Tubadilishe mfumo wa kufikiri

Hivi ingekuwaje kama tungeweza kuutumia ubongo wetu walau kwa asilimia chache za uwezo wake halisi? Hivi ingekuwaje kama kila Mtanzania angeamua kuacha uvivu na kuzifanyia kazi baadhi tu ya seli mabilioni zinazounda ubongo wake? Tungebaki hapa tulipo?

Nina mashaka iwapo kila raia wa nchi hii anajisumbua kujua matumizi sahihi ya ufahamu wake. Kila raia naamini anayo akili nzuri ambayo kama ikitumiwa kwa kiwango kizuri lazima isababishe mabadiliko ya aina fulani. Na tunapozungumzia akili nzuri, haturejei kwa wale wachache waliobahatika kuyakanyaga madarasa.

Kama hivyo ndivyo, kwa nini tunaendelea kurudi nyuma kwa kasi mpya? Kwa nini tuna mazoea mabovu ya kulalamikia mambo ambayo wakati mwingine ni sisi wenyewe tumeyasababisha? Hivi kweli tunatumia akili zetu ipasavyo?

Sababu imekuwa kawaida kusikia malalamiko. Watu tunajua kulalamika. Na kulalamika maana yake ni jitihada za kukwepa majukumu kwa kuwatupia wengine mzigo ambao kimsingi ni wa kwako. Kulalamika ni kule kushindwa kukubali udhaifu wetu. Kujiridhisha nafsi zetu kwamba hatuhusiki na uharibifu wowote tunaoulalamikia. Kulalamika ni kule kujihesabu kwamba si sehemu ya uoza unaouona. Ni kugeuka mchambuzi wa makosa ya wengine badala ya kujichambua mwenyewe.

Kulalamika hakuwezi kutusaidia isipokuwa kupoteza chanzo cha tatizo. Kulalamika kunapumbaza na kuzubaisha. Kulalamika kunalemaza. Kulalamikia wengine hakuwezi kutatua matatizo. Sana sana itakuwa ni dalili za matumizi duni ya akili zetu.

Ninachokusudia kukisema ni sisi wenyewe kujenga tabia ya kukubali makosa yetu. Kubadili mfumo wa kufikiri ambao umetufikisha hapa tulipo. Tugeuze nia zetu wenyewe. Halafu tuchukue hatua katika kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayoikabili jamii yetu.

Kila Mtanzania anayo nafasi muhimu sana katika ujenzi wa taifa hili. Na kwa bahati mbaya sana ni kwamba wengi hatuzijui nafasi zetu katika kuleta mageuzi. Kila mwananchi anao wajibu muhimu sana kwa kugeuza mambo, ikiwa tu atajielewa na kuilewa nafasi yake. Asipofanya hivyo, nafasi ambayo ingejazwa na yeye itaendelea kuwa wazi na kwa namna moja ama nyingine italigharimu taifa hili. Pengo hilo halitajazwa na mwingine.

Hivyo, kabla ya kulalamika, jiliuze wajibu wangu ni upi? Nimeutimiza?

Ni muhimu kuacha kulalama, na badala yake tutafute kile tunachoweza kukifanya kwa ajili ya wengine. Tuache kulalama kwani huenda tunachokilalamikia kimesababishwa na pengo la sisi kutokufanya wajibu tuliopaswa kuufanya. Siku njema.

Tubadili mfumo wa kufikiri.

Maoni

  1. Hapo umegonga penyewe. Ukweli wengi tunasubiri tufanyiwe maamuzi na watu wengine na ndiyo maana kulamimimka huwa ni kwingi na hakuishi.
    Tatizo lingine wengi wetu hatuelewi kama huwa tunafikiri na matokeo yake ni maumivu kila siku.
    Endelea kutupa elimu bwaya ya kujielewa.

    JibuFuta
  2. Kuna mtu aliwahi kusema ubongo wa mswahili unapaswa kuuzwa kwa bei mbaya kwa sababu bado ni mpya na hautumiki.
    Ndio maana ukisoma magezeti utaona jinsi tulivyo wazuri wa usosoni.

    Bwaya safi sana naona umekuja na dira mpya.

    JibuFuta
  3. Nuru na anony, asanteni kwa maoni yenu.

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Mambo ya Kuzingatia Unapoandika Wasifu wa Kazi (Curriculum Vitae)

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?

Tabia za Mtoto wa Miaka 0 – 3 Kimahusiano na Kihisia