Elimu sio cheti na cheti sio elimu

Hivi kwenda shule maana yake nini? Usomi ndio nini? Ni wingi wa "mawe" ya mhusika au ndio nini vile.Usomi ni mpaka uwe na makaratasi mengi au ni maarifa?

Nadhani kuna hitilifu ya mtazamo kuhusu dhana ya usomi. Watu wanatambiana kwa wingi wa makaratasi yanayoitwa cheti, shahada...uzamifu sijui nini na nini. Wanaona raha kuitwa Dakta nanilii!

Nina mashaka na aina ya usomi wa Watanzania tulio wengi. Tunasoma kwa sifa tu lakini hatusaidii chochote katika kuipeleka mbele jamii yetu. Watu wanasoma wapate makaratasi yatakayowapa utajiri. Makaratasi yakayowapa heshima. Saluti. Na mengine mengine. Huu ndio mtazamo wa waungwana tulio wengi. Mtizamo kinyume kabisa.

Sioni maana ya tunuku za makaratasi haya manake yametuletea kero katika jamii. Mosi, watu wamekuwa hawana biashara nyingine "mashuleni" zaidi ya kusomea majalada hayo. Matokeo yake ni zao la wasomi vihiyo wasio na loloooote! Wasomi wanaomaliaza masomo na kusahau kama kuna kusoma. Wanaanza hata kusoma udaku.

Vilevile, ni utamaduni huu wa vyeti ndio unasababisha kutoweka kwa amani miongoni mwa wanafunzi nyakati za mitihani. Naongolea wizi wa Mitihani. Watu hawasomi, mtihani ukifika wanataka nao wapate makaratasi haya. Ujinga!Hapo unazalisha watu wenye kiu ya cheti na sio ukwasi wa maarifa.

Lakini pia, ndio sababu siku hizi Bongo ukiwa na pesa, unapata karatasi lililoandikwa vyovyote upendavyo (yaani chagua lako). Iwe ni cheti, Digrii ya heshima ...uzamivu na nini sijui unapata ukitaka. Ubadhilifu wa vyeti limekuwa suala la kawaida.

Tutawezaje kuwatofautisha wenye maarifa ya kweli na wabadhilifu kama wote wanamiliki vyeti kama "kawa"? Ni kuacha kuthamini elimu ya cheti, badala yake tuhamie katika elimu nyingine kabisa. Elimu isiyothibitishwa na makaratasi bali uwezo wa kuyatumia maarifa kwa faida ya wengi.

Mwaka jana nilimsikia bwana moja akipiga soga na wenzake mara tu baada ya kupangiwa mahala pa kuishi katika chuo fulani. "Aisee hapa itabidi nilale sana". Wenyeji wakacheka kwa tabasamu la mapokezi. "Kwa nini braza?" Wakamtania. "Adivansi nililala sana... lakini bado nikapata prinsipo saba kombi yenyewe ilikuwa PCM". Hapo ulifuatia mshangao na butwaa. "Hee, mwenzetu masomo yako matatu wewe una prinsipo saba umezitoa wapi?". Haikushangaza maana juma lililofuata bwana huyo alibainika kuwa ni mbababishaji na hajawahi kukanyaga madarasa mawili katika sekondari ya juu.

Kuna watanzania wangapi hawajagundulika lakini wamepeta na wamemaliza masomo kwa salama na amani? Kuna PHD bogasi ngapi humu nchini ambazo zimepatikana kimizengwe? Kuna wasomi uchwara wangapi wenye makaratasi mazuri na wameshikilia nafasi nyeti katika nchi hii?

Tukiweza kuondokana na huu ujinga wa kupeana nakaratasi haya tukitiana moyo kwamba ndio kwenda shule, nadhani tutafika mbali sana tena kwa haraka. Kwa nini mtu usinde shule ukafundishwa, ukapata pa kuanzia, ukajijengea uwezo wa kujisomea mwenyewe, halafu ukaishia zako bila kudai jitu linaloitwa cheti? Kwa nini tunathaamini haya makaratasi yanayoweza kughushiwa kiujanja ujanja?

