Machapisho

Inaonyesha machapisho kuanzia 2006

Kumwua Muisrael si kuua?

Wengi wetu tunajua zile amri kumi ambazo Musa/Moshe alizipewa na mwenyezi Mungu ili ziwe dira ya maisha ya wana wa Israel wakati na baada ya safari yao ya jangwani. Tunajua kuwa amri hizo zinatuhusu hata sisi wa kizazi hiki tusiokuwa waisraeli. Katika hizo amri ipo inayosema Usiue. Yaani Mungu akizuia binadamu yeyote kumtoa uhai kwa makusudi binadamu mwenzake. Ninaweza kuonekana wa ajabu nikiuliza: Hivi amri hii ilimaanisha usimwue nani? Ni kuua tunakokufahamu ama kuna neno linaloendelea ambalo huenda lilihaririwa na Moshe? Ninasema hivi kwa sababu, baada ya Musa kufia mlimani, na mamlaka ya kuwaongoza wana wa Israeli kushikwa na Yoshua kuna jambo la ajabu lililotokea. Wale jamaa walipokuwa wakiingia kwenye nchi ya ahadi, Kanani, nchi ambayo ilikaliwa na wenyeji wakati wairaeli wakiishi Misri, yalifanyika mauaji makubwa ambayo hayana tofauti na yale ya kimbari. Watu kwa maelfu walipoteza maisha yao. Mauaji haya ninashawishika kuamini kuwa yaliyazidi yale yaliyotokea Rwanda miaka ya t...

Ubuddha: Miungu hufa na haistahili sadaka

Tuendelee na vidokezo kuhusu dini zetu tukiangazia dini zinazopatikana katika bara la Asia. Baada ya kuangalia Uhindu, sasa bonyeza hapa kusoma maelezo mafupi kuhusu Ubuddha, dini inayoamini kuwa kuishi ni kuteseka na kwamba ni muhimu kujikomboa kutoka katika mateso ambayo humpata kila binaadamu. Wa-Buddha wanaamini kuwa kuna miungu, lakini wakiamini kuwa miungu hiyo hufa kama viumbe wengine, na kwamba miungu hiyo haihusiki kwa namna yoyote na mambo ya uumbaji wa ulimwengu huu, kwa hivyo haistahili kuombwa wala kupewa sadaka.

Uhindu: Dini inayoamini dini zote ni sahihi!

Kwa muda sasa, pale Jikomboe/dini kulikuwa na mjadala kuhusu tofauti ya Dini na Imani ukiongozwa na mwanablogu Mwidimi Ndosi. Mjadala huo hatukuumaliza ili kuruhusu maoni ya wasomaji wengine. Kama unapenda mijadala hii, nakushauri upite hapa halafu uache maoni yako. Wakati mjadala ukiendelea, na mara nyingine nje ya ukumbi, kuna wapenzi wa mijadala hii wanadai ipo haja ya kupeana habari zaidi kuhusu dini ambazo wengi hawazijui. Sababu ya kufahamika ama kutokufahamika kwa baadhi ya dini inaweza kuambatana na nguvu za kisiasa na kiuchumi za wasambaza dini husika. Na ni kweli kwamba waumini wengi huwa hawajishughulishi na kujua dini nyingine zaidi ya hizo wanazoziamini. Siwezi kudai kuwa ninazijua sawasawa, ila ni kule kupenda kufuatilia hapa na pale na kuzungumza na huyu na yule, basi ninakuwa na japo kiberiti kidogo cha kutafutia wapi pa kuanzia na hapo wengine wanaongoza na matokeo yake tunavunja ile mila ya kutokujifunza mengi. Wapo watu wanaodhani kuwa dini zao ndizo zilizo sawa kuli...

Hivi ni laana ama ni mdudu gani?

