Unavyoweza Kukuza Tabia Njema kwa Mwanao -3
TUMEKWISHA kuona kuwa mtoto hakosi
adabu kwa bahati mbaya. Kila anachokifanya kina malengo yaliyojificha. Malengo
haya, kama tulivyoona, mara nyingi hayako sahihi. Ni mbinu tu za kutafuta
ukaribu na mzazi ambazo kimsingi zimejengwa kwenye tafsiri isiyosahihi.
Makala haya yanaangazia malengo mawili
kati ya manne yanayowafanya watoto waonyeshe utovu wa nidhamu. Kadhalika, tunaangalia
namna tunavyoweza kuuelewa ujumbe uliofichwa kwenye malengo hayo.
PICHA: ablf.tk |
Jambo la msingi la kuzingatia ni
kuwa unapoelewa ujumbe wa tabia ya mtoto unakuwa kwenye nafasi nzuri ya
kuchukua hatua sahihi zitakazomsaidia mtoto kurekebisha tafsiri, hisia na
maamuzi potovu aliyonayo.
Kutafuta usikivu
Wakati unaondoka nyumbani,
uliahidi kumletea mwanao zawadi. Ulifanya hivyo kama namna ya kuachana naye kirahisi.
Umerudi nyumbani usiku, umechoka na majukumu yako ya siku. Mwanao amekusubiri
kwa shauku kukuona. Mara unakumbuka, hukuja na zawadi uliyoahidi. Unamwomba
msamaha kirahisi kwa sababu hata hivyo, hukumaanisha ulichokisema.
Kichwani unafikiri namna ya
kukamilisha kazi zinazotakiwa kesho ofisini. Mwanao akiwa amekata tamaa anakuangalia
ukichukua kompyuta na kuelekea mezani. Unamwelekeza kuangalia kipindi cha
watoto kwenye televisheni ili akuche ufanye kazi zinazokusubiri.
Unapoanza kazi, mtoto anaacha
kipindi, anahamia kwako. Inakuwa bughudha. Unamwambia kwa upole arudi kutazama
televisheni kwa sababu, ‘baba ana kazi muhimu anahitaji kuimaliza.’ Unambusu na
kumwelekeza pa kwenda. Baada ya dakika mbili, mtoto anaanza kugombana na
mwenzake. Vilio na kelele. Unainuka kuamua ugomvi usioisha. Mtoto hanyamazi na
kazi yako haiendi.
Anachokifanya mtoto katika
mazingira haya ni kutafuta kusikika kwako. Anaamini humwoni kama mtu
anayehitaji kusikilizwa. Kwa hiyo, kukusumbua, kufanya vitu vya ‘kijinga’, kukung’ang’ania,
kudeka, kupiga kelele ni namna yake ya kutafuta usikivu usiompa.
Watoto huamini tabia hizi tusizozitaka
kama kudeka, kulia lia, kelele zitawaunganisha na wazazi wao. Wasichokijua ni
kuwa, kwa mzazi, tabia hizi ni utovu wa nidhamu. Una wajibu wa kuelewa ujumbe
uliojificha kwenye haya anayofanya mtoto.
Ujumbe wenyewe ni, ‘Ninakukosa. Naomba
uwe na muda na mimi.’ Mzazi anapoamua kumpa muda mtoto muda wake, mtoto
atajisikia kuwa karibu na mzazi na atajiona ni mtu mwenye thamani. Kulia lia,
kelele, ghasia, kudeka, kunaisha.
Ndio kusema, badala ya kumkasirikia
mtoto anayehitaji kuwa karibu na wewe, utamsaidia kwa kuacha unachokifanya na kumpa
usikivu.
Pengine umekuwa na mambo mengi. Hujatulia
nyumbani. Suluhu ni kuwa na muda wa kufanya mambo yanayompa ujumbe kuwa,
‘Ninakupenda. Ninakujali kuliko simu/kompyuta.’
Hiyo, hata hivyo, haimaanishi muda
wote uwe na mtoto. Hapana. Wekeza muda kwa mwanao unapopata nafasi. Weka
utaratibu atakaouelewa. Unaporudi nyumbani pata dakika chache za kujua
anaendeleaje. Fanya maongezi naye akiwa mwenyewe. Mtamkie maneno yanayomjenga.
Nenda na mwanao matembezini
mkafanye kile anachopenda kukifanya. Atajiona mtu mwenye nafasi muhimu kwenye
maisha yako na hatakuwa na sababu ya kuwa msumbufu.
Kulipiza kisasi
Amos ana miaka saba. Baba yake ni
mfanyabiashara na mama ni mtumishi wa serikali. Kwa kawaida, baba yake hutumia
muda mwingi kwenye biashara zake na mama pia husafiri mara kwa mara.
