Unavyoweza Kukuza Tabia Njema kwa Mwanao -2
Mama Neema anarudi nyumbani jioni.
Neema anaposikia mlio wa gari ya mama yake, anatoka nje kwa furaha. Mara moja
anamrukia mama kumpokea kwa bashasha.
Mama amechoka. Amekuwa na siku ndefu kazini. Haonekani kuwa mchangamfu.
Neema anauliza maswali mengi kwa
mama yake. Hajibiwi. Hata pale anapojibiwa, mama haonekani kuwa na uzingativu. Ili
apate nafasi ya kumpumzika, mama anamwelekeza Neema kwenda kufanya kazi za
shule alizokuja nazo nyumbani. Neema anavunjika moyo lakini analazimika
kuondoka.
Baada ya muda mfupi, wageni
wanaingia. Ni rafiki zake mama Neema. Ingawa amechoka, analazimika
kuwachangamkia. Mazungumzo ya mama na wageni yanapambwa na vicheko, utani na
uchangamfu.
Mama anamwita Neema awaletee
wageni vinywaji. Neema yuko mezani. Anajifanya hasikii. Mama anaita kwa mara
nyingine, Neema anakuja bila kuitika. Hasalimii wageni na haonekani kujali.
Mama anajisikia kudhalilika. Anavumilia kwa heshima ya wageni.
Wageni wanapoondoka, mama
anamrudia Neema kwa hasira. Anamkemea kwa kuonesha utovu wa nidhamu tena mbele
ya wageni wake muhimu. Neema hajibu chochote. Mama anaamua kumchapa. Neema
anakwenda kulala akilia.
Kuelewa msukumo nyuma ya tabia
Wazazi wanaweza kuelewa kisa hiki
vizuri zaidi. Mara nyingi watoto huonyesha utovu wa nidhamu kama alivyofanya
Neema. Hatufurahii tabia kama hizi na hivyo tunalazimika kuwaadhibu.
Hata hivyo, wakati mwingine
tunawaadhibu pasipokujua kwa nini wamekosa adabu. Badala ya kuuelewa msukumo ulio
nyuma ya tabia tunayopambana nayo, tunakuwa wepesi kutumia nguvu kutoa adhabu. Lengo
la kutoa adhabu ni kumsaidia mtoto kujifunza tabia njema.
Tunafanya kama tulivyolelewa sisi.
Tulikemewa tulipokosea. Tulichapwa tulipoonesha tabia zisizofaa. Ingawa tunaweza
kuwa wazazi wasio wakweli, lakini tunaamini tulisaidiwa kuwa na tabia njema.
Tunaweza kuwa wagomvi na watu tusiokubali mawazo tofauti lakini bado tunaamini
tulivyo, ndivyo tulivyopaswa kuwa. Kwa msingi huo tunaendeleza mbinu zile zile
zilizotumika kutufanya tuwe kama vile tulivyo tukiamini zilikuwa sahihi.
Tunatumia nguvu kama zilizotumika kwetu.
Kuelewa anachohitaji mtoto
Kila mtoto anatamani kuwa karibu
na mzazi wake. Kuwa karibu kunampa mtoto utulivu. Anajisikia kuwa mtu wa
thamani anapokuwa karibu na mzazi. Ukaribu huo unapokosekana kwa sababu yoyote,
mtoto anajisikia kupungukiwa na kitu muhimu.
Ni sawa na Neema. Mama yake aliposhindwa
kumchangamkia, Neema akajisikia kupungukiwa. Hakuwa na uwezo wa kuvumilia umbali
huo aliouhisi. Ili kurejesha kile anachoona kinachopungua, hakuitika mama
alipomwita. Kwa ufahamu wake, kunyamaza kungemstua mama kuchukua hatua za
kurejesha ukaribu. Haikuwa kama alivyotarajia.
Wakati mwingine, mtoto hukosa
adabu kwa sababu tu anajisikia hawezi kufanya anachotamani. Mazingira
yanapomfanya aamini hawezi, ndani yake kunajengeka msukumo wa kujaribu
kuthibitisha kuwa bado anaweza.
Kuelewa tafsiri za mtoto
Mtoto ana uwezo mdogo wa kuelewa na
kutafsiri mambo. Namna mtoto anavyotafsiri mambo, sivyo sisi watu wazima
tunavyofanya. Kufikiri mtoto anaweza kuona mambo kama vile tunavyoyaona sisi, si
sahihi. Hiyo, hata hivyo, haimaanishi tupuuze hisia za mtoto. Hasha. Tunapopuuza
hisia hizo hata kama ni potofu tunakuza tabia zisizofaa.
