Unavyoweza Kukuza Tabia Njema kwa Mwanao -2

Mama Neema anarudi nyumbani jioni. Neema anaposikia mlio wa gari ya mama yake, anatoka nje kwa furaha. Mara moja anamrukia mama  kumpokea kwa bashasha. Mama amechoka. Amekuwa na siku ndefu kazini. Haonekani kuwa mchangamfu.

Neema anauliza maswali mengi kwa mama yake. Hajibiwi. Hata pale anapojibiwa, mama haonekani kuwa na uzingativu. Ili apate nafasi ya kumpumzika, mama anamwelekeza Neema kwenda kufanya kazi za shule alizokuja nazo nyumbani. Neema anavunjika moyo lakini analazimika kuondoka.

Baada ya muda mfupi, wageni wanaingia. Ni rafiki zake mama Neema. Ingawa amechoka, analazimika kuwachangamkia. Mazungumzo ya mama na wageni yanapambwa na vicheko, utani na uchangamfu.

Mama anamwita Neema awaletee wageni vinywaji. Neema yuko mezani. Anajifanya hasikii. Mama anaita kwa mara nyingine, Neema anakuja bila kuitika. Hasalimii wageni na haonekani kujali. Mama anajisikia kudhalilika. Anavumilia kwa heshima ya wageni.

Wageni wanapoondoka, mama anamrudia Neema kwa hasira. Anamkemea kwa kuonesha utovu wa nidhamu tena mbele ya wageni wake muhimu. Neema hajibu chochote. Mama anaamua kumchapa. Neema anakwenda kulala akilia.




Kuelewa msukumo nyuma ya tabia

Wazazi wanaweza kuelewa kisa hiki vizuri zaidi. Mara nyingi watoto huonyesha utovu wa nidhamu kama alivyofanya Neema. Hatufurahii tabia kama hizi na hivyo tunalazimika kuwaadhibu.

Hata hivyo, wakati mwingine tunawaadhibu pasipokujua kwa nini wamekosa adabu. Badala ya kuuelewa msukumo ulio nyuma ya tabia tunayopambana nayo, tunakuwa wepesi kutumia nguvu kutoa adhabu. Lengo la kutoa adhabu ni kumsaidia mtoto kujifunza tabia njema.

Tunafanya kama tulivyolelewa sisi. Tulikemewa tulipokosea. Tulichapwa tulipoonesha tabia zisizofaa. Ingawa tunaweza kuwa wazazi wasio wakweli, lakini tunaamini tulisaidiwa kuwa na tabia njema. Tunaweza kuwa wagomvi na watu tusiokubali mawazo tofauti lakini bado tunaamini tulivyo, ndivyo tulivyopaswa kuwa. Kwa msingi huo tunaendeleza mbinu zile zile zilizotumika kutufanya tuwe kama vile tulivyo tukiamini zilikuwa sahihi. Tunatumia nguvu kama zilizotumika kwetu.

Kuelewa anachohitaji mtoto

Kila mtoto anatamani kuwa karibu na mzazi wake. Kuwa karibu kunampa mtoto utulivu. Anajisikia kuwa mtu wa thamani anapokuwa karibu na mzazi. Ukaribu huo unapokosekana kwa sababu yoyote, mtoto anajisikia kupungukiwa na kitu muhimu.

Ni sawa na Neema. Mama yake aliposhindwa kumchangamkia, Neema akajisikia kupungukiwa. Hakuwa na uwezo wa kuvumilia umbali huo aliouhisi. Ili kurejesha kile anachoona kinachopungua, hakuitika mama alipomwita. Kwa ufahamu wake, kunyamaza kungemstua mama kuchukua hatua za kurejesha ukaribu. Haikuwa kama alivyotarajia.

Wakati mwingine, mtoto hukosa adabu kwa sababu tu anajisikia hawezi kufanya anachotamani. Mazingira yanapomfanya aamini hawezi, ndani yake kunajengeka msukumo wa kujaribu kuthibitisha kuwa bado anaweza.

Kuelewa tafsiri za mtoto

Mtoto ana uwezo mdogo wa kuelewa na kutafsiri mambo. Namna mtoto anavyotafsiri mambo, sivyo sisi watu wazima tunavyofanya. Kufikiri mtoto anaweza kuona mambo kama vile tunavyoyaona sisi, si sahihi. Hiyo, hata hivyo, haimaanishi tupuuze hisia za mtoto. Hasha. Tunapopuuza hisia hizo hata kama ni potofu tunakuza tabia zisizofaa.

