Ukishasahau ulikotoka huwezi kuwa mzazi mzuri
Sijui kama umewahi kuwaza kama mimi. Je, mafanikio yetu yanawasaidia watoto kuwa binadamu timamu? Je, uwezo tulionao kiuchumi unawezesha watoto kujifunza tabia zitakazowafanikisha kiuchumi? Kuna namna ninaogopa kuwa huenda tunawanyima watoto wetu fursa ya kujifunza maisha katika uhalisia wake. Nafahamu wapo baadhi ya wazazi wamekulia kwenye familia zinazojiweza kiuchumi. Hata hivyo, hiyo haiondoi ukweli kuwa wengi wetu tumetoka kwenye familia masikini na tumekuwa kizazi cha kwanza kupambana na kuuweza umasikini. Je, tunawaandaa watoto wetu kujikwamua kama tulivyojikwamua sisi?
PICHA: Marlous de Milliano |
Tunafahamu namna umasikini unavyofedhehesha. Umasikini unafanya maisha yako yasiwe na uchaguzi. Umasikini unakufanya upate kinachopatikana na sio kile unachokihitaji. Hili, pamoja na ubaya wake, kwa kiasi kikubwa limekuwa kichocheo cha wengi wetu kuwa na hasira kubwa kupambana na umasikini kwa nguvu zote. Bidii ya kazi unayokuwa nayo ni matokeo ya hasira kuwa usipofanya kazi, ni kweli fedheha ya umasikini itaendelea kukuandama. Hakuna anayekuhurumia, kwa hivyo, hata wewe huna nafasi ya kujihurumia.
Umasikini umetufundisha wengi wetu kuwa na nidhamu. Hatukuwa na namna nyingine zaidi ya kujenga nidhamu ya maisha. Unajua usipojinyima, kwa mfano, utaingia kwenye matatizo na hakuna atakayekusaidia. Nidhamu, kwa mukhtadha huu, inakuwa nyenzo uliyonayo ya kujikwamua na aibu unayoiona nyumbani.
Umasikini, kwa upande mwingine, unakufanya uone bila kuishi vizuri na watu utadhalilika. Tulilazimika kuishi vizuri na majirani tukijua kuna kesho. Amana ya masikini ni kuishi vizuri na wenzake. Unajua jua likiwaka kesho, watakaokuokoa ni marafiki, ndugu na majirani. Ingawa hatukuchagua maisha ya namna hii, kwa kiasi kikubwa, tulazimika kujifunza kukaa vizuri na watu kama silaha ya kufanikiwa.
Ninachokiona ni kama, baada ya kufanikiwa kuhama tabaka na kujiitosheleza, kuna namna tunabadilika. Pengine shauri ya kusahau tulikotoka, tunapata watoto tukiwa tayari tumeshapoteza silaha muhimu zilizotupa maisha. Uwezo wako kifedha, kiwango chako cha elimu, mamlaka uliyonayo, kwa mfano, yanakufanya uwadharau wasiojiweza. Unamkemea mlinzi anayekufungulia geti na watoto wanaona. Unamfokea dada wa kazi na watoto wanaona.
Hizi dharau ambazo, pengine shauri ya umasikini hukuziona kwa mzazi wako, zina nguvu ya kupenyeza somo kubwa kuwa unaweza kuwadharau watu na usipatwe na madhara. Somo la hatari sana hili katika malezi. Ukiweza kuwafanya watoto wasiogope kudharau watu, unakuw umewanyang’anya nyenzo muhimu uliyoitumia kujikwamua.
Kingine kibaya ni huruma kupita kiasi kwa watoto. Tunawahurumia mno watoto wasipitie tulichopitia sisi. Tunaogopa ‘wasiteseke’ kwa kujifulia nguo, kuosha sahani, kutembea kwa mguu, kufagi na kazi nyingine za mikono. Tunaamini mtoto kushiriki kufanya kazi kama hizi ni umasikini. Tunaamini fedha inaweza kufanya hayo yote watoto wakafurahia mafanikio ya wazazi wao. Matokeo ya haya yote ni kuwakuza watoto kuwa tegemezi, wakisubiri mgao wa urithi.
Ukiondoka wewe —na Mwenyezi Mungu aepushie mbali—watoto hawa wanabaki na kazi ya kutapanya kile ulichokitafuta kwa jasho. Makosa uliyoyafanya ni kusahau ulikotoka, kusahau kilichokufikisha hapo ulipofika na kufikiri kuwanyima watoto kilichokuwezesha kupambana na umasikini ndio malezi.
Pamoja na nguvu ya kifedha uliyonayo; pamoja na elimu kubwa uliyonayo; pamoja na mafanikio makubwa uliyopata, kutokusahau ulikotoka ni msingi wa malezi. Mwanao kujua lugha ya wazazi wako, kwa mfano, haiwezi kuwa ushamba. Kwenda kusalimia kijijini ulikozaliwa sio umasikini. Kuitwa jina lako la ‘kinyumbani’ sio kuendekeza mizimu. Kuhakikisha watoto hawasahau mila na desturi zilizokulea wewe hayo ndio malezi.
Kazi za mikono sio umasikini. Kulima bustani nyumbani haiwezi kuwa kumtesa mtoto. Kula ugali mbogamboga sio kuishiwa. Kuingia jikoni na kupika sio umasikini. Mtoto kutandika kitanda chake sio ‘kumfuata-fuata’. Kufua nguo zake mwenyewe sio umasikini. Kuosha vyombo alivyotumia sio umasikini. Kudeki sio umasikini. Kumfundisha mtoto kazi za mikono hayo ndio malezi.
Heshima kwa watu wasiosoma kama sisi, wasio na hadhi kama sisi, wasio na fedha kama sisi sio kujishushia heshima. Kusalimia majirani sio kujipendekeza. Kutumwa na wasionacho sio kuidhalilisha familia. Kuomba msaada kwa jirani sio kujidhalilisha. Kuonywa na mtu mzima sio kuidhalilisha familia. Malezi ni pamoja na kuwafundisha watoto kuwa na kuheshimu watu bila kujali hadhi zao.
Sisi tulikosa na tukapata akili. Kwa nini tunataka mtoto aamini huwa tukosi? Mtoto kukosa anachokitaka haimaanishi huna fedha. Kuishi kwa bajeti sio umasikini. Kujua mzazi huna anachoomba sio kujidhalilisha. Kusoma shule za ‘elimu bila malipo’ sio umasikini. Kutembea kwa mguu sio umasikini. Kupanda daladala sio kudhalilisha familia. Kupanda bajaji sio hatari kwa usalama wake. Mtoto kuitafuta hela yake mwenyewe sio kumtesa. Haya tunayofikiri ni umasikini, kimsingi, ndio maisha yenyewe.
Maoni
Chapisha Maoni