Madhara ya Kutoa Ushauri Kienyeji na Kuugeuza Unasihi kuwa Ushauri

Utamaduni wa (kutoa na kuomba) ushauri umejengeka kwenye misingi ya hekima ya wazee walioona mengi, uzoefu wa mtu mzima unaompa uhalali wa kutoa mwongozo wa kufuata kwa anayemzidi. Hata tunaposikia unasihi (counselling), aghalabu, mawazo yetu yanaenda kwenye taaluma ya kushauri watu na kuwaambia cha kufanya ili kutatua matatizo yanayowakabili. Wapo, tena wengi, wanaotafsiri ‘counselling’ kama ushauri. Counselling sio ushauri.

Katika makala haya, ninajenga hoja kuwa kutoa ushauri ni jambo la hatari na kwamba linaweza kusababisha madhara makubwa kwa anayeshauriwa lakini pia hata anayeshauri. Kadhalika, ninalenga kuonesha, japo kwa ufupi kuwa hata kwenye unasihi msingi wa kwanza wa kuzingatia kwa mtoa huduma (aliyefuzu) ni kuepuka kabisa kutoa ushauri kwa mtu. Nakusudia kuonesha nini hasa huwa ni malengo ya unasihi.

stefanamer/Getty Images


Ushauri ni nini? 

Unaposema unamshauri mtu unakuwa na maana gani? Ushauri, kwa kifupi, ni maelekezo mahususi unayompa mtu, maamuzi unayomfanyia mtu ulilenga yawe mwongozo wa nini anapaswa kufanya (au kipi hatakiwi kufanya) kama namna ya kutatua tatizo lake au kufanya maamuzi. Unapomshauri mtu maana yake tayari analo tatizo linalomsumbua, ana mtanziko wa kuelewa aamue nini na wewe unaamini unajua kwa hakika tatizo lake ni lipi, unajua anataka nini, anapaswa kufanya nini na hivyo una taarifa za kutosha na uzoefu utakaomsaidia akiufuata kama majibu ya kile anachotaka kukiamua. 


Ushauri, hata hivyo, ni tofauti na maoni, mawazo na uzoefu unaomshirikisha mtu ukikusudia kumsaidia katika mchakato wa kulitazama vizuri suala lake bila kumpa malekezo ya kipi afanye na kipi asifanye. Unapomshirikisha mtu kile unachoamini unakifahamu, kama ninavyofanya hapa, humshauri. Maoni yanayogeuka ushauri, katika mipaka ya makala haya, ni yale yanayojielekeza kwenye tatizo mahususi uliloambiwa, na kisha yakatolewa kwa namna unayoonesha kuwa mwenye shida anatakiwa kufanya nini kutatua tatizo lake.


Kwa nini watu hushauri? 

Wengi wetu tunaamini kuwa tunapotoa ushauri, faida inayokusudiwa ni kwa ajili ya yule mwenye shida ‘anayeuhitaji sana ushauri wetu.’ Tunaamini tunasukumwa na upendo kumshauri mtu lengo likiwa ni kumsaidia kutatua suala lake. Lakini fikiria kidogo mazingira ambayo umemshauri mtu vizuri na akaukataa ushauri wako. Huwa unajisikiaje? Kwa nini uumie kama lengo la ushauri lilikuwa kumsaidia anayehitaji ushauri wako? 


Fikiria pia umemshauri mtu akautumia ushauri wako kama ulivyomshauri lakini hatimaye mambo yakaenda ndivyo sivyo. Unajisikiaje? Kwa wengi tutajisikia vibaya na huenda tukafanya jitihada za maksudi kujitenga na ushauri tulioutoa. Unatataka ionekane tatizo ni kutokueleweka au basi aliyeshauriwa ameutumia vibaya. 


Huo ni ushahidi rahisi kuwa mara nyingi tunaposhauri msukumo mkubwa tusiousema wazi ni kujisikia tunajua, tuna uzoefu, na hivyo tuna haki ya kumwambia mtu afanye nini na kipi asifanye. Ndio kusema tunashauri  kwa ajili yetu —kulinda hadhi na heshima zetu, tunatumia tatizo la mtu kujaribu kuonesha tunavyomzidi hali inayoweza kutafsirika kaka kujikweza na kujiona bora. Kumbuka tunazungumzia ushauri ule unaomuonesha mwenye shida kuwa tunajua wakati mwingine kuliko yeye.


Hatujui mengi kuhusu mtu

Mambo mengi tunayoambiwa na watu wanaopitia channgamoto fulani ni ukweli nusu ulichaguliwa kuelezea sehemu ndogo ya uhalisia wa jambo.  Nikigombana na rafiki yangu, kwa mfano, nitakuambia ukweli usioharibu heshimu yangu. Nitalalamikia mengi yanayomhusu rafiki lakini wakati huo huo nikificha mapungufu yangu. Isipokuwa kama unachoambia ni kitu cha kawaida lakini mara nyingi watu huchagua cha kusema na hivyo taarifa wanazotupa hazitoshi kuelewa matatizo yao kwa undani wake. Je, kwa mazingira haya ni busara kutumia kidogo unachokijua kumwambia mtu afanye nini? Huoni namna ushauri wako unavyoweza kumpotosha mwenzako?


