Unavyoweza Kukuza Tabia Njema kwa Mwanao -3

TUMEKWISHA kuona kuwa mtoto hakosi adabu kwa bahati mbaya. Kila anachokifanya kina malengo yaliyojificha. Malengo haya, kama tulivyoona, mara nyingi hayako sahihi. Ni mbinu tu za kutafuta ukaribu na mzazi ambazo kimsingi zimejengwa kwenye tafsiri isiyosahihi.

Makala haya yanaangazia malengo mawili kati ya manne yanayowafanya watoto waonyeshe utovu wa nidhamu. Kadhalika, tunaangalia namna tunavyoweza kuuelewa ujumbe uliofichwa kwenye malengo hayo.
PICHA: ablf.tk

Jambo la msingi la kuzingatia ni kuwa unapoelewa ujumbe wa tabia ya mtoto unakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuchukua hatua sahihi zitakazomsaidia mtoto kurekebisha tafsiri, hisia na maamuzi potovu aliyonayo.

Kutafuta usikivu

Wakati unaondoka nyumbani, uliahidi kumletea mwanao zawadi. Ulifanya hivyo kama namna ya kuachana naye kirahisi. Umerudi nyumbani usiku, umechoka na majukumu yako ya siku. Mwanao amekusubiri kwa shauku kukuona. Mara unakumbuka, hukuja na zawadi uliyoahidi. Unamwomba msamaha kirahisi kwa sababu hata hivyo, hukumaanisha ulichokisema.

Kichwani unafikiri namna ya kukamilisha kazi zinazotakiwa kesho ofisini. Mwanao akiwa amekata tamaa anakuangalia ukichukua kompyuta na kuelekea mezani. Unamwelekeza kuangalia kipindi cha watoto kwenye televisheni ili akuche ufanye kazi zinazokusubiri.

Unapoanza kazi, mtoto anaacha kipindi, anahamia kwako. Inakuwa bughudha. Unamwambia kwa upole arudi kutazama televisheni kwa sababu, ‘baba ana kazi muhimu anahitaji kuimaliza.’ Unambusu na kumwelekeza pa kwenda. Baada ya dakika mbili, mtoto anaanza kugombana na mwenzake. Vilio na kelele. Unainuka kuamua ugomvi usioisha. Mtoto hanyamazi na kazi yako haiendi.

Anachokifanya mtoto katika mazingira haya ni kutafuta kusikika kwako. Anaamini humwoni kama mtu anayehitaji kusikilizwa. Kwa hiyo, kukusumbua, kufanya vitu vya ‘kijinga’, kukung’ang’ania, kudeka, kupiga kelele ni namna yake ya kutafuta usikivu usiompa.

Watoto huamini tabia hizi tusizozitaka kama kudeka, kulia lia, kelele zitawaunganisha na wazazi wao. Wasichokijua ni kuwa, kwa mzazi, tabia hizi ni utovu wa nidhamu. Una wajibu wa kuelewa ujumbe uliojificha kwenye haya anayofanya mtoto.

Ujumbe wenyewe ni, ‘Ninakukosa. Naomba uwe na muda na mimi.’ Mzazi anapoamua kumpa muda mtoto muda wake, mtoto atajisikia kuwa karibu na mzazi na atajiona ni mtu mwenye thamani. Kulia lia, kelele, ghasia, kudeka, kunaisha.
Ndio kusema, badala ya kumkasirikia mtoto anayehitaji kuwa karibu na wewe, utamsaidia kwa kuacha unachokifanya na kumpa usikivu.

Pengine umekuwa na mambo mengi. Hujatulia nyumbani. Suluhu ni kuwa na muda wa kufanya mambo yanayompa ujumbe kuwa, ‘Ninakupenda. Ninakujali kuliko simu/kompyuta.’

Hiyo, hata hivyo, haimaanishi muda wote uwe na mtoto. Hapana. Wekeza muda kwa mwanao unapopata nafasi. Weka utaratibu atakaouelewa. Unaporudi nyumbani pata dakika chache za kujua anaendeleaje. Fanya maongezi naye akiwa mwenyewe. Mtamkie maneno yanayomjenga.

Nenda na mwanao matembezini mkafanye kile anachopenda kukifanya. Atajiona mtu mwenye nafasi muhimu kwenye maisha yako na hatakuwa na sababu ya kuwa msumbufu.

Kulipiza kisasi

Amos ana miaka saba. Baba yake ni mfanyabiashara na mama ni mtumishi wa serikali. Kwa kawaida, baba yake hutumia muda mwingi kwenye biashara zake na mama pia husafiri mara kwa mara.

