Una nguvu ya kupambana na hali iliyokuchosha
Umewahi kujiuliza kwa nini mtu anapigwa, anaumizwa, anadhalilishwa na mpenzi wake na bado haoni kama kuna kitu anaweza kufanya? Mwingine anasitisha uhusiano lakini anapoanzisha mahusiano anakutana na mwingine mwenye tabia zile zile alizozikimbia kwa aliyemwacha.
Ili kulitafakari hili, nikusimulie alichokifanya Martin Seligman na Steven Maier mwaka 1965. Washunuzi hawa waliwatia mbwa kifungoni kwa kuwafungia kwenye kizimba kisichowaruhusu kutoka. Mle ndani kizimbani mbwa walipigwa shoti ya umeme mfululizo iliwapa maumivu makali. Hata pale ambapo mbwa angefanya majaribio ya kutoroka asingeweza. Kizimba kilikuwa imara.
Kilichowashangaza Seligman na Maier ni kwamba hata pale walipofungua mlango wa kizimba kuwaruhusu watoke, ingawa mbwa wale walilia kwa uchungu, wakilalamika na kutia huruma, hawakuthubu kujaribu kutoka pamoja na maumivu makali ndani ya kizimba. Hali ilikuwa tofauti kwa kundi jingine la mbwa lililokuwa limefungiwa kwenye kizimba kisicho na shoti ya umeme au kilichokuwa na uwezo wa kutoroka mwanzoni wakati wa shoti. Shoti ilipopigwa tu, mbwa hawa walikimbia na kuruka kizimba kujikoa badala ya kulalamika na kujitia unyonge.
Seligman na Maier wakawa wamegundua dhana maarufu katika ushunuzi inayoitwa #LearnedHelplessness —woga unaojengwa na mazingira magumu kumwaminisha mbwa kuwa hana analoweza kufanya kujiokoa na maumivu makali anayopitia. Mbwa anakuwa ameamini yale maumivu ni ‘kazi ya Mungu.’ Tunajifunza nini na utafiti huu?
Unapokuwa kwenye mazingira yenye hatari, unapoumizwa mfululizo na hupati msaada, jitihada unazofanya hazipeti matokeo, ufahamu unakufundisha kuzoelea maumivu. Unayafanya maumivu unayopitia kuwa sehemu ya maisha yako. Husumbuki tena kujaribu chochote kinachoweza kukuokoa. Unaogopa uhuru wako mwenyewe kutoka kwenye kifungo usichokipenda.
Katika hali kama hii, unaanza kutafuta maelezo mazuri kukufariji.
“Mungu amenichagua kuishi na hili zimwi.”
“Mungu alijua ninaweza kulivumilia.”
“Wanaume wote wanafanana. Hakuna mwanamke asiyeteswa na mapenzi.”
Ukishaanza kujisemesha hivi, unaweza hata kumchukia yeyoye anayejaribu kukuhurumia na madhila unayopitia. Unaweza hata kupambana naye umwadhibu kuingilia mambo yasiyomhusu na kufikiri anaweza kukufungulia milango ujiokoe na hali ambayo mwenyewe unajua ni “fumbo la kiimani.”
Kadhalika, ukishaumizwa vya kutosha, ukafanikiwa kuondoka kwenye uhusiano unaokuumiza, unaweza kujikuta unaogopa mtu anayekupenda, unatishwa na mtu anayeonesha kujali, na matokeo yake ukavutiwa na mtu mwingine mwenye tabia kama zile zile zilizokuumiza. Unajikuta kwenye mzunguko ule ule wa maumivu, unawalalamikia watu kwa kile kile unachokijua lakini kinachoshangaza huondoki na wala hukomi.
Kujiokoa katika hali kama hii kunaanza na kukubali kuwa una nguvu ya kupambana na hali ngumu unayopitia. Hakuna atakayeweza kukuokoa na hali unayoifanya kuwa sehemu ya maisha yako.
Maoni
Chapisha Maoni