Tunayopaswa Kuyafahamu Kuhusu Shule za Msingi za Bweni -2
Tulianza
kujadili namna gani mazingira ya shule za bweni yanavyochangia kuwasaidia
watoto wadogo kuimarika kiakili. Bonyeza hapa kama hukusoma makala hiyo. Tuliona shule za bweni zinaweka mazingira
sisimushi yanayowajenga watoto kiufahamu zaidi kuliko wenzao wanaoishi
nyumbani.
Mambo
kadhaa yanaonekana kuchangia kukuza uwezo huu. Kwanza, tulitaja uwepo wa ratiba
inayoongoza mtiririko wa shughuli za watoto wanapokuwa katika mazingira ya
shule.
Mtiririko
huu haukuonekana kwa watoto wa kutwa. Kwa mfano, watoto wa kutwa kwa kiasi
kikubwa hawakuonekana kuwa na uhakika wa nini wanakifanya baada ya saa za
shule.
Tafsiri yake ni kuwa wazazi hawawezi mazingira yanayomsaidia kujua
anafanye nini wakati gani. Kutokutabirika kwa ratiba kunaongeza uwezekano wa
mtoto kufanya mambo yasiyomsaidia kitaaluma. Kwa mukhtadha huu, shule za bweni
zinampa mtoto faida isiyopatikana nyumbani.
PICHA: unilever.com |
Uangalizi unaoaminika
Uangalizi
katika shule za bweni ulikuwa mzuri ukilinganisha na mazingira ya nyumbani. Uangalizi,
katika mukhtadha huu, ni uwepo wa walezi wanaoaminika wanaohakikisha kuwa mtoto
anapata mahitaji yake ya msingi kwa kipindi chote awapo shuleni.
Kwa
upande mwingine, mazingira ya nyumbani yalikuwa na upungufu wa uangalizi.
Wazazi hawakuonekana kupatikana vya kutosha na wakati mwingine walichelewa
kufika nyumbani. Matokeo yake watoto waliangaliwa na watu wengine waliopatikana
katika mazingira ya nyumbani au karibu na nyumbani.
Kutokuwepo
kwa uhakika wa ungalizi nyumbani, kulilazimisha watoto wakati mwingine kuwa
chini ya uangalizi wa watu wasio na mamlaka. Kukosekana kwa watu wenye sauti ya
kutosha kuwaonya, kuliwaweka watoto kwenye hatari ya kufanya chochote warudipo nyumbani.
Mazingira ya kujifunzia
Aidha,
shule za bweni zilionekana kuweka mazingira bora ya kujifunzia kwa watoto. Hapa
tunazungumzia upatikanaji wa watu wazima wenye uelewa zaidi na utayari wa
kuwapa watoto msaada wa kitaaluma uliohitajika baada ya saa za masomo.
Wakati
watoto wa nyumbani waliweza kufanya shughuli zisizo za maudhui ya kitaaluma
baada ya masomo kama vile kutazama televisheni na michezo isiyopangiliwa,
wenzao wa bweni hawakuwa na nafasi ya kufanya shughuli zisizo na uhusiano na
masomo.
Utaratibu wa shughuli
za nje
Kadhalika,
shule za bweni zilikuwa na utaratibu wa kuwaajiri wafanyakazi maalumu wenye
wajibu wa kufanya shughuli za nje ya darasa kwa niaba ya watoto. Kazi ndogo
ndogo kama kufanya usafi wa mazingira, kusafisha vyombo vya chakula, vyumba vya
kulala na kufua nguo za watoto zilifanywa na wafanyakazi.
Watoto karibu
wote walisema wanasaidiwa kufua nguo, kuogeshwa, kupiga mswaki, kutandika
kitanda na hata kufanya usafi wao binafsi. Ingawa utaratibu huu ulionekana
kudumaza uwezo wao wa kujitegemea kama tutakavyoona mbeleni, bado ulimsaidia
mtoto kuelekeza jitihada kwenye masomo. Hata hivyo, ni dhahiri shule zilifanya
hivyo kukidhi matakwa ya wazazi.
Mazingira
ya nyumbani, kwa upande mwingine, yalimshirikisha mtoto kwenye shughuli nyingi
za nyumbani. Mtoto wa kutwa, kwa mfano, alitumwa dukani, alifanya usafi wake
binafsi kwa msaada wa watu wazima na alifanya kazi ndogo ndogo kulingana na
mazingira yake.