Usomi usitafsriwe kama tunuku ya cheti. Badala yake iwe ni kujipanua maarifa tu bila haja ya kumiliki haya makaratasi ya pesa. Kuna ubaya gani kwani ukienda kutafuata kazi ofisini, mathalani upewe mtihani hapo hapo, ukifaulu...kazini!

Leo si ajabu mwenye maarifa sahihi kuhusu kazi fulani, asipewe fursa ya kuifanya kazi hiyo eti kwa sababu gamba lake halijakaa vizuri. Matokeo yake unakuta wa pili mwenye cheti safi (ambacho huenda kakipata kwa mtindo wa zima moto), na hana ujuzi sawa sawa ndiye anayethaminiwa. Huu ni ugonjwa mbaya sana.

Niliwahi kumsikia rafiki yangu mmoja akitamba kuwa amegonga mwaka wa nne chuo akifaulu testi na hawajawahi kushikwa na hajawahi kukanyaga maktaba ya chuo! Anadai anaponea shingoni kwa kutumia vitini vya darasani. Huu ndio uzandiki tunaouzungumzia.

Nashangaa mtu anaenda kusoma kozi ya kompyuta... mwishoni anadai karatasi linaloitwa cheti ama shahada. Ili iwe nini? Kama ana ujuzi unaotakiwa si aende kazini akauonyeshe huko huko? Tuna ugonjwa wa vyeti ndio maana mitihani haiachi kuvuja. Ndio maana watu wakihitimu shuo wanauza vitabu (kama kweli kuna kununua vitabu siku hizi.) Watu wanasahau kama kuna kusoma tena. Ukimwuliza mtu kwa nini hasomi. Jibu ni rahisi. Hakuna cheti. Siku hizi kila kitu cheti! cheti! cheti! cheti!. Ni manini haya mavyeti?

Kama walivyo na mashaka baadhi ya watukuhusu PHD za waungwana fulani na mimi nina mashaka na usomi wa siku hizi unaohesabika kwa wingi wa makaratasi ya vyeti. Usomi ambao unaongeza tatizo la rushwa. Tatizo la wizi wa mitihani. Wasomi gani wanafaulu hawasaidii chochote katika nchi? Cheti hakiwezi kutukomboa. Ndio maana kuna wenzetu hawana shida navyo wanaenda shule kwa hobi. Si kufuata makaratasi.

Watu wengine wanafikiri usipokuwa na cheti huwezi kufanikiwa maana wanafikiri kufanikiwa ni kujirundikia hela kwa saaaana! Mtizamo huu una kasoro kubwa.

Tujiulize, vyeti tulivyo navyo vinasaidiaje kuikomboa jamii ya kitanzania. Vinatuongezeaje mchango katika kujikomboa kifikra. Haya mavyeti yanatulemaza hayatusaidii kujikomboa. Ni katika mtiririko ule ule wa kuiga mambo ya watu wenye pua ndefu na ngozi nyeupe. Tuachane nayo.

Maoni

 1. Bwaya kuna kazi na hasa sasa Tanzania. Kama utakumbuka salamu zangu za mwaka mpya zilijikita katika kauli hii ya kuhamasisha watu kusoma. Kusoma kumekufa kila mtu anasaka cheti. Sidanganyi kama tunataka kusoma kwa misingi ya vyeti subiri utatazama taifa letu litakavyozidi kutawaliwa na wageni. Tutabinafsisha hata madaraka ya kisiasa maana hatutakuwa na uwezo wa kupanga mambo. Lakini kifanyike nini, mabadiliko yanaanza na wewe kuchukia hali hii na kupigana kusaka maarifa yatakayosaidia kuendesha maisha yako. John Kerry alikuwa akisema, "Najua tunaweza kufanya vema" mwisho wa nukuu na tafsiri ni yangu. Nyerere aliwahi kusema, "Inawezekana, timiza nafasi yako." na mimi nijinukuu sasa, "tutafika, cheza karata yako."

