‘Vijana waache kutumiwa’

JINA LA KAMALA si geni kwa wanablogu wengi. Yeye ni mwendeshaji wa blogu maarufu inayojadili (pamoja na mambo mengine) masuala ya kiutambuzi. Bonyeza hapa kuitembelea. Ndugu Kamala anajulikana pia kwa namna yake ya utoaji maoni huru katika blogu anazozitembelea ambayo hufikirisha na mara nyingine kuibua mijadala zaidi.
Blogu hii ilipata fursa ya kuzungumza naye siku chache zilizopita kuhusu falsafa zake, blogu, dini, siasa na mambo yake binafsi. Karibu kujua zaidi kuhusu mwanablogu huyu anayeblogu kutokea kanda ya ziwa.


________________________________________

Ndugu Kamala, nashukuru kwa kukubali kutumia muda wako ili tuweze kujadiliana masuala mawili matatu. Labda tuanze na falsafa yako binafsi. Unaamini nini katika maisha ambacho ndicho kinachobeba utambulisho wako kama Kamala?

Naamini katika utu, ubinadamu, upendo na umoja. Napenda kuelewa vitu na kudadisi na ndio maana natumia majina ya kihaya tu ninayoelewa maana yake na kwa nini yawepo… napenda kuacha maisha yaende na kufurahi muda wote

Falsafa nzuri. Umetoa mfano wa majina ya kihaya kwa dhana ya udadisi. Nini tafsiri ya majina yako mwenyewe? nakumbuka kuna siku ulisema mahali, ila pengine wapo wasomaji hawapata maana hiyo kule….

Kamala maana yake ni msuluhishaji, anayeyamaliza. Lutatinisibwa ni jasiri asiyetishika, jina hili limeongezwa madoido kadhaa ambayo hata hivyo siyo ya msingi saaana ila kama ulivyo utamaduni wa wahaya hupenda kujisifia na kujikweza. Lutabasibwa ni jasiri mwenye nguvu asiyewezekanika kumbuka majina mengi ya wahaya ni ya kibabe.

Bila shaka maana yake, huwezekaniki na ni jasiri. Tuje moja kwa moja katika suala la blogu zetu. Unasoma blogu ngapi kwa siku/wiki?

Kwa kweli sina idadi kamili…nasoma blog nyingi kufuatana na muda au ufikiwaji. Kwa hiyo najitahidi kusoma nyingi sana niwezavyo kwani napenda kupitia, ila napenda blogu zenye kufikirisha zaidi na zile za mambo ya kiroho na utambuzi

Kwa faida ya wanablogu, unadhani tunawezaje kujikita katika kufikirisha zaidi katika hali ambayo utamaduni wa kufikiri haujawa sehemu ya jamii yetu (yaani tunapenda kusoma habari nyepesi nyepesi zaidi)?

Ni kwa kutokuwa na upande na kuwa na maoni yetu. Kusimamia tunayoyaamini bila kufungwa na upande wowote…kuwa watu wa kijifunza kwa kusikiliza sana na kupenda kujifunza kutokana na mazingira; kusikiliza maoni na mitizamo ya wengine…kujisomea na kuwa na tabia ya kudadisi na kuhoji. ni lazima kuwa wabunifu. Tunahitaji kuwa watu wa kusimamia ukweli wa fikara zetu hata kama ni mchungu kwa wengine au kwetu pia.

Mara nyingine umekuwa ukipotea potea kwenye kijiwe chako pale. Je, ni makusudi?


Sio makusudi. Ni kwa sababu ya safari yaani kuwa mbali na mtandao lakini na wingi wa shughuli za kila siku…huwa nasikitika kwahilo.

Tumeona sasa wanablogu wameanza kukutana. Juzi hapa wapo wenzetu watano walifanikiwa katika hilo. Je, kuna mwanablogu yeyote umewahi kukutana naye uso kwa uso tangu umeanza kublogu? Ilikuwa wapi?

Nimekutana na wanablogu kadhaa kwa nyakati tofauti kama vile Kaluse, Dalali, Tandasi, Mjengwa wote jijini Dar Es Salaam, lakini nimekutana na Chacha Wambura, Strictly Gospel mjini Musoma kwa wakati mmoja mwezi April 2010. Nafanya juhudi za kuwasiliana na wengine na ndio maana niwapo katika mji wowote huwa najitangaza ili kama wapo tutafutane na napanga kufanya juhudi zaidi za makusudi...nafikiria pia ni jinsi gani twaweza kukutana soote kwa pamoja. Ni ndoto ambayo itatimia tu siku moja.