Niliwahi kumsikia "mwinjilisti" mmoja aliyekuwa akichapa injili mitaa ya Kariakoo. Siku hizi ni jambo la kawaida kukuta watumishi hawa wanaoitwa wa Mungu wakifanya "vitu vyao" hadharani bila kujali haki za wengine. Kelele nyiiiingi kisa wanasema habari za Mungu. Kwa hiyo kimsingi haikunishangaza. Huyu bwana alikuwa "siriaz" kweli na kazi yake kiasi kwamba ungemhurumia kumwona akisema na watu wasiomsikiliza wala kujali anachosema. Jua lilikuwa kali na alikuwa kavaa koti zito. Joto la Dasalama tunalijua. Japo sikumsikiliza, nilihisi kazi yake ilikuwa ni "kuwarejesha kondoo katika zizi la Bwana". "Afrika na watu wake, imelaaniwa!" alipayuka huyu bwana huku akitembea kwa madaha. Akageuka huku na kule, akanyanyua biblia yake kuuuuubwa akaendelea: "Enyi uzao wa Hamu, mmelaaniwa na laana yenu inakaa!". Kwangu mimi maneno haya yalininyong'onyeza mithili ya mtu aliyenyeshewa mvua. "Hivi anajivunia nini kusema maneno haya? Hata...

Afrika: Bara linalokimbiwa na Waafrika wenyewe

Katika kujadili matatizo ya bara letu, watu wengi tumekuwa tukiwalaumu wazungu eti kwa kupora mali zetu. Nimesoma vitabu vingi vilivyoandikwa kuhusu Afrika. Nilichokiona katika maandishi ya wengi, ni malalamiko. Tunawalaumu wazungu. Hatusemi chochote kuhusu namna tulivyouchangia umasikini wetu wenyewe. Na inakuwa kama vile ukijaribu kuzungumzia upande wa pili, basi wewe si muungwana. Watu wanakutizama kwa jicho la marienge. Maandishi haya yanakusudia kugeuza kibao cha lawama. Bonyeza hapa kuendelea.

Raha ya kublogu ni uhuru wenyewe

Kwa mara ya kwanza nilisikia neno blogu kwa rafiki yangu aliyekuwa akijitolea kufundisha (volunteer) katika shule moja hapa nchini. Alinionyesha blogu yake na kwa kweli kama zilivyo za wazungu wengi, haikuwa na jambo la maana zaidi ya masimulizi ya hadithi zisizo na mashikio. Nikafungua na yangu, ikifuata nyayo hizo hizo za porojo nyepesi nyepesi. Haikuwahi kuingia kichwani kwangu kwamba inawezekana mtu kuisoma. Nilikuwa na sababu nyingi. Kwanza, rafiki zangu wengi hawakuwa wamehamasika na matumizi ya teknolojia ya habari. Aidha, wachache walioipenda hawakuvutiwa na mambo ya habari habari, wao waliziita za kizee. Nakumbuka tukitoka tuisheni za Makongo, tungeweza kupitia kwenye vioski vya mtandao (cafee) pale Mwenge kuchungulia hili na lile. Wakati mimi nikihangaika kusoma “templates” za blogu, wenzangu walikuwa, na mpaka leo, wanapenda kuangalia mambo flani ya ngono na udaku. Lakini pili sikuwa na wazo kwamba blogu yaweza kuwa uwanja mpana wa kukutana na falsafa mbali mbali. Nilijua ...

Duniani hakuna mwadilifu, wote tunahangaika

Maadili, mfumo wa kubaini jema na baya, hatuzaliwi nayo. Tunazaliwa tunayakuta yapo, yameanzishwa na wengine kwa makusudi yao ili kukidhi haja ya wakati husika. Hata waanzilishi wenyewe wa hayo yanayoitwa maadili yetu, tunakuwa hatuwajui ni akina nani na walitumia vigezo gani kutoka wapi ili kutuundia hayo yanayoitwa maadili. Hapa ninajaribu kuonyesha kuwa kila mmoja anaweza kuwa na mfumo wake binafsi wa maadili. Endelea hapa .

