Unampeleka mtoto mdogo bweni? Fikiria.


Miaka michache iliyopita, mtu ulikuwa ukisikia shule za msingi za bweni, tena kwa watoto wadogo, tafsiri unayopata kwa haraka haraka ni malezi mabovu. Unampelekaje mtoto wa miaka sita bweni? Kuna nini cha maana shule ya bweni kinachohalalisha mtoto kutengwa na wazazi wake? Kwa hiyo, tuliona bweni ni uamuzi wa mzazi asiyeelewa jukumu lake la malezi, mzazi asiyejali, anayeamua kumtelekeza mtoto kwa sababu zisizo na msingi.


Lakini kwa hizi nyakati tulizonazo, tunapokabiliwa na mabadiliko mengi ya kijamii, saa nyingine tunahitaji kuwa na tahadhari tunapofanya mahitimisho ya haraka kwa namna hiyo. Sikiliza simulizi la Aisha, afisa wa benki, mama wa mtoto anayesoma shule ya msingi la bweni.


“Sikuwahi kufikiri ningekuwa mama anayeona bora mtoto aende bweni. Ndugu yangu yamenikuta.” Aisha ana mgogoro mkubwa na mzazi mwenzake. Ugomvi wao, ananiambia, ulifikia ngazi ya uadui. Haikutosha wao kushindwa kuishi pamoja, lakini pia ikawa vigumu kukubaliana nani abaki na mtoto. “Tulivutana sana. Baadae tukamua bora mtoto akae bweni. Sio kitu rahisi kwa mama asikwambie mtu. Nilipata shida sana kukubali mtoto wa miaka saba akakae bweni na utoto wote ule. Lakini nikwambie kitu? Sijutii. Ilikuwa afadhali awe kule kuliko kukaa nyumbani akishuhudia vituko vyetu.”


Migogoro ya wazazi huathiri mazingira ya malezi kwa watoto. Fikiri wazazi kufokeana kwa maneno makali mbele ya mtoto asiye na uwezo wa kuchambua anachokisikia. Aisha aliona bweni linaweza kumtenga mtoto na mazingira hayo.


Pia kuna hili la wazazi kukosa kabisa muda wa kulea. Jeff, baba wa watoto watatu, anafikiri bweni ni mahali salama zaidi kwa watoto wake. Msikilize, “Ukweli sina kabisa muda wa kukaa nyumbani. Kazi zinanibana vibaya sana. Mke wangu naye muda mwingi hayupo nyumbani. Nani anabaki nyumbani kuangalia usalama wa mtoto?”


Katika mazingira kama haya, wazazi wengi huchagua huduma ya malezi ya wasichana wa kazi. Hata hivyo, kuna visa vingi vya watoto kujifunza tabia zisizofaa. “Hawa wadada wanatufaa zaidi kwa kazi za ndani sio malezi. Nimeshawahi kukutana na vitu ambavyo nisingependa vijirudie.” Jeff haelezi zaidi lakini ni ukweli wa mambo kwamba wasichana hawa saa nyingine tunawapa kwenye mazingira ya kubahatisha. Hatujui wanatoka wapi na undani wa tabia zao hatuufahamu. Kuwaachia jukumu la malezi ni sawa na kucheza pata potea na maisha ya watoto wetu.


Hapa ndipo shule za msingi za bweni zinapoziba ombwe linaloachwa na wazazi wenye shughuli nyingi. Gharama kubwa wanayolipa wazazi wasiopatikana ni kuwapeleka mahali ambapo wengine watapatikana kwa ajili ya watoto wao. Ingawa hatuna tafiti rasmi, upo uhusiano wa moja kwa moja kati ya ongezeko kubwa la vitendo vya watoto kudhalilishwa kingono na ongezekano kubwa la wazazi kutokupatikana nyumbani.


Pamoja na shule za bweni kuziba ombwe, ni vyema tukikumbuka kuwa umri wa mwanzo wa maisha ya mwanadamu unadai ukaribu mkubwa wa mzazi kwa mtoto. Lengo ni kuwezesha uwekezaji wa kimalezi, kwa maana ya kumsaidia mtoto kujifunza moja kwa moja kwa mwalimu wake wa kwanza kabisa, ambaye ni mzazi. Tabia nyingi za maana tunajifunza kwa wazazi wetu. Tunajifunza kupitia utu na tabia zao kama wanadamu wanaotuzidi.


“Unajua nimewaza sana kama hiki unachokisema (kuwa mwalimu wa mtoto) ningekiweza,” ananiambia Aisha. “Nimejiuliza sana kama ninafaa kuwa mzazi anayeigwa na mwanae kupitia tabia zangu. Kuna wakati mwanangu alianza kujenga chuki na mimi. Ile kuona tunavyogombana na mwenzangu ilikuwa inamwuumiza. Kuna wakati pia nilikuwa nahamishia hasira zangu kwake. Sipendi awe bweni lakini si ni bora akutane na wengine wanaoweza kumsaidia?” 


Maneno mazito haya. Si wazazi wengi wanaweza kuwa na ujasiri wa kuyatamka wazi. Lakini tukiwa wakweli, saa nyingine, kule kulazimisha kuwa walimu kwa watoto wetu, kumewaharibia maisha yao.  Tumewatumia kama dodoki la kunyonya hasira na machungu yetu ya maisha. Tumewafundisha kuchukia, kulipa kisasi, kuumiza wengine na tabia nyingine zinazoweza kuwa mwiba kwa maisha yao ya baadae. Lakini, pamoja na faida zake, tuna hakika shule za bweni ni mahali salama kwa malezi? 


Niandikie: bwaya@learninginspire.co.tz 

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?