Malezi yanapokuwa ‘rasha rasha’ tuilaumu teknonojia?

PICHA: businessday.ng


Kama ambavyo imeanza kuwa vigumu wengi wetu kumaliza siku bila usaidizi wa zana za teknolojia, ndivyo malezi nayo yanavyoanza kuchukua uelekeo wa kuhitaji usaidizi wa teknolojia. Saa nyingine mzazi usingependa watoto waangalie katuni muda mrefu. Lakini unafanyaje sasa kama wewe mwenyewe hata unapokuwepo nyumbani huna mengi ya kufanya na watoto? Ombwe, kwa kawaida, huwa ni muhimu lizibwe.


Lakini pamoja na kusaidia kujaza ombwe la sisi wazazi kutokuwepo kwenye maisha ya watoto, bado teknolojia inayo mengi yenye manufaa. Kubwa zaidi ni kuwachangamsha watoto kiakili. 


Nitumie mfano wa mwanangu. Hajakamilisha miaka mitatu. Ukikaa naye anayo mengi ya kukusimulia. Uwezo tu wa kusimulia jambo na likaeleweka katika umri wa miaka miwili sikuuona kwa dada yake waliozidiana karibu muongo mzima.

Ingawa bado ni mapema mno kumpeleka darasani, anatambua herufi na tarakimu zote, ana uelewa wa awali wa kuhesabu, anafahamu majina ya rangi nyingi, anawafahamu majina na tabia za wanyama mbalimbali, anaelewa dhana kadha wa kadha ambazo kwa kawaida angetarajiwa ajifunzie shuleni.


Natambua ananufaika na uwepo wa wakubwa zake katika kumchangamsha kiakili. Tafiti zinaonesha kuwa mtoto anapotumia muda mwingi na wanzake wanaomzidi uelewa  anakuwa na nafasi nzuri zaidi ya kujifunza mengi kupitia michezo. Hata hivyo, nafahamu kajifunza mengi zaidi kupitia maudhui anayokutanishwa nayo na teknolojia.


Hapo ndipo ninapoona mantiki ya hoja ya Dk Mugisha. Kwa kizazi hiki, jitihada za kudhibiti taarifa zinazomfikia mtoto zinaweza zisizae matunda. Pengine changamoto kubwa tuliyonayo inaweza kuwa namna ya kumwelekeza mtoto wapi apate maudhui yanayomsaidia kujifunza.


Tunao uhaba mkubwa wa upatikanaji wa maudhui yanayoakisi mila na desturi katika lugha ya Kiswahili. Ubongo Kids, kwa kulitambua hilo, wamejitahidi kutengeneza maudhui yanayowawekea watoto mazingira rafiki ya kujifunza mahiri za kusoma, kuandika na kuhesabu lakini wakati huo huo wakijifunza stadi mbali mbali za maisha.


Safari, hata hivyo, bado ni ndefu. Hofu iliyopo kwa baadhi ya wazazi kuhusu athari za teknolojia ni muhimu ifanyiwe kazi. Tusiposhirikiana kuchukua hatua madhubuti, tunawaweka watoto wetu kwenye hatari ya kweli kweli si tu ya kukutana na maudhui yatakayochafua fahamu zao kimya kimya, bali pia tutakuwa tunalea aina mpya ya uraibu utakaogharimu maisha yao ya baadae. 


Tafiti nyingi, kwa mfano, zimeonesha kuwa teknolojia, pamoja na uzuri wake, inahusishwa na tatizo la watoto kukosa uzingativu, kukosa subira, kujifunza ubabe, ugomvi na kushindwa kushirikiana na wenzao.


Ili kukabiliana na changamoto hiyo ya uholela wa taarifa, nafasi ya mzazi katika kumwongoza mtoto namna bora ya kutumia mitandao haiwezi kukwepeka. Je, ni wazazi wangapi wanapatikana vya kutosha kufuatilia na kuratibu yale watoto wanayojifunza wenyewe? Hapa ndipo inapokuja mantiki ya msimamo wa Gwamaka.  Hatuwezi kukwepa haja ya dhati ya wazazi kufanya maamuzi magumu yanayolenga kuongeza uwajibikaji wetu katika malezi.


Hatuwezi wote kufanya kama alivyofanya Gwamaka na mke wake. Katika mazingira ya sasa, yanayodai vingi, hili la mmoja kubaki nyumbani linaweza lisiwe rahisi. Kuna mazingira, kwa mfano, wazazi wote wawili mnaweza kulazimika kupambana kutafuta riziki mbali na nyumbani. 


Hata hivyo, kwa kutazama changamoto iliyopo ya uholela na kuzagaa kwa taarifa, tunahitaji maamuzi yanayolenga kuyapa malezi kipaumbele katika mipango yetu ya maisha. Tunahitaji kutambua kuwa malezi ya watoto kuwa hayaahirishwi.


Tunapotumia muda mrefu kazini, jambo ambalo saa nyingine halikwepeki, tusiache kukumbuka kuwa tunaacha ombwe nyumbani. Tunaondoka asubuhi na mapema nyumbani na kurudi usiku, tusiache kukumbuka ombwe linaloweza kukaribisha mbadala wetu.


Tunaweza kuridhika kutoa maelekezo kwa dada wa kazi, “Dada uhakikishe watoto wamepata muda wa kulala. Uzime televisheni.” Saa nyingine dada huyu anayetegemewa kuchukua nafasi ya wazazi naye anasubiri wazazi muondoke atumie uhuru wake kuangalia chochote anachotaka.


Hapo ndipo huibuka hoja nyingine ngumu ya kuwapeleka watoto kwenye malezi ya mbali na nyumbani. Miaka michache iliyopita, mtu ukisikia shule za msingi za bweni, tulitafsiri kama uamuzi unaomnyanyasa mtoto. Lakini tukiwa wakweli, saa nyingine inaweza kuwa salama zaidi mtoto kuwa bweni kuliko kubaki nyumbani na hakuna anayefuatilia kujua anajifunza nini.

Niandikie: bwaya@learninginspire.co.tz



Maoni

  1. บริษัท slot pg จะเล่นเกมไหน ก็สนุกสนานสุดสนุก และรับเงินรางวัล PGSLOT ในเกมมาก สล็อตเว็บไซต์ตรง เปิดให้บริการ พร้อมเกมสล็อต ที่จะทำให้ท่าน รับเงินรางวัลมั่นใจ เกมใหม่พลาด

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Mambo ya Kuzingatia Unapoandika Wasifu wa Kazi (Curriculum Vitae)

Uislamu ulianza lini?

Tabia za Mtoto wa Miaka 0 – 3 Kimahusiano na Kihisia