Namna Shule za Msingi za Bweni Zinavyoathiri Tabia za Watoto -3

KATIKA makala yaliyopita, tumeona kuwa shule za msingi za bweni zinachangia kuwanyima watoto fursa ya kujifunza ujuzi wa kujitegemea. Uwezo hafifu wa kujifunza stadi za maisha, kwa kiasi kikubwa, unachangiwa na matarajio makubwa ya kitaaluma waliyonayo wazazi kwa watoto wao.

Wamiliki na waendeshaji wa shule za bweni, kimsingi, wanaitikia wito wa wazazi wanaotarajia watoto wao kujifunza maarifa ya shule zaidi hata ikibidi kwa gharama ya kudumaza maeneo mengine muhimu ya kimakuzi.

Katika makala haya, tunaangazia mifano michache ya namna shule hizi za bweni zinazovyochangia kuwaathiri watoto kitabia. Mifano hii inatokana na ulinganisho wa tabia za watoto wanaosoma shule za bweni na wale wanaorudi nyumbani kila siku.

PICHA: pinterest.com

Tabia zilizolinganishwa

Watoto walilinganishwa kwa tabia kadhaa chanya na tabia hasi zilizochaguliwa. Tabia chanya ni zile tabia zinazomfanya mtoto ajichukulie vyema yeye mwenyewe na hivyo kuwachukulia wengine vizuri. Mfano ni kucheza na kushirikiana na wenzake, namna anavyoweza kufuata maagizo anayopewa na watu wazima, anavyojiamini, anavyoheshimu watu wazima na kuwapenda watoto wenzake.

Tabia hasi ni zile zinazotokana na mtoto kujisikia vibaya kihisia na hivyo kushindwa kuishi vizuri na watu wengine wanaomzunguka ikiwa ni pamoja na ndugu aliowaacha nyumbani.

Mfano wa tabia hizi ni hisia za upweke na kutegwa na watu wake wa karibu; kuwa na aibu na woga wa kufanya mambo; tabia ya kupenda kudeka, hasira zisizo na maelezo; udokozi wa vitu visivyo vyake; kuonekana anakosa amani na kulia lia bila kuwa na sababu za msingi.

Tabia za watoto wa bweni

Watoto wa bweni, kwa kiasi kikubwa, walionekana kuwa na changamoto nyingi za kitabia kuliko wenzako wanaoishi nyumbani. Ingawa kwa haraka haraka watoto hawa walionekana kuwa wachangamfu zaidi kuliko wenzao wanaoishi nyumbani, uchunguzi wa kila ulionesha kuwa walikuwa wamejenga tabia hatarishi kuliko wenzao. Kwa mfano, wengi wao, hasa wa darasa la kwanza, walikuwa wapweke na walikuwa na tabia ya kuwadekea walezi wao.

Tabia hii inaweza kuelezwa kama matokeo ya kukaa mbali na familia zao kwa muda mrefu, hali inayoweza kutafasiriwa na mtoto kama kutelekezwa. Mathalani, watoto hawa walionekana kujenga imani kwa watu wengine zaidi kuliko wazazi au ndugu zao. Wenzao walioishi nyumbani, walionekana kuwa na imani na mzazi au ndugu wa karibu kuliko mtu mwingine yeyote akiwemo mwalimu.

Kadhalika, watoto wa bweni walionekana kuwa na tabia ya kuwa na hasira zisizo na maelezo ya msingi. Kwa mfano, mtoto wa bweni angeweza kukorofishana na mwenzake  kwa jambo dogo kuliko mwenzake anayeishi nyumbani.

Changamoto za kimalezi 

Tofauti hiyo ya kitabia kati ya watoto wa bweni na wale wa kutwa inaonekana kuchangiwa, kwa kiasi kikubwa, na aina ya malezi yaliyopatikana katika mazingira hayo ya bweni yanayomwathiri mtoto kwa namna kadhaa.

Mosi, mtoto wa bweni anakosa mtu wa karibu anayeweza kumsikiliza kibinafsi na kujua ana shida gani, ana wasiwasi na matarajio yapi na mambo mengine binafsi. Ukaribu huu kati ya mlezi na mtoto unakosekana katika mazingira ya bweni kutokana na idadi kubwa ya watoto wanaoangaliwa na walezi wasiokidhi mahitaji halisi.

Kwa kawaida, mtoto mdogo anahitaji kujenga ukaribu na watu anaowaamini. Anahitaji mtu mzima anayeweza kuwa tayari kusikiliza mashtaka yake, matumaini yake na hata masimulizi ya fahari za mambo mema anayoyafanya mchana kutwa. Mtu wa namna hii anapokosekana mtoto hujikuta katika hali ya upweke na kupungukiwa.

Katika shule kadhaa zilizotembelewa, kwa mfano, mlezi mmoja aliwaangalia watoto zaidi ya 100 kwa wakati mmoja. Katika mazingira haya, ni vigumu kwa mtoto mmoja moja kupata mtu anayeweza kumsikiliza na kutatua changamoto anazokabiliana nazo kibinafsi.

Watoto walilelewa kimakundi na mahitaji yao yalifikiriwa kiujumla jumla kwa kuongozwa na utaratibu rasmi. Mathalani, walezi walihakikisha mtoto anapata chakula, anakuwa msafi, analala mahali salama. Hata hivyo, walikiri hawakuwa na uwezo wa kumsikiliza mtoto mmoja mmoja. Muda huo haukuwepo.

Upweke wa kihisia

Aidha, katika mazungumzo na watoto, ilikuwa bayana kuwa wengi wao hawakupata nafasi ya kuonana na wazazi wazo kwa zaidi ya miezi mitatu. Wazazi, pengine kwa sababu za msingi kabisa, waliwatuma watu wengine kwenda kuwaona watoto kwa niaba yao.

Watoto walijikuta kihisia wakiishi mbali na watu wazima. Walimu walijali taaluma. Walezi walijali usalama wao kimwili. Wazazi nao walijali kusikia wanaendelea vizuri. Watoto hawa walioishi katika mazingira ya kutengwa kihisia waliamua kutengeneza uhusiano wa kubahatisha na watoto wa umri wao.

Haikuwa ajabu, katika muktadha huu, kusikia watoto wengi wakijifunza tabia zinazowazidi umri. Hawakuwa na mtu mzima wa karibu kutathmini yale wanayojifunza wakiwa na wenzao ambao kimsingi wanafanana nao kiakili.

Unafuu wa mazingira ya nyumbani

Ukilingalisha na watoto wanaoishi nyumbani, tofauti i dhahiri. Mtoto wa nyumbani anaweza asipate fursa ya kukaa na mzazi wake kwa ukaribu. Lakini angalau yeye anakutana naye mara kwa mara hata kama si kwa ukaribu anaouhitaji.

Inawezekana mzazi kwa sababu yoyote ile hapatikani vya kutosha nyumbani, lakini kuna namna mtoto anaweza kuwasiliana naye. Sambamba na hilo, mtoto anayeishi nyumbani anaweza pia kuonana na ndugu zake karibu kila siku. Ndugu hawa wa karibu wanakuwa na fursa ya kujua mwenendo wake na hata kuchukua hatua fulani mapema. Mtoto wa bweni hana fursa hii.

Inaendelea

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo ya Kuzingatia Unapoandika Wasifu wa Kazi (Curriculum Vitae)

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Tabia za Mtoto wa Miaka 0 – 3 Kimahusiano na Kihisia

Haiba ni nini?