Watoto Wagomvi, Wasumbufu na Wenye Utukutu katika Umri wa Miezi 0 – 36
Tangu tumeanza mfululizo huu, tumejaribu kuonesha namna
tabia za mtoto zinavyohusishwa na malezi ya mzazi kuliko vinasaba. Kwa ujumla
tumeona kile anachokifanya mtoto ni matokeo ya kufikiwa au kutokufikiwa kwa
matarajio yake. Katika makala haya tunaangalia kundi la watoto wenye tabia za
ugomvi, utukutu, ukaidi na usumbufu na kuona namna mazingira ya kimalezi
yanavyochangia hali hii.
Hawajiamini na
hawamwamini yeyote
Kwa ujumla hawa ni watoto ambao hawaoneshi shauku wala
sababu ya kutafuta ukaribu na mzazi. Ni watoto ambao tunaweza kusema wamekulia
katika mazingira magumu ya kimalezi. Badala ya wazazi wao kuwasaidia kufikia
matarajio yao kama watoto, ni wao ndio wanaotumika kama ngao ya wazazi kuficha au
kutatua matatizo yao. Badala ya mzazi kuwa chanzo cha mtoto kujisikia usalama, kinyume
chake kinatokea. Mzazi anakuwa chanzo cha hofu, mashaka, wasiwasi na hasira.
Inavyokuwa ni kwamba mtoto anapokwenda kwa mzazi kwa
matarajio ya kutulizwa, anajikuta anapuuzwa, anaadhibiwa, anakemewa, anatishiwa
na hata kudhalilishwa. Mazingira ya hofu yanajengeka. Njia pekee ya kujihami ni
mtoto ‘kumpotezea’ mzazi na kuongeza umbali. Maana yake ni kwamba, hakuna
anachoweza kukifanya mtoto kwa mzazi wake kinachoweza kurejesha ukaribu na
upendo anaoutarajia. Kila anachokifanya kinaongeza hofu na hali ya
kutokujiamini.
Mtoto anakuwa mwoga, anakata tamaa na kuvunjika moyo. Anapoteza
imani kwake yeye mwenyewe na kwa wengine. Imani kwake inakwisha kwa sababu
anajiona kama mtu aliyekataliwa na kushindwa kumfanya mzazi wake ampende. Hisia
hizo humfanya pia amwone mzazi kama mtu asiyeaminika, mkatili, asiyejali, anayetisha
na asiyefaa kuwa karibu naye.
Athari kwa mtoto
Katika kipindi cha miezi sita, mtoto wa kundi hili haonekani
kuwa na furaha. Uso huoonesha wasiwasi na hofu na hulia lia muda mwingi shauri
ya uchungu na kujiona amepuuzwa. Tabia yake akiwa na watu haitabiriki sana
katika kipindi hiki ingawa hofu na wasiwasi vinatawala maisha yake. Anaweza
kuogopa baadhi ya watu hasa anaojua hawamjali. Wakati mwingine anaweza kuwa na
tabia ya kuwang’ang’ania watu fulani fulani anaohisi wanaweza kumpenda.
Mtoto anayekulia katka mazingira magumu Picha: who.int |
Anapoachwa na mzazi wake wakati mwingine halii na hana
wasiwasi ingawa yapo mazingira anaweza kuwa na tabia ya kulia. Kutokulia ni
mafanikio ya jitihada zake za kumpotezea mzazi ambaye kwa ujumla haonekani kuwa
mzazi anayejali. Mzazi anaporudi, mtoto huwa hana habari ingawa wakati mwingine
huweza kuonesha jitihada za kutambua ujio wa mzazi.
Anapofikia miaka mitatu, sura ya ugomvi huwa bayana. Ni mgomvi
anapocheza na mara zote huonekana kufurahia maumivu ya wenzake. Haonekani kuwa
na huruma wenzake wanapolia na uso wake hauna uchangamfu wa kawaida kwa watoto
wa umri wake. Anaonekana ni mpole lakini kwa hakika ni maumivu yanamfanya awe
na moyo uliozizima. Hutumia ugomvi au hasira kama kinga ya kuficha hisia kwamba
yeye ndio tatizo.
