Mwaka wa malengo mahususi ndio huu
Mwaka unaishia leo. Watu wengi watakwambia jitathmini. Kuona wapi ulikosea. Wapi ulilikoroga. Wapi ulifanya vizuri na mambo kama hayo. Binafsi sioni sababu yoyote ya kufanya hivyo. Sioni sababu ya kufanya hicho kinachoitwa tathmini ya mwaka. Sababu ni kwamba hata kama ungegundua wapi ulikoharibu, huna unachoweza kufanya zaidi za kujiumiza moyo. Utaumia moyo, na historia itabaki pale pale. Maana historia ilikwisha kuandikwa. Kama ulishindwa mwaka huu, hesabu ni upepo umepita. Hata kama ungegundua wapi ulifanya vizuri, ukweli ni kwamba hayo wameshapita. Yaache yaende. Hakuna haja ya kulewa sifa zisizoweza kukusaidia leo. Siafa za jana zinabaki kuwa za jana. Huna sababu ya kuangalia nyuma. Historia haiwezi kukusaidia. Una sababu ya kuiacha ipite vile ilivyokuwa. Nionavyo mimi, huu ni wakati wa kutazama mbele. Kuwa na malengo. Usipojua unakokwenda, utaishia kokote. Wafanyakazi waangalie namna watakavoboresha utendaji wao wa kazi. Wanafunzi wajiangalie watakavyoweza kusoma kwa bidii. ...