Bongo inaumwa kisichoonekana (2)

TUMEKWISHA kuona namna nchi yetu inavyopiga hatua kubwa za kimaendeleo. Na sina shaka kwamba msomaji atakuwa amebaini kwamba hizo zinazoonekana kuwa hatua za kimaendeleo zina walakini. Aidha, tulikuwa tumeishia katika kuyatazama hayo yanayoitwa maendeleo katika sekta ya elimu yanavyolisaidia taifa.

Muunganiko wa muhimu ukawa ni kwa vipi rasilimali watu ambayo taifa halikuwa nayo miaka iliyopita, inatusaidia katika kusukuma “maendeleo” mbele?

Hapa tungependa kudodosa namna ambavyo ukuaji wa taaluma katika maeneo mbalimbali unavyosukuma mbele maendeleo yetu ili kujaribu kuona ulikolalia ugonjwa wa taifa.

*******************************************************

Tumekuwa tukifundisha wanasheria kwa miongo kadhaa sasa. Hawatoshi, lakini wapo na wnafanya kazi zao katika maeneo mbalimbali nchini. Je, watu hawa wametusaidiaje kuondokana na unyanyasaji wa kisheria tunaoupata katika jamii zetu? Taaluma ya sheria imegeuka kuwa mashindano ya kupangilia hoja ili kushinda kesi zisizo na tija. Hakuna tofauti na enzi za “debate” shuleni. Sheria imegeuka kuwa kitanzi cha maendeleo ya nchi yetu (maana ujambazi wa kodi za wananchi unaratibiwa na wanasheria waliobebea kuficha haramu inayotendekea maofisini). Hapa tunaona ya kwamba ongezeko la ujuaji wa sheria kwa baadhi ya raia wenzetu linaendana na ukuaji wa ujambazi wa mali ya umma. Usiwe na haraka ya kujua sababu.

Vile vile inasikitisha kwamba baada ya miongo kadhaa ya kufunza wachumi na wahasibu, uchumi wetu umefikia hapa ulipo. Pamoja na takwimu za kisomi eti uchumi umekuwa kwa asilimia kadhaa, ukweli ni kwamba uchumi wetu umechoka. Tumeendelea kuwa tegemezi pamoja na kuwa na Maprofesa wa uchumi kwenye ofisi nyeti za kifedha. Nchi ya watu milioni arobaini inapanga bajeti kwa mategemeo ya kuokolewa na wajomba (na wameanza kututelekeza). Kwa nini tunashindwa kujitegemea?

Walipa kodi (wakubwa kwa wadogo) wanawalipa watu binafsi na si serikali. Wakizipeleka serikalini, wnaapanga namn aya kuzikwapua tusigundue. Kwa maana nyingine taaluma zao haziwasadii kutekeleza majukumu yao –kama kudhibiti mfumuko wa bei na kudorora kwa shilingi– na badala yake zinawasaidia kujiletea maendeleo yao wenyewe kwa haraka. Kwa hiyo utaona, katikati ya wachumi hawa, wizi wa kitaalamu ni lazima ushike kasi zaidi kwa ushirikiano wa karibu kabisa wa wanasiasa. Kwa maana hiyo umasikini ni lazima uongozeke kwa wananchi waliowengi wakati ubilionea ukinukia kwa wenzetu wachache wanaoishi kwenye ofisi za kifedha.

Pia “taaluma” ya siasa inazidi kupata umaarufu. Sihitaji takwimu kuhitimisha kwamba si muda mrefu, idadi ya wagombea wataizidi ile ya wapiga kura. Ndiko tunakoelekea. Najua kila mtu ana haki ya kikatiba ya kututumikia. Lakini inaonekana kwamba utumishi maarufu umekuwa ni huu wa kwenye siasa. Kwa nini tusiwatumikie wananchi kupitia ofisi nyinginezo za utumishi wa umma? Kwa nini tunazitelekeza ofisi muhimu kwa uzalishaji na badala yake sote tunaanadamana kwenda kutumika kwenye ofisi zinazotumia kuliko kuzalisha? Kwa nini maprofesa wa utatibu wanaacha wagonjwa na kwenda kugombea ubunge? Wanamwachia nani wagonjwa? Kwa nini maprofesa wa mawasiliano wanaacha taaluma zao na kuamua kwenda kupigana vikumbo “kuwatumikia wananchi”? Kwa nini wataalamu wa Fizikia na Nyuklia wanajutia taaluma zao na kukimbilia siasa? Why?

