Kanuni muhimu za kuwa baba anayejua wajibu wake

Da'Subi wa blogu maarufu ya habari wavuti.com ameweka makala yenye kanuni muhimu kwa wale wanaotaka kuwa akina baba bora. Makala hiyo iliandikwa awali kwa Kiingereza na Leo Babauta ambaye amekuwa baba kwa miaka 21 na ana watoto sita.

Leo anayataja mambo matano muhimu ikiwa unataka kuwa baba anayejua wajibu wake kwa watoto wake. Hapa tumeyaeleza kwa ufupi kwa lugha ya Kiswahili:
  1. Upendo. Huu ndio wajibu mkuu kuliko wajibu wowote unaoweza kuwa nao kama baba. Anasema kuwapa chakula, malazi, mavazi ili wakue, si kazi ngumu. Kazi ni kumfanya mtoto ajisikie kupendwa, hali ambayo ndiyo itakayofinyanga tabia yake ukubwani. Kipimo cha mafanikio ni ikiwa unaweza kumfanya mwanao ajisikie kupendwa,
  2. Kuwa mfano. Maisha unayoishi yana maana kubwa kwa wanao kuliko maneno unayowaambia. Unachofanya ndicho kinachochukuliwa serious. Ukizoea kuwaadhibu, ndicho wanachojifunza. Ukiwabana sana, hawajifunzi kutushirikisha walivyonavyo. Kama unataka wanao wale chakula bora, anza wewe. Ukitaka wasome, onyesha mfano.
  3. Wakumbatie. Ni bora kuwakumbatia kuliko kuwaadhibu. Kwanza ni njia nyepesi ya kuonyesha upendo. Hiyo haimaanishi hawakosei, maana hata sisi tunakosea. Tunawaadhibuje wao, ikiwa sisi hatungependa kuadhibiwa? Anasema, njia bora ni kuwa mwelewa. Kuvaa viatu vya mwanao. Fikiri nini kingesaidia, jadilini tatizo lilivyo, kuliko kukimbilia kuadhibu. Badala ya kukazania ubaya, onyesha mtu mwema anapaswa kuwaje.
  4. Waamini. Waache wajaribu na washindwe. Onyesha kwamba kukosea ni sahihi vilevile, na kujaribu ni sawa. Usiwafanye waogope kujaribu kitu. Ukifanya hivyo, watakuwa mazezeta. Onyesha kutokuogopa kushindwa wewe mwenyewe, waelewe kushindwa ni sehemu ya majaribio. Ukiwaamini watajiamini. 
  5. Wape fursa ya kuwa wanavyotaka kuwa. Usitake unachotaka wewe ndicho wawe wao. Wewe ni wewe, na watoto wanacho wanachopenda wao. Mwache mtoto ajipambanue kwa njia yake. Afanye chaguo lake mwenye, makosa yake mwenyewe, na wewe msaidie kihisia. Cheza michezo yao ya kitoto. Toka nao. Zungumza nao. Wasimulie hadhithi. Fuatilia wanavyovipenda iwe muziki, dansi, na kadhalika.
Asante sana Da'Subi kwa hekima hizi.

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3

Pay $900? I quit blogging

Fumbo mfumbie mwerevu