Sayansi itufunze kuwa hatujui

Ushahidi mwingine kwamba viumbe hawawezi kuwa wamebadilika kama wanavyodai mashabiki wa nadharia za Darwin upo kwenye stadi za chembechembe hai za viumbe (seli). Kisayansi, ni jambo lililo wazi kwamba msingi wa kiumbe yeyote ni seli. Seli hizi zimeundika kimfumo. (Unakumbuka tafsiri ya mfumo?) Kila seli inayo vipengele vingi vidogovidogo ambavyo hufanya kazi kubwa kuliko kiwanda chochote kinachofahamika kutengenezwa na mwanadamu. Utendaji huu unawezekana kwa sababu kila kipengele kinatengemea kipengele kingine kiasi kwamba kimoja kikiwa na hitilafu hata ndogo sana , hakuna kinachoweza kuendelea. Na hitilafu hii ndogo kwenye seli moja ikiachwa iendelee basi, hatma yake huweza kuwa ‘ugonjwa’ wa kiumbe mzima na hata janga kubwa zaidi.

Ni jambo jema kwamba elimu hii ya kujua utendaji muhimu wa kiwango cha seli umewezeshwa na sayansi halisia. Uvumbuzi wa darubini ndio ulimwezesha mwanadamu kuyajua yote haya ambayo hata hivyo yalikuwepo hata kabla ya sisi kuyajua.
Mawazo kwamba kiumbe anaweza kubadilika ni uongo wa wazi, kwa sababu haiwezekani kabisa mfumo ndani ya seli ubadilike na kuruhusu kufanyika kwa mfumo mwingine kirahisi rahisi. Labda ili kulieleza hili, tuzungumzie kitu kinachoonekana. Tuangalie jicho. Jicho limeundwa na vitu vingi ambavyo si lazima kujua majina yake. Kila kimoja kila kazi yake maalumu,na kisipoweza kuifanya kazi hiyo vizuri, jicho zima linakuwa kwenye hatari ya kutokutimiza wajibu wake (kuona). Hiki ndicho ninachokiita mfumo.

Itakuwa ni ajabu kudai kwamba jicho zima zima zinaweza kugeuka na kuwa kitu kingine kwa kuongeza tu miaka ya mabadiliko hayo! Yaani haiwezekani ukadai jicho litabadilika kuwa kitu kingine kwa kivuli cha ‘...yatatokea miaka bilioni moja ijayo...’ Kama tu seli moja haiwezi kubadilika kuwa kitu kingine seuse kiungo kama jicho!
Huu, kwa hakika ni ushahidi wa wazi kwamba suala la mabadiliko linaloelezwa kwa bidii na ‘wanasayansi’ wa aina ya Darwin, ni jambo lisilowezekana isipokuwa kwa kuamua kuamini hivyo.

Ninasikitika kwamba wasomi wanatufundisha kuamini uzandiki huu wa kitaaluma ambao hauna mashikio ya sayansi ya kweli kweli sipokuwa ikiwa tutazisoma kwa kutumia imani kama zile nyingine zinazoitwa ‘za kienyeji’.
Sayansi ya kweli inatusaidia kujua namna ambavyo viumbe na ulimwengu wote umefanyika kwa namna ya ajabu. Sayansi, tukiiangalia kwa haki, inatusaidia kuelewa ukomo wa fahamu zetu sisi kama viumbe.

Maarifa ya sayansi, kama kweli tuna akili timamu, yanatusaidia kujua mfumo unaodhibiti mwenendo wa universe na hivyo kumtukuza Yeye aliyevifanya.
Ni upuuzi kufikiri kwamba ‘ukigundua’ namna moyo unavyofanya kazi, basi maana yake humhitaji Mungu. Ungejua kwamba kufahamu utendaji wa moyo si kugundua, bali kujua kitu ambacho hukuwa unakijua kabla, ungekuwa mpole.
Sayansi haina kingine cha kufanya kwenye suala la maumbile (nature) isipokuwa kujua tu namna maumbile hayo yanavyofanya kazi.

Newton alipojua kanuni inayoongoza kani uvutano, alitusaidia kujua namna ya kuitumia kanuni hiyo vile ilivyo itusaidie katika maisha yetu,na sio kuibadili utendaji wake. Ukishajua nini kinasababisha jiwe likirushwa juu lisiende moja kwa moja, huna cha kufanya zaidi ya kutumia kanuni hiyo ya maumbile katika maisha yako. Ukiisha kujua kuwa nikirusha chombo angani kwa mwendo kasi wa kilomita kumi na mbili kwa sekunde, chombo hicho hakitarudi duniani, hiyo haiwezi kukufanya uibadili kanuni hiyo. Utaitumia kanuni hiyo kupeleka vifaa vyako katika anga za juu, lakini huna cha zaidi unachoweza kufanya kupingana na kanuni hiyo ya maumbile.

Hatuwezi kudhani kuwa hatuna tunachokitaji tena kwa sababu tu tumejua namna mimba inavyotungwa. Ni sayansi inayotusaidia kujua kilichopo tayari, na sio kufanya kisichokuwapo. Mtu yeyote anaweza kupata mimba hata kama hajui namna mimba hiyo inavyotungwa. Anayejua namna mimba hiyo inavyotungwa hawezi kufanya zaidi ya kanuni ya maumbile ya uzazi. Anachotuzidi sisi wengine ni namna anavyoweza kucheza na kanuni hiyo ya maumbile,na sio kuibadilisha.

