Unavyoweza Kukuza Tabia Njema kwa Mwanao -1
Fikiria mwanao ana umri wa miaka
kumi na minane na anaondoka nyumbani kwenda kujitegemea. Je, ungependa awe mtu
mwenye tabia zipi? Ungependa mwanao anapoondoka nyumbani kwako kwenda kuanza
maisha mapya awe mtu wa namna gani? Sifa zipi, ujuzi upi, haiba ipi ungependa imtambulishe
akiwa mtu mzima?
Jiulize, wakati mwanao anaanza
maisha ya ndoa, ungependa mwenzi wake aone tabia zipi kwake? Kama ni ajira,
ungetamani awe na sifa zipi zitakazomsaidia kufanya vizuri kazini? Ungependa
aishi namna gani na watu?
Katika mazungumzo yangu na wazazi,
nimekuwa nikiwaomba wanitajie sifa wanazoamini watoto wao wanazihitaji ili kuwa
watu wenye furaha, wanaoishi vizuri na wanaoweza kutegemewa na jamii.
Sifa zinazojitokeza mara nyingi zaidi
ni kujiheshimu na kuheshimu wengine, uaminifu, uadilifu, uwajibikaji na bidii
ya kazi. Nyingine ni moyo wa kiasi na nidhamu, ushirikiano na watu, ujasiri, uvumilivu
na uwezo wa kutatua changamoto za kimaisha.
Inawezekana kwa uzoefu na
mazingira tofauti uliyonayo, orodha yako inaweza kuwa na sifa tofauti na hizi
zilizotajwa. Hata hivyo, pamoja na tofauti zinazoweza kujitokeza, bado kuna uwezekano
kuwa sifa hizo hazitakuwa mbali sana na hizi zilizotajwa.
Nafasi muhimu ya malezi
Imejengeka dhana kuwa mtoto
huzaliwa na tabia zake. Kwamba jitihada za mzazi zina nafasi ndogo ya kujenga
tabia fulani anazotamani mwanae awe nazo. Athari ya mtazamo kama huu ni mzazi
kujipunguzia wajibu kwa imani kuwa ‘tabia ya mtoto ni kazi ya Mungu.’
Hata hivyo, bado wazazi wenye
mtazamo huu hufanya jitihada fulani za kuhakikisha watoto wanajenga tabia
njema. Watoto huadhibiwa, hukaripiwa na wakati mwingine hulazimika kusikiliza maelekezo
ya kimaadili kama jitihada za kuwanyoosha wawe vile wazazi wanavyotamani wawe.
Pamoja na kutambua ukomo wa
jitihada za kimalezi katika kujenga tabia njema, bado ni dhahiri malezi yana
nafasi kubwa. Tabia wanazokuwa nazo watoto zinategemea namna wanavyolelewa
tangu wakiwa wadogo.
Mbinu tulizozizoea
Pamoja na kuwa wazazi hutamani
watoto wao wawe na tabia njema, mara nyingine mbinu tunazotumia kufikia lengo
hilo huweza kutengeneza matatizo ya kitabia yasiyotarajiwa. Mbinu zilizozoeleka
hulenga kufanyia kazi kile tunachojisikia kama wazazi kuliko kushughulikia kile
alichokikosa mtoto ambacho kimsingi ndicho kilichomfanya akosee.
Makosa ya kitabia wanayoyafanya na
watoto mara nyingi hulenga kufidia kile wanachohisi kukikosa kwetu wazazi wao.
Kwa mfano, mtoto anayejisikia kutengwa, hutumia mbinu ya kudeka na kulia akitafuta
kusikilizwa. Kwa kuwa mzazi hajajiuliza kwa nini mtoto analia lia bila sababu, hukerwa
na tabia hii na kuamua kumchapa.
Mzazi anapomchapa ana nia njema kabisa
ya kuhakikisha kuwa mtoto anajenga tabia zinazokubalika katika jamii. Lengo la adhabu
inayotoelewa na mzazi ni kujaribu kumnyoosha mwanae afanane na matarajio aliyonayo.
Lakini adhabu hiyo inapotolewa bila kuelewa msukumo ulio nyuma ya kile
kilichofanywa na mtoto, tatizo jipya linaweza kuzalishwa.
