Unavyoweza Kukuza Tabia Njema kwa Mwanao -4
Katika makala yaliyopita
tumejifunza aina mbili za misukumo ya utovu wa nidhamu. Kwanza, tumeona mtoto
huweza hufanya ukorofi kutafuta kusikilizwa. Anaposumbua na hata kudeka bila
sababu, mara nyingi, anajaribu kutuambia kuwa hatujampa muda wa kuwa karibu
naye. Anafanya hivyo kutafuta usikivu wetu.
Pia, tumeona wakati mwingine mtoto
husukumwa na hisia za kutaka kulipiza kisasi. Kama ilivyo kwa mtu mzima, mtoto
naye anazo hisia. Anaweza kuumizwa na kauli na matendo anayoyatafsiri vibaya.
Jitihada za kupunguza maumivu yake huishia kuwaumiza na wengine.
Namna gani tunawasaidia watoto
kuondoa tafsiri hizi potofu, huamua aina ya tabia watakazojifunza. Katika
makala haya tunaangazia malengo mengine mawili yanayotengeneza msukumo wa
kukosa nidhamu.
PICHA: NUBI Magazine |
Kutafuta ushawishi asionao
Richard mwenye miaka nane hana
adabu nyumbani. Hasikii anachoambiwa na yeyote isipokuwa anapotishiwa kwa
kiboko. Juzi ameonywa na baba yake aache tabia ya kuzurura mitaani. Aliitikia,
lakini leo pia ameendelea kuzurura.
Muda mwingi anagombana na mdogo
wake. Ni mlalamishi na mara nyingi humshtaki mdogo wake kwa wazazi.
Anapokuwa shuleni, Richard ana
sura tofauti. Nidhamu yake ni ya hali ya juu kwa walimu na wenzake. Ni vigumu
kuamini Richard huyu anayeshindana na wazazi wake nyumbani ni mnyenyekevu na
msikivu anapokuwa suleni. Kitu gani kinamfanya Richard awe mtukutu anapokuwa
nyumbani?
Richard anajiona kama mtu asiye na
ushawishi kwenye familia yake. Ujeuri anaojaribu kuufanya unamsaidia kufidia
hali ya kukosa ushawishi anayojisikia ndani yake. Anafikiri kwa kujaribu kushindana
na wazazi kunamhakikishia ushawishi anaohisi hanao.
Kwa kawaida, watoto kama walivyo
watu wazima wanahitaji kuwa na mamlaka. Mamlaka ni ushawishi anaokuwa nao wa
kusababisha kitu kikafanyika. Watoto wanapopewa fursa (inayolingana na umri
wao) ya kujisikia kuwa wana ushawishi kwenye familia wanajiona wana mamlaka.
Mfano, shughuli kama kuongoza ibada, kuombea chakula, kupanga ratiba zao kwa
msaada wa wazazi zinawajengea imani kuwa wana mamlaka.
Richard anafanya vituko kwenye
familia kwa sababu amekosa imani hiyo. Anagombana na mdogo wake mara kwa mara
kwa sababu anahisi ndiye mwenye ushawishi. Maneno kama, ‘Unakoseaje wakati wewe
ni mkubwa kuliko mwenzako? Acha ujinga’ yanamnyang’anya mamlaka anayodhani
anayo.
Mtoto anayejihisi hana mamlaka ni
mgomvi, hukejeli wengine, huwa na madai mengi, hulazimisha ukubwa kwa wengine.
Vile vile, ana tabia ya kukubaliana na maagizo lakini hafanyi; mbishi na mkaidi;
si msikivu na wakati mwingine huwa na dharau kwa watu wanaomzidi.
Kimsingi, anafanya yote hayo kwa
lengo la kumnyong’onyeza mtu mwingine mwenye mamlaka kwake ili kumfanya ajione
‘hawezi kumfanya kitu.’ Kumtawala mtoto kupita kiasi kunaweza kuzaa hali hii.
Unaposhindwa kumpa nafasi ya kutumia utashi wake, mathalani kuamua wapi
akacheze, unamnyang’anya imani kuwa ana ushawishi kwenye familia.
Hali hii huzaa mashindano ya chini
chini kati ya mzazi na mtoto. Mzazi anaogopa kumpa mtoto nguvu ya kufanya
chochote. Mtoto naye anatamani kuwa na sauti angalau kwa mambo yanayomhusu.