Dan Vinci Code: Ukweli unaouma?

Picha
Dan Brown mwandishi wa kitabu kinachokwenda kwa jina la Da Vinci Code , kafanya kile ambacho binadamu wengine hatuthubutu hata kukijadili. Kaamua kuchokonoa mambo ya kiimani ambayo watu tunakwepa kuyahoji, kwamba hayajadiliki. Ni dogma. Trela ya filamu yake hii hapa . Katika Da Vinci code, Dan Brown anajaribu kuchimbua “kweli” zilizojificha nyuma ya ukristo, “kweli” ambacho zimefunikwa na kanisa ili kuwapumbaza watu waamini kwamba Jeshua alikuwa mwana wa Mungu. Kwa kadiri ya Da Vinci Code, ukweli wenyewe ni kwamba Ukristo ulianzishwa na “nabii wa kawaida” ambaye hastahili kujidai kwamba ana uungu (divinity) wowote. Nabii mwenyewe ni Yesu Kristo. Kwa hakika, alimwoa Mariam Magdalena, ambaye baadaye ndiye aliyemchagua kuliongoza kanisa baada ya kifo chake. Suala hili, kwa mujibu wa Da Vinci Code, liliwakasirisha sana wanafunzi wake na baada ya kusulubishwa kwake, Mariam Magadalena ilibidi atimuliwe, ndipo akakimbilia Ufaransa na mtoto wao waliomzaa na Yeshua “mume” wake. Mwandishi anas...

Ben Carson: "Mswahili" bingwa Marikani

Afrika imejaa watu ambao wakizitumia mbongo zao ipasavyo wanatikisa kabisa historia ya Dunia hii. Wanatetemesha! Mifano ya waafrika waliosumbua historia yetu ni ndefu. Tatizo letu kubwa ni kwamba hatuwaoni mabingwa wengi walio nje na ulingo wa siasa. Ben Carson , ni Mmarikani mweusi, daktari bingwa wa Nyurolojia (Neurosurgeon)katika hospitali ya Johns Hopkins aliyewahi kutenganisha mara kadhaa mapacha waliounganika vichwa vyao. Kishawahi kuja Afrika, kuwatenganisha watoto wenye matatizo hayo ambao wanaishi mpaka leo. Ben hutumia masaa mengi kwa siku akifanya upasuaji wa “Mbongo” za watoto hasa wenye matatizo ya uvimbe kwenye ubongo. Bonyeza hapa kupata simulizi zake kwa ufupi. Mtandao wa Topblacks umetambua mchango wake unaoleta heshima kwa weusi wa nchi hiyo. Huyu bwana, pamoja na kuwa Daktari wa Tiba za Afya, ameandika vitabu kadhaa akijaribu kutoa wosia kwa vijana hasa wanafunzi wa shule namna ya kufanikiwa katika masomo. Anao pia mfuko wa kusomesha vijana wanaofanya vizuri. Huu ...

Ni lini tutajifunza kujifunza?

Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) ulikuwa na kasoro kubwa. Kasoro hizi zinaelezwa kujikita kuanzia kwenye utengenezwaji wake (in put) na utekelezaji wenyewe ambao ulileta matokeo yaliyotafsiri mpango mzima kuwa uliharibika. Sirikali ya uwazi (utandawazi) na ukweli ililaumiwa sana kwa kutokuwasikiliza wananchi ambao ndio wadau wakuu wa haya yanayoitwa maendeleo ya elimu. Malalamiko yalielekezwa katika mitaala yenyewe iliyoletwa kinguvu nguvu kwa msukumo wa Bosi wa Elimu wa wakati ule, Yusufu Mungai. Mitaala ambayo mtu unashindwa kuelewa hivi ilikuwa inatetea itikadi gani na kwa maslahi ya nani. Watoto wetu wakafutiwa masomo ya Historia, Uraia na Jiografia. Masomo ambayo yalikuwa yanajaribu kuwajenga moyo wa uzalendo watoto wa Kitanzania. Badala yake likaletwa somo linaloitwa Maarifa ya Jamii ambalo mumo watoto walijazwa maarifa ya mambo yanayohusiana na utandawazi na viwanda vya ulaya na mengine mengine ambayo kimsingi mtoto wa Mtanzania wa kawaida anayaona kuwa ndo...

