Bongo inaumwa kisichoonekana

Ni wazi kuwa nchi ya Bongo ya miaka kadhaa iliyopita, si hii ya leo. Mambo mengi ya msingi yanabadilika na kwa kweli yanabadilika kwa kasi kubwa. Hata hivyo, ningependa kuonyesha kwamba tatizo tunalokabiliana nalo katika nchi yetu limejificha katikati ya haya tunayoyaona kama maendeleo. Tatizo hilo haliwezi kutatuliwa kwa kusogeza zaidi maendeleo kwa wananchi wala wala kwa kuanua demokrasia zaidi wala kukusanya kodi zaidi wala kwa kuongeza wasomi zaidi. Tatizo hilo linaweza kutatuliwa kwa kupembua upotofu wa aina ya maendeleo yetu tunayoonekana kuyataka zaidi na tukiyapata tunayatangaza kupitiliza.

Tutazame maendeleo katika sekta ya mawasiliano. Nchi hii haijawahi kushuhudia maendeleo yaliyofikiwa hii leo katika teknolojia ya mawasiliano. Tuko juu katika nyaja ya mawasiliano baada ya kuwa tumefungua milango yote miaka ya tisini. Yapo makampuni kibao yenye wateja wanaokaribia milioni ishirini kati ya raia milioni arobaini. Na wote hao wanapigiana simu na kuandikiana ujumbe mfupi wa maneno. Wanatumia fedha kidogo walizonazo kuwafanya mawasiliano ama wanalazimishwa kutumia simu ili washinde bahati nasibu ya nyumba, magari, bajaji, mamilioni na hivi karibuni kukwea pipa kwena kutazama fainali za kombe la dunia.

Ni wazi kwamba makampuni haya ya kigeni yanatengeneza mabilioni ya shilingi kwa gharama ya umasikini wa watanzania. Pengine wanalipa kodi. Lakini ni hakika kwamba mabilioni yote hayo wanayasombwa kwenda nje ya nchi. Sie tunaachwa na “maendeleo” ya kuongea masaa ishirini na nne kwa shilingi. Tumeendelea sana.

Siku hizi nchi imeunganishwa na mtandao wa mawasiliano ya tarakilishi. Tunapata habari zote tunazozihitaji kupitia wavuti, blogu, twita na kadhalika. Habari tunazozihitaji ni pamoja na utamaduni wa nje unaotuelekeza namna ya kutengeneza na kutumia fedha. Tunafundishwa thamani ya fedha kwa maisha ya mwanadamu. Uthamani huu mpya wa fedha ambao hapo awali jamii yetu haikuujua, umesaidia sana kuharakisha “maendeleo” katika nchi yetu. Kwa maana nyingine, kupanuka kwa mtandao wa mawasiliano, kunapanua pia maendeleo yanayotokea nje kuja ndani na si kinyume chake. Maana yake ni kwamba jamii yetu inaumwa. Yenyewe haijua-gi kuchagua namna ya kuendelea kwa kutumia ustaarabu wake inaoamini kwamba una maana katika kuleta maendeleo ya kweli yanayoendana na maisha halisi ya hapa tuliko. Badala yake hata ustaarabu wake yenyewe haiujui, na hivyo inakuwa rahisi sana kustaarabishwa na maendeleo yanayotoka nje kuja ndani ambayo hatari yake huwa kubwa kuliko huko yalikotokea. Pamoja na yote hayo, bado haya nayo ni maendeleo.

Barabara (tena za lami) zinajengwa kuizunguka nchi kwa lengo la kuyaharakisha maendeleo ya wananchi na wakati huo huo kurahisisha misafara ya viongozi na mwenge wa uhuru. Japo ni kweli kwamba miradi mingi ya ujenzi inategemezwa kwa mikopo ya wajomba, bado tunaweza kuona unafuu mkubwa kimawasiliano. Saa hizi unaposoma haya, unaweza kusafiri sehemu kubwa ya nchi hii ukipitia kwenye lami hata kama (lami hizo) ni deni la taifa.

Utakuwa na bahati mbaya sana kama unaishi sehemu isiyo na maslahi kwa wenye nchi wala wafadhili wa maendeleo yetu. Ni hakika lami mtaendelea kuisikia kwa majirani kwa miaka mingi ijayo. Tazama wenzio wanavyofaidi mikopo ya wajomba. Baada ya barabara za kusini kutengemaa kufuatia mafanikio yao ya kutuzalia mnene wa Taifa hili, sasa ndugu zangu Wambulu nao wanakaribia kula matunda ya kumtoa mmoja wa wanene wa chama na serikali. Barabara zinazoingia Babati, makao makuu ya Mkoa mpya ulianzishwa ili kusogeza maendeleo karibu na wananchi waliomzaa mnene wa nchi Muiraq, zinashughulikiwa kwa kasi. Barabara ya kutokea Minjingu – Babati na ile ya Babati –Singida, mkandarasi yuko kwenye saiti kutekeleza ilani ya chama.

Habari njema kwa wakazi wa Mpanda na Rukwa. Baada ya kusota kwa miaka mingi kwa kosa la kushindwa kutupatia wakuu wa chama na serikali, sasa nao mizengwe haitakuwepo tena. Hivi karibuni watafaidika na utaratibu tuliojiwekea katika nchi hii wa kusogeza maendeleo karibu na wananchi wanaotoa mchango wa “kiuongozi” katika taifa letu.

Kigoma hatuwatanii. Wala Tabora wala Singida wala Shinyanga. Wao ni ama wajipangange wao wenyewe, au waneemeke na maendeleo yanayopelekwa kwa wachangiaji wakuu wa maendeleo.

