Mtoto ni nani?

Sheria na mikataba mbalimbali inayozungumzia huduma na haki za mtoto, inamtambulisha mtoto kama mtu yeyote mwenye umri wa miaka chini ya 18. Hata hivyo, kutumia umri kama msingi wa tafsiri ya utoto hakuwezi kutusaidia kujua kwa nini mtu mwenye umri huo aitwe mtoto. Katika makala haya, ningependa tumtazame mtoto kwa kuangalia mitazamo tofauti katika jitihada za kumtofautisha mtoto na mtu ‘mzima’ bila kutumia idadi ya miaka kama msingi mkuu.

Mitazamo mbalimbali ya dhana ya utoto
Mosi kabisa, kuna mtazamo wa ukuaji. Hali ya ukuaji wa mwili inayosababisha mabadiliko yanayoendana na upevukaji, mabadiliko ya homoni, uelewa wa mtu na kadhalika huweza kuchukuliwa kama kigezo cha kumtofautisha mtoto na mtu mzima. Mtoto tunamtazama kama mtu mwenye viungo viteke vinavyoendelea kukua, wakati mtu mzima ni yule asiyefikia kimo cha upevukaji. 

Mabadiliko yanayoongoza ukuaji wa mtoto yanaweza kupimwa na njia za kisayansi ili kuelewa maendeleo ya jumla yanayofanana kwa watoto wote bila kujali wanakoishi na athari nyinginezo za kimakuzi. Ingawa kigezo hiki hakizingatii ukweli kwamba kila mtoto ni mtu tofauti na watu wengine wa umri wake, bado kwa kutumia wastani wa yale yanayoonekana kuwa ‘kawaida ya watoto wa umri fulani,’ tunaweza kuwachukulia wengine wenye tofauti na kawaida hiyo kuwa na ukuaji usio wa kawaida. 

Kadhalika, tafsiri ya mtoto inaweza kuathiriwa kwa kiasi kikubwa na historia, tamaduni na mienendo ya jamii. Uelewa wa nini kinamfanya mtu ahesabike kuwa mtoto na wakati gani watoto hukoma kuitwa watoto na kuingia kwenye utu uzima, unatofautiana katika jamii zetu.  Ndio kusema utoto ni dhana inayoweza kuumbwa kwa namna mbalimbali kutokana na mahitaji ya jamii yenyewe na sio lazima iwe mahitaji ya mtoto mwenyewe. 

Katika jamii nyingi za ki-Afrika kwa mfano, matukio fulani yanaweza kuchukuliwa kuwa mpaka wa utoto na utu uzima. Kuna mila kama jando/unyago, ndoa na kadhalika vinavyotazamwa kama kivuko cha utoto kwenda utu uzima. Pia zipo imani/mila za kidini zenye matukio ya namna hiyo kama kipaimara, sakramenti ya kwanza na kadhalika. Haya yote ni matukio yenye ‘uwezo’ wa kumvusha mtoto kwenda utu uzima bila kueleza ni mambo gani hasa yanamfanya mtu aonekane ni mtoto au mtu mzima. 

Aidha, mtazamo mwingine wa kumwangalia mtoto kwa jicho la mahitaji yake ya kimsingi na namna tunavyoweza kuyajibu mahitaji hayo. Mtazamo huu unatumika na mashirika, taasisi na watu wenye kufikiri namna ya kutoa huduma za ustawi wa watoto kisera na kisheria. Hawa wanatumia mahitaji ya mtoto kupanga kile wanachotaka kukifanya kwa mtoto na hivyo kuamua nani ni mtoto na nani siye.

Kwa mfano, watetezi wa haki za watoto huweza kumchukulia mtoto kama mtu yeyote mwenye umri fulani asiye na uwezo binafsi wa kujitetea na hivyo kuhitaji kulindwa na unyanyasaji au ukiukwaji wa haki zake fulani fulani. Kadhalika, kuna mashirika kama yale yanayowatafutia ufadhili watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu. Kwao mtoto anaweza kuwa mtu yeyote anayemtegemea mtu mwingine katika kupata mahitaji yake bila kuzingatia sana umri. Mtoto anaweza kuwa hata baba wa miaka 25 almuradi bado yuko kwenye orodha ya wanufaika wa ‘mradi wa kuwasaidia watoto.’

