Siku nilipokutana na Ojano Kimara

Nakata mitaa Posta mpya. Ni alasiri. Ninakumbuka ahadi ya kwenda kwa rafiki yangu Ojano, Kimara Baruti. Foleni ndefu. Jumlisha joto. Uchovu. Basi nakata tamaa ya kutimiza ahadi yangu hiyo. Ni saa kumi na dakika tano.

Ojano anataka kufufua blogu yake. Alianza kublogu miaka miwili iliyopita, bahati mbaya akapumzika bila kuaga. Ni masomo yalipunguza kasi yake hatimaye, yakamnyamazisha kimojaa. Hivi sasa anayo ari ya “kuzaliwa upya”. Anatamani kuanza ukurasa mpya. Ni mawazo hayo yananipa nguvu ya kuingia kwenye ki-haisi. Huyooo naenda Kimara Baruti kumrudusha Ojano kundini. Nyumbani kwake sikujui. Ameahidi kunifuata kituoni.

“Vipi umefika wapi?” Ananiuliza. Saa zimeenda. Imekuwa saa kumi na moja na nusu Ubungo kwenyewe sijafika.
“Niko njiani…foleni inanichelewesha”. Jiji halifai siku hizi. Idadi ya magari inazidi idadi ya watu. Barabara ni finyu mno. Maelfu ya dakika yanapotelea barabarani kila siku. Siku hizi imekuwa ni sababu tosha ya kujitetea unapochelewa mahali.

Urefu wa foleni unayo faida moja kwetu sisi waenda kwa daladala: Huo ndio muda muafaka wa kujisomea. Kusoma kwenye daladala kunapunguza muda wa kusikiliza kero za konda na abiria wabishi. Kusoma kunakuziba mdomo usiseme seme bila kuhusisha eneo la juu ya masikio.

Basi ninachomoa kitabu changu nasoma. Mara nashtukia niko kituoni Kimara Baruti.
“Niko kituoni Kimara Baruti…” Namwandikia mwenyeji wangu.
“Punde nakuja”. Naendelea kukata kurasa wakati huo nikimsubiri Ojano. Watu wengi kituoni pale. Wengine ni abiria. Wengine wachuuzi. Wengine wakitukanana nk nk nk.

“Angalia mbele yako…mwenye kaptula ndio mimi”. Namwona kwa mbali upande wa pili wa barabara.

“…ujue nilikuwa naangalia mtu ambaye atakuwa ameshika kitabu anasoma. Nilijua utakuwa unasoma hata gazeti…” Anatania huyu bwana.

Haya. Tumeingia kwake. Nakuta vitabu kwa safu kama kawaida ya huyu bwana. Ni mwalimu kwa maneno na matendo. Kanunua kimoja kipya anamtumia mke wake aliyeko Uholanzi. Familia ya kusoma hii. Mara mtandao unaanza kugoma goma. Mara kirusi analeta tishio. Tunahangaika naye mwishowe natushinda akili. Somo la kublogu linaishia hapo hapo. Tunaamua kujadili mambo mengine.

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?