Tunayopaswa Kuyafahamu Kuhusu Shule za Msingi za Bweni
Katika
miaka ya hivi karibuni, shule za msingi za bweni zimekuwa maarufu. Kimsingi, si
tu shule za msingi, lakini hata shule za awali za bweni. Hivi sasa, miji karibu
yote katika nchi hii inazo shule kadhaa zinazopokea watoto wadogo na
kuwasomesha kwa mfumo wa bweni.
Takwimu
rasmi za hivi karibuni hazipatikani. Lakini kwa mujibu wa Wizara ya Elimu,
mwaka 2012 nchi yetu ilikuwa na shule za msingi zipatazo 684 zenye huduma ya bweni.
Shule hizi zinafahamika pia kama shule zinazotumia Kiingereza kama lugha rasmi
ya kufundishia, yaani English Medium, zikimilikiwa na watu binafsi au taasisi
zisizo za umma.
Kufikia
mwaka 2013, mikoa yote kwa Tanzania bara, isipokuwa Lindi ilikuwa na shule
hizi. Hata hivyo, mikoa inayoongoza kwa wingi wa shule za bweni ni Dar es
Salaam, Arusha, Kilimanjaro na Mwanza.
Ongezeko
kubwa la mahitaji ya shule hizi za bweni linaweza kuelezeka kwa sababu kadhaa.
Mosi, ni matarajio makubwa waliyonayo wazazi kwa elimu ya watoto wao. Ukubwa wa
matarajio hayo unachochea kufanyika kwa jitihada za kila namna katika kuhakikisha
kuwa watoto wanapata elimu bora pengine kuliko ile waliyoipata wazazi.
Kwa kuwa
mzazi angependa mwanae afanye vizuri kitaaluma, shule ya bweni inakuwa sehemu
ya jawabu mujarabu. Kwa kumpeleka mtoto kwenye shule ya bweni, mzazi anaamini huko
mtoto atajengewa mazingira ya kumsukuma kujifunza bila bughudha.
Aidha,
kuna suala la changamoto za kimalezi wanazokabiliana nazo wazazi. Migororo ya
kifamilia inayozorotesha mahusiano baina ya wazazi, huweza kusababisha uhitaji
wa shule ya bweni kwa nia ya kumlinda mtoto na matatizo yasiyomhusu. Katika
mazingira haya, inawezekana wazazi wasingependa kukaa mbali na watoto lakini
wakijikuta hawana uchaguzi mwingine bora zaidi ya kumpeleka mtoto katika shule
ya bweni.
Kadhalika,
yapo mazingira ambayo wazazi hawawezi kuwa karibu na watoto wao. Aina ya kazi
wanazofanya wazazi zinaweza kuwafanya washindwe kuwapa watoto huduma za karibu.
Katika mazingira ambayo wazazi wanalazimika kuwa nje ya familia kwa muda mrefu
kwa sababu za kikazi, shule ya bweni inakuwa mbadala wenye unafuu.
Shule
hizi, hata hivyo, zimepigwa marufuku kwenye nchi nyingi ikiwemo Rwanda. Hata
hapa kwetu, mwaka 2015, serikali kupitia Wizara ya Elimu iliwaonya wazazi juu
ya hatari ya kuwapeleka watoto wadogo kusoma kwenye shule za bweni. Hoja ni
uwezekano wa watoto hawa wadogo kiumri kupatwa na madhara anuai ya kitabia yanayotokana
na mazingira ya bweni. Tamko hili rasmi lilizingatia ukweli kuwa katika siku za
hivi karibuni kumekuwepo ongezeko kubwa la shule za bweni.
Tunapozungumzia
shule za msingi za bweni, kimsingi, tunazungumzia shule zinazopokea watoto
wadogo kuanzia miaka mitatu hadi 12 wanaotengwa na familia zao kwa lengo la
kuwapatia elimu inayokwenda sambamba na malezi.