Uwezo unaowapambanua watoto kwa ujumla
Katika mipaka ya makala hii, tutajaribu kuangalia tafsiri ya mtoto kwa kutumia mtazamo wa yale anayoweza/asiyoweza kuyafanya kama matokeo ya ukuaji wa mwili. Kiujumla, tunaweza kusema mwili wa huyu anayeitwa mtoto unaendelea kuumbika na kuongezeka kwa kasi kufikia umbile na umbo kamili linalochukuliwa kuwa la mtu mzima. Huyu ni mtu anayejifunza kuutumia na kuufanya mwili wake umwezeshe kukabiliana na changamoto za kimazingira. Ukuaji huu wa mwili unaenda sambamba na ukuaji wa uwezo mahsusi katika maeneo makuu matatu; kiufahamu, kimaadili na kimahusiano, vyote vikimtambulisha mtoto bila kujali sana umri wake.

Kiufahamu/kiakili
Kwa ujumla, watoto si watu waliozidiwa akili na watu wanaoitwa watu wazima bali ni watu wanaofikiri na kuyatazama mambo tofauti na mtu mzima. Mtazamo huu wa kitoto hubadilika kadri ukuaji wa mwili unavyoendelea kutokea si kwa maana ya kuwa bora kuliko ulivyokuwa awali bali kuwa tofauti na ulivyokuwa ili kumsaidia kukabiliana na changamoto za kimazingira.

Mtoto hazidiwi ufahamu na mtu mzima. Picha: Sayuni Philip
Mtoto, kwa maana hiyo, ni mtu asiye na uwezo wa kutambua mtazamo tofauti na alionao yeye. Mtu asiyefikiri kwamba mtu mwingine anaweza kufikiri tofauti na yeye. Sababu kubwa hapa ni kwamba ufahamu wake bado unaumbika na kwa kiasi kikubwa hauna tajiriba inayokidhi kulitazama jambo kwa nyanja kadhaa kwa wakati mmoja.

Fikra za mtu huyu anayeitwa mtoto zinaishia katika kile kinachoonekana, kwa maana ya kutokuwa na uwezo wa kutafakari yasiyoonekana au kutegemea yanayoonekana ili kufikiri. Ndio kusema mtoto kiufahamu anahitaji kuona kitu halisi ili kuweza kufikiri. 

Kimaadili/kiroho
Kadhalika, mtoto anatambua mema na mabaya lakini kwa kutumia sababu tofauti na zile za mtu mzima. Mfano wa sababu zinazotumika na mtoto kutofautisha jema na baya ni matokeo ya kilichofanyika, namna mahitaji yake binafsi yalivyokidhiwa, kufikia matarajio ya jamii inayomzunguka kwa maana ya kuiga yanayofanywa na yanayoonekana kukubalika na wale wenye mamlaka.

Kwa mfano, jema kwa mtoto ni lolote lenye matokeo yenye kumnufaisha yeye. Kitendo anachokifanya na kinachomletea matokeo mazuri kwake huo ndio wema. Ubaya kwa upande mwingine, ni lolote lile linalofanywa na mwingine au analolifanya yeye lisilo na matokeo yenye manufaa kwake au lisilokubalika na wanaomzunguka. 

Tunaweza kusema kwamba mtoto anaweza kutenda jambo pasipokujua athari za anachokifanya almuradi tu anachokifanya kinamletea manufaa fulani kwake. Kwa kutambua kwamba mtoto hufanya bila kutafakari athari kwa upana wake, sheria kwa kutumia kigezo cha umri, zinamlinda mtoto hata anapofanya jambo lenye uhalifu ndani yake. 

Tofauti na mtoto, mtu mzima anachukuliwa kuwa yule anayeongozwa na dhamira yake na sio matarajio ya wengine katika kutanguliza ustawi wa watu wengine zaidi yake yeye. Kwa kutumia tafsiri hii, maana yake mtu mwenye miaka 35 anayefikiria na kutanguliza ustawi wake mwenyewe na kuongozwa na matarajio ya wengine bila kutafakari kwa mapana athari za anachokifanya ni mtoto ingawa anawajibikia matendo yake kisheria. 

Kihisia/Kimahusiano
Mtoto ni mtu anayetumia hisia zaidi kama namna ya mawasiliano yake na watu wengine ingawa hana uwezo wa kuelewa wala kudhibiti hisia zake zinapohitilafiana na hisia za wengine. Anakasirika kusema ametishwa. Analia kusema hajaridhika au anahitaji.  Pamoja na kuwasiliana kwa kutumia hisia, mtoto hana uwezo wa kuelewa hisia za wengine na kujua kilicho nyuma ya hisia fulani ingawa hali hii hubadilika kadri anavyokua. Ni kwa sababu hiyo, mtoto huhusiana na wanaonufaisha/wanaompa faida ya moja kwa moja mfano mama, dada na kadhalika. Hali hii huendelea kubadilika kadri anavyokua.

