Mahusiano yenye ‘utulivu’ bila amani
Chanzo: stock.adobe.com |
Hivi umewahi kutaka kumwambia mtu jambo unaloona ni muhimu lakini ukakosa namna nzuri ya kumwambia?Unatamani ujumbe ufike lakini maneno sahihi ya kuubeba huna. Unafanyaje?
Wengine huamua kuacha. Kuliko kumwuumiza mwenzako, huona bora mtu uugulie maumivu ndani kwa ndani. Mwingine hajali. Huamua bora ‘kutema nyongo’ hivyo hivyo bila kujali maumivu yatakayoyasababishwa na ujumbe. Wanachosahau, matokeo yanayotokana na kujiumiza kwa kuuzuia ujumbe yanaweza kuwa sawa na madhara ya kuuachia ujumbe kiholela bila kujali maumivu ya atakayeupokea.
Mawasiliano ni sayansi yenye nafasi nyeti katika mahusiano. Ukikosea kanuni, mawasiliano yana nguvu ya kuleta uharibifu mkubwa unaoweza kugharimu afya ya mahusiano. Mawasiliano ni sanaa pia. Namna unavyosema jambo ni muhimu wakati mwingine kuliko hata ujumbe wenyewe. Ukishindwa kuchagua maneno sahihi na mazingira sahihi ya kusema jambo unaweza kufubaza uzito wa ujumbe wako. Thamani ya unachokisema inabebwa pia na namna unavyochagua kukisema.
Fikiria mazingira
ambayo mke anatamani mumewe afahamu mahitaji yake fulani fulani lakini hawezi
kusema waziwazi. Saa nyingine sijui ni namna tulivyolelewa? Huenda. Kueleza
hisia zetu waziwazi kwa wazazi wetu kulituingiza matatizoni. Tukajifunza kumbe
usalama ni kuwaachia wengine kazi ya kujua tunachokihitaji. Ukubwani matokeo
yake ndio haya sasa. Mke anamlaumu mumewe kimya kimya kwa kutokufanya kitu
ambacho hata hivyo hakumwambia. Kwa nini mke hasemi anachokitaka? Anaamini, “Sitakiwi
kujieleza. Mwanaume anayenipenda lazima ajue mahitaji yangu bila kumwambia!” Hatukufundishwa
mawasiliano nyumbani.
Ukichunguza migororo
mingi ya ndoa hukosi kuona namna inavyochipukia kwenye mzizi mnene wa uwezo hafifu
wa wapenzi wawili kuwasiliana. Hatujui sayansi ya mawasiliano katika ngazi zake mbili. Kwanza,
ni namna ya kufikisha ujumbe kwa anayekusudiwa. Hili ni gumu kweli. Ugumu wake
ni hofu ya uwezekano wa kumwuumiza mlengwa. Mifano unayo. Sivyo? Una kitu unataka
kusema lakini unaogopa matokeo yake. Unaogopa namna kitakavyopokelewa. Mazingira magumu kweli. Kama ulilelewa kujali hisia za
wengine unaamua bora kunyamaza. Lakini kadri unavyoshindwa kuusemea moyo ndivyo
unavyozidi kuwa mpweke na kulimbikiza matatizo yasiyotatuliwa.
Lakini pia wapo
wanaojali ujumbe kuliko anayeupokea ujumbe husika. Hawajali utajisikiaje. Ukitema ukimeza shauri yako. Muhimu kwake kasema.
Ujumbe unakuumiza hajali. Kwa nini inakuwa hivi? Tunarudi kule kule. Malezi. Mtu
aliyelelewa kwenye mazingira yasiyojali hisia zake, huwa hapati shida kuumiza
hisia za mtu. Nafsi nyingi zimeumizwa kwa tabia hii ya kutokujali hisia za
anayeupokea ujumbe huo. Hiyo ndio ngazi ya kwanza ya mawasiliano.
Ngazi ya pili inamhusu
anayefikishiwa ujumbe. Mwenzako akikuambia
jambo unalichukuliaje? Sasa hapa pia kuna mengi. Mwingine utamwambia jambo na ataishia
kulidogosha, kulipuuza, au basi tu kukuhukumu. Bila shaka una uzoefu na kauli
kama hizi, “Usijisikie vibaya bwana. Usiogope bwana. Hili jambo dogo sana!” Mtu
unajiuliza, “Mwenzio tayari najisikia vibaya. Unaposema nisijisikie vibaya una
maana gani?” Kumbe badala ya kumwelekeza mwenzio namna ya kujisikia, ungeanza
na kuelewa hisia zake pengine ungemsaidia.
Hapa pia hatukwepi
athari za malezi. Wengine wetu tumelelewa kuamini kwamba hasira, hofu,
wasiwasi, hatia hizi ni hisia mbaya na hivyo hatutakiwi kuwa nazo. Tulikemewa
na kuchapwa kwa kuonesha hisia hizi. Ukubwani tunajipa kazi ya kuhakiki hisia
za watu badala ya kujitahidi kuzielewa. Mzizi mwingine wa migogoro.
Mke, mathalani, anajisikia
mpweke mume wake anapokuwa nje usiku. Kusema hisia zake kunatafsiriwa kama kulalamika.
“Kwa nini ujisikie mpweke na unajua ninachokifanya ni kwa faida yako?” Kuambiwa
hivi, mke naye ananyong’onyea, “Najisikia upweke kweli. Kwa nini hutaki
kunielewa?” Mume anafura, “Nikuelewe nini? Kwani hujui ninachofanya huku
niliko?”
Haya mazoea ya
kuwanyima watu kusema vile wanavyojisikia ni sehemu ya tatizo katika mahusiano.
Badala ya kuzipokea hisia za mtu vile zilivyo, tunakuwa wepesi kuzichambua na
kuonesha kuwa hazina mashiko. Tunapofanya hivi, saa nyingine bila kujua, yule
mwenye hisia hizo anajisikia kutokueleweka. Unapojisikia kutokueleweka, mara ya
kwanza, mara ya pili, mara ya tatu, unaanza kusita kusema hisia zako. Unagundua
kumbe hata ukisema ni kazi bure. Kusema ni kujisumbua na utaishia kuzodolewa. Ufumbuzi
ni kujijengea handaki lako. Unatulia.
Mazingira haya ya
watu kuamua kutulia hutengeneza utulivu usio na amani. Watu hawagombani lakini mioyo
yao imevurugika. Hawawezi kuongea, hawawezi kuusemea moyo, kwa sababu jaribio
lolote la kuzungumza litawasha moto. Nani anataka moto? Bora kunyamaza. Mkifikia
hapo, sasa sisi washunuzi letu kwenu huwa ni neno moja tu. Tafuteni msaada wa
namna ya kuwasiliana kwa utulivu.
Niandikie: bwaya@learninginspire.co.tz
win9999 คาสิโนออนไลน์ โด่งดังที่ได้รับการยินยอมรับและก็โด่งดังเป็นเว็บไซต์ pg slot ที่ไม่ผ่านเอเย่นต์ มีระบบระเบียบการดูแลรักษาความปลอดภัยและก็ระบบการทำงานอย่างมือโปรของเรา
JibuFutaทาง เข้า pg soft ออนไลน์ สำรวจโลกของความบันเทิงออนไลน์ที่น่าตื่นเต้นกับ เปิดเผยเกมแพลตฟอร์มนี้อย่างละเอียดและเป็นเอกลักษณ์ PG ค้นพบแนวทางที่ครอบคลุมทุกสิ่งที่คุณต้องรู้เกี่ยวกับเว็บไซต์
JibuFuta