Kusamehe Wazazi Wako Kunavyoweza Kubadilisha Maisha Yako

Kuna tabia fulani tunaweza kuwa nazo ambazo, kwa hakika, tunajua zinatufananisha na wazazi wetu. Tunafanya vitu fulani, wakati mwingine bila hata kujua, lakini vinafanana na yale tuliyowahi kuwaona wazazi wetu wakiyafanya.

Ipo mifano mingi kuelezea jambo hili. Baba, kwa mfano, unaweza kuwa na tabia ya hasira kali. Mwanao akifanya kosa dogo unakuwa mwepesi wa kukemea. Wakati mwingine, unatoa adhabu kubwa mno zisizolingana na makosa halisi ya mtoto. Ukichunguza vizuri unakuta kumbe ndivyo alivyo na baba yako.

Kwamba baba yako pengine alikuwa na tabia ya kufoka mara kwa mara hata kwa mambo ambayo kwa hali ya kawaida ni madogo. Wewe wakati huo ukiwa mdogo hukupenda kumwona mzazi wako akifoka hadharani. Sasa hivi bila kujielewa unajikuta na wewe unayafanya yale yale ambayo hukuyapenda kuyaona kama mtoto.

Wapo wazazi ambao ni wepesi kuchapa watoto. Wanafanya hivyo wakifikiri wanawasaidia watoto kujenga tabia njema. Si kwamba wazazi hawa wanapenda kuwachapa watoto wao. Hapana. Kimsingi, hata wao walipokuwa watoto hawakupenda kuchapwa. Waliogopa kuchapwa. Leo wao kama mzazi wanakuwa wepesi kuchapa.

Mwanao anaweza kufanya kosa dogo. Ungeweza kabisa kulipuuza au kulitatua kwa njia ya kirafiki. Lakini bila hata kujua sababu, unajikuta umemfokea, umemchapa na hata kumdhalilisha. Hasira zikipoa baadae, unajilaumu kwa nini umefanya hicho ulichokifanya.

Si kwa watoto pekee. Inaweza kuwa hata kwa mwenzi wako. Unaweza kutamani kabisa kuongea kwa lugha ya kistaarabu kwa mpenzi wako, lakini unajikuta unafoka na kulalamika. Unatamani maisha fulani ya ukaribu lakini hufanyi. Kila unapojaribu, nafsi inakuwa kama inakuzuia kutekeleza jema unalolijua. Badala yake unashangaa unamfanyia baya usilolikusudia unalokuja kulijutia baadae.

Aidha, inaweza pia kuwa kwa wazazi wako mwenyewe. Unatamani kuwatendea wema wazazi wako lakini huwezi. Unatamani ungekuwa karibu nao, uongee nao kwa nidhamu lakini moyo wako unakuwa mzito. Ni kama unaishi na uchungu fulani dhidi ya wazazi wako ambao kimsingi huelewi chanzo chake.
PICHA: Ebony Magazine

Utoto unaoishi ndani yetu

Wataalamu wengi wa saikolojia wamejaribu kuchunguza jambo hili. Katika tafiti zao wamejaribu kujua kwa nini wakati mwingine tunafanya mambo tusiyoyakusudia. Kwamba tunashindwa kufanya mazuri tunayotaka lakini tunafanya mabaya tusiyoyakusudia.

Upo ushahidi wa kutosha kuwa matukio anayokutana nayo mtu tangu akiwa tumboni mwa mama yake yanayo nguvu kubwa ya kuamua mustakabali wake. Matukio yanayotupata katika umri mdogo yanatuumba kuwa vile tutakavyokuwa ukubwani.
Kwa mfano, inawezekana wazazi wako walipigana mbele yako ulipokuwa na umri wa miaka miwili. Katika umri huo, hukumbuki kilichotokea na hata wazazi wenyewe walifikiri huelewi. Hawakujali.

Hata hivyo, ambacho hawakujua ni kuwa katika umri huo angalau ulikuwa na akili za kukufanya ujisikie vibaya kuona hicho ulichokiona kikifanywa mbele yako. Pengine ulilia kuona mama yako akipigwa. Uliogopa kumwona baba yako akifoka mbele yako. Leo unapojaribu kuvuta kumbukumbu hizo huwezi. Lakini akili yako, inayo kumbukumbu sahihi ya mambo hayo.

