Unamsaidiaje Mtoto Asiyefanya Vyema Kimasomo?

PICHA: BBC News


Kwa mzazi mwenye mtoto anayesoma shule, ni rahisi kuelewa inakuwaje pale unapokuwa na uhakika mwanao ana uwezo mzuri lakini matokeo anayoyapata shuleni hayalingani na uwezo wake. Kama mzazi unayejali unajaribu kufanya wajibu wako, unamsaidia kazi za shule, unamwekea mazingira mazuri yanayomhamasisha kujisomea akiwa nyumbani, unashirikiana na walimu wake, lakini bado matokeo yanakuwa kinyume.

Hii ndiyo hali aliyopitia rafiki yangu na mke wake. Mtoto wao wa miaka 9 anayesoma darasa la nne alikuwa anafanya vizuri darasani. Alipofika darasa la tatu, maendeleo yake yalianza kusuasua. Kwa mujibu wa wazazi, maendeleo yake darasani yaliendelea kuwa mabaya siku hadi siku.

Kazi za shule ambazo mtoto alipaswa kuzifanya akiwa nyumbani wakati mwingine hazikukamilika. Kulikuwa na namna fulani ya uzembe. Kuona hivyo, wazazi waliamua kufuatilia shuleni kupata ushauri. Walimu hawakuonesha wasiwasi na uwezo wa mtoto ingawa wazazi bado waliamini mtoto alikuwa na uwezo wa kufanya vizuri zaidi.

Mama, ambaye ni mwalimu wa sekondari, aliamua kuchukua hatua ya kuhakikisha anakuwa karibu na mtoto kumsaidia kufanya kazi za shule. Pia, wazazi kwa pamoja walijitahidi kuweka mazingira rafiki nyumbani kwa lengo la kumwezesha mtoto kupata muda wa kufanya kazi za shule bila usumbufu. Utaratibu mzuri wa kutazama televisheni uliwekwa kuongeza uzingativu wa mtoto kwenye masomo. Vifaa vya kieletroniki kama tablet viliwekwa mbali na mtoto.

Pamoja na kuchukua hatua hizo, bado hapakuwa na badiliko la dhahiri. Ilibidi wazazi wawe wakali kidogo na kutumia adhibu ilipobidi. Kwa mujibu wa mama, adhabu zilikuwa na lengo la kumfanya mtoto akamilishe kazi alizopewa shuleni. Kila mtoto alipofanya vibaya, mama kwa ushirikiano na baba walitoa adhabu.

Hata hivyo, matokeo yake bado yaliendelea kuwa kinyume. Adhabu na ukali vilianza kujenga hali ya woga na wasiwasi kwa mtoto, kiasi kwamba kila alipowaona wazazi nyakati za jioni, alijawa hofu. Kilichowastua zaidi wazazi ni kujengeka kwa tabia ya uongo kwa lengo la kuficha kazi alizokuwa amepewa shuleni.

Punguza shinikizo la mafanikio

Kisa hiki kilinikumbusha hali niliyowahi kukutana nayo nyumbani. Mwanangu hakuwa na tabia ya kukamilisha kazi anazopewa bila kukumbushwa. Tabia hii, kama mtoto wa rafiki yangu, ilichangia kuzorotesha maendeleo yake darasani. Kwa kuamini kwamba alikuwa na uwezo mkubwa asioutumia, mimi na mke wangu tulianza kumwadhibu.

Kwanza, tulimzuia kwenda kucheza na wenzake baada ya masomo. Pia, hatukumruhusu kutazama vipindi vya televisheni. Ingawa alianza kufanya kazi za shule bila kusukumwa, ile furaha yake kama mtoto ilipotea. Wakati mwingine alifanya kazi huku machozi yakimtiririka. Kosa moja lilimaanisha kukemewa na kusimangwa.

Nakumbuka siku moja asubuhi wakati anaondoka kwenda shuleni kufanya mtihani wa majaribio ya mwezi, alidai anaumwa. Kwa kumtazama, nilihisi amejawa hofu ya matokeo mabaya. Niliamua kumwondolea wasiwasi. Nilimwambia asiwe na hofu kwa sababu nilikuwa na imani naye na sikuwa na hofu kwamba angefanya vizuri. Lakini pia, nilimweleza kwamba hata kama asingefaulu vizuri, bado nilikuwa na imani yake.

Mtoto aliposikia hivyo, alibadilika haraka. Uso wake ulichangamka na akaondoka kwa furaha. Siku chache baadae alipokuja na karatasi za mitihani, matokeo hayakuwa mazuri kama nilivyotarajia. Dalili kwamba hakuwa amefanya vizuri ni kuficha baadhi ya karatasi.