Wikiendi moja, baba anamchukua
Amos na mdogo wake kwenda matembezini.
Amos anabembea, anaogelea na kushiriki kwenye michezo ya kila namna.
Rebeca ni mdogo wake wa miaka mitatu. Hawezi kushiriki michezo mingi. Wakati
Amos anacheza, wazazi wake wanajitahidi kuwa karibu na Rebeca.
Baba anamrusha rusha Rebeca juu
huku mama akichekelea kwa pembeni. Amos anajifanya haoni lakini uvumilivu
unamshinda anaposikia Rebeca akiambiwa ni mzuri kuliko watoto wote.
Muda wa kuondoka umefika. Amos
haongei kwenye gari. Mama yake anajaribu kumsemesha lakini Amos anajifanya
hasikii. Njiani, unazuka ugomvi na mdogo wake. Baba anajisikia kukata tamaa
inakuwaje Amos anakuwa mgomvi.
Anamkumbusha Amos kuwa ni dhambi
kugombana na mdogo wake. Nyumbani hali ni hiyo hiyo. Amos amekasirika. Baba
anaamua kumchapa kwa kuwa na kisirani.
Tabia alizoonyesha Amos ni
kulipiza kisasi. Amos amekasirika kuona Rebeca ‘anamzidi kete’ kwa wazazi.
Kunyamaza, kugombana kunampunguzia maumivu yake kwa sababu anakuwa amelipiza
kisasi. Mtoto anayelipiza kisasi hutukana, hupigana, hudanganya, anaweza kuiba,
kuharibu vitu, na hata kuamua kushindwa kitu kwa makusudi.
Huenda umeshakutana na mazingira
kama haya. Mtoto anaweza kufanya kitu kinachokuudhi, kinachokatisha tamaa,
kitakachokusukuma kumwadhibu. Mtoto anapofanya tabia kama hizi, anajaribu
kusema moyo wake umeumia.
Unaweza kumwuumiza mtoto bila
kujua. Kuwa na matarajio makubwa kupita uhalisia kunaweza kumwumiza mtoto.
Unamfanya ajisikie, ‘Kwa hiyo baba inaonekana utanipenda pale tu nitakapofaulu
na kuwa malaika.’ Hisia hizo pekee zinaweza kuwa chanzo cha maumivu makubwa
moyoni.
Wakati mwingine, mtoto anakuwa
ameumizwa na mtu mwingine. Labda mwalimu shuleni amemwambia ‘Mjinga sana wewe.’
Anarudi na kisasi nyumbani. Maumivu ya kuambiwa ni mjinga yanamsukuma kuwafanya
wengine wajione wajinga kama yeye. Anapofanya hivyo, anajaribu kupunguza
maumivu ya nafsi yake.
Hulka ya mwanadamu ni kuwaumiza
wanaomwumiza. Mzazi anapoumizwa na mtoto mwenye kisasi, naye husukumwa
kumwumiza kwa kumwadhibu. Kwa juu juu tunafikiri tunamsaidia kurekebisha tabia.
Lakini adhabu tunayompa inamfanya mtoto aumie zaidi. Akiumia, ndani yake
anajenga hitaji la kutaka kulipiza kisasi zaidi.
Kuzuia mzunguko huu wa kisasi, ni
vyema kwanza kuelewa ujumbe uliojificha kwenye tabia mbovu anazozionyesha
mtoto, ‘Nimeumia; naomba uelewe hisia zangu.’ Mtoto anayejisikia kuumia analipa
kisasi kutafuta namna ya kusaidiwa kupunguza maumivu yake. Kwa mshangao wake,
mara nyingi, kinachotokea ni kinyume. Wazazi ‘humsaidia’ kwa kumwumiza zaidi.
Wakati mwingine, kumwumiza mtoto
kunaweza kuonekana kama ni kutatua tatizo. Mtoto anaweza kutulia kwa sababu tu
anaogopa kuumia zaidi. Lakini kufanya hivyo kunamfundisha kuwa wazazi
hawaaminiki. Mazingira haya ya kutokuaminika yanajenga ukuta kati ya mzazi na
mtoto hata kama kwa nje, mambo yanaweza kuonekana kuwa shwari.
Kwa ushauri elekezi kwa masuala ya malezi na makuzi niandikie: christianbwaya@gmail.com, 0754-870-815
Kwa ushauri elekezi kwa masuala ya malezi na makuzi niandikie: christianbwaya@gmail.com, 0754-870-815
Maoni
Chapisha Maoni