Siri za Watu Wanaotekeleza Maazimio ya Mwaka Mpya

TULIJADILI baadhi ya sababu zinazofanya watu washindwe kutekeleza maazimio wanayoyaweka kila mwaka mpya unapoanza. Tuliona sababu kubwa tatu; kuweka maazimio kwa msisimko tu wa kuingia mwaka mpya usioenda sambamba na tafakari ya kina; kuweka malengo mapana mno yasiyopimika; na pale malengo yanapohusisha mabadiliko ya tabia, kutokujua uliko mzizi wa mabadiliko hayo.
 Kwa kuwa utafiti unaoenesha ni asilimia 10 tu ya watu wanaoweka maazimio ya mwaka mpya ndio huyatekeleza, makala haya yanaangazia siri kubwa tano zinazotumiwa na watu hao wachache.

Melengo yawe mahususi

Usiweke malengo mapana yasiyolenga jambo mahususi. Vunja vunja wazo kuu ulilonalo liwe malengo madogo madogo yanayolenga jambo moja utakaloiishi kila siku.

Kwa mfano badala ya kuazimia kujenga tabia ya jumla kusoma vitabu, vunja vunja lengo hilo liwe kusoma kitabu kimoja kwa juma moja. Ukisema unalenga kujenga tabia ya kusoma, haieleweki unalenga kusoma vitabu vipangi kwa mwezi, miezi sita na hata miezi 12. Lengo la kusoma kitabu kimoja kila juma ni mahususi na utaweza kulitathimini.

Kama unataka kuwa na uhusiano imara na familia yako mwakani, fafanua kwa namna gani. Je, unataka kujenga mazoea ya kuwahi nyumbani kila siku baada ya kazi? Je, unataka kutoka na wanao kila mwisho wa juma? Fanya malengo yako yawe madogo madogo na yapimike kwa muda maalumu. Ukifanya hivyo, utaisaidia akili yako kujua kitu gani hasa kinakusudiwa na utaongeza uwezekano wa kutekeleza lengo husika.

Weka mfumo wa kupima utekelezaji wake

Utekelezaji wa malengo mengi, kwa kawaida, huhusisha mabadiliko ya tabia. Huwezi kubadili tabia usiyoweza kuipima. Hakikisha malengo yako yanapimika kadri unavyoendelea kuyatekeleza.

Ili uweze kupima, weka muda maalumu wa kuyatekeleza. Deadline. Andika malengo yako mahali ikusaidie kukumbuka. Malengo yasiyoandikwa yanabaki kuwa ndoto tu. Ndoto hazitekelezeki kirahisi.

Kama unalenga kupanua biashara yako kwa mwaka huu, fikiria utakavyoweza kupima upanuzi huo. Je, utatazama kiasi cha mtaji unaoongezeka? Je, ni kiasi cha bidhaa unachoouza, idadi ya wateja unaowapata? Utapimaje? Lazima uwe na utaratibu utakaokusaidia kupima unavyotekeleza malengo yako kadri muda unavyokwenda.

Waambie watu unaowaamini ulichopanga

Wakati mwingine ni rahisi kuachana na mipango uliyojiwekea kadri muda unavyokwenda. Sababu ni kutokuwa na mfumo wa kukuwajibisha pale unapoteleza. Ni muhimu kuwa na watu watakaokufanya ujisikie vibaya kuachana na mpango wako.

Baada ya kuhakiki malengo yako, fikiria watu wako wa karibu unaoweza kuwaambia kile ulichokipanga. Kama maazimio yako yanamhusu mkeo/mumeo, mshirikishe malengo yako mapema. Kama malengo yanawahusu wanao, waambie.

Kwa kufanya hivyo, unatengeneza mfumo wa kukuwajibisha pale unapoanza kususua susua.  Itakusaidia kuwa na hamasa ya kufanyia kazi malengo yao kuliko yanapokuwa siri yako mwenyewe.

Kadhalika, unapolenga kubadili tabia fulani usizozipenda waambie watu. Ikiwa unataka kuacha sigara, pombe au tabia fulani wanazozijua rafiki zako, tangaza wazi wazi. Waambie unataka kuacha sigara, pombe au uzinzi. Wanapojua mpango wako unajiweka katika mazingira ya kulazimika kutekeleza ili usionekane mtu wa maneno yasiyo na vitendo.

Muhimu kuzingatia kuwa watu wanaweza kuwa kikwazo cha malengo yako. Huwezi kuambatana na watu wanaoshabikia sigara, pombe na uzinzi na ukategemea ufanikiwe kuachana na tabia hizo. Amua kukaa mbali na watu wenye tabia unazolenga kuachana nazo.  Ambatana na watu wenye tabia unazotaka kuzijenga.

Kama unataka kuanza kusoma, jenga urafiki na watu wanaopenda kusoma. Kama unataka kuwa na familia imara, jenga urafiki na watu wenye familia imara. Kama unataka kuwa na mafanikio kitaaluma, ambatana na watu wenye ari ya kusoma. Watu wenye tabia unazotaka kuzijenga, watakusaidia kuwa na motisha ya kwenda unakotaka kwenda.

Usisubiri kesho, anza mara moja

Mara nyingi watu husahau malengo yao kwa sababu wanasubiri kuanza kesho. Wanaahirisha kwa sababu wanajifariji kuwa bado wanajipanga. Lakini kadri muda unavyokwenda, wanajikuta wakikosa hamasa.

Usisubiri kesho kuanza kufanya kitu sahihi. Anza mara moja. Kama lengo ni kuanza kusoma, kanunue kitabu leo anza kukisoma hata kama unafikiri huna muda. Muda haukusubiri, utengeneze. Azimia kutengeneza muda wa kusoma. Utaweza.

Kama unalenga kuongeza akiba kila mwezi, usisubiri mwezi ujao. Anza mwezi huu. Weka akiba kabla ya kufanya matumizi. Ukisubiri mwezi ujao, hutaanza. Ni rahisi kuahirisha kile usichoona sababu ya kukifanya leo.

Furahia hatua ndogo unayopiga

Huwezi kutekeleza lengo kubwa bila hatua ndogo. Jifunze kufurahia hatua ndogo unayopiga almuradi inakusaidia kuelekea kwenye lengo kubwa. Usisubiri utekelezaji mkubwa ili ufurahie.

Hata unapokwama, usikate tamaa na kughairi maazimio yako. Songa mbele. Kama unataka kupunguza uzito, usikate tamaa unapogundua uzito ndio kwanza unaongezeka. Furahia hatua yoyote ndogo unayopiga.

Watu wengi hujisikia vibaya wanapoona hawawezi kukiishi kile walichokipanga. Ili wasijisikie vibaya wanaamua kughairi mipango yao. Usiwe mtu wa namna hiyo. Wakati mwingine jirihusu kujisikia vibaya ili uwe na motisha ya kupambana kutekeleza malengo yako. Usikubali kujisikia vizuri kwa kuachana na malengo yako. Fanya maamuzi.


Fuatilia Gazeti la Mtanzania kila Alhamisi kwa Makala kama hizi.

Maoni

  1. Asante mkuu kwa makala nzuri imeniongezea uelewa

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?

Pay $900? I quit blogging