Usiyempenda anaweza kuwa baba wa mwanao?

 


Watoto wanahitaji uwepo wa mzazi. Simulizi la Slaquara lilitukumbusha hakuna muujiza kwenye malezi. Mzazi unavuna ulichopanda. Renee anakazia funzo hilo. “Umeongelea athari za umbali kati ya mzazi na mwanae. Nayajua maumivu yake,” anasita na kufafanua, “Sikumbuki lini niliongea na mama yangu. Siwezi kusema ni adui yangu lakini sio mtu naweza kumtegemea kwa lolote.”

 

“Mara ya mwisho kuonana naye ni miaka miwili iliyopita alipokuja kusuluhisha mgogoro wangu na mzazi mwenzangu,” leso anayoitumia kujifutia inalowa machozi. Renee anaikunjua na kuigeuza kutafuta penye ukavu. “Nilimpa nafasi ya pili akaitumia vibaya. Badala ya kusikiliza upande wangu anielewe, aling’ang’ania kuwa upande wa yule mwanaume akinilazimisha kuishi naye. Hakutaka kabisa kuelewa kwa nini nilichagua abaki kuwa mzazi mwenzangu na si zaidi ya hapo.”

 

Mgororo huu mkubwa wa mzazi na mwanae umeanzia wapi? Renee anasimulia, “Nimekuzwa kama mtoto yatima. Nasimuliwa baba alipofariki nikiwa mdogo sana, mama alinipeleka kwa shangazi. Shangazi alipambana kuhakikisha ninasoma na kupata mahitaji yangu. Lakini kilichonisumbua ni yale maumivu ya kumkosa baba. Kilichokuwa kinauma zaidi mama nilijua yupo lakini sikujua yuko wapi. Shangazi labda alilinda hisia zangu kwa hiyo hakuwahi kunipa majibu yanayoeleweka zaidi ya kuniambia anaishi Mwanza aliko bibi.”

 

Mazungumzo yetu na Renee yanageuka kuwa maombolezo. Kashikilia leso aliyoigeuza pande zote na bado imelowa machozi, “Usiombe hiyo hali ya mtoto unamhitaji mzazi wako usiyejua yuko wapi.”

“Nilisoma bweni shule ya masista. Kuna ule upweke unapoona wenzako wanatembelewa na wazazi wao. Siku moja kama kichaa nilitoroka nyumbani nikapanda basi niende Mwanza.” Renee hakuwa mkubwa kivile. Mtoto wa shule ya msingi. Nauli ni hela aliyokuwa anaficha kidogo kidogo. Taarifa kubwa iliyomwongoza ni kazini kwa bibi. “Nilifika ofisini saa za jioni. Nikauliza. Labda kwa ule mshangao wa kuona mtoto mdogo nimetoka Dodoma kuja kumtafuta bibi Mwanza watu walinisaidia. Baada ya kuhangaika sana nikampata.”

 

“Bibi aliponiona aliangua kilio. Hatukuwa tumeonana miaka mingi lakini ninafanana sana na mama. Basi kesho yake bibi akanipeleka kwa mama. Furaha isiyo kifani kumwona mama yangu mzazi.”

 

Kilichomshangaza Renee ni mama kutokuonekana kujali. Hakuwa na ule msisimko wa kuonana na mwanae. “Nimekaa naye kama mwezi lakini nilianza kuhisi kuna tatizo. Nilijiuliza maswali mengi. Labda mama na baba walikuwa na ugomvi. Nilijiona kama sihitajiki kwenye maisha ya mama yangu.”

 

Renee anayakumbuka maisha ya utoto wenye upweke. Hakuwa na mtu wa karibu kumsikiliza. Balehe ilimvamia hajajiandaa. Hakuwa na mtu mzima wa kumfunda zaidi ya marafiki rika ambao nao hawakuwa wanajitambua.

 

Kupitia marafiki Renee alikutana na mwanaume asiyemfahamu sana. Ombwe la kueleweka likawa kama limejazwa. Mara ya kwanza Renee anakutana na mtu ‘anayempenda’ na ‘kumjali.’ Hasimulii mengi lakini anaonekana kufurahia kipande hicho cha maisha yake. Lahaula. Msisimuko unageuka shubiri. Renee ana mtoto na mwanaume mtu mzima. Mambo mengi hapa Renee anasita kunisimulia lakini baadae anagundua mtu pekee aliyemwamini tayari alikuwa na familia yake. Je, akubali nafasi ya uke wenza? Kesi inatua kwa mama.


“Kuolewa siku hizi ni bahati. Olewa na mwanaume huyu mwanangu. Nani atakubali aibu ya wewe kuwa mama asiye na mume?” Renee anakumbuka wosia wa mama. “Ushauri huu unatoka kwa nani?” Renee anauliza na kujijibu, “Si huyu mama aliyenipuuza kwa miaka yote? Huu ushauri ‘mzuri’ unaotolewa leo ni kwa ajili yangu au basi mama anataka kunitumia kwa faida yake?”


Renee amefanya maamuzi. Harudi nyuma. Hatakubali kuolewa na mwanaume tapeli. Lakini vipi uhusiano wa mwanaume huyo na mwanae umekaaje? Maelezo marefu. Ninakumbuka alivyomalizia, “Nafahamu maumivu ya kumkosa baba. Huyu jamaa ameniumiza sana na sitakaa nimsamehe. Lakini, kwa mazungumzo haya, kitu siwezi kuendelea kufanya ni kumnyima mwanangu haki ya kuwa na baba yake. Natafuta msaada wa namna ya kutenganisha maisha yangu binafsi na hitaji la mwanangu la kuwa na baba yake.” Renee anafikiria namna mtu asiyempenda anavyoweza kuwa baba wa mwanae.


Niandikie: bwaya@learninginspire.co.tz 

Maoni

  1. Binafsi nimekuwa natamani kutoka katika changamoto hii lakini naona si rahisi, watoto kukua bila wazazi wetu ni janga hatari sana kwa kizazi hiki.
    Kuna muda naona ni bora kuwa yatima kuliko kuwa na wazazi kivuli na ambao hujui kama wanakufikiria au wapo busy na familia zao nyingine.

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mambo ya Kuzingatia Unapoandika Wasifu wa Kazi (Curriculum Vitae)

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Zijue Tabia Nne za Kiongozi Bora Kazini

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3