Unafanyaje kutathmini mabadiliko yako?

Picha: Mpiga picha simkumbuki. Mwaka ni 2004.

Tunabadilika jamani. Sijui nyie wenzangu. Labda ni mimi peke yangu lakini saa nyingine ni vigumu kujiona tunavyobadilika. Usipopata mrejesho kutoka kwa watu unaweza kufikiri uko vile vile. Lakini ukweli ni kwamba tunabadilika.


Tuanze na maumbile ya mwili. Mwili ukibadilika ni rahisi kuona. Hukuwa na kitambi, kwa mfano, sasa unacho. Tumbo nalo huwa halina-ga adabu. Badiliko lake linakuja taratibu sana. Halichomozi kwa siku moja. Unaweza ukawa unakula bila mpango, huoni ukibadilika. Unachukulia kawaida. Kuja kustuka, aloo kulitoa inakuwa shughuli. Ukiacha tumbo, kwangu kuna hili la macho. Ilinichukua muda mrefu kukubali kuwa sioni mbali. Nilikuwa nalazimika kufinya macho. Naona kawaida. Baadae sikuwa na namna. Ikabidi kukubali kuvaa miwani. Ushahidi mwingine huo. Mabadiliko hayana-ga haraka. Huja taratibu sana.


Kingine mavazi. Tazama picha inayoambatana na maandishi haya. Hapo ni miaka 18 imepita. Huyo mwenye tai ni mimi. Sijui nini kilitokea hapo katikati nikaachana kabisa na tai. Halafu hata sikuacha ghafla. Ilianza kidogo kidogo. Siku hizi ohooo navaa hadi fulana na suruali zisizohitaji ushirikiano na pasi. Nini kimefanya nikaacha kuvaa tai na ninaridhika na suruali zisizohitaji kunyooka? Hapo sasa ndo' tunakuja kwenye badiliko ya kitabia.


Tabia ngumu kidogo kuiona. Naamanisha haionekani. Tuseme tabia haionekani na ndio maana hata ukibadilika hugundui kirahisi. Unaamka, unaenda kwenye shughuli zako, unakutana na watu, unarudi nyumbani, unalala. Siku imeisha. Halafu huoni unavyobadilika. Miaka inaenda, miaka inarudi, unadhani uko vile vile lakini ukweli ni kwamba mitazamo yako, fikra zako, maoni yako, tabia na maamuzi yako vyote hivyo vinabadilika.


Sijui wewe huwa unatathmini vipi mabadiliko yako ya kitabia. Lakini mimi huwa natazama aina ya marafiki ninaokuwa nao kwa kila hatua ya maisha yangu. Kundi la kwanza ni wale wasiobadilika. Hawa kadri unavyokua wapo. Hawapotezi. Mara nyingi huwakilisha sehemu ya maisha yetu isiyobadilika. Ninao kadhaa. Sio wengi. Kundi la pili, ni wale wapya wanaochukua nafasi ya wale ninaopotezana nao kwa sababu mbalimbali.

Fuatilia. Marafiki wanasema mengi kuhusu tabia zetu. Unajua huwezi tu kuambatana na mtu ikiwa hakuna kinachowaunganisha. Ukichunguza vizuri aina ya watu ulionao karibu utafahamu umebadilika kuelekea kushoto au kulia.

Lakini pia, mimi hutathmini aina ya matukio niliyowahi kukutana nayo. Kuna nyakati za machozi. Hizi huwa hazituacha-gi tulivyo. Mie sitosahau miaka miwili migumu. Mwaka 2015. Halafu kuna 2019. Miaka hii ni ilinibadilisha mno na nikaona bayana. Lakini pia kuna nyakati zinazotupa furaha. Ninazo nyakazi hizi na ninaweza kukumbuka namna zilivyonibadilisha. Kumbe yale tunayoyapitia yana mchango wa kutuumba kuwa vile tulivyo.

Tathmini ya matukio yaliyowahi kunikuta huwa naifanya kupitia shajara (diary). Mara kadhaa huwa nasoma shajara za miaka iliyopita na kutafakari niliyoyaandika. Ninaposoma, kuna wakati najicheka, najipongeza, najihurumia na kujitia moyo. Lakini pia kuna barua nilizokuwa naandikiana na rafiki zangu na kadhalika. Ninaposoma miandiko hiyo ya zamani, kwangu inakuwa rahisi kuona namna mitazamo yangu kuhusu maisha inayobadilika.

Kingine, nadhani, ni aina ya watu wa kukupa mrejesho. Sio kila mrejesho una nia njema. Si ndio? Wengine ni ile miluzi mingi. Ukiwasikiliza sana utapotea. Unsha'nfahamu? Lakini kuna watu wakikuambia kitu unakiamini. Hata wewe unao. Unawakumbuka? Muhimu sana kuwa na watu katika maisha yako unaowaruhusu kukupa mrejesho wa namna unavyobadilika kitabia.

Huyu niliyepiga naye picha, amebaki kuwa mmoja wa watu muhimu wanaonipa mrejesho wa kuaminika kuhusu mabadiliko yangu. Tathmini yake huwa naichukulia kwa uzito unaosahili. Najua anachokisema kina nia njema hata kama kinauma. Nimejifunza kumsikiliza.


Wakati huu picha hii inapigwa, mwaka 2004, ungeniuliza miaka 18 ijayo ninatarajia kuwa nani, nikifanya nini, nikiwa wapi, ukweli nisingepatia hata kwa asimilia 10. Wazungu wanasema, I had no idea. Namshukuru sana Mungu kwa vile anavyojua kesho zetu vizuri zaidi kuliko sisi. Kuna vingi hatujui kuhusu maisha yetu. Hatari sana kukaa mbali na Yeye ajuaye vizuri kesho zetu. Unshan'fahamu? Sawa sawa? (Unakumbuka zile sawa sawa za Maalim Seif?) Basi. Usisahau kutathimini mabadiliko yako.

Niandikie: bwaya@learninginspire.co.tz

Maoni

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Haiba ni nini?

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3

Uislamu ulianza lini?