Wasiwasi na hofu humfaya ashindwe kujifunza vizuri kama
watoto wengine wote wa makundi mengine. Badala ya kujifunza, hutumia muda mwingi
kupambana na wenzake ili kujisikie nafuu moyoni. Wakati mwingine anapokutana na
watoto ‘rafiki’ wasioendekeza ugomvi, huweza kuwa na tabia ya kuficha hisia
zake za ghadhabu na kisasi asichokijua kwa kujaribu kuonesha tabia njema usoni.
Hata hivyo, ni mwepesi mno wa kupandwa jazba yanapotokea mazingira ya kumfanya
aonekane dhalili.
Matatizo yanaanzia
kwa mzazi mwenyewe
Tafiti zinazonesha hali hii hutokea zaidi watoto
wanapolelewa na wazazi waliowahi kukumbwa na matatizo mazito katika maisha yao.
Ingawa si wazazi wote wenye historia nzito huwa na malezi ya namna hii, hata hivyo kuishi na visasi, hasira na uchungu
usioshughulikiwa kunaongeza uwezekano wa malezi ya namna hii.
Mzazi aliyewahi kuachika/kutelekezwa/kudhalilishwa/kukataliwa
na mtu muhimu kwenye maisha yake na bado angali akiombolezea hali hiyo, anaweza
kuingia kundi hili. Anaweza kuwa mzazi aliyeishi kwenye mateso ya namna fulani
katika utoto wake au aliyekumbana na matatizo ya udhalilishaji na hajaweza kusamehe
bado. Hali kama hizi huwafanya wazazi kama hawa hujikuta wakilipiza kisasi kwa
wengine bila wao wenyewe kutambua. Kisasi hicho kinaweza kuhamia kwa watoto wao
wenyewe.
Shauri ya kuwa na visasi mioyoni mwao huwa na tabia ya kuadhibu
watoto hali wakiwa na hasira. Wengine huwatukana watoto matusi mazito. Tafiti
zinaonesha kwamba asilimia 80 ya watoto wa kundi hili, wanalelewa na wazazi
wanaotumia adhabu kali na matusi, hali inayoweza kutafsiriwa na mtoto kama
kukataliwa na kudharauliwa.
Kadhalika, wazazi wenye tabia ya ulevi uliopindukia, wanaotumia
pombe kama namna ya kusahau matatizo yanayowakabili. Unywaji wa pombe unapopita
kiasi huambatana na ‘kurukwa na akili’, hali inayoweza kusababisha mzazi huyu kuonesha
tabia ambazo kwa hali ya kawaida asingezionesha mbele ya mtoto.
Sambamba na hao, tabia ya ubabe na matumizi ya nguvu kwa
watu wengine katika mazingira ambayo mtoto anashuhudia huchangia tatizo. Mzazi
mwenye tabia ya kupigana, kumtukana na hata kumdhalilisha mwenzi wake mbele ya
macho ya mtoto hujenga hofu katika moyo wa mtoto hata kama zipo jitihada za
kumwonesha mtoto upendo. Mtoto anayekulia mzingira haya hukua akiamini hayo
ndio maisha na huweza kuiga tabia hiyo.
Kwa ujumla tunaweza kusema, tabia ya ujeuri, ugomvi na utukutu
kwa kiasi kikubwa huanzia kwa wazazi wanaoishi na matatizo yasiyotatuliwa. Matatizo
haya huwafanya washindwe kutambua uhusiano wa makosa yao na maisha ya mtoto. Matokeo
yake ni watoto wenyewe kuanza kujibebesha mzigo kwamba tatizo ni wao.
Hata hivyo, mzazi mwenye makovu ya kihisia moyoni anaweza
kabisa kuwa na upendo kwa mwanae. Wapo wazazi ambao pamoja na kuwa na uchungu
mkubwa moyoni wameweza kuwatumia watoto kama namna ya kupata faraja. Wazazi hawa wametumia malezi kama namna ya
kushughulikia matatizo yao kwa kuwakinga watoto na yaliyowapata wao. Matokeo
yao wamekuza watoto ‘rafiki’ kama tulivyoona kwenye kundi la kwanza. Maana yake
ni kwamba, kupitia kipindi kigumu katika maisha si lazima kuathiri malezi yako.
Unaweza kabisa kukuza watoto wema kama ukitambua na kufanyia kazi kile kinachohitajikakwa makuzi na malezi ya mwanao.
Inaendelea
Maoni
Chapisha Maoni