Hapa yanawezekana matatu. Kwanza inawezekana elimu ya kimagharibi waliyonayo haina mahusiano ya moja kwa moja na maisha yetu ya kila siku. Hiyo ni kusema huenda elimu ya sasa haitilii mkazo masuala yanayotatua matatizo yetu na badala yake tunajikuta hatuwezi kutatua matatizo yanayotuhusu moja kwa moja kwa kutumia elimu hiyo. Pili watu tunasoma almuradi tunakusanya vyeti bila kujua tunataka nini na tupitie wapi kukipata. Hatuujui utume wetu na malengo yetu katika maisha. Maana haiwezekani usote darasani kusomea udaktari halafu uishie kuwa mwanasiasa. Tatu huenda katika nchi yetu, tumefika mahali ukiwa nje ya mduara wa watawala, huwezi kuambulia chochote. Njia nafuu ni kujiingiza katika mduara huo (wa ulaji) ili na wewe ujitengenezee mduara kwa ajili ya wanao na marafiki zako. Matatu haya ni ugonjwa, ila la tatu ni baya zaidi lililosababishwa na mawili yaliyotangulia.

Kama ingewezekana, ningeshauri nchi hii ifute wanasiasa kwa muda. Wanasiasa hawa hawana lolote la maana zaidi kufikiria zaidi ama namna ya kuingia kwenye mduara wa kula au jinsi ya kujikita zaidi katika mduara huo. Athari ya yote haya ni kuathirika kwa sekta nyinginezo ambazo zinaharibikiwa kwa gharama ya kuendesha siasa. Hivi sasa karibu kila msomi anasoma ramani ya namna ya kuingia kwenye mduara wa siasa ili ale kama wenzake. Yaani kwa maneno ya moja kwa moja, kila mtu sasa hivi anafikiria fedha za haraka haraka zinazopatikana kupitia “kuwatumikia wananchi.” Halafu ni ajabu tunajiuliza ufisadi unatokea wapi.

Naelewa kwamba ni haki ya kila raia “kututumikia” kupitia nafasi za kisiasa. Hata hivyo, mbio hizi za kila mtaalamu kuitelekeza taaluma yake aliyoisotea kwa miongo kadhaa, ni dalili kwamba tumeamua “kuendelea” zaidi kwenye sekta ya siasa kuliko kujiletea maendeleo ya kweli kupitia sayansi na teknolojia. Rasilimali zote sasa zimeelekezwa kwenye siasa. Ukitaka kuelewa vizuri hili, tafuta kujua bunge limejitengea asilimia ngapi ya pato la taifa katika kutekeleza majukumu yake. Hapo hujazungumzia asilimia ya kuendesha serikali inayopanuka kila siku (kwa mduara ule ule).

Matokeo yake yanaibuka matabaka ya wanasiasa wanaoogelea kwenye ukwasi wa kufuru pamoja na maswahiba wao walio kwenye ofisi nyeti za kitaaluma na kundi duni la wapiga kura linalojumuisha wafanyakazi wa kada ya chini (wanaombiwa hata laki tatu hawastahili kwa mwezi) na raia wanaokula kwa jasho lao. Hilo kundi la kwanza linaishi maisha ya tofauti mno na maisha ya hili na pili kiasi kwamba haliwezi kuelewa kabisa matatizo ya hawa wa pili.

Nikupe mfano mmoja. Kwa muda mrefu kundi la pili (likiongozwa na wafanyakazi) limekuwa likilalamika wazi wazi kwamba maisha yamekuwa magumu tofauti na ahadi ya chama kinachopindua kwamba maisha bora kwa kila mtanzania yanawezekana. Kundi la kwanza (linalokula na halijui shida) linajibu kwamba kila mtu afanye kazi kwa bidii maana “maisha bora hayadondoki kama mana jangwani”.

Mtu unajiuliza ni bidii ipi wanayoitaka hawa watawala? Bidii ipi zaidi ya hii ya walimu kufundisha darasa la wanafunzi 100 kwa kutumia kitabu kimoja? Eti bidii! Kuna ya zaidi ya hiyo? Halafu mwisho wa mwezi mwalimu huyu aliyeteseka kufukia mashimo ya uzembe wa watawala wake anamalizia “mshahara” wake kwenye madeni ya mwezi uliopita. Na si kweli kwamba serikali haina “hela”. Fedha za kusafirisha misafara ya watawala na wasaidizi (na wasaidizi wa wasaidizi wao) eti kukagua maendeleo mikoani na kuitangaza nchi ughaibuni, wanazo. Fedha za kuteketeza katika kutengeneza mikoa na wilaya zisizo na sababu, wanazo. Fedha za “kupanua demokrasia” kwa kuongeza idadi wa majimbo ya ubunge zipo. Kwa maneno ya karibu zaidi, fedha za kujipendelea wao na vyama vyao na maswahiba wao “hasikosekana-gi”. Tatizo ni zile za kuhudumia raia wasio na hatia.