Wikiendi moja, baba anamchukua Amos na mdogo wake kwenda matembezini.  Amos anabembea, anaogelea na kushiriki kwenye michezo ya kila namna. Rebeca ni mdogo wake wa miaka mitatu. Hawezi kushiriki michezo mingi. Wakati Amos anacheza, wazazi wake wanajitahidi kuwa karibu na Rebeca.

Baba anamrusha rusha Rebeca juu huku mama akichekelea kwa pembeni. Amos anajifanya haoni lakini uvumilivu unamshinda anaposikia Rebeca akiambiwa ni mzuri kuliko watoto wote.

Muda wa kuondoka umefika. Amos haongei kwenye gari. Mama yake anajaribu kumsemesha lakini Amos anajifanya hasikii. Njiani, unazuka ugomvi na mdogo wake. Baba anajisikia kukata tamaa inakuwaje Amos anakuwa mgomvi.

Anamkumbusha Amos kuwa ni dhambi kugombana na mdogo wake. Nyumbani hali ni hiyo hiyo. Amos amekasirika. Baba anaamua kumchapa kwa kuwa na kisirani.

Tabia alizoonyesha Amos ni kulipiza kisasi. Amos amekasirika kuona Rebeca ‘anamzidi kete’ kwa wazazi. Kunyamaza, kugombana kunampunguzia maumivu yake kwa sababu anakuwa amelipiza kisasi. Mtoto anayelipiza kisasi hutukana, hupigana, hudanganya, anaweza kuiba, kuharibu vitu, na hata kuamua kushindwa kitu kwa makusudi.

Huenda umeshakutana na mazingira kama haya. Mtoto anaweza kufanya kitu kinachokuudhi, kinachokatisha tamaa, kitakachokusukuma kumwadhibu. Mtoto anapofanya tabia kama hizi, anajaribu kusema moyo wake umeumia.

Unaweza kumwuumiza mtoto bila kujua. Kuwa na matarajio makubwa kupita uhalisia kunaweza kumwumiza mtoto. Unamfanya ajisikie, ‘Kwa hiyo baba inaonekana utanipenda pale tu nitakapofaulu na kuwa malaika.’ Hisia hizo pekee zinaweza kuwa chanzo cha maumivu makubwa moyoni.

Wakati mwingine, mtoto anakuwa ameumizwa na mtu mwingine. Labda mwalimu shuleni amemwambia ‘Mjinga sana wewe.’ Anarudi na kisasi nyumbani. Maumivu ya kuambiwa ni mjinga yanamsukuma kuwafanya wengine wajione wajinga kama yeye. Anapofanya hivyo, anajaribu kupunguza maumivu ya nafsi yake.

Hulka ya mwanadamu ni kuwaumiza wanaomwumiza. Mzazi anapoumizwa na mtoto mwenye kisasi, naye husukumwa kumwumiza kwa kumwadhibu. Kwa juu juu tunafikiri tunamsaidia kurekebisha tabia. Lakini adhabu tunayompa inamfanya mtoto aumie zaidi. Akiumia, ndani yake anajenga hitaji la kutaka kulipiza kisasi zaidi.

Kuzuia mzunguko huu wa kisasi, ni vyema kwanza kuelewa ujumbe uliojificha kwenye tabia mbovu anazozionyesha mtoto, ‘Nimeumia; naomba uelewe hisia zangu.’ Mtoto anayejisikia kuumia analipa kisasi kutafuta namna ya kusaidiwa kupunguza maumivu yake. Kwa mshangao wake, mara nyingi, kinachotokea ni kinyume. Wazazi ‘humsaidia’ kwa kumwumiza zaidi.

Wakati mwingine, kumwumiza mtoto kunaweza kuonekana kama ni kutatua tatizo. Mtoto anaweza kutulia kwa sababu tu anaogopa kuumia zaidi. Lakini kufanya hivyo kunamfundisha kuwa wazazi hawaaminiki. Mazingira haya ya kutokuaminika yanajenga ukuta kati ya mzazi na mtoto hata kama kwa nje, mambo yanaweza kuonekana kuwa shwari.

Kwa ushauri elekezi kwa masuala ya malezi na makuzi niandikie: christianbwaya@gmail.com, 0754-870-815

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mambo ya Kuzingatia Unapoandika Wasifu wa Kazi (Curriculum Vitae)

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Fumbo mfumbie mwerevu

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3