quit blogging