Kinachofanya mahusiano yake na wengine kuwa ya upande mmoja, yaani yanayomnufaisha yeye ni kutokuwa na uwezo wa kufikiri mahitaji ya wengine. Anadai kula yeye bila kujua anayempatia chakula amekula ama la. Analia kudai msaada bila kujua anayeombwa msaada naye anaweza kuomba msaada kwa mwingine. Kimahusiano tunaweza kusema anaamini wengine wanayo majibu ya mahitaji yake na yeye ni mnufaika asiyewajibika.  

Tunaweza kumsaidiaje mtoto?
Kwa ujumla tunaweza kusema mitazamo inayojaribu kumtambua mtoto inatofautiana na wakati mwingine kupingana kulingana na mahitaji ya anayetafsiri. Wakati sayansi inaweza kutupa sifa za mtoto pasipokujali amekulia katika mazingira gani, jamii husika nayo inaweza kuja na tafsiri yake inayoendana na mazingira yake kumwumba mtoto. 

Yapo mazingira ambayo mtoto huonekana  kama mtu asiye na hatia na ambaye hukosea kwa kutokuelewa. Kwamba utoto ni umri wa kutokuhukumiwa kwa matendo yake na hivyo ni wajibu wa jamii kumlinda mtoto na mabaya ya watu wazima, kumsamehe anapokosea na kumrudisha kwenye mstari wa jamii kwa uangalifu ili hatima yake aishi kwa furaha na amani.

Lakini yapo mazingira ya kijamii yanayomtazama mtoto kama mtu anayezaliwa na uovu na uhalifu wa asili. Mtazamo huu ndio unaotufanya wakati mwingine tuamini kwamba watu wazima wanayo mamlaka ya kuwastaarabisha na kuwaadhibu watoto wanapokosea kwa sababu hukosea kwa makusudi shauri ya asili ya uhalifu iliyo ndani yao. Ubatizo wa watoto kwa baadhi ya imani za kidini ni mfano wa matambiko yanayokusudia kung’oa asili hii ya uovu inayoaminika kuambatana na mtoto tangu anapozaliwa.

Vyovyote iwavyo, mtoto  anachukuliwa kuwa tofauti na mtu mzima. Mtoto kwa ujumla anaonekana kuwa mtu anayehitaji kusaidiwa kukabiliana na changamoto za dunia kwa kuelewa mahitaji yake. Na kwa kuangalia tafsiri hizi, tunaweza kuona kwamba mtoto anaweza kuwa mtu yeyote pasipo kujali umri wake ingawa kwa mtazamo wa kisaikolojia, mara nyingi sifa za utoto huishia katika umri wa miaka 12. Huyu ndiye mtu ambaye kuanzia makala inayofuata kutaanza kuusaili uwezo na mahitaji yake kiumri.
christianbwaya@gmail.com

Maoni

 1. Napenda kuchangia kidogo hili suala. Ajabu ni kwamba hata mimi, na mvi zote hizi, bado najitambua na kujitambulisha kama mtoto kwanza katika familia yetu. Dhana hii ya "mtoto" wa fulani hafutiki hata ukawa mzee wa miaka 80.

  Katika blogu zangu miezi ya hivi karibuni nimeandika kuhusu mazungumzo yangu na Mzee Patrick Hemingway, mtoto pekee aliyebaki wa mwandishi maarufu Ernest Hemingway. Lakini huyu mzee tunayemwita mtoto ana umri wa miaka 87.

  JibuFuta
 2. Nakushukuru sana Profesa Mbele kwa kuipanua dhana ya 'mtoto'. Nakumbuka hata babu yangu hujirejea kama 'mtoto wa tatu' katika familia yao. Kumbe kijamii suala si umri kwa maana ya idadi ya miaka wala uwezo. Ni namna linavyoumbwa na tamaduni na mazoea yetu. Shukrani sana :)

  JibuFuta
 3. Ingiza maoni yako...tuwalinde Watoto,nipo kasulu kigoma

  JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Pay $900? I quit blogging

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Haiba ni nini?