Matatizo yanayosonga nafsi ya mtu na kumnyima amani, mara nyingi, ni msongamano wa mengi yanayopandana hatua kwa hatua. Hatuongei na mke wangu, kwa sababu, zilizojengeka kwa muda mrefu. Saa nyingine tatizo langu moja huleta tatizo jingine kwa mwenzangu ambalo nalo linaleta tatizo jingine kwa mwenzangu. Huwezi kuelewa tatizo langu kwa kutazama jambo fulani na ukaliachia hapo. Tena, mara nyingine, unalazimika kutumia muda mwingi wa kuuliza na kulielewa tatizo kwa upana na kina chake badala ya kukimbilia kunileta jibu la haraka.


Unakutana na mtu analalamika hapendwi wakati ukifuatilia mzizi wa wazo hilo ni yeye mwenyewe kutokujipenda na kujisamehe. Kila anapoingia kwenye mahusiano anaharibu kwa sababu yeye ndiye tatizo lisiloonekana waziwazi. Ukisikiliza anacholalamikia ukafikiri tatizo ni kutokupendwa unaweza ukatoa ushauri utakaoendelea kumdidimiza kwenye tatizo lake wakati kumbe anachokilalamikia ni kiashiria tu cha tatizo kubwa lisiloonekana waziwazi na linalohitaji muda wa kutosha kulielewa.


Kwa nini hatu hutafuta ushauri?


Hapa kuna mengi ya kutafakari. Kwanza, kuna hili la nafsi kuzidiwa. Mtu anapotafuta msaada kwa jambo linalogusa siri zake, kwa mfano, kuna uwezekano mkubwa anakuwa amechoka kubeba mzigo mzito. Saa nyingine sehemu ya ufumbuzi wa shida yake ni kuwa na mtu anayesikiliza basi. 


Pili, kutokuwa na imani kuwa anaweza kutatua tatizo lake yeye mwenyewe —hopelessness. Kuna wakati mtu anajiona kama hana uzoefu, hana taarifa za kutosha kumsaidia kufanya maamuzi. Kaja kuomba ushauri kwa vile hajiamini na sio kweli kwamba hana majibu. Pia kuna tafiti zinaonesha kuwa watu kutafuta ushauri wakiwa na majibu tayari. Mara nyingi wanapoomba ushauri wanatafuta uungwaji mkono zaidi kuliko kutafuta majibu.


Ukilielewa hili, unaweza ‘kumshauri’ mtu kitu kinachoendana na kile alichokuwa amepanga tayari kukifanya na ukashangaa anakushukuru kwa ushauri mzuri —umemwambia alichotaka kukisikia. Usipojua mtafuta ushauri anaweza kuwa na majibu tayari na anachokitaka ni sapoti ya maamuzi yake unaweza kujiingiza kwenye matatizo ya ushauri wako unaweza kukataliwa.

Tunatofatiana

Umewahi kuwaza ni kwa kiwango gani tunatofautiana? Tunaamini vitu tofauti. Tunaogopa vitu tofauti. Tuna matamanio tofauti. Tuna malengo tofauti. Tunaishi maisha tofauti. Kinachofanya kazi kwenye mazingira yako, sio lazima kifanye kazi kwenye mazingira ya mwingine. Unachofikiri ni sahihi kwako kinaweza kuwa sumu inayoua kwa mwingine. Hili ni gumu kwa sababu kwa kawaida binadamu huamini anachoamini yeye ndio sahihi na wengine ‘wanatakiwa’ kukiamini. 


Ukilielewa hilo hutajipa kazi ya kuwa mwalimu wa maisha ya watu. Unaweza kuharibu maisha ya mtu kwa kufikiri uzoefu wako unatosha kuwa majibu ya matatizo ya watu wote bila kujali mazingira yao. Kabla hujaharakisha kutoa ushauri wa nini mtu afanye, jisumbue kidogo kuielewa dunia yake —anaamini nini, tunu zinazoongoza maisha yake ni zipi, misimamo yake ni ipi, nini hawezi kukibadilisha na kadhalika na kadhalika.

Unajua matokeo ya ushauri wako?

Umewahi kufikiri ni kwa kiwango gani unawajibika na ushauri wako au unafikiri unaweza kushauri tu na ukayakimbia matokeo? Umejiandaa kwa matokeo ya ushauri wako? Gharama ya ushauri ni kuwajibika matokeo ya ushauri wako. Unapomwambia mtu akafanye nini kutatua tatizo lake, jiandae kwa matokeo ya ushauri wako. Ukimshauri mtu akalime, unawajibika na matokeo atakayokutana nayo shambani. Ukimshauri kijana amuoe fulani, unawajibika na yatakayotokea kwenye ndoa. Kama hauko tayari kubeba lawama za moja kwa moja au za kimya kimya, basi tafakari upya unapotaka kumpa mtu ushauri. 

