Changamoto ya kumpa 'mtumwa wa ndani' jukumu la malezi ya watoto

SIKU ZA NYUMA, familia zilikuwa tofauti na ilivyo leo. Akina mama walikaa nyumbani kulea watoto. Waliitwa mama wa nyumbani. Kazi yao kuu ilikuwa ni kuitunza nyumba kwa maana ya familia. Ni baba ndiye aliyekuwa na wajibu wa kutafuta mkate wa familia iwe kwa ajira, kujiajiri au namna nyingine.  Ilikuwa hivyo kwa sababu watoto wa kike walionekana si sawa na wenzao wa kiume. Hawakuwa na haki ya kusoma, na hivyo kujikuta katika mazingira ambayo hawakuwa na uchagazi mwingine zaidi ya 'ajira' ya kutumika nyumbani. Ndivyo ilivyokuwa katika jamii nyingi hasa barani Afrika.

Leo hii mambo yamebadilika. Wanawake wanahitaji, na kwa kweli wanastahili haki na fursa ya kama ilivyo kwa wanaume. Hii leo, watoto wa kike wanasoma sana. Sawa na, hata zaidi ya, watoto wa kiume. Na matunda ya fursa sawa kwa wote kielimu, yamekuwa ni fursa sawa kiajira pia. Haki zimekuwa sawa. Sasa hivi hata waajiri wametambua kuwa akina mama wanaweza. Akina mama ni waaminifu. Wanashika madaraka makubwa makazini, na wanafanya vyema, tena mara nyingine kuliko wanaume.

Afrika imeshuhudia wakuu wa nchi wanawake. Nchi mbili zimeongozwa na akina mama. Mashirika makubwa yenye heshima, yameongozwa kwa mafanikio na akina mama. Nje ya Afrika, kadhalika, wapo akina mama wengi walioshika nafasi za juu katika nchi na mashirika yanayoheshimika kimataifa. Na wamethibitisha kuwa wanaweza. Imani kwa akina mama imeongezeka. Kwa hiyo ni wazi kuwa jitihada za kuwawezesha wanawake zimezaa matunda.

Changamoto za kimalezi zinazojitokeza

Katika mazingira ambayo mama huyu anayelazimika kufanya kazi nje na nyumbani kwake na anao watoto/mtoto wa kumlea,  zipo changamoto kadhaa zinajitokeza. Iliyo kubwa zaidi ni malezi ya watoto hao in their absence. Ni utaratibu upi utatumika kumpa mtoto malezi yanayostahili, wakati huu ambapo mama, kama alivyo mwanaume, analo jukumu jingine la kumridhisha mwajiri, kwa mfano?

Katika kujaribu kutatua changamoto hiyo, akina mama wengi waajiriwa, hasa Afrika, huchagua njia kuu mbili katika kuhakikisha kuwa watoto wao nao wanapata huduma bora za kimalezi wanazostahili wakati mama wako wakiwa kazini.

Moja, ni kufanya utaratibu wa kumtumia mtu mwingine mbali na yeye mama atakayewaangalia watoto. Hapa kuna baba mwenye nyumba (sijui ni wangapi wanaweza kuchukua jukumu hili?), akina dada wa kazi (mahausigeli), ndugu wa damu wenye muda wa kumwangalia mtoto, au akina mama wa kukaa na mtoto kwa muda wa mchana. Hizi zote twaweza kuziita huduma zisizo rasmi kwa malezi ya mtoto kutokana na ukweli kwamba hazitolewi na watu wenye ujuzi wa malezi na makuzi ya mtoto. Ndizo, hata hivyo, zinazotumiwa na wengi shauri ya unafuu wake.

Pili, ni utaratibu wa kumpeleka mtoto katika vituo vinavyotoa huduma ya kulelea watoto kwa makundi kwa muda wa mchana. Katika utaratibu huu mama humkabidhi mwanae kwa mlezi mtaalamu kuanzia asubuhi na humfuata mtoto huyo jioni/mchana baada ya kazi. Huduma hizi zina tofauti tofauti kulingana na umri wa mtoto ikiwa ni pamoja na shule za awali (ukiacha malezi, mtoto hupatiwa elimu), shule za kulala (kwa watoto wa kuanzia darasa la kwanza) na huduma nyinginezo kadhalika. Zote hizi tunaweza kuziita huduma rasmi za malezi ya mtoto zitolewazo kwenye vituo vinavyoeleweka na kutambuliwa kisheria.