Hapa akiwa na mwana wa mwanablogu mwenzetu | Picha kwa hisani ya Kamala

Safi sana. Hongera kwa kukutana na wanablogu wengi kiasi hicho na bila shaka ndoto yako ya wanablogu wote kukutana i mbioni kutimia. Sasa kwa idadi ya blogu za Kiswahili tulizonazo mpaka sasa, unadhani tumepiga hatua yoyote? Kwa kiwango gani?

Hatua tuliyopiga ni uhuru wa mwandishi kutoa habari aliyonayo. Kwa hiyo kila mwenye blogu atakacho kutoa hukitoa bila urasimu wowote na hivyo uhuru wa maoni au habari upo japo kiwango bado kinakutana na ukosefu wa internet kwa wa-Tanzania walio wengi ila angalau taarifa zinaandikwa na historia zinarekodiwa.

Je, unadhani blogu zetu zina upungufu wowote ule? Kwa maoni yako, tunawezaje kuboresha zaidi blogu zetu.

Tunahitaji kuamini katika uhuru zaidi wa kuwa huru bila kuegemea upande, tusitoe kibubusa (dogma) bali tuwe huru na kuvutia wasomaji huru ili kuleta dhana ya uhuru wa maoni. Tujisikie kuwa na deni kwa wasomaji wetu na hivyo tuache kupotea kwenye blogu zetu, tujitahidi kuwepo kwani wasomaji wanatutegemea.

Tuje kwenye blogu yako mwenyewe, nini hasa falsafa kubwa/kipaumbele cha blogu yako?

Ni kujitambua, kuleta mawazo huru, kujiuliza maswali magumu na kuleta mfumo mpya wakufikiri na sio kuacha watu wachache watusaidie kufikiri.


Kuhusu mfumo huo mpya wa kufikiri unaoungolea, wapi pa kuanzia?


Kujitambua, kujibainisha, kujua nafasi yetu na kutokuwaachia watu wengine watusaide kufikiri. kudadisi na kuhoji kila jambo. Kuwa na mada zenye kufikirisha zenye kuleta mitizamo mipya na zinazochokonoa fikra zaidi kwenye blogu zetu. Ni lazima tutizame mambo katika uhalisia wake. Tahajudi yaweza kusaidia katika hili.

Una maoni gani kwa anonymous na dhana ya uhuru wao maoni? Kuna watu wanakuwa na mashaka na umuhimu wao katika blogu; wanasema kwa nini mtu mwenye mawazo yanayojenga akimbilie kujificha kwanza ndio aseme? Una maoni gani na hili...

Anony!! kuna wakati wanaonekana kuchanganya au kakera na hata kushangaza labda, Lakini unaposema maoni yanayojenga, unamaanisha nini?? nani mwenye mamlaka ya kujua kuwa maoni fulani yanajenga??mtoa maoni (akiwemo anony) au msoma maoni (mwenye blogu)?? Lakini je, wewe hujawahi kuwa anony?? Naamini katika uhuru wa maoni na hivyo ni vigumu sana kwangu kumsemea mtu. Kwa hiyo ma-anony pia wa uhuru wao na kuna umuhimu wa kuwa anony wakati mwingine. Bila shaka ma-anony wanajisikia huru wakiongea yale wayaongeayo.


Sawa sawa. Nadhani ujumbe umefika. Je, ulianzaanzaje kublogu?


Niliona blogu za kiswahili nikiwa mwanafuzi wa computer science (sayansi ya tarakilishi) mwaka 2006 nikaamua kujifunza kutengenza blogu na ndo nikaanza kublogu.

Oh, kumbe kitaaluma wewe ni mtaalamu wa computer. Hongera sana. Unawasaidiaje wanablogu wasio na taaluma yako katika kuboresha nyenzo za blogu zao?

