Tumeiachia teknolojia itulelee watoto wetu?
Picha: reviewed.com |
Jijini Dodoma. Jioni ya
Jumatano. Kikombe cha kahawa kinanikutanisha na maswahiba Gwamaka na Dk Mugisha.
Tumezungumza mengi. Kisha mada inabadili uelekeo, “Unajua nikiangalia namna hawa
wadogo zetu wanavyoyachukulia mahusiano sipati picha itakuwaje kwa watoto wetu.”
Mada mpya ya malezi inachukua nafasi yake. Dk Mugisha anakiita kizazi hiki generation
X, kumaanisha kizazi kilichozaliwa kwenye teknolojia.
Kawaida, kila kizazi huona
kilikuwa afadhali kuliko kizazi kinachofuata. Hata wazazi wetu, kimsingi, walikuwa
na wasiwasi na sisi. Lakini ni ukweli pia kuwa mabadiliko makubwa ya
kiteknolojia tunayoyashuhudia hivi sasa yamebadili kabisa namna tunavyoishi na
kuchukulia mambo.
Gwamaka anaona huu urahisishwaji
wa kupata taarifa umeunda tatizo jipya tunalohitaji kulitazamwa. “Teknolojia imerahisisha
mno watu kuyatangaza maisha yao mitandaoni. Tunajilinganisha mno na kuyatazama
maisha kwa mizania ya vitu. Hili linaweza kuwasumbua sana vijana wanaochipukia
hivi sasa.”
Tafiti zinasemaje? Upo
uhusiano mkubwa kati ya utumiaji wa mitandao na ongezeko la maradhi ya sonona. Mitandao
ya kijamii, mathalani, inaongeza uwezekano wa watu kujilinganisha na watu ambao,
wakati mwingine, hawawafahamu. Maendeleo haya yanatengeneza changamoto mpya
kama anavyoeleza Gwamaka,
“Nafasi ya mzazi kuwa mtu pekee
anayesikika zaidi mwanzoni mwa maisha ya mtoto imeanza kupotea. Mtoto anakutana
mapema na watu wengi maarufu wanaomvutia na kuathiri mitazamo yake kuliko hata
mzazi wake.”
Hoja nzito hiyo inamfanya Dk
Mugisha aweke kikombe cha kahawa mezani. Kakumbuka jambo. “Juzi nilitaka kujua katuni
zinawafundisha nini watoto wangu. Nikawadadisi. Hutaamini. Ule uwezo wa
kuwachambua wale characters (wahusika) wa katuni ulinishangaza. Watoto walielezea
characters wanaowapenda na wasiowapenda na wakatoa sababu.”
Siku hizi si ajabu watoto wa miaka miwili kulilia simu za wazazi wao. Kwa vile saa nyingine tunaepuka ule ‘usumbufu’ wa kushiriki shughuli zao hatusiti kuwapa. Gwamaka, kwa upande wake, anaona ni muhimu kuanza kudhibiti taarifa zinazomfikia mtoto mapema akiwa bado mtoto. “Nimeweka televisheni nyumbani mwaka jana. Muda mrefu hawakuwa na cha kuangalia.” Tunacheka kwa mshangao kidogo.
Kwa siku za leo, familia za mijini kutokuwa na luninga si
jambo linaloweza kueleweka. Kwa nini Gwamaka alifikia uamuzi huo? “Najijua. Sina
huo muda wa kujua chaneli gani inawafaa watoto. Nikaona bora isiwepo. Huwa natamani
tungekuwa na chaneli halal
zinazowafaa watoto. Tungekuwa na watu wanaofanya kazi ya kuhakiki na kukusanya
vipindi vinavyowafaa watoto ili hata usipokuwepo nyumbani unakuwa na uhakika watoto
wanaangalia vitu sahihi.”
Utoto ndio msingi wa tabia
nyingi za ukubwani. Kuna vitu vikishaingia kwenye ufahamu wa mtoto inawezekana
ikawa kazi ngumu kuvitoa baadae. Mtoto hujifunza zaidi kwa kuiga kuliko
mafundisho ya maneno. Kwa msingi huo teknolojia inaweza kuwa nyenzo ya kuwarahisishia
watoto kuiga uangamifu wao.
Dk Mugisha, kwa upande
wake, anafikiri ni muhimu mtoto kujifunza mapema kuchagua kilicho sahihi. “Kwangu
watoto wana uhuru. Ninavyoona muhimu zaidi si kuwanyima taarifa bali kukuza
uwezo wao wa kuchambua maudhui wanayokutana nayo. Kwa nyakati zetu mtoto
asipopata ujuzi huu nyumbani akienda shule atapata tabu.”
Siku hizi mtoto wa miaka
mitatu tayari kavaa sare za shule na ana begi mgongoni. Mengi anayokutana nayo
kule yana nguvu ya kufuta chochote cha maana alichojifunza nyumbani. Sijui kama
wazazi wengi wanapofikiri mtoto aende shule gani huwa wanatazama zaidi ya
matokeo ya mitihani.
Gwamaka na mke wake walifanya
maamuzi magumu, “Unajua utoto ni umri wa kutengeneza operating system (mfumo wa
kufikiri). Mtoto anasoma shule gani hili
sio jambo la kuchukuliwa kirahisi. Sisi tunatofautiana na wazazi wengi wa
kisasa. Tuliamua malezi yawe kazi rasmi kwa mke wangu. Ilibidi yeye abaki
nyumbani tuwe na uhakika mmoja wetu yupo nyumbani kufuatilia kwa karibu ukuaji
wa watoto.”
Dk Mugisha anakuna kichwa. Haamini
anachosikia. Mke wa Gwamaka kasoma. Katunukiwa Shahada yake Mlimani. Kwa nini waliamua
abaki nyumbani? “Kwetu malezi sio kazi ya kumwachia dada wa kazi. Ofisi ya mke
wangu tuliamua iwe nyumbani. Shughuli zake haziwanyimi watoto haki ya kuwa na
mtu wa kumwiga.” Katika nyakati hizi za usawa wa kijinsi(a) hili la mmoja
kubaki nyumbani si jambo jepesi kufanyika. Tutaanzia hapa Jumapili.
Niandikie: bwaya@learninginspire.co.tz
Maoni
Chapisha Maoni