Huduma zisizo rasmi za malezi ya mtoto

Kama tulivyotangulia kusema hapo awali, huduma hizi si rasmi kwa sababu zinatolewa na watu wasio na utaalamu wala ujuzi unaotambulika rasmi. Ni huduma za kimazoea.

Kwanza kabisa, tuna ma-house girl. Hawa ni watoto au vijana wadogo ambao wamekulia katika mazingira ya kawaida, ambayo mara nyingi hayawafanyi kuelewa thamani ya malezi ya watoto au basi wakielewa, hawajui wafanyeje. Ni watoto wasio na elimu na ari ya kazi shauri ya kugombezwa na akina mama waajiri ambao mara nyingi huwa na matarajio makubwa kuliko kile wanachoweza kukifanya wao kama watoto. Hivyo hali ya kutokuelewana kati ya mama mwajiri na mtoto huyu wa kazi husababisha hasira, uchungu na visasi ambavyo, kwa masikitiko, huishia kwa mtoto asiye na hatia.

Ni bahati mbaya pia kwamba matarajio yetu hujenga tabia. Na bahati mbaya nyingine ni kwamba hatujishughulishi kujenga mahusiano mema na akina dada hawa na kuwafanya wajisikie kuwa sehemu ya familia. Mfano, wazazi huweza kutoka kimatembezi na watoto wao na kumwacha dada wa kazi akishughulika nyumbani. Kusahau kuambatana na binti wa kazi, ambaye kwa wazazi, anaonekana kuwa mfanyakazi asiye sehemu ya familia, hujenga hisia kwamba binti huyu si sehemu ya familia. Tunawafanya wajione kama watumwa.

Ni kawaida ukasikia akina dada hawa wakifanya kazi zaidi ya masaa 18 kwa siku. Ni wa kwanza kabisa kuamka, na huenda wakawa wa mwisho kulala. Wanachoka na bado tunawakemea na kunyanyasa, kwa sababu tu hawafanyi yale ambayo kiukweli hatujawaelekeza, na ukiongeza kutokutabirika kwetu kuwa tunataka nini, misuguano haiwezi kukwepeka.

Ndio maana visa vya akina dada hawa kuteswa na kuumizwa vimekuwa vikisikika mara kwa mara kwenye vyombo vya habari. Badala ya akina dada hawa kuwa watoa huduma ya malezi majumbani kama ilivyotarajiwa, wamejikuta wakiwa wahanga wa biashara ya usafirishaji wa binadamu.
Yusta Lucas, mfanyakazi wa ndani mhanga wa utesaji. Picha: Matumizi ya umma

Kwa upande mwingine, wapo akina dada wa kazi za ndani wanaosemekana kuwafundisha watoto tabia zisizofaa, na hata kuwatendea mabaya watoto, pengine kama njia ya kulipiza kisasi kwa waajiri wao au bila wao kujua. Wapo watoto waliofundishwa uchoyo, kutokuheshimu wengine na kadhalika, bila wazazi kujua. Hili hutokea kama matokeo ya kulelewa na wasichana ambao kimsingi hawajui namna nyingine zaidi ya kuwa wachoyo, kutokuwa na heshima na kadhalika. Wengine tunaambiwa, wamekuwa na mahusiano na baba wa watoto wanaowatunza nyumbani. Si habari ambazo yeyote angependa kuzisikia.


Shauri ya hayo, pengine ndio sababu wengine wanaamua kuishi na ndugu (mtoto wa shangazi, mjomba, dada, kaka na kadhalika) anayeonekana kuwa anaweza kuishi na mwanao kuliko huyu asiye binti asiyejulikana amekulia wapi na nani na anatabia zipi zisizojulikana wazi. Wazazi huona ni rahisi zaidi kumchukulia ndugu wa damu kama sehemu ya familia kuliko akina dada wasiojulikana wamekulia wapi. Lakini hata hivyo, mazingira ya kuishi na ndugu atakayekusaidia kumlea mwanao, yameanza kubadilika kwa kiasi kikubwa.

