Vazi la Taifa: Imeshindikana?

Yapo mambo mengi ambayo tumekuwa tukiyaimba tangu kupata uhuru lakini mpaka leo inasikitisha kuona kuwa yameshindikana. Tuanadanganyana.

Mfano ni hili suala la umasikini wetu. Watawala wamekuja na kuondoka, lakini tatizo liko pale pale. Tunaambiwa kuwa "bado tunaweka misingi ya maendeleo yetu, tufunge mikanda!". Miaka 40 na ushei hakuna lolote!

Niliwahi kusoma makala ya Bwenge katika Gazeti la Rai nikachoka kabisa. Kwamba Chama cha Mapinduzi kimekuwa kikitumia maneno kwa ufundi na ungalifu mkubwa ili kukwepa hoja za wananchi kuhusu mambo ya msingi.

Bwenge anatoa mfano wa yale mabango ya Kampeni ya CCM yaliyokuwa na picha ya mgombea wao wa Urais (Sasa Rais) na ile ya Mzee Mkapa. Upande wa Mkapa unakutana na maneno "uchumi unakua, ajira zinaongezeka n.k" Profesa Bwenge anasema CCM hawakutumia "me" (sijui ndio herufi au neno sijui)ili kusema "uchumi umekuwa". Wakiulizwa mbona tunalala njaa, jibu linakuwa rahisi: "Ndio. Lakini tumesema uchumi unakuwa". Maneno ya kujitetea. Ukiangalia kwa makini, ni kweli kabisa.

Nchi yetu ina uswahili mwingi, vitendo haba. Tunaendelea na maisha. Maigizo mengi uhalisia hakuna. Hadhira inadanganywa. Maisha yanaendelea.

Ninazungumzia vazi la Taifa. Mijadala ya vazi la Taifa imekuwa ikiibuka na kuzama. Lakini jambo moja linaonekana kuwa wazi: Kwamba suala hili limeshindikana. Sijui tatizo lenyewe liko kona ipi ambayo kamwe haififiki!

Mwaipopo aliwahi kuandika kutukumbusha kuhusu nguvu ya mawazi. Kwamba ni utambulisho ambao tunaweza kujivunia miongoni mwa watu wa mataifa mbalimbali.

Wainajeria mavazi yanajulikana. Ukimwona kokote unajua alikotoka, kwa kuangalia mavazi yake. Ndugu zetu hao wamefanikiwa katika hili. Na wanaona fahari kutoka kikwao kwao. Ndio utambulisho wao miongoni mwa mataifa.

Sisi je? Tumefikia wapi na mjadala huu? Tumeishiwa pumzi? Kikwazo ni nini hasa?

Nadhani tatizo ni mtazamo wetu mbovu ambao umejaa utandawazi mpaka tunafika mahali tunasahau kabisa mambo ya kwetu!

Niliwahi kusoma mawazo ya Ndesanjo, nikajikomboa. Ndesanjo alikuwa anahoji sababu za Mawaziri wote kuvaa suti za kizungu(Pamoja na Waziri wa Utamaduni mwenyewe) wakati Mawaziri wa enzi za Uhuru walivaa ya Kiafrika. Nilipozitazama picha hizo alizokuwa anazizungumzia nikajisemea "Lakini kweli!". Kwamba tunakokwenda sio. Tutafika mahali tutakuwa hatuna kitu chochote tunachoweza kujidai kuwa ni chetu. Tunakuwa tumetandawazishwa kabisaaa!

Tumefikia wapi katika mjadala wa kitaifa kuhusu vazi la Taifa letu? Mwaka jana kuliibuka hoja hiyo, tukadhani hewala, wakati umefika. Lakini wapi bwana kumbe ni maneno tu!

Nadhani mjadala huu bado utakuja tena kwa wakati wake. Utakufa kama kawaida. Sababu ni kwamba: Watanzania hawana chao tena. Utandawazi umefanya kazi yake. Wacha tuvae tunavyotaka.


Wazungu watatushangaa maana tunapenda kujidhalilisha wenyewe. kwa nini wasitushangae?.

Maoni

  1. Samahani maoni yangu hayalingani na habar hii. Nilitaka kuongeza jambo fulani katika utangulizi wako kwamba u'mwalimu. Taaluma njema hii na wamebarikiwa wale wamejitolea kuwa walimu.

    Nimeonja uwalimu kwa muda. Hawa vijana wachanga wamenoa akili zangu pia. Nikidhani labda katika utangulizi wako utataja pia hawa vijana watakufaidi. Si lazima ubadilishe, ni maoni tu.

    JibuFuta
  2. kaka kazi nzuri hiyo leo nilikuwa natembelea kijiwe chako, kanifurahisha sana huyo msandawe.

    JibuFuta
  3. Mtandawazi asante sana kwa cahngamoto. Ninaamini unayosema. Lakini naamini nikipitiapitia mistari ya ufahamu kwenye kibaraza cha Ndesanjo, ninaweza kufanya kitu.

    JibuFuta
  4. Bwaya

    Hatimaye natinga kwa mara ya kwanga hapa nyumbani kwako. Kwa hakika unachokisema kuhusu mustakabali wa taifa hasa kwa upande huu wa vazi la taifa unasikitisha.

    Yamefanyika mengi lakini tumeishia kwenye mjadala na hatimaye eti wakapatikana washindi wa vazi la taifa na ikawa ni suti 'simple' kama alivyotuonyesha ndugu yetu michuzi katika vielelezo vyake vya jana.

    Nafikiri kuna tatizo la msingi vazi la taifa linashindikana kwa sababu kuu mbili au tatu , mosi diversity ya makabila yetu ni mengi kuliko ya Nigeria kama sikosei.
    Halafu pili hatuna ule utaifa kujivunia cha kwetu. Wanaijeria wanajivunia unaijeria kama Wachina wanavyojivunia uchina na kama Waskochi wanavyojivunia uskochi.
    Hebu mfano tuangalie jamii 'zilizochanganyikiwa' kama za Marekani hivi wale wana vazi la taifa. Haya ndiyo mawazo yangu ndugu yangu Bwaya.

    JibuFuta
  5. Mwaka jana nchini Kenya wamezindua vazi la taifa. Eti shilingi milioni 50 za Kenya zilitumika kusaka vazi hili. Kwa kiasi fulanilinarandana na lille la Nigeria japo limetiwa Uswahili kwa kiasi fulani. La kushangaza ni kwamba viongozi wenyewe hawako mstari wa mbele kulivalia hata inapokuwa sikukuu za Kitaifa.

    Nikidhani tunastahili kupokea vazi la Nigeria kama kitambulisho cha vazi la Kiafrika kisha nchi mbalimbali ziongeze kipengele fulani kidogo tu ili kulitofautisha na lile na Nigeria.

    JibuFuta
  6. Tulipokee vazi la Nigeria kama kitambulisho cha bara Afrika. Kisha tubadilishe kiasi kidogo tu ili kulipa sura ya nchi. Kwa njia hii nikidhani tutawaonyesha ulimwengu kwamba Afrika ina sauti moja.

    JibuFuta
  7. Nami nimeingia kwako Bwaya. Hongera kwa kazi nzuri! Nimefurahia.

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Haiba ni nini?

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Uislamu ulianza lini?

Makundi Manne ya Tabia za Watoto Kitabia