Tutafakari hatari ya ‘malezi ya bweni’


PICHA: Aparna

Wazazi hawaamui tu kuwapeleka watoto wadogo kusoma shule za msingi za bweni. Ukiwasikiliza, mara nyingi wanakuwa na sababu za msingi kufanya maamuzi hayo magumu. Masuala kama migogoro ya kifamilia, wazazi kutokupatikana nyumbani, kutokuaminika kwa walezi mbadala mfano, wadada wa kazi, ni baadhi ya sababu zinazowafanya wazazi waamue kulipa gharama kubwa ya kuwakabidhi watoto kwa walezi wanaoaminika shuleni.


Nafahamu wapo wazazi wanaochukulia shule za bweni kama sehemu ya kuonesha uwezo wao wa kifedha. Kwa mfano, baadhi ya wazazi hususani wale wenye uwezo wa kifedha, huzifikiri namna nzuri ya kuonesha ‘kujali elimu ya mtoto’ ni kumpeleka kwenye shule ya gharama kubwa na hata ikibidi shule ya msingi ya bweni ‘ili mtoto akazingatie masomo na apate muda wa kutulia.’ Hawa ni wachache lakini wapo. Shule pia zinazowaaminisha wazazi kuwa taaluma inapatikana bweni nazo zipo. Saa nyingine ni mchanganyiko wa nia njema, biashara au basi tu kukosa uelewa.


Ukweli unabaki kwamba shule za bweni kwa watoto wadogo zimeanza kuwa maarufu kwenye jamii yetu. Tulizingumzia baadhi ya sababu zinazowafanya wazazi walazimike kufanya maamuzi magumu. Hata hivyo, tafiti hasa zinazoangazia malezi wanayoyapata watoto wadogo kwenye shule hizi za bweni hazipatikani. Hii ndio hasa ilikuwa sababu iliyonisukuma kuangazia eneo hili la malezi. Ninayoyaandika sikusimuliwa.


Kati ya mwaka 2014 na 2015 nilifanya utafiti kwenye shule hizi za bweni kama takwa la shahada ya Uzamili ya Ushunuzi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Nililenga, pamoja na mambo mengine, kulinganisha mazingira ya kimalezi kwa watoto wa bweni na wenzao wanaosoma kutwa kwa maana ya kulelewa nyumbani.


Maeneo linganishi yalikuwa makubwa mawili. Kwanza, usisimushi wa kiufahamu, kwa maana ya namna mazingira yanavyomchangamsha mtoto kiakili. Lakini pili, usisimushi wa kimahusiano na kihisia, kwa maana ya namna mazingira hayo yanavyojali hisia za mtoto na kufanya ajisikie salama.


Katika kutafuta taarifa, nilichagua idadi sawa ya watoto wenye miaka sita na saba kwa darasa la kwanza na pili mtawalia kwa kutwa na bweni kwa kile shule. Nilizungumza na watoto wenyewe kwa minajili ya kupata uzoefu wao lakini pia kutathimini uwezo wao wa kiakili, kihisia na kimahusiano. Pia nilizungumza na wazazi wao moja baada ya mwingine kwa minajili ya kupata uzoefu wa wazazi kuhusu tabia za watoto wao kihisia, kimahusiano na kiakili.


Matokeo ndio yalinishangaza kidogo. Kwanza, watoto wengi wa bweni, hasa darasa la kwanza, walinisimulia vile wanavyopata shida kukabiliana na maisha ya kutengwa na wazazi. Simulizi za watoto hawa zilionesha bayana kuwa wengi walichukulia kupelekwa bweni kama kutengwa, kutokupendwa na kuadhibiwa. Walikuwepo pia wachache waliojitutumua kuonesha kuwa kukaa nyumbani na wazazi na familia ni kudeka, kutokukua, utegemezi na ‘utoto.’ Namkumbuka mmoja mwenye miaka sita aliniambia kwa kujiamini kabisa, “Nimeshakuwa mkubwa bwana. Kukaa kaa na wazazi ni mambo ya kitoto.” Huyu kishunuzi keshajifunza kujihami na uhalisia mchungu kuwa yuko mbali na wazazi.


Nilitaka pia kujua mtoto anamwamini nani? “Unapokuwa na kitu kinachokusumbua, unaenda kumwambia nani?” Swali hili halikuwa gumu kwa watoto wa kutwa. Wengi waliwataja wazazi wao au mmoja wa wanafamilia. Hili ndilo lililotarajiwa. Lakini kwa watoto wa bweni majibu yalikuwa na mkanganyiko. Wengi walikosa mtu mahususi wa kumtaja na waliobaki waliwataja watoto wenzao. Katika mazungumzo na wazazi wao, tofauti hiyo ilionekana bayana. Kuishi mbali na wazazi kunawafanya watoto wakose mtu wa kumwambia shida zao. Hali hii inaweza kuwa na madhara makubwa hasa katika nyakati hizi za kukithiri kwa matukio ya udhalilishaji wa kingono kwa watoto.


Aidha, walezi wa watoto wa bweni walikuwa na masimulizi mengi yanayofikirisha. Nakumbuka visa vya watoto wa darasa la kwanza kufungasha virago vyao usiku wa manane wakitaka kupelekwa nyumbani kwa lazima. Nakumbuka visa vya watoto kujikojolea kitandani, kuogopa kulala wenyewe usiku. Niliona pia dalili za watoto wengi wa bweni kuwa wakorofi, wasiojali au kuwa wakimya kupitiliza.


Ingawa kwenye eneo la usisimushi wa kiufahamu watoto wanaoishi bweni walionekana kuwa bora zaidi ukilinganisha na wenzao wanaoishi na wazazi wao, bado ungeweza kuona mabadiliko ya vile wanavyojitazama, namna wanavyoishi na watu, namna wanavyojifunza maisha na kadhalika. 


Hatari kubwa zaidi niliyoiona katika mazingira ya bweni ni kukosekana kwa mtu mzima anayefuatilia kwa karibu mahusiano baina ya watoto na kile ambacho watoto wanajifunza kwa watu wazima wasio sehemu ya familia zao. Haya ni mambo yanayowasha masikio ikiwa kama jamii tunalenga kujenga kizazi cha watu wanaothamini familia.


Niandikie: bwaya@learninginspire.co.tz

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?