Ni sawa na kuwa ndani ya gari linalotembea. Ile kujua tu kuwa uko ndani ya gari, haiwezi kukufanya uwe tofauti na abiria mwenzio asiyejua kuwa yumo ndani ya gari. Wote wawili (unayejua na asiyejua) mtaendelea kusafiri kwa mwendo kasi ule ule wa gari.
Hiyo maana yake ni kwamba maarifa ya sayansi yanapaswa kutufanya tuwe watu wanyenyekevu, wepesi wa kukubali (ku-appreciate) uwezo wa Mwenyezi Mungu aliyeziunda kanuni za maumbile ambazo kamwe hatuwezi kufanya kinyume cha kanuni hizo. Sayansi ni ushahidi wa karibu kwamba kwa kweli, mwanadamu hajui kama anavyodhani. Na kama kuna kujua, basi ni kwa ukomo ulio mbali sana na ujuzi wa kweli kweli.

Inaendelea

Maoni

  1. Nimeupenda mfano wako wa watu kuwa ndani ya gari moja, mwendo kasi mmoja.....
    Imenipa nuru ya fikra

    JibuFuta
  2. siamini kabisa kwamba bila wanasayansi km Newton, Enstain maisha yangekuwa maguma na sikubaliani na hilo kwani linakinzana na mfano wako wa kuwa kwenye gari moja

    wanasayansi wanapinga Dini na sio Mungu. nadharia za kidini ndizo wazipingzo na yule unayemwita Mungu sio lazima aitwe Mungu na watu wote kwani kila mtu anatumia jina lake na ndiyo maana wanasayansi wanakataa umwita Mungu lakini wanakubaliana na uweppo wa Nguvu kuu, nature nk

    juu ya kumfikia Mungu wanasayansi wa kidunia wanaweza wasielewe kwani hii inahitaji sayansi ya kivyake maarufu kama sayansi ya kiroho ´´science of the soul´´

    nadharia ya evolution na ile ya creation ni kitu kimoja kiziangalia vizuri zinaongelea kitu kimoja katika mazingira tofauti

    eti kuna tofauti gani kati ya Ngedere, Nyani, tummbili na Sokwe mtu?? ipo ila ni ndogo na hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Mtu wa kale aliyeishi misituni namaporini. wakati huo hakujua kuoga, kunyoa nywere, ndevu na hata mavuzi. hakujua kupika wala kuchoma chakula alikula tu vibichi na zaidi alikuwa vegeterian km sokwe au Nyani. sasa hayo ni historia, hiyo sio evolution????

    JibuFuta
  3. Chib,

    Asante kwa kushiriki mjadala huu.

    Kamala,

    Hakuna sayansi inayoamini uwepo wa nguvu uliyooiita kuu. Nature na nguvu hiyo ni vitu tofauti.

    Evolution unavyoizungumzia hapo ni kitu tofauti na mabadiliko ya kimaumbile. Nadhani utakuwa unazungumzia historia ya kawaida ya maendeleo ya mwanadamu.

    Nakubaliana kuwa kumfikia Mungu kwa sayansi ya dunia tunayoiongelea ni jambo lisilowezekana. Lakini kwa mtazamo wangu, sayansi hii hii inaweza kukusaidia kuujua uwezo wa Mungu.

    Nakubaliana na wewe kuhusu kuingiliana kwa nadharia za chanzo cha uhai na viumbe (ile ya kidini/imani na kisayansi) ingawa zote zina misingi tofauti tofauti.

    Asante kwa mawazo yako katika mjadala huu.

    JibuFuta
  4. Kuna wawezao kukubishi Mkuu Bwaya kwa kutumia experiment kama hizi za nano Tekinology wamuonyeshazo Obama hapa :http://us.cnn.com/video/?/video/tech/2009/10/23/sot.mit.obama.tour.nanotech.cnn

    Ntatafuta link igusayo experiment ionyeshayo jinsi unavyoweza kubadili kwa spidi cell ya kidole cha mtu itengeneze sikio lamtu kwa panya kwa kuispidizisha tu kama wachezayo navyo MAJINIOLOGISTI katika genetics.

    Pia wapo watakao kubishia kwa kuangalia tu jinsi cell ziwezavyo badilika na kufanya ugonjwa wa nguruwe uwe ugojwa wa watu kwa kubadili tu characteristics zake.

    JibuFuta
  5. Nachojaribu kusema ni kwamba kuna waaminio kuwa kwa kuwa unaweza kumanipulate seli kwenye maabara basi na nature yenyewe inauwezo wakugeuza sell katika mazingira kama Darwin alivyodai

    JibuFuta
  6. Simoni, bahati njema hili (la cloning) nimetoka kulipandisha kwenye ukurasa wa kwanza sasa hivi. Nadhani ukipitia pale, tutajadiliana zaidi.

    Asante sana kwa kuchangia maoni. Jambo hili ni mjadala unaohitaji tofauti za mawazo.

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?

Pay $900? I quit blogging