Kwa mfano, mtoto anafanya vurugu
kwa lengo la kupata usikivu wa mzazi. Badala ya kusikilizwa, mzazi anaongeza
adhabu. Katika mazingira haya, mtoto anaweza kukosa imani na uwezo wa mzazi kuyaelewa
matatizo yake. Badala ya kujenga tabia njema, akajenga hisia za kisasi na uasi
dhidi ya mamlaka ya mzazi.
Aidha, mbinu nyingine tunayotumia wazazi
ni ile ya kuwapa watoto ‘mawaidha’ yanayoelekeza kile tunachofikiri wanapaswa
kukifanywa. Tunafanya hivi kwa nia njema ya kumjengea mtoto tabia iliyo njema.
Hata hivyo, utaratibu huu wa
kutegemea ‘mahubiri’ mara nyingi hauleti matokeo yanayokusudiwa. Mzazi wa namna
hii anaweza kushangazwa na usikivu hafifu anaokuwa nao mwanae. Kwamba pamoja na
mzazi kutumia muda mwingi kumwelekeza mwanae namna ya kuwa mtu mwema, akashangazwa
na matokeo. Mtoto anakuwa kinyume cha matarajio.
Changamoto ya kutegemea ‘mawaidha’
ni kuwa wakati mwingine hayafanikiwi kujibu matatizo halisi ya mtoto. Mfululizo
huu wa ‘mahubiri’ ya kimaadili una hatari ya kumfanya mtoto asione sababu ya
kuyafuatilia. Wakati mwingine mtoto hujikuta
anajenga upinzani wa kichini chini dhidi ya kile anachoambiwa.
Matokeo yanaweza kuwa mabaya zaidi
inapotokea mzazi haishi kile anachokifundisha. Hali hii humfanya mtoto akose
imani na maadili ‘yanayohubiriwa’ na mzazi. Kwa namna hii, mzazi anajikuta
akipoteza mamlaka yake kama mzazi mwenye sauti inayosikika moyoni mwa mtoto.
Mbali na kufunza maadili, wazazi
wengine hutumia mbinu ya kuminya uhuru wa watoto. Mzazi wa namna hii humlinda mtoto
kupita kiasi akifikiri kwa kufanya hivyo anamwokoa na hatari anazoweza kukabiliana
nazo. Mtoto anajikuta hana nafasi ya kuchagua zaidi ya kufuata kile kinachoamuliwa
na mzazi.
Moja wapo ya athari ya kuwadhibiti
mno watoto ni kuwafanya wakose uwezo wa kufanya maamuzi sahihi bila kutegemea
mwongozo wa watu wengine. Mtoto wa namna hii hawezi kuwa na maamuzi yanayoanzia
ndani yake. Hufanya kitu kwa sababu anafikiri ndicho kinachotarajiwa na
wanaomzunguka. Mtoto huyu anapopata uhuru, mathalani kwenda shule ya bweni, hugeuka
na kufanya mambo ambayo mzazi anaweza kushangaa kuyasikia.
Msingi wa makuzi ya tabia
Tukitaka kujenga tabia njema kwa
watoto wetu, tunahitaji mbinu tofauti. Tunahitaji kuchochea chemichemi ya tabia
zinazochipua kuanzia ndani. Tunahitaji mbinu zinazofanya mabadiliko ya tabia
yaanze mioyoni mwao na sio kuwafanya walazimike kufanya yale wanaojua
tunahitaji kuyafanya.
Tukitaka kumnyoosha mtoto awe na
tabia njema zinazoanzia ndani yake, tabia zitakazoambatana naye hata
atakapokuwa mtu mzima, tunahitaji kuanzia kwenye mahitaji yake.
Tunahitaji kumfanya mtoto ajione
anaeleweka. Tusipoweza kumfanya mtoto akajisikia anaeleweka, hatuwezi
kufanikiwa kumjengea tabia njema. Ili tuweze kumjengea hali ya kueleweka, tunahitaji
kuwekeza katika ukaribu. Ukaribu maana yake ni ule urafiki unamfanya mtoto
asijikie kuwa mtu wa thamani mwenye nafasi muhimu katika maisha ya mzazi wake.
Ukaribu huu, kati ya mtoto na mzazi wake, ndio msingi wa tabia njema kwa mtoto.
Inaendelea
Maoni
Chapisha Maoni