Tumkaribishe mgeni jamani!

Nadhani zile makala za Ndesanjo zinafanya kazi kubwa kuliko tunavyodhani. Hatimaye Bw. Albert William ambaye alikuwa Afrika ya Kusini wiki jana katika mpango uitwao "Teaching and AIDS Pandemic" , amekata shauri rasmi. Yeye anasema anapendelea kutumia ung'eng'e zaidi. Kong'ori hapa kumtembelea mgeni kama ilivyo ada. Mpango huu unafanyika katika Afrika ukilenga kuvunja kimya na kuangalia upya namna ya kupambana na Janga la UKIMWI kwa kuwatumia waelimishaji katika sekta ya elimu "Teacher Educators". Huyu bwana ana mengi ya kusema kuhusu masuala haya ya UKIMWI.

Elimu yetu haikidhi haja

Elimu tunayoipata darasani imekaa kikoloni sana kiasi kwamba tunafunzwa kuwa watumwa waaminifu zaidi kuliko kujikomboa na wale maadui tunaodai kuwa tunapambana nao. Ujinga, maradhi na umasikini. Tatizo linaanza katika mitaala yenyewe inayosisitiza kujifunza mambo ya watu wengine ambayo hayana uhusiano na maisha yetu ya kawaida baada ya masomo ambayo kimsingi ni ya kijijini. Tunalishwa falsafa za kigeni zaidi kiasi kwamba tunafika mahali tunadharau kila kinachoonekana kuhusiana na ukwetu-kwetu. Kuna ukweli fulani kuwa watu "waliokwea madarasa" hawataki tena kwenda vijijini kutoa mchango wao katika maendeleo. Hiyo ni kusema kwamba elimu hii inaonekana kushawishi waungwana kukimbilia mijini huku wakiwaacha wale waliowapeleka shule wakiendelea kuteketea vijijini kwa matatizo yanayotatulika. Elimu yetu inatusaidia kukariri na kuhamisha mawazo ya watu badala ya tafakuri za kina katika maisha. Ndio maana inakuwa ngumu kwa wengi wetu kuhamishia mawazo ya darasani kuja mtaani. Maana m...

Vazi la Taifa: Imeshindikana?

Picha
Yapo mambo mengi ambayo tumekuwa tukiyaimba tangu kupata uhuru lakini mpaka leo inasikitisha kuona kuwa yameshindikana. Tuanadanganyana. Mfano ni hili suala la umasikini wetu. Watawala wamekuja na kuondoka, lakini tatizo liko pale pale. Tunaambiwa kuwa "bado tunaweka misingi ya maendeleo yetu, tufunge mikanda!". Miaka 40 na ushei hakuna lolote! Niliwahi kusoma makala ya Bwenge katika Gazeti la Rai nikachoka kabisa. Kwamba Chama cha Mapinduzi kimekuwa kikitumia maneno kwa ufundi na ungalifu mkubwa ili kukwepa hoja za wananchi kuhusu mambo ya msingi. Bwenge anatoa mfano wa yale mabango ya Kampeni ya CCM yaliyokuwa na picha ya mgombea wao wa Urais (Sasa Rais) na ile ya Mzee Mkapa. Upande wa Mkapa unakutana na maneno "uchumi unakua, ajira zinaongezeka n.k" Profesa Bwenge anasema CCM hawakutumia "me" (sijui ndio herufi au neno sijui)ili kusema "uchumi umekuwa". Wakiulizwa mbona tunalala njaa, jibu linakuwa rahisi: "Ndio. Lakini tumesema uchumi un...

