Unajua kugombana bila kufukua makaburi?
Picha: pixabay |
“Msitumie vibaya elimu zenu bwana,” Godi anaanzisha sogo kijiweni. Unamkumbuka? Kaona kukaa haitoshi. Kasimama kabisa. Mikono inapepea hewani kusisitiza hoja, “Haya mambo yameanza leo? Ndoa zilikuwepo tangu enzi na enzi na hapakuwa na shida. Sasa nyie leo mnasema eti sisi wanaume ndio hatujui mahitaji ya wanawake? Mbona wazee wetu hawakujua hayo yote na bado ndoa zilidumu.”
Siku hizi ukitaka kuwachokoza wanaume
ongelea matukio ya wanawake kunyanyasika. Salu kakaa pembeni anausoma mchezo.
Tabasamu lake linaunga mkono hoja.
Hata hivyo, naona naye uvumilivu
umemshinda. Kaamua kuulinda uanamue, “Hizi harakati zenu za kuwabeba wanawake
zitatuharibia ndoa. Mie nawaambieni. Mnawatetea sana wanawake na watapata
vichwa kweli. Wakitushinda tuwaleteeni basi.” Joto limepanda. Hisia hizi za akina Salu si za
kupuuza. Mgogoro unapotokea kwenye ndoa, anayebebeshwa mzigo wa kutokufanya
wajibu wake, mara nyingi, ni mwanamke. Msikilize Peki anavyogongea muhuri dhana hiyo:
“Biblia imeshaeleza wazi. Enyi
wanawake watiini waume zenu. Hakuna kisichoeleweka hapo. Ukishakosekana
utii hakuna muujiza. Tena kuna mahali imesema mwanamke mpumbavu hubomoa ndoa
yake kwa mikono yake mwenyewe. Sasa nyie ndio mnataka ionekane upumbavu wote ni
wa mwanaume.”
Peki amesimika mtazamo wake kwenye
imani. Tunamchokoza aseme anavyoelewa kifungu cha wajibu wa mume kumpenda mke
wake. “Kwani yeye hajui nampenda? Niache hela nyumbani, nilipe bili zote na
bado aseme simpendi? Tusichoshane bwana!”
Tunamwuuliza Peki ikiwa yale mapenzi ya uchumba bado anayo. Peki anashusha jazba kidogo. Dalili kuwa kakumbuka alivyobadilika. Enzi hizo anaanzisha uhusiano na dada aliyekuja kuwa mke wake asingeyasema hayo anayoyasema. Simu hazikuwa zinakatika kirahisi. Mitoko sana. Kwa kifupi, muda wote alipambana kiume kuonekana anajua mapenzi. Nini kimebadilika baada ya ndoa?
“Saa nyingine ni kwa vile ukishakuwa
na mtu ndani unamzoea na unaanza kumchukulia poa,” Peki anajibu kinyonge. Majid
anafafanua zaidi mabadiliko hayo, “Ni kwa vile tu hawa wanawake hawajisumbuagi
kuelewa hali halisi. Ukishaoa kuna kuongezeka kwa majukumu. Fahari kubwa ya
mwanaume inakuwa kuona familia haidhaliliki. Mwanaume wa ukweli anaelekeza
nguvu kupambana kuweka chakula mezani. Sasa unategemea nini mambo yakiwa mengi
hivyo?”
Godi kachangamka sasa. Majid kausemea
moyo wake. Hajali anatafuna nyama. Maneno yanamponyoka, “Huo sasa ndio ukweli kabisa. Sasa mbona
hamuwaambii wake zetu waelewe? Mtu unapambana kutwa nzima na kazi unapata wapi
muda wa zile meseji za uchumba? Usipofanya hivyo wanaanza kusema unachepuka.
Tuteteeni.” Kijiwe kinapooza kidogo. “Haya mabadiliko yanayoendana na umri
yakieleweka vizuri migogoro itapungua.”Agenda imeungwa mkono.
“Lakini tusisahau. Hata mwanamke
akielewa una majukumu mengi, hiyo haimfanyi asahau yale mahitaji yake ya kike. Njaa
ya mwanamke kupendwa haiishi.”
“Hapo sasa nakubaliana na wewe. Hata
ukijua huna ‘afu tatu mfukoni, bado njaa itauma. Njaa na kinachoendelea mfukoni
havina uhusiano,” Peki analegeza msimamo na kuendelea, “Ujue hawa wake zetu nao
saa nyingine ni kama watoto. Ukiacha kumdekeza dekeza basi anasahau mazuri yote
unayoyafanya.”
“Kingine labda tujifunze kuwasiliana,”
sehemu ya pili ya hoja inaanza. “Unaongeaje unapokuwa na hasira? Usiruhusu
mazungumzo na mke wako ukiwa umekasirika. Hasira haina hekima. Ukikasirika
unakuwa mbinafsi. Unajifikiria mwenyewe tu. Ukiona umekasirika, nyamaza. Huwezi
kunyamaza ondoka.”
“Hiyo ngumu. Mimi huwa nikikasirika
raha yangu ni kuongea ili uumie. Nikishaona umeumia natulia.” Tunacheka wote.
Majid amekuwa mkweli. “Ukishafahamu hasira hukuchochea umwuumize mtu,
unajifunza namna ya kumudu hasira zako.”
Hii kitu ilikuwa inanisumbua sana
mwanzoni. Nikishakasirika ni kushambulia tu. Hasira ikiisha ninakuja kujuta
nilichokisema. Niliharibu sana familia yangu kwa kulopoka maneno makali. Lakini
baada nilitafuta msaada. Siku hizi angalau najua namna ya kugombana.
“Kwanza ninaelezea hisia zangu zaidi.
Badala ya kumwekea mwenzangu maneno mdomoni mwake, ninaelezea namna jambo lilivyoniumiza
mimi. Najielekeza kujisemea mimi na sio kushambulia.”
Lakini pia situmii maneno makali yanayoonesha kuwa aliyekosea hiyo ndio tabia yake. Maneno kama, ‘ndio tabia yako,’ ‘nakufahamu wewe’, ‘hii sio mara ya kwanza, ‘huniheshimu,’ huwa yanachochea huyo unayetaka akuelewe naye ajihami kwa kujibu mashambulizi. Hamuwezi kufika mwisho. Nimejifunza kutumia lugha inayoelezea kile tu kilichotugombanisha. Sifukui makaburi hata kama ningetamani niyafukue yanisaidie kujibu mapigo.
“Kweli
hatuachi kujifunza. Hivi kumbe sikuwa najua kugombana?” Peki anachomekea. Wote
tunaangua kicheko. Majid kapaliwa. Hajui kucheka akiwa kagida.
Niandikie: bwaya@learninginspire.co.tz
Maoni
Chapisha Maoni