Mawazo yako ndiyo nguvu uliyonayo

Upo uhusiano mkubwa sana baina ya namna unavyofikiri, na jinsi unavyoishi. Kushindwa kwako, hakutegemeani na nguvu yoyote ulivyonayo isipokuwa ufahamu wako. Kuanguka kwako hakutegemei maadui wengi ulionao, isipokuwa aina ya mtazamo ulionao. Kurudi nyuma kwako hakutegemei historia yoyote uliyowahi kuwa nayo, isipokuwa namna unavyoendekeza mawazo yako ya kushindwa.

Naelewa kwamba panahitaji mjadala wa kina kuhusu kipi kinachomtawala mwenzie: mawazo yetu ndiyo yanayotuongoza ama ni sisi ndio tunayaongoza mawazo. Hapo inapidi tushukie penye uelewa na namna mawazo yetu yanavyojengeka vichwani mwetu.

Kwa haraka haraka, nadhani, twawaza vile tulivyoviingiza ubongoni iwe kwa hiari yetu wenyewe ama pasipo hiari hiyo. Kwa maneno mengine sisi ndio watawala wa mawazo yetu.

Hiyo ni kusema kwamba unavyojiona, ndivyo ulivyo. Ukijidharau, hakuna mtu atakuja kukufanyia kazi ya kukuonyesha thamani uliyonayo. Ukianza leo kujiona masikini, ni wazi kuwa akili yako itakubaliana nawe na kusema kweli, utakuwa umeukaribisha umasikini wako kwa mikono yako miwili.

Ningependa kukuachia ujumbe huu mchana wa leo;

Katika kila unalojaribu kulifanya, dhania kwamba haiwezekaniki jambo hilo likashindwa kwa namna yoyote. Kwa sababu, haiwezekani ukashindwa katika jambo lolote, isipokuwa kama utakubali akilini mwako kwamba umeshindwa.

Achana na mawazo ya kushindwa shindwa. Achana na watu ambao hawaishiwi stori za ubaya ubaya. Amua kuyaelekeza mawazo yako kwenye mafanikio. Kwa sababu mawazo yako ndiyo nguvu yako kuu uliyonayo! Itumie nguvu hiyo!

Maoni

  1. Kazi nzuri Bwana Bwaya.
    Ahsante sana kwa kufundisha maarifa haya ya utambuzi,
    Tukipata watambudhi kadhaa kama wewe basi jamii yetu itabadilika.

    PRIVATE

    Kaka nilikutumia ujumbe kwenye simu yako ya kiganjani jana lakini sikupata majibu, kulikoni..........

    JibuFuta
  2. mmmm mkuu hiii ya leo hii kali. ngoja nataka niseme kitu ebuuh nikumbuke kwanza. mmmm mada ni kali sana imenigusa nashindwa kuandika zaidi. kwaheriiiii

    JibuFuta
  3. Hapo kaka umesema, werevu wataelewa,
    Umesema kitu chema, na ndivyo inavyokuwa,
    Umejawa na hekima, chakula umepakuwa,
    Bwaya umesema kweli.

    Shurti tujifikiri, mustakabali wetu,
    Tuwe na fikra nzuri, ikibidi mara tatu,
    Siyo tu tunakariri, na kujiona si kitu,
    Bwaya umesema kweli.

    JibuFuta
  4. @ Kaluse, simu ya kiganjani inayoachwa nyumbani, wakati mwenye nayo yuko matembezini huitwaje? Sijapata jina zuri kuiielezea. Nadhani ulishanisamehe.

    @ Mpangala, asante kwa kuendelea kutembea kibaraza hiki. Ninathamini snaa mchnago wa mawazo ya watu kama ninyi. Endelea kuwapo kaka.

    @Mtanga, napenda sana kusoma mashairi yako. Una uwezo mkubwa sana katika tungo. Hongera sana kaka.

    JibuFuta
  5. mawazo matamu kama CHUKALI vipi unakula sana CHUKALI ya wamakonde wewe?

    JibuFuta
  6. Bwaya mada yako hii ni nzuri sana,nimeikubali lkn kuna mambo kadhaa ya kuongeza.
    Binafsi naona mawazo yangu pekee hayatoshi ktk kunifanya nifikie malengo yangu.
    Kushindwa ktk jambo fulani kunaashiria kikomo cha mawazo niliyokuwa nayo kuhusiana na jambo hilo.Hii inamaanisha kuwa msaada wa kimawazo unahitajika ktk hali hii, kinyume na hapo unaweza fanikiwa lakini ni baada ya kupoteza muda mwingi.
    Mtu anayekumbatia mawazo yake tu,ana hatari kubwa ya kushindwa kujitambua,kuwa mtu wa kutokubali mabadiliko na kuwa mtu wa kujaribujaribu kwani wakati wote atakuwa anajaribu kupima mawazo yake.
    Mtu kushindwa jambo kunatokana na kutumia mawazo yake binafsi kupita kiasi."hivi unapoamua kufanya jambo kwa upeo wako,na jambo lile likashindikana,unajifunza nini?usahihi wa mawazo yako unapimwa na nini?
    "kukubali au kupokea mawazo ya mtu na kuyafanyia kazi na kuyaunganisha na ya kwangu ni matokeo ya kutumia nguvu niliyonayo yaani mawazo yangu"
    umeshawahi kujiuliza, "UNA UWEZO KIASI GANI WA KUYATAWALA MAZINGIRA ULIONAYO?(kuna wakati mawazo ya mtu yanaweza kutumiwa na mtu mwingine na huyu mtu akafanikiwa na pia kutokufanikiwa na kujuta na kusema bora angebaki na mawazo yake.Lakini yote haya ni katika kutumia mawazo kama "NYENZO" pekee niliyonayo kwani maamuzi(mawazo) ndio yalipelekea kutumia wazo la mwingine.samahani Bwaya,nimetumia nyenzo badala ya nguvu,unanaje lakini!)da! Mada ngumuuu sana!

    JibuFuta
  7. Anachosema anon hapo juu ni changamoto muhimu sana. Tujiulize wote je, ni kweli kuwa mawazo yetu yanatutosha? Lakini je, tunapochambua mawazo ya wenzetu, tunajuaje kwamba yana msaada kuliko yale tuliyonayo? Mada tamu sana hii na pana mno.

    JibuFuta
  8. Nadhani kuna haja ya kuangalia namna mawazo yetu yanavyoweza kutegemea mawazo ya wengine na vile vile namna, kama anavyosema Mtingwa, ambavyo mawazo yetu yanaathiri namna tunavyoyachambua mawazo ya wengine. Je, unapokubali wazo la mwingine kipi kimekusaidia, mawazo yake, ama mawazo yako?

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Pay $900? I quit blogging

Haiba ni nini?

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Heri ya mwezi mpya!