Kwanini watu huwasema vibaya wenzao?

Binadamu wengi hatupendi tusemwe vibaya. Tunajisikia kuvunjika moyo tunapohisi kuwa yupo mwenzetu anaona fahari kuyasema mapungufu yetu bila staha. Kama wewe si mmoja wapo samahani. Wenzako ndivyo walivyo.

Sababu ni kwamba binadamu tunapenda kuonekana wa thamani hata kama mara nyingine thamani hiyo tunayoidai hatunayo. Tunalo hitaji la kuona kuwa wengine wanatuheshimu, kututhamini na kuwa na maoni chanya kutuhusu. Kinachotofautiana, ni kiwango.

Hebu fikiria. Mfanyakazi mwenzako anakujia na kuuponda utendaji wako wa kazi uso bin uso. Bila adabu. Bila staha. Ama mwenzi wako anakukosoa mbele za watu kuhusu mambo ambayo yanawahusu ninyi wawili. Ama mkuu wako wa kazi anapokuhamakia kikaoni. Ama rafiki yako anakusemea mbovu mtaani. Kwa wengi wetu, japo katika viwango tofauti, itauma.

Sasa ni hivi: Hivyo unavyojisikia ndivyo binadamu wengine wanavyojisikia ukiwaponda.

Ni ajabu na kweli. Sisi hawahawa, tunaodai heshima kwa nguvu, ndio hao hao tunaoona raha kuwashushia wenzetu thamani yao. Tunakuwa na maoni angamivu ‘yanayowachafulia hewa’ wenzetu.

Wengine wetu tumeizoea tabia hii kiasi cha kutokukumbuka ni lini na wapi ‘tuliwachafulia’ wenzetu hewa kwa maoni yetu mabaya yaliyotolewa bila matumizi sahihi ya hekima. Tumefika mahala pa kuweza ‘kumtapikia’ mtu na sie tunaendelea na bizinez azi yuzhwo.

Kwa nini tabia hii muflisi imeshamiri kwa watu wengi? Tabia ya kutamani kuwakatisha tamaa, kuwashusha moyo, kuwaponda wengine bila sababu ya msingi inatokana na nini?

Tabia hii ina mizizi yake katika namna tunavyojichukulia sisi wenyewe na tunavyowachukulia wengine.

Mtu aliye mwepesi kutoa maoni hasi (angamivu) kwa mtu mwingine anatupa picha kubwa kuhusu kilichopo kichwani mwake. Kwamba haiamini thamani aliyonayo na hivyo anajiaminisha kuwa anaweza kuipandisha kwa gharama ya wengine. Yaani kuwashushia wengine hadhi zao ili yeye aonakane bora kuliko alivyo.

Hivyo ni sawa kabisa tukisema kwamba wepesi wa ‘kuwachafulia hewa’ wenzetu unaendana moja kwa moja na kiwango chetu cha wasiwasi wa hadhi tulizonazo.

Tuangalie mifano michache. Chukulia kijana asiyejiamini anavyojaribu kumpata msichana kwa kuwasema vibaya vijana wengine anaohisi wanamwinda msichana huyo huyo. Ama “msomi” anayelazimisha kuonekana ‘kipanga’ kwa kuponda masomo ya wengine: “…mwanaume mzima kabisa eti anasoma sosholojia?...yaani unasoma Kiswahili na Historia masomo la kike?...”

Ama mwandishi anayetafuta sifa za bure kwa kuwaita wenzake ‘makanjanja’. Ama mwanasiasa asiye na sera wala mwelekeo, mwenye kazi ya kutafuta namna ya kuwapaka wenzake matope ili kuhalalisha ulafi wake.

Hao wote hapo juu, wanashirikiana tatizo. Wanatafuta kujipandishia hadhi kwa gharama ya maumivu ya wengine. Hawajiamini. Ni muflisi.

Kwa hiyo, kumsema mtu vibaya iwe kwa uwazi ama kwa siri, ni taarifa kamili kwamba anayefanya hivyo anayo hitilafu kubwa ya namna anavyotumia ubongo wake katika kujielewa yeye mwenyewe.

Wapo watu ukikutana nao tu, unajiandaa kusikiliza mabaya ya watu. Mafundi wa maoni angamivu. Matusi mara nyingine. Maneno ya kukinaisha. Kukatisha tamaa wengine. Kuwashusha moyo. Hawa ni watu waliojichokea. Watu wasiojielewa. Hivyo kufanya hivyo ni jitihada zao za rafu katika kujaribu kujifariji na masaibu yao.

Tufanyeje. Nadhani itakuwa ni kazi bure kukushauri tu uachane na tabia hii. Hutaweza. Utataka usiwaseme watu vibaya, yatakushinda. Utatamani usiwavunje wenzako moyo, lakini bado utaendelea kuwaumiza zaidi.

Kuacha tabia hii ni mchakato na si tukio la kufumba na kufumbua. Mchakato wenyewe unatakiwa kuanzia hapa: Ujielewe wewe ni nani, na ujikubali hivyo ulivyo. Uanzie hapo. Ujitengenezee dira/mwelekeo wako mwenyewe. Ujielewe.

Ukijielewa na kujikubali, utashangaa mambo yatabadilika. Utajikuta unawasema watu vizuri. Una maoni ya kuwajenga na kuwatia moyo wenzako. Na hata unapotaka kukosoa, unajua namna ya kufanya hivyo kwa hekima na adabu. Sababu anayejielewa hanaga sababu ya kuwaharibia wenzie ili yeye apate heshima. Anayejielewa hana sababu ya kugombana na watu bila sababu.

Ukiisha kujielewa sasa aya hii itakusaidia: Kabla hujaongea lolote kwa yeyote wakati wowote ule, ni vizuri kuvuta pumzi… kisha jiulize: Je, kwa nini ninataka kusema haya ninayofikiri kusema? Je, maneno haya ninayotaka kusema yatamsaidia msikilizaji? Je, ni kweli nitajitengenezea uhalali wa kweli kwa kusema maneno haya? Je, nikinyamaza, kuna hasara yoyote itatokea? Majibu yakiwa hapana, ni vizuri kunyamaza.

Upo usemi mmoja naupenda. Kwamba mpumbavu anyamazapo, huhesabika kuwa ni mwenye hekima.

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?