Elimu yetu haikidhi haja

Elimu tunayoipata darasani imekaa kikoloni sana kiasi kwamba tunafunzwa kuwa watumwa waaminifu zaidi kuliko kujikomboa na wale maadui tunaodai kuwa tunapambana nao. Ujinga, maradhi na umasikini.

Tatizo linaanza katika mitaala yenyewe inayosisitiza kujifunza mambo ya watu wengine ambayo hayana uhusiano na maisha yetu ya kawaida baada ya masomo ambayo kimsingi ni ya kijijini. Tunalishwa falsafa za kigeni zaidi kiasi kwamba tunafika mahali tunadharau kila kinachoonekana kuhusiana na ukwetu-kwetu.

Kuna ukweli fulani kuwa watu "waliokwea madarasa" hawataki tena kwenda vijijini kutoa mchango wao katika maendeleo. Hiyo ni kusema kwamba elimu hii inaonekana kushawishi waungwana kukimbilia mijini huku wakiwaacha wale waliowapeleka shule wakiendelea kuteketea vijijini kwa matatizo yanayotatulika.

Elimu yetu inatusaidia kukariri na kuhamisha mawazo ya watu badala ya tafakuri za kina katika maisha. Ndio maana inakuwa ngumu kwa wengi wetu kuhamishia mawazo ya darasani kuja mtaani. Maana mengi ya tuliyasoma hayaonekani mtaani. Yanakuja kuonekana kidogo katika ngazi za juu zaidi ambazo hufikiwa na asilimia isiyozidi mbili. Ndio maana wasomi wanakuwa tofauti sana na jamii kiasi kwamba wanajenga tabaka lao wenyewe. Kwa msomi kuishi vizuri na jamii, inaamanisha kuaishi kwa uangalifu sana na uwezekano ni kwamba anatumia kiasi kidogo sana cha maarifa yake ya darasani.

Wapo wenye dhana kwamba elimu inarahisisha kujiletea utajiri wa fedha na kila kitu. Lakini imegundulika kwamba watu wenye elimu huwa hawaupati huo utajiri wanaoutaka. Wanaishia kuajiriwa na watu waliokuwa wa kawaida sana madarasani. Kwa maana nyingine, elimu ni kizuizi cha utajiri.

Ni kwa mtazamo huo, ninakuja kinyume kabisa na mfumo wa elimu rasmi (formal) ambao unatushibisha mambo mengi yasiyo na uhalisia katika maisha tunayoishi katika jamii zetu. Ya nini kuendelea na mfumo huu wa kitumwa? Nini faida ya kuwa na elimu ambayo haikusaidii kuishi vizuri na wenzako?

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Pay $900? I quit blogging