Elimu sio cheti na cheti sio elimu

Hivi kwenda shule maana yake nini? Usomi ndio nini? Ni wingi wa "mawe" ya mhusika au ndio nini vile.Usomi ni mpaka uwe na makaratasi mengi au ni maarifa? Nadhani kuna hitilifu ya mtazamo kuhusu dhana ya usomi. Watu wanatambiana kwa wingi wa makaratasi yanayoitwa cheti, shahada...uzamifu sijui nini na nini. Wanaona raha kuitwa Dakta nanilii! Nina mashaka na aina ya usomi wa Watanzania tulio wengi. Tunasoma kwa sifa tu lakini hatusaidii chochote katika kuipeleka mbele jamii yetu. Watu wanasoma wapate makaratasi yatakayowapa utajiri. Makaratasi yakayowapa heshima. Saluti. Na mengine mengine. Huu ndio mtazamo wa waungwana tulio wengi. Mtizamo kinyume kabisa. Sioni maana ya tunuku za makaratasi haya manake yametuletea kero katika jamii. Mosi, watu wamekuwa hawana biashara nyingine "mashuleni" zaidi ya kusomea majalada hayo. Matokeo yake ni zao la wasomi vihiyo wasio na loloooote! Wasomi wanaomaliaza masomo na kusahau kama kuna kusoma. Wanaanza hata kusoma udaku. Vilevil...

Tatizo ni dini au watu wenyewe?

Nimefuatilia kwa makini mjadala ulianzishwa na Idya Nkya kwenye blogu yake kuhusu dini. Nimesoma michango ya wanafalsafa waliochangia. Majadala ni mkali na unatia changamoto kweli. Nilivutiwa kuundeleza mjadala huu chumbani hapa chuoni na ilikuwa ni kasheshe tupu tulipokuwa tukijadili suala hili. Mjadala ulikolezwa na mistari ya Ndesanjo inayokwenda kwa jina la Yesu/Isa na watanzania , Mtu ni utu si dini na nyinginezo nilizozitoa pembezoni mwa kibaraza chake upande wa kulia. Dini nyingi tulizobebeshwa (tulizozishika?) zina mafundisho mazuri. Zinatufundisha kuwa watu wazuri katika jamii. Zina makatazo mengi ambayo kimsingi yanalenga kutuchonga tuwe jamii yenye watu waungwana, wastaarabu ambao hatimaye wanaahidiwa maisha ya umilele. (Jambo zuri hili!) Dini zote lengo lake ndilo hilo. Pamoja na kwamba Ndesanjo ana wasi wasi na baadhi ya mafundisho ya dini hizo. Lakini ningependa kuamini kuwa dini zote (nyingi)maudhui yake yanashahibiana na yana faida yakifanyiwa kazi. Tofauti kubwa ni n...

Hiki ni kichekesho cha MMEM!

Mwishoni mwa mwaka jana, Wizara ya elimu iliitia "kash kash" asasi isiyo ya kiserikali iitwayo HakiElimu. asasi hiyo ilikuwa na matangazo mengi katika vyombo ya Habari yakielezea kwa kina hali halisi ya elimu nchini. Msisitizo wao ulikuwa katika kumulika matokeo ya Mpango wa (Maendeleo) ya Elimu ya Msingi, yaani MMEM. Kwa wengi wetu, matangazo hayo yalikuwa yakiutoboa ukweli wa wazi mkabisa ingawa Sirikali haikuutaka. Ukweli wenyewe ni pamoja na kuwapo kwa ubadhilifu mkubwa wa fedha za Mpango uliofanywa na walimu wakuu wakishirikiana na wakubwa kinyume na malengo husika. Ushirikishwaji duni wa wananchi katika Mpango mzima lilikuwa ni tatizo lingine lilobainishwa, kutokuwapo kwa kipaumbele cha kujenga shule za wanafunzi wenye ulemavu, mbinu zisizofaa zinazotumiwa na walimu katika ufundishaji na mengine mengi. Hayo yalikuwa kweli tupu, na haikuhitaji shahada ya uzamili kuujua. HakiElimu hata hivyo, walikuwa wamefanya utafiti wa kutosha katika hilo. Sirikali kwa kutumia ngu...