Mtoto huyu,
kwa kawaida, hukabidhiwa kwa mamlaka za shule na hukaa mbali na familia yake
kwa muda unaoweza kufikia na hata kuzidi miezi saba kwa mwaka. Katika kipindi
chote hiki, mtoto huishi na watoto wenzake shuleni chini ya uangalizi wa walezi
na walimu. Wazazi na ndugu wanaotambuliwa na uongozi wa shule ya bweni
huruhusiwa kumtembelea mtoto.
Tafiti zilizofanyika
Hakuna
tafiti nyingi zimefanyika kuchunguza shule hizi katika mazingira yetu. Hata
hivyo, mwaka 2015 mwandishi wa makala haya alifanya utafiti katika shule hizi
za msingi za bweni. Lengo la utafiti huo uliokuwa sehemu ya tunuku ya kitaaluma
lilikuwa kulinganisha mazingira ya kimalezi katika shule hizo na yale ya
nyumbani wanakoishi watoto.
Watoto
waliokuwa wakisoma kwenye shule moja kwa mfumo wa kutwa na bweni wenye umri wa
miaka sita kwa darasa la kwanza na miaka saba kwa darasa la pili
walilinganishwa kwenye maeneo makuu manne kama ifuatavyo; umahiri wao kiakili
na kitaaluma kama vile uwezo wa lugha, kuhesabu, kuandika; tabia mahususi za
watoto mfano namna wanavyojiamini, mahusiano yao na wengine; aina ya malezi
wanayoyapata watoto na namna mazingira hayo yanavyowasaidia watoto kujenga
uwezo wa kujitegemea.
Itakumbukwa
kuwa katika siku za nyuma hapakuwa na utamaduni huu wa kuwapeleka watoto wadogo
kusoma mbali na familia zao. Tulizoea kuona watoto angalau wenye miaka kuanzia
13 na kuendelea wakipelekwa kwenye shule za sekondari za bweni. Mambo
yamebadilika.
Kama
tulivyokwisha kubainisha, pamekuwa na ongezeko la mahitaji ya shule hizi kwa
ngazi ya chekechea na madarasa ya awali. Hata hivyo, hakuna ushahidi wa
kiutafiti unaoweza kuwasaidia wazazi kufanya maamuzi sahihi wanapofikiria
kuwapeleka watoto wao kwenye shule hizi.
Utafiti
uliotajwa ulilenga kuchunguza kwa kiasi gani mazingira ya bweni kwa watoto
wadogo wa miaka sita na saba yanaweza kufanana au kutofautiana na mazingira ya
nyumbani ambayo wengi tunayafahamu.
Mazingira sisimushi
kitaaluma
Shule za
bweni zilizohusishwa katika utafiti huo zilionekana kuwa na mazingira bora
zaidi kitaaluma ukilinganisha na mazingira ya nyumbani wanakoishi watoto.
Upimaji wa umahiri wa watoto kiakili na kitaaluma ulionesha wazi kuwa, kwa
ujumla, watoto wa bweni walikuwa na uwezo mzuri wa kitaaluma.
Kwa
watoto wa miaka sita, ilionekana kuna tofauti kubwa kati ya watoto wa bweni na
wenzao wanaosoma kwa mfumo wa kutwa. Hata hivyo, tofauti hiyo ilikuwa ndogo kwa
watoto wa darasa la pili mwenye miaka saba.
Katika
kuchunguza sababu za tofauti hiyo, mambo kadhaa yalijitokeza. Kwanza, kuwepo
ratiba isiyobadilika kwa watoto wa bweni. Mtoto anayelala shule, kwa mfano,
alikuwa na uwezo wa kujua wakati upi anapaswa kufanya nini kuanzia anapoamka
mpaka anapokwenda kulala. Mtoto anayejua utaratibu anaopaswa kuufuata kwa siku
anakuwa na utulivu wa kiakili kuliko mwenzake asiyejua kitu gani kitafanyika
wakati gani.
Inaendelea
Ahsante sana Mr Christian Bwaya kwa makala hii
JibuFutaAhsante sana Mr Christian Bwaya kwa makala hii
JibuFuta