Namna Shule za Msingi za Bweni Zinavyoathiri Tabia za Watoto -3
KATIKA
makala yaliyopita, tumeona kuwa shule za msingi za bweni zinachangia kuwanyima
watoto fursa ya kujifunza ujuzi wa kujitegemea. Uwezo hafifu wa kujifunza stadi
za maisha, kwa kiasi kikubwa, unachangiwa na matarajio makubwa ya kitaaluma
waliyonayo wazazi kwa watoto wao.
Wamiliki
na waendeshaji wa shule za bweni, kimsingi, wanaitikia wito wa wazazi wanaotarajia
watoto wao kujifunza maarifa ya shule zaidi hata ikibidi kwa gharama ya kudumaza
maeneo mengine muhimu ya kimakuzi.
Katika
makala haya, tunaangazia mifano michache ya namna shule hizi za bweni
zinazovyochangia kuwaathiri watoto kitabia. Mifano hii inatokana na ulinganisho
wa tabia za watoto wanaosoma shule za bweni na wale wanaorudi nyumbani kila
siku.
PICHA: pinterest.com |
Tabia zilizolinganishwa
Watoto
walilinganishwa kwa tabia kadhaa chanya na tabia hasi zilizochaguliwa. Tabia
chanya ni zile tabia zinazomfanya mtoto ajichukulie vyema yeye mwenyewe na
hivyo kuwachukulia wengine vizuri. Mfano ni kucheza na kushirikiana na wenzake,
namna anavyoweza kufuata maagizo anayopewa na watu wazima, anavyojiamini,
anavyoheshimu watu wazima na kuwapenda watoto wenzake.
Tabia
hasi ni zile zinazotokana na mtoto kujisikia vibaya kihisia na hivyo kushindwa
kuishi vizuri na watu wengine wanaomzunguka ikiwa ni pamoja na ndugu aliowaacha
nyumbani.
Mfano wa
tabia hizi ni hisia za upweke na kutegwa na watu wake wa karibu; kuwa na aibu
na woga wa kufanya mambo; tabia ya kupenda kudeka, hasira zisizo na maelezo;
udokozi wa vitu visivyo vyake; kuonekana anakosa amani na kulia lia bila kuwa
na sababu za msingi.
Tabia za watoto wa
bweni
Watoto wa
bweni, kwa kiasi kikubwa, walionekana kuwa na changamoto nyingi za kitabia
kuliko wenzako wanaoishi nyumbani. Ingawa kwa haraka haraka watoto hawa
walionekana kuwa wachangamfu zaidi kuliko wenzao wanaoishi nyumbani, uchunguzi
wa kila ulionesha kuwa walikuwa wamejenga tabia hatarishi kuliko wenzao. Kwa
mfano, wengi wao, hasa wa darasa la kwanza, walikuwa wapweke na walikuwa na
tabia ya kuwadekea walezi wao.
Tabia hii
inaweza kuelezwa kama matokeo ya kukaa mbali na familia zao kwa muda mrefu,
hali inayoweza kutafasiriwa na mtoto kama kutelekezwa. Mathalani, watoto hawa
walionekana kujenga imani kwa watu wengine zaidi kuliko wazazi au ndugu zao.
Wenzao walioishi nyumbani, walionekana kuwa na imani na mzazi au ndugu wa
karibu kuliko mtu mwingine yeyote akiwemo mwalimu.
Kadhalika,
watoto wa bweni walionekana kuwa na tabia ya kuwa na hasira zisizo na maelezo
ya msingi. Kwa mfano, mtoto wa bweni angeweza kukorofishana na mwenzake kwa jambo dogo kuliko mwenzake anayeishi
nyumbani.
Changamoto za kimalezi
Changamoto za kimalezi
Tofauti
hiyo ya kitabia kati ya watoto wa bweni na wale wa kutwa inaonekana kuchangiwa,
kwa kiasi kikubwa, na aina ya malezi yaliyopatikana katika mazingira hayo ya
bweni yanayomwathiri mtoto kwa namna kadhaa.
Mosi, mtoto
wa bweni anakosa mtu wa karibu anayeweza kumsikiliza kibinafsi na kujua ana
shida gani, ana wasiwasi na matarajio yapi na mambo mengine binafsi. Ukaribu
huu kati ya mlezi na mtoto unakosekana katika mazingira ya bweni kutokana na
idadi kubwa ya watoto wanaoangaliwa na walezi wasiokidhi mahitaji halisi.
Kwa
kawaida, mtoto mdogo anahitaji kujenga ukaribu na watu anaowaamini. Anahitaji
mtu mzima anayeweza kuwa tayari kusikiliza mashtaka yake, matumaini yake na
hata masimulizi ya fahari za mambo mema anayoyafanya mchana kutwa. Mtu wa namna
hii anapokosekana mtoto hujikuta katika hali ya upweke na kupungukiwa.
Katika
shule kadhaa zilizotembelewa, kwa mfano, mlezi mmoja aliwaangalia watoto zaidi
ya 100 kwa wakati mmoja. Katika mazingira haya, ni vigumu kwa mtoto mmoja moja
kupata mtu anayeweza kumsikiliza na kutatua changamoto anazokabiliana nazo
kibinafsi.
Watoto
walilelewa kimakundi na mahitaji yao yalifikiriwa kiujumla jumla kwa kuongozwa
na utaratibu rasmi. Mathalani, walezi walihakikisha mtoto anapata chakula,
anakuwa msafi, analala mahali salama. Hata hivyo, walikiri hawakuwa na uwezo wa
kumsikiliza mtoto mmoja mmoja. Muda huo haukuwepo.
Upweke wa kihisia
Aidha, katika
mazungumzo na watoto, ilikuwa bayana kuwa wengi wao hawakupata nafasi ya
kuonana na wazazi wazo kwa zaidi ya miezi mitatu. Wazazi, pengine kwa sababu za
msingi kabisa, waliwatuma watu wengine kwenda kuwaona watoto kwa niaba yao.
Watoto
walijikuta kihisia wakiishi mbali na watu wazima. Walimu walijali taaluma.
Walezi walijali usalama wao kimwili. Wazazi nao walijali kusikia wanaendelea
vizuri. Watoto hawa walioishi katika mazingira ya kutengwa kihisia waliamua
kutengeneza uhusiano wa kubahatisha na watoto wa umri wao.
Haikuwa
ajabu, katika muktadha huu, kusikia watoto wengi wakijifunza tabia zinazowazidi
umri. Hawakuwa na mtu mzima wa karibu kutathmini yale wanayojifunza wakiwa na
wenzao ambao kimsingi wanafanana nao kiakili.
Unafuu wa mazingira ya nyumbani
Ukilingalisha
na watoto wanaoishi nyumbani, tofauti i dhahiri. Mtoto wa nyumbani anaweza
asipate fursa ya kukaa na mzazi wake kwa ukaribu. Lakini angalau yeye anakutana
naye mara kwa mara hata kama si kwa ukaribu anaouhitaji.
Inawezekana
mzazi kwa sababu yoyote ile hapatikani vya kutosha nyumbani, lakini kuna namna mtoto
anaweza kuwasiliana naye. Sambamba na hilo, mtoto anayeishi nyumbani anaweza pia
kuonana na ndugu zake karibu kila siku. Ndugu hawa wa karibu wanakuwa na fursa
ya kujua mwenendo wake na hata kuchukua hatua fulani mapema. Mtoto wa bweni
hana fursa hii.
Inaendelea
Maoni
Chapisha Maoni