Kuwasaidia wengine??? naomba nisijisemee ili kuzuia changamoto za kihaiba (ego) kuingilia nafasi yangu ila kumbuka kuwa msomi wa computer sio kigezo pekee au muhimu cha kujua kublogu, kutengeneza blogu na kuziendesha kwani hata ukiangalia blogu yangu utaona mapungufu kibao, niko bize. Lakini kuna wanablogu wengi ambao nimesaidiana nao katika kuingia kwenye tasnia hii, naomba nisiwataje

Mara nyingi umezungumzia mitazamo mibovu unayoiona katika jamii yetu. Unadhani ni hasa chanzo cha mitazamo hiyo?

Chanzo ni kibubusa, yaani kuacha watu watusaidie kufikiri, kutokujitambua na kutotafuta mitizamo mipya

Una mtazamo gani kuhusu dini na jamii?

Dini na jamii ziweze kufanya yale zinazoyafundisha lakini ziwe dini za ukweli na sio dini za kugombanisha watu wala kuwatenga…ziwe dini za kuunganisha binadamu si za kuleta vurugu.Ila naona kama dini zetu tulizonazo ni za kuepuka kama tunataka kwenda mbele. Natamani watu waone tofauti iliyopo kati ya dini na waanzilishi wake. Pia kati ya dini na vitabu vya dini hizo (misaafu)… pia kati ya vitabu hivyo na waanzilisha wa dini hizo, waanzilishi wadini na Nguvu Kuu (Mungu?). Tunahitaji uhuru katika dini, uhuru wa maoni na mitizamo na si kikwara ya kukufuru nk au kwenda motoni. Dini zisiegemee kutoza fedha tu bali kuleta mabadiliko.

Je, u muumini wa dini yoyote kati ya hizi maarufu zilizopo?

Dini zipi zilizopo?? Inawezekana kuna dini usiyoijua. Ila nilipokuwa Dar nilikuwa nikienda kanisani na kuimba kwaya…ila nilipohamia mikoani naona kama maji yako shingoni. Lakini mimi naamini katika dini ya upendo na heshima kwa kila kiumbe hiyo ndiyo universal religion ninayoiamini. Hata hivyo, ni lazima tujue au tukumbuke kuwa dini zoote huongelea kitu kile kile kwa lugha tofauti, mazingira tofauti na tamaduni kutokana na uanzilishi wake. Ukiunganisha mafundisho ya dini hizi zoote, utapata universal religion ambayo ndiyo ninayoiamini.

Una maoni yoyote kwa vijana wa kizazi cha leo katika Tanzania?

Vijana ni lazima wajitambue, watafute utume wao na kuutumikia, ni lazima wajue ya kuwa wapo hapa (kwenye miili) kwa lengo fulani na ni lazima walitimize lengo hilo. Ni lazima washike mienendo yao mipya. Vijana wanapaswa kujua ya kuwa jamii yote inawategemea yaani watoto na wazee. Ni lazima waache kutumiwa na ni lazima watambue nafasi zao katika jamii…vijana wanapaswa kujua ya kuwa ujana ni wakati muhimu sana kwamba kila ugunduzi au ukombozi huletwa na vijana. Ni lazima wafanye kazi kwa bidii lakini ni lazima wajue nafasi zao. Lakini wajue kuwa ujana unapita na wengi wanatamani kurudia ujana kwa hiyo wauishi ujana wao wasijetamani kuurudia pale utakapokuwa umepita.

Ukizungumza kwa mifano binafsi: una utume gani hasa ambao wewe binafsi unautumikia? Unatumiaje ujana wako Ndugu Kamala…

Duhu! kujisemea ni tatizo ila ninaelimishana na vijana katika mambo mbali mbali ya kiutambuzi, ujasiriamali, siasa na yale ya kijamii. Ninapeana ushauri mbali mbali na kujifunza mengi kutokana na vijana wenyewe.


Mwisho tumalizie kwa maisha yako binafsi. Unajishughulisha na nini Kanda ya ziwa? Vipi mwamko wa blogu huko?

Kanda ya ziwa naishi, nablogu, nalima, naandika, natafiti, nahamasisha, ni fundi, ni kiongozi wa familia, mwanaharakati, ni mwanamazingira, mshauri, mwanautambuzi nk nk. Mwamko wa blogu sijui ila juhudi zahitajika kuuamsha.
Bila shaka utakuwa wa kwanza kumsha ari hiyo kwa kipindi utakachokuwa huko. Hakuna mwanablogu yoyote uliyeonana naye ukiwa huko?
Nimeonana na kuwasiliana na mmoja wao na wengine. Ni kweli najaribu kuamsha ari lakini bado ni changamoto iliyoko mbele yangu...