Mama yake na Neema, kwa mfano,
hakusumbuka kuelewa tafsiri za Neema. Hakuwa na habari kuwa Neema anajaribu
kuelewa kwa nini mama hajanichangamkia lakini wageni walipokuja
aliwachangamkia. Mama Neema hakufikiri mambo madogo namna hiyo.
Lakini kwa mtoto, kama Neema, hilo
ni suala kubwa. Akili yake haifikirii kwa mantiki anayoitumia mama. Muda wote ufahamu
wa mtoto hufanya kazi ya kutafsiri, kutengeneza hisia, kuamua na hatimaye
kufanya kitu kinachokwenda sambamba na tafsiri potovu aliyoitengeneza, hisia
potovu alizonazo, na maamuzi potovu aliyoyafanya. Hayo yote kwa pamoja ndiyo
yanayochochea utovu wa nidhamu.
Neema hakuamua kunyamaza kwa
makusudi. Alipompokea mama yake, alikuwa na matarajio fulani. Alitegemea mama
yake angemchangamkia. Labda angembeba, angembusu na kumkumbatia. Mama hakufanya
hivyo. Kwamba hajafanya hivyo, haimaanishi mama hampendi Neema. Hapana. Moyoni
mwa mama, Neema ni mtu wa thamani hata kama hajambeba, hajambusu, hajamwambia
anampenda na hajamkumbatia.
Lakini kwa Neema, ‘Kama hujafanya
lolote kati ya hayo, hunijali!’ Hii ni tafsiri potofu inayojengwa na akili za
kitoto. Wageni walipoingia, mama alilazimika kuchangamka. Neema anachunguza, ‘Kwa
nini mama amekuwa mchangamfu wageni walipoingia?’ Anajisikia vibaya moyoni. ‘Mama
hanijali. Haoni thamani yangu kama mwanae.’ Hizo ni hisia potofu zinazotokana
na tafsiri potovu.
Hisia hizi zinamfanya Neema afanye
maamuzi. ‘Nitamwuumiza kidogo na yeye.’ Hiki ni kisasi. Mama yake anapomwita,
Neema anafanya kama alivyoamua. Ananyamaza. Mama yake hajaweza kutafsiri kwa
nini Neema anafanya hayo anayoyafanya.
Ndivyo tunavyofanya wazazi wengi.
Tunatazama utovu wa nidhamu unaofanywa na watoto kirahisi. Mtoto
anapokunyamazia kama alivyofanya Neema basi unachukulia kuwa hiko ni kiburi,
dharau, kuharibika, mapepo na majina mengine mabaya. Kwa kuwa hatupendi tabia hizi,
tunakasirika na kutumia nguvu kupambana nazo. Ndivyo alivyofanya mama Neema.
Tunavyorekebisha tafsiri potofu
Jambo la kuelewa, hata hivyo, ni
kuwa unaposhughulikia upotovu huu unaouona kwa mtoto kwa kutumia mbinu za
kibabe unakuza tatizo badala ya kulitatua kama tutakavyoona mbeleni. Adhabu
inaweza kuwa suluhu ya muda mfupi lakini isisaidie kujenga uhusiano mzuri kati
ya mzazi na mtoto.
Kwa mfano, baada ya Neema
kuchapwa, kesho yake inawezekana hakumsalimia mama na pengine alienda shule
bila kuaga. Hafanyi hivyo kwa bahati mbaya. Anatumia njia potofu kutuma ujumbe
uliojaa moyoni mwake, ‘Mama hunipendi. Hunijali!’ Hana ujasiri wa kusema maneno
hayo. Anatumia lugha ya ishara kufikisha ujumbe kwa mzazi wake.
Nafasi yako kama mzazi ni kufanya
juhudi za kuelewa ujumbe huu unaobebwa na tafsiri, hisia na maamuzi potovu
anayoyafanya mtoto. Unapoweza kuelewa ujumbe huu, unaweza kurekebisha tafsiri,
hisia na maamuzi ya mtoto. Ukifanya hivyo, mtoto hatajisikia kupuuzwa,
kutokuthaminiwa, kutokupendwa na hatimaye atakuwa tayari kukupa ushirikiano
unaoutaka.
ITAENDELEA
Maoni
Chapisha Maoni