Kondomu na UKIMWI, wapi na wapi?

UKIMWI unatowesha maisha ya watanzania wengi kwa kasi isiyo ya kawaida. Na bahati mbaya, janga hili linaangamiza maelfu kwa maelfu ya vijana wanaopotoshwa na wazee kwamba watumie kondomu, eti kinga thabiti ya kuwalinda na UKIMWI. Vijana ambao kimsingi ni nguzo muhimu katika Taifa kwa nyanja zote. Nimesikia mijadala mbalimbali inayojaribu kuhalalisha matumizi ya kondomu. Yupo Pardi Maarufu anayepigana kufa na kupona, kupitia magezeti kuhakikisha kuwa anawaweka sawa wazinzi na washerati wote ili watumie kondomu. Sumaye na Watawala wengine, wameonyesha bidii sana katika kuangamiza jamii kwa kusisitiza matumizi ya kondomu. Kondomu ambazo zimeendeleza maambukizi ya UKIMWI kwa kasi ya kutisha. Yeye anasema anawagawia watoto wake “kinga” kila siku ili wakafanye mambo yao kwa nafasi zao. Lakini jambo la kujiuliza ni kwamba, hivi kondomu zimesaidia kwa kiasi gani kupunguza maambukizi ya UKIMWI? Pamoja na matangazo yaliyotanda kila kona ya miji yetu na katika vyombo vya habari, ...

Makala hii ingesomwa tungekuwa tulivyo?

Nimeirejea makala ifuatayo kwenye maktaba ya Mheshimiwa Ndesanjo. Kimsingi napenda uandishi wake. Nimekumbana na makala hii ambayo sina hakika kama ilisomwa na watanzania. Nasisitiza kwamba tuna kazi ya ziada kuwabadilisha wapende kusoma. Unapokuwa na jamii ya watu wanaopenda udaku inakuwa tabu. Mtoto anakua anakuta baba ni mpenzi wa magazeti ya udaku. Na yeye anakuwa mdaku hali kadhalika. Akiwa kwenye mtandao hataacha kuangalia ngono. Masuala nyeti hana muda nayo. Nina wasi wasi kama tutaweza kufikisha ujumbe wa kubadilika kwa jamii ya jinsi hii (isiyopenda maandiko). Ndio maana hata suala la elimu ya uraia limekuwa gumu, maana andiko lenyewe lenye elimu hiyo halisomwi. Tutafute mbinu ya kuwabadilisha watu wa jamii yetu ambao nadiliki kusema wanateketea. Sijaribu kusema kwamba wanabalika, lakini nadhani, kasi hairidhishi. Sijui kama tunaweza kuwakuta huko huko kwenye magezi ya udaku?

Hivi makala hizi zinasomwa kweli?

Leo nilikuwa natembea tembea nyumbani kwa Ndesanjo Macha. Nimejifunza mambo mengi nyumbani kwake. Makala nyingi zimejaa maudhui mazito ambayo kusema kweli yana nafasi kubwa katika kuibadilisha jamii ya kitanzania. Tatizo ni kuwa Watanzania wengi anaowaandikia hawana muda na makala ndefu kama zake. Wanataka makala za ngono, fupi fupi zenye masimulizi ya kimapenzi! Makala kama zake, sina hakika kama kweli zinasomwa na wengi, hasa vijana ambao kama wangezisoma zingewasaidia. Swali nililotoka nalo ni kwamba makala kama hizi zinawasaidia wanaozisoma? Hivi wanazisoma hata hivyo?