Pichani Kamala katika pozi |Picha kwa hisani yake mwenyewe

Una kipi ambacho ungependa kuwaambia wasomaji wako ambacho unaamini hawakijui kabisa kuhusu wewe?

Labda ni migogoro kati yangu na familia yangu (niliyotokea). Kwamba pamoja na utambuzi niko mbali na wanafamilia woote, sielewani nao. Ni familia ya kilokole lakini ndugu na ndugu hawaongei au mzazi na mwana pia hawaongei.

Pole sana kwa hayo. Je, umejaribuje kuitumia elimu ya utambuzi kuleta mabadiliko kwa wanandugu hao?

Ki utambuzi kuna watu tu. Mambo ya ndugu, rafiki jamaa nk, ni vibandiko vya ziada. Lakini pia ninao ndugu wengi sana ukiwemo wewe na wengine. Kwa hiyo, hali hii kwangu ni furaha, ni faraja na nafurahia…maisha yanaendea ni changamoto nzuri za kufanya maisha yawe na maana zaidi


Nakushukuru sana kwa mazungumzo haya. Bila shaka yamewapa fursa wanablogu kupata mengi zaidi kuhusu wewe. Asante sana Ndugu Kamala.


Asante pia kwa kuniuliza maswali haya, naamini hii ni sehemu ya mafanikio ya blogu yangu. Nashukuru sana.

Asante sana kaka.

>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>
Tutakuwa tukiwaletea majadiliano na mwanablogu mmoja wapo kila inapowezekana. Anayefuata anaweza kuwa wewe!

Maoni

  1. Hongera Bwaya na Kamala kwa mahojiano mazuri.

    Labda naomba kutofautiana tu katika suala zima la blogs za kufikirisha au kwa kizungu critical thinking.Pamoja na kwamba kuna umuhimu sana kwa blogs za namna hiyo,blogs zenye mambo mepesi mepesi nazo zina mchango wake katika jamii.Tuzipe nafasi yake.Cha msingi ni watu kuwa na original contents.Blog nyingi hivi sasa zina habari zinazofanana sana.Matokeo yake ni kwamba tunakuwa reporters zaidi ya bloggers ambao kimsingi tunatakiwa kuwa na kusema wazi maoni yetu,fikra zetu nk.Kwa maoni yangu blogs zitumike zaidi katika kupashana habari,kushauriana,kujulishana yanayojiri na kuacha kuzifanya ziwe sehemu muhimu ya habari na mawasiliano.

    JibuFuta
  2. ni mahojiano mazuri sana na ni tofauti safi sana. Natumai wengi watasoma hapa.Asanteni wote kaka Bwaya na Kaka Kamala.Upendo Daima.

    JibuFuta
  3. Ni mahojiano yaliyokwenda shule, naimeyakubali......nimependa mfumo wako wa kuuliza maswali na ninaomba ruksa yako kutumia mfumo huu kufanya mahojiano na wadau mbali mbali ambapo nami nitakuwa nikiweka mahojiano hayo hapo kwangu ili tupate kujifunza wote

    JibuFuta
  4. Mahojiano haya yametulia na nimeyapenda.
    Naomba nikiri kuwa blog ya utambuzi na kujitambua imetokana na mchango wa rafiki yangu huyu Kamala.
    Na kama sio yeye kunishauri ni blog baada ya kusimama kuchapishwa kwa gazeti la jitambue, labda nisingekuwepo kwenye tasnia hii ya blog.

    JibuFuta
  5. Poa sana.Watu kama Kamala enzi za mwalimu ndio walikuwa wanaitwa wasaliti.Lione hilo! iweje mtu asiwe na dini?

    Mzee mmoja niliwahi kumwambia Dini ni bangi,tangu siku hiyo haongei nami na ilitokea baada ya mabishano kibao.

    JibuFuta
  6. Poa sana hiyo. Naomba uendelee na kwa wengine bila special note

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Tabia za Mtoto wa Miaka 0 – 3 Kimahusiano na Kihisia

Pay $900? I quit blogging