‘Homework’ Zinavyodumaza Ukuaji wa Watoto Wadogo


PICHA: PhillyVoice


Ukiwauliza wazazi kitu gani wanafikiri kikisitizwa mapema zaidi kwa watoto kitawasaidia kufanikiwa, wengi  watakwambia elimu. Kwa sababu hiyo, wazazi hasa wasomi wanaharakisha kuwapeleka shule watoto wenye umri mdogo.

Ninawafahamu watoto wengi wa miaka minne wanaosoma darasa la kwanza. Wazazi wa watoto hawa wanafanya hivyo wakiamini mtoto akisoma mapema, maana yake uwezekano wa kufanikiwa maishani unakuwa mkubwa.

Shuleni pia, watoto hawa wanakutana na walimu wanaofanya kila linalowezekana kuhakikisha ‘wanafaulishwa’ mitihani. Sababu ya walimu kufanya hivyo, kama nilivyogusia kwenye makala yaliyopita, ni kujaribu kukidhi matarajio yetu sisi wazazi.

Mbali na mtoto kufundishwa mambo mengi yanayomzidi umri wake, kuna hili la walimu kuwapa watoto kazi nyingi wanazotakiwa kuzikamilisha baada ya muda wa masomo. Kazi hizi, maarufu kama ‘homework,’ zinafahamika kama kazi za nyumbani.

Faida

Kazi hizi za nyumbani zina nafasi ya kutengeneza daraja muhimu kati ya mazingira ya shule na nyumbani. Mwalimu anapompa mtoto kazi hizi, kimsingi anatarajia kumfanya mzazi awajibike kutengeneza mazingira ya kitaaluma nyumbani.

Mathalani, mzazi atalazimika kuacha kazi nyingine na kumsaidia mtoto kukamilisha kazi. Kufanya hivi kunamlazimisha mzazi kujenga ukaribu na mwanae na pia atafuatilia maendeleo yake kimasomo. Mawili haya yanasaidia kutilia mkazo kile ambacho mwalimu anakuwa amekifundisha darasani.

Kadhalika, ‘homework’ zinamfudisha mtoto tabia ya kuwajibika. Inaeleweka kwamba mtoto anaporudi nyumbani na kazi za shule, akili yake inakuwa na kazi ya kuhakikisha wajibu aliopewa na mwalimu shuleni unakamilika.

Harris Cooper, wa Chuo Kikuu cha Duke amefanya tafiti nyingi kuhusiana na utamaduni huu. Profesa Cooper anasema, “Kazi za nyumbani ni utaratibu mzuri wa kujifunza. Kuna faida kadhaa, lakini faida hizo zinategemea umri wa mtoto.”

Kwa watoto wa madarasa ya awali (yaani shule ya awali na msingi), Harris Copper anafikiri inatosha shughuli ya mtoto kufanya kazi za shule iishie darasani.

Mwalimu akitumia muda wake vizuri darasani, hana sababu yoyote ya kumpa mtoto kazi za ziada kwa sababu hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya wingi wa kazi za nyumbani na mafanikio ya mtoto kimasomo.

Nikijitolea mfano mimi mwenyewe, pamoja na kuwa mtoto wa mwalimu, sikumbuki ni lini niliwahi kukaa nyumbani nikifanya kazi za shule nikiwa nasoma shule ya msingi. Kazi zote za shule ziliishia shuleni na niliporudi nyumbani nilifanya mambo mengine yasiyo na uhusiano na shule.

Baada ya masomo, ratiba ya nyumbani ilikuwa ni kumsaidia mama kufanya kazi za mikono kama kusafisha vyombo, kufua nguo zangu, kuteka maji, kutumwa dukani na shughuli nyingine za kawaida.

Nilipokamilisha shughuli nilizopewa, nilikwenda kucheza na kufanya shughuli nilizozipenda kama kucheza mpira, kuruka kamba, kuchora na hata  kusoma hadithi. Bado, hata hivyo, nilitumia muda wangu wa shule vizuri na nilifanya vizuri shuleni.

Tafiti tofauti

Etta Kralovec, Profesa wa Elimu, Chuo Kikuu cha Arizona anasema, “Tafiti ziko wazi kabisa kuwa masaa mawili ya kufanya kazi za shule baada ya muda wa shule, yanatosha kwa mtoto mkubwa (wa sekondari.) Lakini kwa mtoto mdogo (shule ya msingi), kazi za nyumbani hazina faida ya maana.”

Binafsi nimekuwa nikifuatilia kazi ambazo watoto wengi wa madarasa ya chini wanapewa kuzikamilisha nyumbani. Nyingi, kwa kadri ninavyoziona, hazina ulazima wowote zaidi ya kujaribu kumwaminisha mzazi kwamba kuna kitu kinafanyika shuleni.

Kwa mfano, kazi nyingi ni za kukariri kwenye vitabu, ambavyo mara nyingi havijapitiwa kwa makini na wataalam kujiridhisha ikiwa vinafaa kwa watoto wadogo.

Pia, baadhi ya vitabu vina masimulizi yenye maudhui yasiyolingana na umri wala utamaduni wetu lakini ndio vitabu ambavyo watoto wetu wanatumia muda mwingi kuhangaika navyo kukamilisha kazi za nyumbani.


