Blogu inavyosaidia kujiona unavyokua na kubadilika

Nilianza kublogu mwaka 2005. Takribani miaka tisa. Wakati huo nilikuwa kinda. Kijana mdogo. Blogu kwangu ilikuwa kama sehemu ya kusema ninayofikiri bila kuhofu.

Nimekuwa na utaratibu wa kurudia niliyowahi kuyaandika enzi hizo. Wakati mwingine ninacheka. Ninaweza kuona namna mtazamo wangu ulivyokuwa ukibadilika hatua kwa hatua hasa katika masuala ya dini na imani.

Watu hutarajia mwandishi asibadilike. Maana kwao, mwandishi ni mlishaji. Hajifunzi. Mimi si mwandishi. Ni mwanablogu. Tofauti ya mwandishi na mwanablogu ni kwamba, wa pili anaingiliana sana na hao anaowaandikia. Anajifunza. Anabadilika. Mtazamo unabadilika. Wa kwanza sina hakika na yote hayo.

Kwa hiyo, ninafurahia kubadilika. Zamani nilikuwa mbishi. Niliona raha kusumbuana na wabishi wenzangu. Siku hizi sibishani sana. Ninasikiliza zaidi. Zamani nilikuwa mwongeaji. Siku hizi nimekuwa na aibu. Nina haya. Yote hayo ni mabadiliko. Yawe chanya ama hasi. Lakini bado ni mabadiliko.

Kufikia miaka ya 2010 hapa kumefumuka mitandao mingi ya kijamii. Micro-blogging. Zimekuwa maarufu sana. Mtumiaji haitaji kutumia muda mwingi kupangilia maneno kama ilivyo, mara nyingi, kwenye blogu. Sentensi moja inaweza kutosha kufikisha ujumbe. Hiyo ni moja wapo ya sababu ya kupendwa sana kwa mitandao hiyo. Urahisi wake kwa mwandishi na anayesoma.

Kuna kila dalili kuwa blogu zimeonekana kuwa kazi ngumu isiyo na faida. Watu wamehamia kwenye micro-blogging. Jambo jema.

Miye nimeamua kujikita kwenye uwanja huu nilioanza nao nikiwa kijana mteke miaka hiyo tisa. Naamini umuhimu wa blogu haujaisha. Bado tunahitaji maarifa zaidi katika blogu ambayo ni nadra kuyajadili kwenye mitandao mingineyo ya kijamii inadai sentensi moja.

Sikuwahi kuhama blogu. Na sitahama. Mara zote nimekuwa kwenye blogu ya Global Voices inayoendeshwa na watu wengi. Nikaamua kuweka nguvu zangu kule kukuza kiswahili mtandaoni. Hata hivyo, nimeona ninaweza kupangilia muda wangu vyema ili nami niweze kusema niliyo nayo kibarazani kwangu.

Nimeyasema hayo yote kukubaribisha upya. Karibu tujadili. Siamini katika kujaza maarifa. Naamini katika maswali na majadiliano. Ingawa, inapobidi, huenda nikasema hili na lile. Yote ni katika kujadiliana. Tumerudi.

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Fumbo mfumbie mwerevu

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3

Pay $900? I quit blogging