  JibuFuta
 2. Na mimi nikunukuu; "Tutafika, cheza karata yako".

  JibuFuta
 3. Ehuu! Kupumua huko ni kwa sababu mbili mosi ni kumaliza kusoma makala hii. Pili ni kupatikana tena kwa ndugu Bwaya. Sio katika viunga vingine bali cha kwake mwenyewe, maana kungine huja mara apatapo wasaa.

  Kubwa ni hoja yako. Haya masuala unayoleta ndio mwale unaoonyesha tafsiri halisi ya elimu. Makene amesahau hili lakini analifahamu vema kuwa "Elimu ni kile kinachosalia baada ya kujifunza." Mie naongezea kidogo kuwa masalio hayo yaonyeshe mafanikio yanayoonekana katika jamii husika.

  Nikija kwenye vyeti naona wengi wetu tunavitamani kwani ni hirizi ya kupata kazi kama alivyowahi kusema-ga Mtakatifu Nyerere wakati fulani. Ukishapata kazi tu basi waweza hata kukitia moto endapo hutarajii kuhama katika kazi hiyo. Kinachotufanya wengi wetu tunga'ng'anie kumiliki rundo la astashahada,shahada, shahada ya uzamili na ile ya udaktari ni kupata kazi ambayo mtu mwingine aliibuni. Mara chache huwa tuna mtazamo wa kubuni kazi zetu wenyewe kutokana na taaluma zetu. Hili limeshadidiwa sana na waajiri ambao hutaka alama za juu, na sio ushahidi wa ufanisi wa kutukuka. Kwa mtindo huu nani atataka cheti cha chini, achilia mbali kutokihitaji kabisa.

  Pengine nimalizie na rai kuwa kwa kuwa utamaduni wa kupeana vyeti umeanza dahali nyingi tu basi ni vema sasa shinikizo liwe katika ushindani wa nani anajua zaidi na sio nani kafaulu zaidi. Mfano mdogo ni kuwa ughaibuni wakikwita kwenye usaili ni hatua ya mwanzo tena ndogo tu. Shughuli utaiona kwenye usaili ambao mosi utataka kudhihirisha yale uliyoyasoma lakini la muhimu ni kutaka kujua ufahamu wako hata wa mambo mengine, pengine katu hukuyadhania. Hapo ndipo wengi wetu tunapigwa bao. Sio nchini kwetu ambako msaili anakuuliza mulemule ambamo umesoma na ukimjibu vema basi kazi umepata.

  Alamsik Binuur.

  JibuFuta
 4. Kama tutaweza kutofautisha maana ya maneno 'KUINGIA' na 'KUTOKA' mahali, bilashaka hapo patakuwa msingi mzuri wa kubadilishia masuala yetu yaliyoharibika zamaaaani sana. Wakati wengi wetu tunaamini kuwa tumesoma, ukweli ni kuwa hatukusoma kwa maana hatukuingia madarasani bali tulipitia shule fulani fulani tu

  JibuFuta
 5. kuna tofauti kubwa baina ya KUPITA na kKUINGIA mahala fulani, na pengine hili ndilo linalowafanya baadhi ya watu kuamini kuwa wao ndio waliosoma sana huku wengine wakiwa katika daraja la UPE.(sijataja mtu mie, atakayejishuku shauri yale)

  Kama tungeliweza kujua tofauti ya maneno hayo kikamilifu, bilashaka hali isingelikuwa mbaya kwa kiwango hiki cha sasa, ambapo wengi wetu tunaamini kuwa tumesoma, kumbe hatukusoma wala nini, kwa maana HATUKUINGIA madarasani, bali TULIPITIA katika shule fulani fulani tu