Changamoto

Mtoto anayeanza shule, anahitaji kusaidiwa kupenda kujifunza na kuona shule ni mahali pazuri. Utamaduni huu wa kuwapa watoto kazi nyingi, hata hivyo, unawafanya watoto hawa waanze kuchoka shule.

Fikiria mtoto wa miaka mitatu anayehitaji kucheza, anajikuta kwenye mazingira ambayo kuna mtu anamlazimisha kujua kujumlisha na kutoa.

Ingawa ni kweli mtoto anaweza kujifunza kwa lazima, lakini kufanya hivyo kunaweza kumdumaza mtoto kwenye maeneo mengine muhimu ya ukuaji. Mfano mdogo, watoto wengi hujikuta kwenye migororo mikubwa na wazazi wao kwa sababu tu hawajafanya kazi za shule.

Badala ya kukaa na kuwafundisha watoto wao maadili, tunu za maisha na kuwakuza kiroho na hata kujenga mawasiliano ya karibu, wazazi wengi wanaishia kufokeana na watoto kwa sababu tu hawajakamilisha kazi za nyumbani.

Mara nyingi watoto hawafanyi kazi hizi si kwa sababu ni wavivu, wajeuri au si wasikivu. Hasha. Mara nyingi sababu ni ukweli kwamba tumewaingiza kwenye mduara wa shinikizo la kitaaluma mapema zaidi kuliko umri wao.

Kujenga utegemezi

Fikiria mtoto ameshindwa kufanya kazi alizotakiwa kuzifanya kwa uzembe. Katika mazingira kama haya, mzazi anageuka kuwa afande anayehakikisha kazi zote zimefanyika hata kama mtoto mwenyewe kimsingi haoni maana ya kile anachotakiwa kukifanya.

Inapotokea  mtoto hana uwezo wa kuzifanya, badala ya mzazi kubeba wajibu wa kukazia yale ambayo mtoto alijifunza shuleni, mzazi anaamua kuzifanya mwenyewe kwa niaba ya mtoto, ili mwalimu shuleni asione mtoto hana mtu wa kumsaidia anaporudi nyumbani.

Hapa tunatengeneza tatizo jingine la mtoto kujenga utegemezi kwa watu wazima na kumnyang’anya mtoto tabia ya kuwajibika kwa mambo yanayohusu.

Ingawa kumsaidia mtoto kukamilisha kazi zake inaweza kuonekana kama mchango chanya wa mzazi kwa mtoto, tabia hii inaweza kupanda mbegu ya kuwategemea watu wengine hata atakapokuwa mtu mzima.

Ushauri

Shughuli zisizo za kitaaluma moja kwa moja zina nafasi kubwa ya kumfundisha mtoto vizuri zaidi kuliko kazi za nyumbani. Kwa mfano, kuwasomea na kuwasimulia watoto hadithi ni namna bora zaidi ya kuwafundisha watoto mambo wanayoyahitaji katika maisha yao ya kila siku.  

Baada ya shughuli ya kujifunza shuleni, ni vyema nyumbani pawe sehemu ya kumfanya mtoto ashiriki shughuli nyingine akiwa na familia yake.


Pia, tuweke mazingira ya mtoto kutumia akili yake katika kuyachunguza mazingira yake kupitia michezo na kazi za mikono. Shughuli hizi tunazoona hazina maana, zina nafasi kubwa ya kukuza uwezo wa mtoto kukumbuka, kuzingatia, kufikiri kwa haraka, kukaa na wenzake na hata kuvumbua vipaji vyake ambavyo wakati mwingine hatuvigundui kwa sababu muda wote tunataka afanye hesabu, asome na aandike.

Maoni

  1. nimefurahishwa na mada hii nzuri bwana Bwaya ingawa Homework zangu za ukubwani zimefanya nichelewe kuweka hoja zangu, lakini naungana kabisa na hoja yako kuhusu Homework.
    Binafsi nakumbuka sana wakati nakua kijijini huko ambako kwa kweli ufaulu ni mdogo, maswala haya ya Homework yalikuwa hayapo kabisa, Ingawa tulikuwa hatufurahii shule kwa sababu ya viboko, ila muda wa nyumbani ulikuwa hauna maswala ya Homework.

    Nadhani basi inabidi wazazi waelimishwe namna bora ya kuspend muda na watoto wao, na pia shule hizi zielemishwe pia. Si siku nyingi iligundulika kuwa uwezo wa watoto kujua kusoma ,kuandika na kuhesabu ulipungua sana kiasi kwamba Baadhi ya watoto walikuwa wakimaliza elimu ya msingi bila kuwa na uwezo wa kusoma kitabu cha darasa la tatu kwa usahihi!

    pengine ni kwa sababu homework nyingi ambazo pia hulazimika kufanywa na wazazi ili mwanae kesho asioneakana mjinga shuleni !

    swala la kujiuliza, mwalimua anaandaliwa kweli ili kuwa na namna bora ya kumaliza kila kitu? je ikiwa darasa lina wanafunzi 50, na nyenzo hakuna? na je wazazi ambao pia hawaelewi na hawana muda? Je nafasi ya katuni na toy ambazo sasa zinatawala muda mwingi wa watoto?

    ahhah

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Haiba ni nini?

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Makundi Manne ya Tabia za Watoto Kitabia

Uislamu ulianza lini?