Shauri ikiwa una uhakika kwa 100% kuwa unachoshauri kitatokea. Kama jambo lina ushahidi wa kisayansi, kwa mfano, litoe kama shauri ukijua kwa hakika kuwa likifanyika litatua shida ya mtu. Kama huna uhakika huo, au unataka uzoefu ulioupitia wewe ndio iwe sheria ya maisha, jitahidi kutokujipa umuhimu sana kwenye maisha ya watu.


Nini kifanyike?

Ikiwa kushauri ni hatari kwa kiasi hicho, tufanye nini basi? Mbadala wa ushauri ni nini? Nina mapendekezo kadhaa. Sijakushauri. Shirikisha uzoefu wako bila kuulazimishia kwa mwenzako. Unaweza kusema unavyoliona jambo pasipokumaanisha mwenzako naye aone unavyoona wewe. Kusema ulifanyeje ulipokuwa kwenye mazingira kama hayo, ni tofauti na kumwambia mwenzako akafanye nini. Usiwe mwepesi kushauri. Kama huna uzoefu na jambo hilo, halijawahi kukuta, hujawahi kulipitia, pengine wewe sio mtu sahihi.


Mpe mwenzako taarifa muhimu unazoamini zitamsaidia kufanya maamuzi. Kwa mfano, badala ya kumwambia mtoto akasome masomo fulani, unaweza kumsaidia kumpa taarifa aone masomo hayo yanampeleka wapi na anahitaji sifa zipi kujiunga nazo. Usishauri. Shirikisha taarifa. Kumpa mwenzako taarifa si sawa na kumwamlia akafanye nini. Kama unaona taarifa ulizonazo zitamchanganya zaidi, tafuta namna ya kuzirahisisha. Kama huna taarifa unazoamini zinaweza kumsaidia mwenzako basi huenda wewe sio mtu sahihi. 


Kama nilivyokwisha kugusia, watu wengi wanatafuta mtu wa kuwasikiliza zaidi kuliko mtu wa kuwaambia wakafanye nini. Sikiliza shida ya mwenzako. Msikilize kuliko kumwambia akafanye nini. Onekana unajali. Sikio linalosikiliza linatosha kumpa mtu nguvu ya kutatua matatizo yake. Ili uweze kumsikiliza mtu, muhimu kujifunza kukwepa kuhukumu na kuharakisha kuelewa usichoelewa.  Rudia unachoambiwa kwa maneno yako. Uliza na mpe nafasi mwenzako aseme. Huna sababu ya kutolea maoni kila unachoambiwa. Saa nyingine tingisha kichwa panapohitaji uoneshe kuguswa.


Lakini pia, heshimu matatizo ya watu kwa kutokuyarahisisha. Namna moja ya kufanya hivyo, ni kumwelekeza kwa mtaalam anayeweza kumsaidia kutatua tatizo lake. Usijipe utaalam wa mambo usiyoyaelewa kwa upana wake. Kama unampenda mwenzako, mwambie awasiliane na nani unayeamini atamsaidia.

Dhana ya unasihi

Unasihi (counselling) si taaluma ya kutoa ushauri kinyume na inavyosikika. Unasihi ni taaluma ya kusikiliza watu, kuwapa sikio linaloelewa bila kuhukumu mtu, ni taaluma ya kuwatupia watu mbeleko inayowakumbusha kuwa hawako peke yao wanapotafuta majibu ya matatizo yanayowasumbua. Katika kufanya hivyo, unasihi unamuwekea mazingira salama mtu anayesikilizwa kujiamini zaidi, kuona nyenzo alizonazo kwenye mazingira yake, zinazoweza kutumika kulitatua tatizo lake, kufika mahali akagundua kumbe anaweza kukusanya nguvu zake na nyenzo alizonazo kulikabili tatizo lake bila utegemezi uliopindukia kwa mnasihi. 

Kadhalika, ni kweli yapo matatizo yanayohitaji maelekezo mahususi kulingana na uelewa wa kitaalam. Katika mazingira haya, mnasihi anatarajiwa kuwa mtaalam aliyebobea kwenye mirengo mbalimbali ya ushunuzi (psychology) inayomsaidia kulitazama tatizo la mtu kwa mapana na hivyo kumsaidia kulishambulia kwa mbinu zilizothibitika (evidence-based) lakini zinazoendana na mazingira aliyonayo.  Uelewa huu unaotumika kumsaidia mtu kamwe si maoni wala uzoefu binafsi bali uelewa unaotokana na mirengo ya kishunuzi.

Kwa hivyo, mtu yeyote anayekimbilia kukupa majibu yenye sura ya, “mbinu sita za kutatua mgogoro wako,” “Fanya hivi kumtuliza mume wako,” “Usioe mwanamke wa hivi,” “Kama hawezi kufanya hivi huyo sio mume,” huenda si mnasihi au anatumia vibaya unasihi na pengine anafanya biashara kwa kutumia matatizo ya watu. 






Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Pay $900? I quit blogging

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3

Haiba ni nini?

Kama sio utumwa ni nini hiki?

Uislamu ulianza lini?

Tabia za Mtoto wa Miaka 0 – 3 Kimahusiano na Kihisia