Mfumo wa kale wa kuishi na 'extended family' umeanza kupotea. Maisha hayaruhusu. Ndugu hawa wanahitaji kusoma. Na mara nyingine wanakuwa na madai makubwa tunapoishi nao. Matokeo yake, pamoja na kwamba tunaweza kuwafahamu zaidi kuliko 'mahausigeli', na kwamba wanaweza kuwa na huruma na rehema kwa wanetu tunapokuwa makazini, bado inaonekana kuwa gharama halisi za kuishi nao ni kubwa kuliko kuishi na mtu asiye ndugu.

Ninamkumbuka mama mmoja aliyekabiliana na changamoto ya kupishana na mtoto wa ndugu yake. Kwake, ni afadhali kupishana na dada wa kazi asiye ndugu badala ya mtoto wa shangazi, mjomba, dada au kaka. Anasema, unapotofautinaana na mtoto wa dada yako, shauri ya mambo madogo madogo ya kifamilia, anaweza kuyapeleka kwa ndugu, na hivyo tofauti zenu zikavuka mipaka zaidi na kuathiri mahusiano ya kifamilia. Anasema, wakati mwingine, kupishana hutokea kwa sababu ya matarajio makubwa anayokuwa nayo ndugu, kuliko uhalisia.

Ndio maana wengine wanaamua kuwatumia akina mama wanaofahamiana nao, uchaguzi wenye faida zake pia. Hawa ni akina mama ambao pengine wanalea watoto wao nyumbani, yaani ni mama wa nyumbani wanaoweza kufika nyumbani na kukaa na wanao kwa makubaliano maalum. Kwanza hulazimiki kuwa na makubaliano magumu, nje ya kuwekeana muda maalumu wa yeye kumwangalia mwanao hasa nyakati za mchana. Mama anaporudi kazini, basi muda wa kazi wa mama mlezi, unakuwa umeisha. Na faida nyingine ni uzoefu wa malezi anayoweza kuwa nayo mama huyu kuliko binti mdogo aliyetoka kijijini.

Hata hivyo, changamoto yake ni kuwapa akina mama wanaoweza kufanya kazi hii kwa makini bila mafunzo yoyote rasmi. Gharama zao zaweza kuwa kubwa kuliko zinazoweza kudaiwa na binti wa kazi, wakati ni kweli pia hawana mafunzo yanayoweza kukuhakikishia malezi yanayotarajiwa.

Tunawezaje kuboresha huduma hizi ziweze kutufaa?

Changamoto hizi za huduma za malezi yasiyo rasmi, zinawafanya akina mama wengi kuwa na mashaka nazo. Wengine wanaona bora kuwapeleka watoto wao kwa babu na bibi. Kwa siku za leo, inaonekana kwa wengi kuwa si busara kufanya hivyo. Uelewa wa malezi unawafanya wazazi wengi kutaka kukaa na watoto wao na hivyo kuwa na fursa ya kuwafundisha yale wanayodhani watoto wao wanayahitaji. Kumpeleka mtoto kwa babu au bibi, kwa wengi ni sawa na kuchukulia kirahisi suala la malezi ya mtoto uliyemzaa kwa hiari yako. Kwa hiyo, kutokana na ukweli kwamba huduma za malezi rasmi ya watoto kwenye vituo maalumu ni za gharama ya juu, akina mama wengi wanakuwa kwenye wakati mgumu.

Katika mazingira ambayo huduma hizi zisizo rasmi hazikwepeki, iwe kwa gharama au vinginevyo, pengine ni muhimu kujadili namna gani tunaweza kupunguza uwezekano wa kumfanya msichana wa kazi kujisikia mtumwa mwenye jukumu nyeti la malezi ya watoto. Je, tunaweza kuwafanya akina dada wa kazi za ndani kutulelea wanetu pasipo kuwa na visasi, hasira na hata ukatili kwa wanetu? Vipi mapendekezo haya?