Kwa hakika mambo hayo tuliyokutana nayo kama watoto yanawakilisha maisha yetu ya utotoni. Maisha hayo yanaishi ndani yetu. Ni sehemu ya maisha yetu ya utu uzima. Utoto huo una tabia ya kuibuka mara kwa mara leo hii tukiwa kama watu wazima.

Wajibu wa kuwasamehe wazazi

Huenda wazazi wako walifanya vitu usivyovipenda. Pengine walikuwa na tabia ya kutukanana mbele yako ukiwa mtoto. Uliumia kama mtoto. Ukafikiri imeishia hapo. Lakini unapotazama maisha yako sasa hivi kama mzazi unagundua na wewe unafanya yayo hayo yaliyokuumiza. Huoni shida, kwa mfano, kumkosea nidhamu mwezi wako mbele ya watoto wako kama alivyofanya mzazi wako.

Mahali pa kuanzia katika kushughulikia tatizo hili, ni kuwasamehe wazazi wako kwa yale yote waliyoyafanya pengine bila kujua. Hawakufahamu kuwa yale waliyoyafanya mbele yako yangechangia kukufanya vile ulivyo. Walifikiri ulikuwa mdogo sana kuweza kuelewa.

Pengine walikuchapa wakiamini kwa kufanya hivyo walikuwa wanakusaidia kujenga tabia njema. Hawakujua kuwa kukuchapa kulikufundisha mazoea mabaya ya kutumia nguvu katika kutatua matatizo yako. Fimbo walizokucharaza zilitengeneza kisasi usichokitambua ndani yako. Ndio maana na wewe umekuwa mwepesi kutumia fimbo kama namna ya kuwaadabisha wanao.

Unahitaji kuondoa kisasi hicho kilichojiumba ndani yako. Namna moja wapo kukusaidia kushughulika na kisasi hicho ni kuamua kwa dhati kuwasamehe wazazi kwa makosa yao.

Mara nyingi vijana wametembea na visasi mioyoni mwao bila kujua. Pengine, kwa mfano, wakiwa watoto waliomba fedha kwa wazazi wao na kujibiwa bila staha. Akili zao zilihifadhi uchungu wa hisia za kunyimwa mahitaji yao. Leo kama watu wazima wanajikuta wakiwa wazito kuwasaidia watoto wao wenyewe. Wanatamani watoto wao waonje ugumu kama ule walioupitia wao.

Kwa kawaida, ni rahisi kufikiri kwa sababu wewe ulipitia malezi fulani basi na mwanao analazimika kupitia njia ile ile uliyopitia wewe. Unaona kama kumfanya apate wepesi ni kumpendelea isivyo haki. Akili inaamini kumpa mtoto haki ambayo wewe hukuipata ni kumpa asichostahili. Hali hii ya kumnyima mwanao yale anayoyastahili kwa sababu tu pengine wewe hukuvipata ndiyo inayoitwa kisasi.

Wakati mwingine kinyume chake hutokea. Tunajikuta tukifanya kinyume na mabaya yaliyofanywa na wazazi wetu. Kwa mfano, inawezekana leo wewe kama mzazi hujali kufuatilia kile anachokifanya mtoto. Unamwacha awe huru kupindukia kwa sababu tu hukupenda namna wazazi wako walivyokubana enzi za ujana wako. Sasa hivi ukiwa mzazi, unajikuta ukimpa mtoto uhuru holela unaoweza kumletea matatizo.

Inawezekana pia umekuwa mpole kupindukia. Hukupenda ukali wa wazazi wako. Matokeo yake watoto wanaweza kufanya makosa yanayostahili adhabu lakini ukawa mzito kuwaadhibu. Ukimya wako unaweza kumshangaza hata mzazi mwenzako. Lakini kumbe unafanya hivyo kwa sababu hujamsamehe mzazi wako aliyekuadhibu kwa kufanya yasiyofaa.


Inaendelea

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?