Kwa hiyo barabara zinajengwa na zinaonekana. Haya ni maendeleo makubwa sana kuwahi kufikiwa katika historia ya taifa letu lenye amani na utulivu.

Uwekezeji umeshika kasi. Kila mahali pamewekezwa. Na wawekezaji wenyewe ni wageni wanaoshirikiana kwa karibu na wenyeji wenye madaraka. Tunapata kodi na hivyo kuongeza pato la taifa. Hii ni habari njema kwa kila “mpenda” maendeleo. Kama hatuna teknolojia, kwa nini tusiwakaribishe wenye nayo waje kutusaidia kuyafukua madini huko yaliko? Nyakati zimebadilika na uwekezaji ndiyo sera ya dunia. Maendeleo yanaletwa kwa kubinafsisha.

Maji yapo. Kama hujawahi kusikia, usikie sasa hivi. Nchi ya Bongo inachangia karibu asilimia thelathini (kama sijapunguza) ya vyanzo vya maji ya dunia. Tumebarikiwa kweli kweli. Bahati mbaya mpaka leo, maji ndiyo kipengele muhimu cha kuombea kura. Kukosekana kwa maji ni mtaji wa kisiasa pengine. Hata hivyo, juhudi za kusambaza maji zinaendelea vizuri. Nisingependa tutumie muda mrefu kuzungumzia jitihada hizi, labda tuone mfano mmoja tu.

Huko Monduli wamebahatika kupata mkopo wa mjomba kusogeza maji karibu na wananchi. Maji yale bado hayaonekani ila matumaini yapo. Pamoja na kwamba mabilioni ya mkopo huo yalishatolewa siku nyingi (kabla mnene hajatimuliwa ofisini) zipo tetesi kuwa maji yanasubirishwa mpaka wakati wa uchaguzi ili wananchi wapige kura wakishuhudia utekelezaji wa ilani ya chama na serikali yake. Wengine wanaamini Mabilioni yale “hayatatosha” kupeleka maji kule kwa sababu za kiulaji. Sijui zaidi, lakini ni wazi mikopo mikubwa mikubwa inaelekezwa maeneo muhimu ili kuharakisha maendeleo.

Kwa upande wa elimu nako si mbaya sana. Wasomi wanaongezeka nchini Bongo, tena kwa kasi. Hivi sasa idadi wa madaktari wa falsafa ni kubwa. Najua idadi hiyo ya madokta imepata ushirikiano mkubwa wa ukuaji wa sekta ya utengenezaji wa vyeti vya dharura kukidhi mahitaji wa makuwadi wa elimu. Natambua pia haka kamtindo cha karibu kila mwanasiasa kuzawadiwa ubini wa “Dokta” bila kazi ya maana kamechangia sana. Lakini kitakwimu tumo ndugu.

Na hasa baada ya serikali ya chama cha kupindua kuwalazimisha wananchi kujijengea shule zao wenyewe, watoto wengi sasa wanaweza “kupasi” na kuingia sekondari bila misukosuko ya enzi zile.

Mie si wa siku nyingi. Lakini nakumbuka miaka ya tisini, shule nzima na hata kata nzima wanaochaguliwa kuingia kidato cha kwanza walikuwa hawamalizi vidole vya mkono kuwahesabu. Hivi sasa yapo maeneo ambayo bila “kuwapasisha” wanafunzi wote wa kata husika, madarasa yatabaki wazi kwa sababu majengo ya shule yameongozeka zaidi na zaidi. Haya ni maendeleo kwa sababu hata kama si rasmi, ni wazi kwamba sasa elimu ya sekondari ni ya lazima kwa kila Mtanzania.

Ni hivyo kwa sababu mbali na wanafunzi waliofeli “kuwezeshwa” kupata nafasi ya “kupasi” kwenda sekondari, bado hata huko sekondari kwenyewe, hakuna kizuizi chochote cha kupembua wanaostahili kuingia kidato cha tatu. Maana yake ni kwamba kila mwanafunzi yeyote mwenye namba ya usajili anapokanyaga kidato cha kwanza ni lazima atamaliza kidato cha nne panapo majaliwa ya uzima awe na mwalimu asiwe nae, asome asisome.

Katika hali kama hii, ingefaa basi kama serikali ingefanya maamuzi kwamba pasiwe na ulazima wa mwanafunzi “kupasi” kwenda shule nyingine, na badala yake amalizie sekondari katika shule hiyo hiyo aliyoanza nayo wakati anajiunga na darasa la kwanza. Kufanya hivyo kutapunguza usumbufu wa kuwahamisha wanafunzi kutoka shule moja kwenda nyingine kwa sababu ambazo si za msingi.

Kwa ufupi kabisa, hayo ni baadhi ya maendeleo ambayo kila Mtanzania anaweza kuyaona. Itatuchukua muda mrefu kujaribu kuyaorodhesha.

Sasa naomba tuangalie namna maendeleo katika sekta ya elimu yanavyolisaidia taifa.

Kwa hakika, maendeleo ya elimu yameongeza rasilimali watu ambayo taifa haikuwa nayo miaka iliyopita. Idadi ya wataalamu katika kila sekta imeongezeka. Na si tu utaalamu bali ubobevu. Tunao wabobevu katika kila sekta. Je, wingi wao na uwepo wao unatusaidiaje katika kusukuma “maendeleo” mbele?

Inaendelea....

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Haiba ni nini?

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Makundi Manne ya Tabia za Watoto Kitabia

Uislamu ulianza lini?