Pamoja na
faida ya mtoto kushiriki shughuli hizi, hata hivyo ni dhahiri zilichukua muda
ambao ungeweza kutumiwa kwa shughuli za kimasomo.
Izingatiwe
kuwa ulinganisho huu ulifanywa kwa kutumia watoto wa shule ile ile ingawa
walitengwa kwenye makundi ya kutwa na bweni kuwezesha kufanya ulinganisho kwa
ufasaha.
Dhana ya kujitegemea
Kujitegemea
ni ujuzi wa kufanya shughuli zinazolingana na uwezo wa mtoto bila kuhitaji
msaada mkubwa wa watu wazima. Kwa mfano, mtoto anapoweza kupiga mswaki bila kutegemea
usaidizi wa watu wanaomzunguka, tunaweza kusema, hapo anajifunza kujitegemea.
Kinyume
chake ni mtoto kushindwa kuwa na ujuzi wa kufanya vitu vingi vinavyomwezesha
kumudu mazingira yake. Hapa tunazungumzia kujiogesha, kujipaka mafuta, kuosha
vyombo, kufua nguo, kuvaa viatu, kufunga kamba za viatu na stadi nyingine za kila
siku.
Aidha,
kujitegemea kunakwenda sambamba na uwezo wa mtoto kumudu viungo vya mwili wake
kumwezesha kufanya kile anachotaka kukifanya kwa muda muafaka. Kwa mfano, mtoto
mdogo anapojifunza ni muda gani anaweza kujisaidia kulingana na mahitaji ya
mazingira alimo, hapo tunasema, mtoto ameanza kujitegemea.
Kujitegemea,
kimsingi kunajegwa na kuimarishwa na mazingira ya kimakuzi. Mlezi au mzazi
anahitaji kujenga mazingira sisimushi yanayomjengea mtoto uwezo wa kujiamini na
kufanya vitu vinavyolingana na umri wake.
Ni muhimu
kuzingatia kuwa ujuzi anaojifunza mtoto unaimarika kadri umri wake
unavyoongezeka. Mtoto wa mwaka mmoja, mathalani, hawezi kufanya yanayofanywa na
mtoto wa miaka mitatu. Hata hivyo, kwa msaada wa karibu, mtoto aliye tayari
kimwili na kiakili huanza kujifunza ujuzi muhimu anaouhitaji kwa maisha yake.
Shule zinadumaza stadi
za maisha?
Kwa
haraka, mtu anaweza kufikiri shule za bweni zinasaidia kujenga stadi za maisha
kwa mtoto. Hata hivyo, hali halisi ni tofauti. Mazingira ya shule za bweni yanaonekana
kuwa na uwezekano mkubwa wa kudumaza uwezo wa watoto kujitegemea na kujifunza
stadi za maisha kuliko mazingira ya nyumbani.
Watoto
wengi wa bweni hawana uwezo wa kufanya shughuli nyingi za msingi bila msaada wa
watu wazima. Kwa mfano, katika utafiti uliotajwa, wengi hawakuwa na uwezo wa
kujifanyia usafi binafsi bila usaidizi wa walezi wao.
Kadhalika,
tabia ya kulowanisha vitanda iliripotiwa zaidi kwa watoto wa bweni kuliko
wenzao wanaoishi nyumbani. Idadi ya watoto walioripotiwa kukojoa vitandani
ilikuwa kubwa kwa upande wa bweni kuliko wale wanaolala nyumbani.
Ikumbukwe
kuwa hapakuwa na msisitizo wowote kwa watoto hawa wa shule za bweni kushiriki
shughuli za mikono kama wenzao walioishi nyumbani wala ukaribu wa kutosha kati
ya walezi na watoto. Shughuli karibu zote za mikono zilifanywa na watu maalum.
Ingawa lengo linaonekana ni kuwafanya watoto waelekeze juhudi zaidi kwenye
taaluma, kwa kiasi kikubwa, matokeo yake yalikuwa ni kudumaza uwezo wa watoto
kujitegemea na kujifunza stadi za maisha.
Inaendelea
Maoni
Chapisha Maoni