Wanatusihi tujitume na kufanye kazi kwa bidii “kujiletea maendeleo”. Hivi kuna bidii zaidi ya kufanya kazi kwenye mazingira mabovu ambayo hata serikali yenyewe imeyasusa? Hatuwezi kumfinya raia kwa namna ambayo pamoja na kujituma kufanya kazi, hana cha maana anachoingiza mfukoni, halafu tumgeukie na kumbeza raia huyo huyo eti “maisha bora hayashuki kama mvua!”. Raia ambaye pato lolote analolipata kwa suluba haliwezi kumpatia mahitaji yake ya msingi kwa sababu ya mpao wa kufuru wa bei ya vitu na huduma tunambeza eti “maisha bora hayadondoki kama mana jangwani…fanyeni kazi!...acheni uvivu!” Hivi ni kweli? Hivi ni kweli kwamba watanzania ni wavivu?
Ukweli ni kwamba katika nchi ya Bongo, watu wanachapa kazi sana, lakini mfumo uliopo uliosukwa na serikali yenyewe unawakwaza. Wananchi wanatumia akili nyingi sana kuendelea kuishi katika mfumo huu. Vijana wanatembeza bidhaa za kichina kutwa nzima hakuna wanachoambulia. Wanajituma kwa kubeba mizigo mizito na kufanya kazi halali za suluba hakuna wanachopata. Wakulima wanapoteza muda na rasilimali zao bure halafu mwisho wa siku mazao yao yanaishia kukopwa ama kununuliwa kwa bei ya kutupa. Hawa wafanye kazi kwa bidii ipi? Wagombee udiwani ndio tuone wana bidii?

Sababu ya haya yote ni kwamba walio kwenye madaraka hawajui shida za wananchi.

Ni hawa hawa wanasiasa ambao ili kutekeleza malengo yao ya kisiasa wameingilia taaluma za uzalishaji kama tulivyoona hapo juu, sasa wamo mpaka kwenye taaluma zinazohusiana na kuwahabarisha wananchi namna wanavyoongozwa. Na kwa kuwa ugonjwa ni ule ule, wanasiasa wamefanikiwa sana. Hebu na tuone.

Sasa hivi kuna vyuo vikuu visivyopungua vitatu vinavyofunza raia wenzetu namna ya kuhabarisha wananchi kupitia magazeti, radio na televisheni. Kwa maana nyingine nchi sasa ina wanahabari “wasomi” zaidi na wengi kuliko ilivyowahi kuwa huko nyuma. Yaani magazeti hii leo yanaoongozwa na wasomi wa habari na mawasiliano. Radio zinatangazwa na watu wenye shule ya kueleweka. Hali kadhalika luninga na vyombo vingine vya habari. Lakini huhitaji kusambaza dodoso kwa wananchi ili kuona namna vyombo hivi vya habari vinavyoongoza kwa uhalifu. Ni uhalifu kuanzia kwenye maadili mpaka kwenye uhalifu wa kuwapumbaza wananchi kuamini kisichokuwepo.

Ndugu msomaji, bila shaka utakuwa unajua kuwa hivi sasa yapo magazeti ambayo ajenda kuu ni kuwadanganya wananchi. Hayana aibu kuwapamba majambazi wa nchi yetu ili eti tuwaone kuwa ni watu watakatifu wanaoonewa na mahasimu wao kisiasa. Kuna magazeti ambayo huna hata haja ya kuyasoma maana unajua wazi kuwa mle ndani lazima kuna vichaa wakiongozwa na mhariri msomi wanaandika makala za kuwasuuza wahandisi wa umasikini wetu (mafisadi).

Zipo televisheni zinazoongozwa na wabobevu wa habari waliowahi kutamba katika vyombo vya kimataifa ambazo hazina wajibu mwingine zaidi ya kuharibu taswira ya wapinzani wa watawala (walio ndani ya chama kinachokula hivi sasa na vile vinavyongoja kula baadae) na hivyo kujenga taswira chanya isiyokuwepo ya chama na serikali. Sasa tunajiuliza kama usomi wa habari ndicho tunachokihitaji, ni usomi wa aina gani zaidi? Maana wapo, lakini hawafikiri zaidi ya kula na kunywa.

Sasa ningeweza kukupa mifano mingi sana ya namna maendeleo tunayoyaona yasivyo na maana yoyote kwa wananchi wa Tanzania. Ningeweza kuendelea kukuonyesha zaidi namna ongozeko la rasilimali watu linalotokana na kupanuka kwa elimu linaenda sambamba na maendeleo ya uhalifu wa rasilimali za nchi na haki za raia.

Maana hasa ya haya yote ni kwamba tunakosa kitu fulani kama taifa. Na ukosefu wa kitu hicho umeanzia ngazi ya familia hadi Magogoni. Maana yake ni kwamba haina haja tena ya kuongeza vyuo vikuu kufundisha wataalamu ambao wakimwangwa mtaani wanaongeza uhalifu wa maendeleo badala ya kutusaidia. Nchi hii haina haja tena ya kuendelea kuongeza majimbo ya uchaguzi ili “kupanua demokrasia” ambayo ni hakika itapanua demokrasia ya ukwapuaji wa kodi za wananchi na misaada ya wajomba.

Nchi hii inayo haja kubwa ya kujitazama upya. Kutafuta mwelekeo mpya. Kutafuta tafsiri sahihi ya kile kinachomaanishwa na neno maendeleo. Hapo ndiko tutakapoanzia siku nyingine.

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Haiba ni nini?

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Makundi Manne ya Tabia za Watoto Kitabia

Uislamu ulianza lini?