Nguvu ya kumwamini

Niliamua kusimamia kile ambacho nilikuwa nimemweleza kabla. Ingawa haikuwa rahisi kumpongeza, nilijikaza na kumpongeza kwa kufanya vizuri. Hakuonekana kuamini. Nilimwambia nina imani na uwezo wake. Niliweka msisitizo kwenye karatasi alizokuwa amefanya vizuri. Nikamweleza kwamba nina imani kwamba anaweza, hata kama kuna baadhi ya maswali hakuyapata.

Maneno hayo yalimwingia. Niliuona uchangufu wake. Uso wake ulichanua. Hatia ilipotea. Kwa kuamini hakuwa kwenye ‘kibano’ cha hukumu ya wazazi alinionesha karatasi nyingine alizokuwa amezificha. Tulianza kuaminiana. Tuliweka mikakati ya kupata alama kubwa zaidi kwenye masomo kwa namna ambayo ilionesha nina imani naye.

Kutambua jitihada

Baada ya siku hiyo, nilianza kuona mabadiliko. Mtoto alianza kujituma kwa furaha. Alionekana kujua anachokifanya. Kila niliporudi nyumbani ilianza kuwa mwepesi kunijulisha kile alichojifunza shuleni. Kwake, ilikuwa ni fahari baba yake kusikia anavyoendelea kujifikia malengo tuliyojiwekea pamoja. Nilimpa ushirikiano na kutambua juhudi zake. Kama wazazi tulifanya maamuzi ya kumpongeza kwa kila hatua anayoichukua na kumwonesha kwamba tuna imani na yeye.

Tangu wakati huo hatujalazimika kutumia adhabu, kumkemea wala kumshinikiza kufanya kazi za shule. Lakini amekuwa na hamasa ya kujituma yeye mwenyewe ili kututhibitishia kwamba imani tuliyonayo kwake haikuwa bure. Maendeleo yake shuleni yamekuwa bora zaidi.

Punguza matarajio

Pengine na wewe ni mzazi kama mimi na rafiki zangu niliosimulia kisa chao awali. Unajitahidi kuhakikisha mtoto anafanya vizuri shuleni lakini hujaona matokeo unayoyatarajia. Umemchapa mtoto, umemkemea, umefuatilia shuleni, lakini bado mambo hayajabadilika. Usikate tamaa. Kuna uwezekano mkubwa kwamba matarajio uliyonayo kwa mwanao ni makubwa kuliko hali halisi. Pamoja na uzuri wake, matarajio makubwa yanaweza kuwa na matokeo mabaya.

Fikiria mtoto amekuja nyumbani na alama 73/100 wakati wewe kama mzazi unatarajia alama 95/100. Utajisikiaje? Ni wazi utachukulia kwamba mtoto ‘anaendekeza uzembe.’ Katika mazingira kama haya, tunaweza kusema, unayo matarajio makubwa yatakayokufanya ama usimpongeze au umkemee kwa kufanya uzembe. Lakini je, ni lazima mtoto apate alama 95/100?

Nimejifunza kwamba matarajio makubwa kuliko kiasi inaweza kuwa adhabu mbaya kwa mtoto. Mtoto anapojisikia hajaweza kufikia matarajio hayo, anaanza kukata tamaa. Moyo wake unanyong’onyea kwa kujiona hawezi. Inapofikia hapo, mtoto anaweza kujenga mtazamo hasi na shule. Mtazamo hasi unapochukua nafasi, mtoto anapoteza hamu ya kujifunza.


Mwoneshe anaweza

Mtoto anayejiona hawezi ni rahisi kudanganya. Ni kama mwanangu ‘aliyeugua’ siku ya mtihani. Kuugua kulikuja kama namna ya kujihami na matokeo yanayoweza kuthibitisha kwamba ni kweli hawezi. Uongo ulichukua nafasi kama namna ya kulinda uhusiano wake na wazazi. Kule kuamini kazi za nyumbani zingemwingiza kwenye matatizo ya kuadhibiwa, aliona ni afadhali ‘kuzipoteza’ ili awe salama.


Nimejifunza, kama mzazi, ukiweza kuwa na ujasiri wa kumwamini mtoto bila kujali hali yake, ukiweza kumthibitishia kwamba huna shaka na uwezo alionao, hiyo inatosha kuibua uwezo wa ajabu ndani yake. Mtoto anayejua kuwa wazazi wake wanaona kitu ndani yake, wanajisikia fahari naye, anakuwa na hamasa kubwa ya kuthibitisha kwamba hawajakosea kumwamini. Tujifunze kutambua uwezo usioonekana ndani ya wanetu ili kuuchochea udhihirike kwa mafanikio tunayoyataka.

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Mambo ya Kuzingatia Unapoandika Wasifu wa Kazi (Curriculum Vitae)

Uislamu ulianza lini?

Tabia za Mtoto wa Miaka 0 – 3 Kimahusiano na Kihisia