 1. Kufahamu historia ya binti. Ametoka familia gani, aliishi vipi na familia yake, misimamo yake, imani, angalau mambo ya msingi. Hayo yanawezekana ikiwa tutampata kupitia watu tunaowafahamu vizuri na ndio watakaotusaidia kupata habari za msingi za familia yake. Si busara kuishi na mtu asiyefahamika vizuri kwa kisingizio cha 'ntamjulia wapi huyu?' Faida ya kumfahamu vizuri binti, tena kwa mapema, ni kuwa na wakati mzuri wa kuamua ikiwa anatufaa ama la. Tunapomfahamu, ni rahisi kumwelewesha misimamo ya familia yetu ili apate kujue anakaa na watu wenye mtazamo gani. Kuishi na binti asiyeelewa misimamo na itikadi za familia husababisha kutokutabirika kwa misimamo yetu na huu ndio msingi wa mitafaruku isiyo ya lazima.
 2. Kumfanya ajue anachotakiwa kukifanya. Kumwelekeza matarajio yetu sisi kama wazazi wa mtoto. Tumpe ratiba na utaratibu unaoeleweka. Ni sawa na job discription tuliyopewa na mwajiri tulipoanza kazi au kupandishwa cheo. Pengine si busara sana kutegemea kutoa maelekezo yasiyoisha kila siku wakati mwingine kwa njia ya simu. Chukulia mfano mama aliye kazini, anayewasiliana na binti kila dakika kutoa maelekezo ambayo angeweza kuyatoa kabla ya kuondoka nyumbani na yakaeleweka: "Mtoto ameamka? Amenawa? Umempigia mswaki? Amekunywa maziwa? Umemvalisha nguo?...halafu uhakikishe hajichafui...kumbuka..." Maelekezo mengi tena yale yale kila siku yanayochosha na ni kero kwa mabinti hawa. Matokeo yake, binti hafanyi anachopaswa kufanya, ama kwa makusudi au kwa kuzidiwa na majukumu mengi yasiyoeleweka sawia matokeo yake ni mitafaruku.
 3. Kujenga mahusiano mazuri na binti. Wazazi, hasa mama, wanawajibika kumfanya binti wa kazi kuwa sehemu ya familia. Ajisikie kupendwa kwa dhati. Wazazi wawe na mtazamo kuwa binti si mfanyakazi bali msaidizi wa kawaida, mwenye hadhi ya mtoto wa familia. Na kufanya hivyo si kumpendelea. Hakuna haja ya kuwa na wasiwasi na kuogopa kumpa heshima hiyo. Haitupunguzii lolote. Unaonaje wageni wanapotembelea hapo nyumbani ukamtambulisha 'mdogo wangu huyu...ananisaidia sana kazi hapa nyumbani' na yeye akisikia? Matokeo yake yanaweza kuwa makubwa ikiwa atalinganisha na namna tunavyomtendea kama binadamu hapo nyumbani. Fikiria anaweza kujisikiaje anapojiona kuwa sehemu ya picha rasmi za familia zinazoning'inia ukutani? Hakuna binadamu mwenye roho ngumu kiasi cha kutokujisikia vizuri anapoona watu wanamthamini kwa dhati kiasi hicho!
 4. Kumpa huduma anazostahili. Pamoja na kujitahidi kumlipa mshahara wake kwa wakati, si vibaya kwa sisi wazazi kumpa huduma nyinginezo zinazoweza kumfanya akaziona kama marupurupu. kwa mfano kumtengenezea utaratibu wa kwenda shule, ikiwezekana. Kuhakikisha anaelimika. Kumpa zawadi, angalau kama tunavyowapa wanatu. Ni wazi kuwa hata sisi, tunatarajia kupewa huduma tunazostahili na waajiri wetu. Tunatarajia kupewa 'na mengineyo' na waajiri wetu. Kwa nini hatufanyi vivyo hivyo kwa mtu anayetuwezesha kutekeleza majukumu yetu, na kubwa zaidi kukaa na mtoto wetu tena kwa muda mrefu kuliko sisi?
 5. Kuonesha mfano mzuri. Hatuwezi kutarajia binti wa kazi aishi vizuri na watoto, wakati sisi mwenyewe hatuoneshi kuwajali watoto tukiwepo nyumbani. Tuoneshe thamani ya malezi kwa vitendo. Tuoneshe kwa vitendo namna tunavyotarajia mtoto anapaswa kuhudumiwa. Binti atajifunza kwa vitendo. Hakuna sababu ya kuwa na hasira zisizo na sababu. Hakuna haja ya kufoka ili kudai kueleweka. Tusiache kufanya majukumu yanayotupasa kama akina mama tuwapo nyumbani. Tuache uvivu. Tupike, tutenge chakula mezani, tufue nguo za watoto na waume zetu ikibidi. Haipendezi kukwepa majukumu tunayoyaweza sisi wenyewe kwa kisingizio cha kuwepo binti wa kazi. Binti atatuheshimu na uwezekano wa matatizo mengine unaweza kupungua.
 6. Tuwapo nyumbani tutumie muda wa kutosha na mtoto.  Binti wa kazi amelelewa kwenye mazingira tusiyoyajua, hata kama tunaweza kuwa na taarifa kadhaa za kujua alikokulia. Pasipo yeye kujua, tena bila makusudi, dada wa kazi anaweza kujikuta akipanda mbegu isiyofaa kwa wanetu. Ni vizuri kuhakikisha tunafuatilia maendeleo ya kitabia ya wanetu mara tunaporudi nyumbani. Na tunaweza kufanya hivyo kwa kujenga mahusiano ya karibu na wanetu kama tulivyowahi kujadili katika makala hii iliyopita. Tukumbuke, anayetumia muda mwingi na watoto wetu, ndiye mwenye uwezo wa kuwekeza anachotaka kwenye akili zao. Tusiruhusu binti wa kazi ajenge pendavyo mwenye moyo wa mtoto, kwa sababu tu sisi mwenyewe hatutumii muda wa kutosha na mtoto.