  JibuFuta
 6. Elimu ndio ufunguo wa maisha. Ufunguo unaoweza kufunga au kufungua kulingana na matumizi. Elimu ya kupitia shule hii na ile inayotunikiwa cheti imetusaidiaje kujikomboa? Jibu ni kwamba tumebaki kujisifu kuwa tumekanyaga madarasa wakati "madarasa" hayo hayajatusaidia katika kuwakomboa watu wetu. Elimu imetufungia nje. Imetufanya watumwa.
  Wapo watu ambao elimu ya cheti iliwashinda lakini ndio walioleta mageuzi katika dunia ya leo. Watu kama akina Isaac Newton, Faraday na wengine. Hawakuwa na cheti lakini mambo yao yanawatambulisha kuliko hata vyeti kama wangevipewa.
  Binafsi, sifikiri kama kuingia ama kutoka mahali (iwe chuo sijui shule na nini) kutatusaidia sana. Maana inawezekana kabisa hata usiingie kokote lakini bado ukawa na nafasi kubwa ya kutoa mchango wako kwa jamii.
  Ukifuatilia watu walioingia hapa na pale unakuta wameharibikiwa tu maana wanajijengea tabaka lao tofauti na wananchi wa kawaida ambao ndio wengi. Hasara tupu, ndio matokeo.

  JibuFuta
 7. Nimekutana na maaandiko ya Mwanafalsafa mmoja wa Kibrazil, Paul Freire aliyeamini kuwa katika jamii ya kijangili, elimu hutumika na wachache (bourgeoiseie)kama chombo cha kinyonyaji cha kuwakandamiza wananchi wasionacho ambao ndio wengi kimsingi.
  Ukandamizajai huu unaanzia katika utoaji wa makaratasi ya vyeti eti ndio uthibitisho kuwa fulani kaelimika.
  Hili ni tatizo ambalo linatupeleka pabaya. Turejee wosia wa Makene ule wa mwaka mpya. Tujisomee.
  Msangi, unapimaje "kwenda darasani" na "kupitia" hapa na pale?

  JibuFuta
 8. Freire aliamini kuwa elimu ni ile inayoweza kuwezesha wale watu Fanon aliwaita "waliolaaniwa." Hakuone umuhimu wa elimu inayoandaa watu ili wakaajiriwe wapate mshahara bila kuweza kubadili jamii inayowazunguka.

  Kuna chuo India kinaongozwa na Bunker Roy kinaitwa Barefoot College. Moja ya kanuni za chuo hiki ni kuwa ukimaliza masomo hupewi cheti. Chuo hiki nia yake ni kuendeleza maisha vijijini, unapompa "msoni" cheti unampa tikiti ya kuhama vijijini kwenda mijini!

  JibuFuta
 9. Bwaya, nitajibu hoja zako kwenye ile makala kuhusu dini.

  JibuFuta
 10. Usomi ni mojawepo ya uwekezaji mtaji. Kama wanavyowekeza wafanyibiashara, wasomi nao wanawekeza katika elimu. Katika mataifa ya Afrika swala la maarifa haliji kwanza. Linalotangulia ni jinsi ambavyo mtu atakuwa na ukiritimba katika eneo fulani utakaompa ugali wa kila siku.

  David Kyeu, mwalimu mwenzako mkenya

  JibuFuta
 11. Samahani ingawa haya siyo maneno yanayo endana na kichwa cha habari lakini naomba nitoe tangazo langu kuhusu blog.

  TANGAZO:

  Baada ya uchunguzi wa hali ya juu nimegundua jawabu la kuondoa Blogger NavBar (Sehemu ya juu kabisa ya Blog yako inayo onesha search this blog).

  Hii kutokana na ya kwamba watu wengi uwa wanachukizwa na jinsi hiyo NavBar ilipo.

  Jawabu la hili swali unaweza kusoma kwa kubonyeza hapa

  Kama ukipata tatizo au maswali zaidi naomba niandikie na nitakujibu asap.

  Nashukuru,
  ©2006 MK

  Imetengenezwa na kuletwa kwenu na ©2006 MK

  JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mbinu za Kumfundisha Mtoto Kusoma Akiwa Nyumbani

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3

Fumbo mfumbie mwerevu

Mambo ya Kuzingatia Unapoandika Wasifu wa Kazi (Curriculum Vitae)