Mama yake na Neema, kwa mfano, hakusumbuka kuelewa tafsiri za Neema. Hakuwa na habari kuwa Neema anajaribu kuelewa kwa nini mama hajanichangamkia lakini wageni walipokuja aliwachangamkia. Mama Neema hakufikiri mambo madogo namna hiyo.

Lakini kwa mtoto, kama Neema, hilo ni suala kubwa. Akili yake haifikirii kwa mantiki anayoitumia mama. Muda wote ufahamu wa mtoto hufanya kazi ya kutafsiri, kutengeneza hisia, kuamua na hatimaye kufanya kitu kinachokwenda sambamba na tafsiri potovu aliyoitengeneza, hisia potovu alizonazo, na maamuzi potovu aliyoyafanya. Hayo yote kwa pamoja ndiyo yanayochochea utovu wa nidhamu.

Neema hakuamua kunyamaza kwa makusudi. Alipompokea mama yake, alikuwa na matarajio fulani. Alitegemea mama yake angemchangamkia. Labda angembeba, angembusu na kumkumbatia. Mama hakufanya hivyo. Kwamba hajafanya hivyo, haimaanishi mama hampendi Neema. Hapana. Moyoni mwa mama, Neema ni mtu wa thamani hata kama hajambeba, hajambusu, hajamwambia anampenda na hajamkumbatia.

Lakini kwa Neema, ‘Kama hujafanya lolote kati ya hayo, hunijali!’ Hii ni tafsiri potofu inayojengwa na akili za kitoto. Wageni walipoingia, mama alilazimika kuchangamka. Neema anachunguza, ‘Kwa nini mama amekuwa mchangamfu wageni walipoingia?’ Anajisikia vibaya moyoni. ‘Mama hanijali. Haoni thamani yangu kama mwanae.’ Hizo ni hisia potofu zinazotokana na tafsiri potovu.

Hisia hizi zinamfanya Neema afanye maamuzi. ‘Nitamwuumiza kidogo na yeye.’ Hiki ni kisasi. Mama yake anapomwita, Neema anafanya kama alivyoamua. Ananyamaza. Mama yake hajaweza kutafsiri kwa nini Neema anafanya hayo anayoyafanya.

Ndivyo tunavyofanya wazazi wengi. Tunatazama utovu wa nidhamu unaofanywa na watoto kirahisi. Mtoto anapokunyamazia kama alivyofanya Neema basi unachukulia kuwa hiko ni kiburi, dharau, kuharibika, mapepo na majina mengine mabaya. Kwa kuwa hatupendi tabia hizi, tunakasirika na kutumia nguvu kupambana nazo. Ndivyo alivyofanya mama Neema.

Tunavyorekebisha tafsiri potofu

Jambo la kuelewa, hata hivyo, ni kuwa unaposhughulikia upotovu huu unaouona kwa mtoto kwa kutumia mbinu za kibabe unakuza tatizo badala ya kulitatua kama tutakavyoona mbeleni. Adhabu inaweza kuwa suluhu ya muda mfupi lakini isisaidie kujenga uhusiano mzuri kati ya mzazi na mtoto.

Kwa mfano, baada ya Neema kuchapwa, kesho yake inawezekana hakumsalimia mama na pengine alienda shule bila kuaga. Hafanyi hivyo kwa bahati mbaya. Anatumia njia potofu kutuma ujumbe uliojaa moyoni mwake, ‘Mama hunipendi. Hunijali!’ Hana ujasiri wa kusema maneno hayo. Anatumia lugha ya ishara kufikisha ujumbe kwa mzazi wake.

Nafasi yako kama mzazi ni kufanya juhudi za kuelewa ujumbe huu unaobebwa na tafsiri, hisia na maamuzi potovu anayoyafanya mtoto. Unapoweza kuelewa ujumbe huu, unaweza kurekebisha tafsiri, hisia na maamuzi ya mtoto. Ukifanya hivyo, mtoto hatajisikia kupuuzwa, kutokuthaminiwa, kutokupendwa na hatimaye atakuwa tayari kukupa ushirikiano unaoutaka.



ITAENDELEA

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?

Pay $900? I quit blogging