Anapokosa sauti, mtoto anajenga upinzani.
Mtoto wa namna hii anayejisikia kubanwa, hufika mahali pa kutishia
mamlaka yako kwa kukataa kufanya unachomwagiza.
Kumwadhibu mtoto anayetishia
mamlaka ya mzazi ni kuendeleza tatizo. Namna nzuri ya kumsaidia mtoto wa namna
hii ni kumfanya ajisikie mshindi. Kukiri makosa yako kunaweza kurudisha imani
yake kwako. Hili, hata hivyo, si jambo rahisi.
Kwa wazazi wengi, kukiri kosa ni
sawa na kujidhalilisha. Wanafikiri mtoto akijua umekosea, atajenga kiburi.
Matokeo yake wanaendelea kushindana kwa kutoa adhabu ambazo kimsingi zinaongeza
uadui. Wakati mwingine jibu ni kuwa tayari kushuka chini na kuachia kiasi cha
mamlaka yako.
Kujiona hawezi
Tunazaliwa na hitaji la kujiona
tunaweza. Ili mtu ajisikie anaweza, lazima kwanza aweze. Anapoweza kufanya kitu
kwa mafanikio, anajenga hali ya kujiamini. Mtu anayejiamini anakuwa tayari
kujaribu kufanya vitu vipya bila wasiwasi wa kushindwa.
Watoto wanaoamini hawawezi mara
nyingi wanakuwa na wasiwasi na uwezo wao. Mazingira ya kimalezi yamewakatisha
tamaa. Ndani yao inatoka sauti inayonyong’oneza, ‘Unaweza kufanya nini mtu kama
wewe? Huwezi chochote!’
Mtoto wa namna hii huonyesha
alivyokata tamaa kwa namna mbali mbali. Anaweza kujitenga na wenzake; hayuko
tayari kujaribu chochote na wakati mwingine huwa na tabia ya kujitamkia maneno
yenye kuthibitisha kuwa yeye ni mtu dhaifu.
Tutumie mfano wa Bakari mtoto wa
miaka tisa. Bakari hapendi kufanya vitu bila kuambiwa. Mara nyingi ataamka na
hakumbuki kupiga hata mswaki mpaka aambiwe. Akila ataacha vyombo pale pale
mpaka mama amkumbushe kuviondoa. Kwa umri wake ungetegemea akiamka ajiandae
aende shule. Lakini hata kuamka ni mpaka awepo mtu wa kumkumbusha. Kwenda shule
ni ugomvi kwa sababu hataki kuachana na wazazi. Ukimwangalia kwa haraka,
unaweza kusema ni mvivu na goigoi.
Ukiwauliza wazazi wake,
wanakwambia wanampenda sana. Muda mwingi wako naye na hawamwachi. Mama yake
anajitahidi kumfanyia karibu kila kitu. Anamfungia kamba za viatu, anamchania
nywele na kila kitu. Saa ya kufanya kazi za nyumbani anazopewa shuleni, mama na
baba watashindana kumsaidia hesabu zote.
Wazazi wanafanya yote hayo kwa nia
njema. Wanampenda Bakari. Wana matarajio makubwa kwake na wanajitahidi
kuhakikisha kuwa mwanao hapati shida.
Mara chache ambazo Bakari
anajaribu kufanya kitu, wazazi wanakuwa wepesi kugundua makosa. Bakari
anapokuja na alama 70, mama na baba watakuja juu. Wanahitaji kuona 95 kwenye
mtihani ujao.
Bakari amejikuta akijenga fikra
potofu kuwa hawezi. Ingawa wapo watoto wengine ukiwaambia hawawezi ndio kwanza
wanajenga hamasa ya kukuthibitishia kuwa wanaweza, kwa Bakari hali ni tofauti.
Matarajio makubwa ya wazazi ambayo katika hali halisi hayafikiki, yanamfanya
ajihami kwa kutokujaribu. Bakari hasaidiwi kwa kusimangwa. Msaada anaouhitaji
ni kutiwa moyo kuwa anaweza.
Kwa ushauri elekezi kwa masuala ya malezi na makuzi niandikie: christianbwaya@gmail.com, 0754-870-815
Maoni
Chapisha Maoni