Kusema hayo, hatujihakikishii kwamba lazima binti wa kazi atakuwa mkamilifu tena mara moja. Lakini angalau tunaweka mazingira ya kufahamu kama tatizo ni binti mwenyewe au ni sisi ndio wachangiaji wa mzunguko wa tatizo. Naelewa, wapo mabinti wamekulia katika mazingira yaliyowafanya wakawa watu wasioridhika. Naelewa kuna watu unaweza kuwapenda kwa dhati na kuwahudumia lakini wasitambue. Lakini vile vile, naelewa, kuyafanya haya angalau kutasaidia kuelewa mzizi hasa wa tatizo.

Hata hivyo, changamoto za huduma hizi zisizo rasmi za malezi, ndizo zilizowasukuma akina mama wenye uwezo kuamua kuwapeleka watoto wao kwenye vituo rasmi vinavyotoa huduma za malezi ya watoto. Katika makala yanayofuata tutatazama kwa kina huduma hizo kuona faida na hasara zake.

Maoni

 1. Majibu
  1. Asante sana Nuru kwa kutembelea humu. Karibu tena!

   Futa
 2. ahsante christian.ni kweli tufanye kazi kupunguza.ila ujue watu wengi tumeajiriwa lakini hatuna mafunzo ya kuwa waajiri.mtu aamatendea mfanyakazi wake kama ambavyo akifanyiwa analalaika au kuandamana.kumbuka hawa hawana motisha,wala.safari,wala training,wala kupandishwa cheo na watu wachache sana wana wapa jd,mkataba na benefits zingine, hawana muda wa kazi,na muda wa kupumzika,au kukutana na marafiki,yet hata kima cha chini hawapewi ...ungekuwa wewe uko hivo kazini kwako ingekuwaje?

  JibuFuta
 3. Albert. Nakubaliana na mtazamo huo. Wengi wetu hatujaweza kuwa na sifa za waajiri. Tutakapoweza kuelewa mahitaji yao kama binadamu na kuwatendea kama tunavyotaka kutendewa sisi, naamini tutaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa matatizo yanayotokana na akina dada hawa.

  JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mambo ya Kuzingatia Unapoandika Wasifu wa Kazi (Curriculum Vitae)

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Fumbo mfumbie mwerevu

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3