Athari za Matarajio na Malezi ya Mtoto wa Miaka 0-3

Umewahi kujiuliza kwa nini watoto wengine ni waoga na wenye aibu wanapokuwa na watu wakati wengine wana ujasiri hata kusimama na kuzungumza mbele ya hadhara ya watu wazima? Kwa nini mtoto mwingine huonekana kupenda sana watu lakini huwa mgomvi na mwenye kutatua migogoro kwa kupigana?  Iweje watoto watofautiane tabia katika mazingira ambayo wakati mwingine wanakuwa wamezaliwa katika familia moja? Hilo ndilo tunalolenga kulitazama kwa mhutasari.

Katika sehemu hii ya mfululizo wa malezi na makuzi ya watoto, tunajaribu kuonesha namna tabia za mtoto zilivyo matokeo ya kujibiwa kwa matarajioyake yanayotokana na mazingira ya ukuaji. Tunaangalia namna haiba/tabia za mzazi zinavyoweza kujenga matarajio yanayoshabihiana  au kuhitilafiana na matarajio ya mtoto mwenyewe na hivyo kuathiri tabia yake. Mwelekeo wetu mkuu ni kuangalia msingi wa mahusiano ya mtoto na mzazi ikiwa ni pamoja na watu wanaomzunguka. 

Kwa mhutasari, matarajio na haiba ya mzazi huzalisha makundi makuu manne ya watoto kulingana na namna wanavyojiona wao na kuwaona wengine. 

 1) watoto wenye ujasiri na kuwathamini wengine ambao hupenda na kupendwa kirahisi na kadri wanavyokuwa huwa na mahusiano yasiyo na ajenda binafsi na wengine

2) watoto wanaojiamini lakini hawawathamini watu wengine ambao kwa kawaida hukwepa watu na kadri wanavyokua huonekana wenye aibu/ukimya/dharau/kiburi

3) watoto wasiojiamini lakini wanaowathamini na kuwaaamini wengine kupita kiasi na kujikuta wakitaka mno kuwapendeza na kuwaridhisha watu wengine kwa sababu raha yao haianzii ndani bali kuwa 'watu wa watu'

4) watoto wasiojiamini/kujithamini wala kuwaamini na kuwathamini watu wengine kiasi kwamba kwa kawaida hujenga tabia ya kuwadhibiti wengine kwa ugomvi/ujeuri/ukaidi

Mambo yasipobadilika kadri wanavyokua, tabia hizi za kimahusiano huimarika kulingana na umri kama tutakavyoziona katika mfululizo huu. Tutaangalia makundi haya kwa awamu mbili. Katika sehemu hii, tutatazama kundi moja la kwanza na namna yanavyotokana na malezi. Makundi mengine matatu  tutayatazama kwa pamoja katika makala inayofuata.

Watoto wanaojiamini na kuwathamini wengine
Hawa ni watoto wenye uhakika kwamba wanapendwa na kuthaminiwa na  wazazi wao. Hawana wasiwasi na usalama wao na wanajua kimbilio lao ni wazazi wao. Ingawa kweli hata watoto wengine huwa na chembechembe fulani za kuwafanya wazazi kuwa kimbilio, imani ya watoto wa kundi hili kwa wazazi wao inawafanya hata wao wajiamini kuliko watoto wa makundi mengine matatu. 

Kwa ujumla, ni watoto wanaovutia kukaa nao kwa sababu si wasumbufu, wana nyuso zenye tabasamu muda mwingi na ni wepesi kushirikiana na wengine tangu wakiwa wadogo. Katika umri wa miezi sita, imani yao kwa watu hudhihirika kupitia wepesi wao wa kuzoea nyuso ngeni tabia ambayo ni nadra kwa makundi mengine. Hawana tabia ya kulia kulia wala kuwaganda wazazi kwa sababu tayari wanao uhakika kwamba wazazi wao wapo na wanawajali. Hulia pale wanapohitaji kuwasiliana na wazazi. Na kwa sababu mzazi ana wepesi wa kusikia, hawana sababu ya kulia mara kwa mara.

Mtoto wa kundi hili anaweza kugundulika tangu akiwa na umri pungufu ya miezi sita.  Anapoachwa na mzazi wake anayekwenda kazini asubuhi, kwa mfano, mara nyingi  anaweza kulia kama watoto wengine. Tofauti yake ni wepesi wa kunyamaza na kuendelea na michezo mingine baada ya mzazi wake kuondoka. Hali hii ni tofauti kabisa kwa watoto wengine kama tutakavyoona. Huyu analia kwa kuthamini uhusiano wake na mzazi ingawa anaamini mzazi hatamtelekeza.

Kichanga cha siku kadhaa. Picha: Jielewe
Wanapofikia umri wa kati ya miaka miwili na mitatu ambapo tayari huwa na uwezo wa kutumia lugha, mtoto wa kundi hili ni mkweli na hajaribiwi kusema uongo.  Anachokisema ndicho kilicho moyoni bila kujali matokeo ya ukweli huo. Tabia hii ya kusema ukweli, kama tutakavyoona hivi punde, hutokana na kuelewa kwamba chochote akisemacho hata kama hakikubaliki kwa mzazi hakimdhuru yeye kwa maana ya kumsababishia adhabu au kukataliwa.

Kadhalika, mtoto wa kundi hili ana hali ya kujiamini dhahiri inayodhihirika katika michezo yake. Tangu anapokuwa mdogo huonekana ana utundu fulani wa ‘kuhangaika’ kuyachunguza yale yanayomzunguka. Hatulii 'tuli’ lakini si msumbufu. Ana tabia ya kujitegemea katika kuanzisha na kutekeleza anachokianzisha bila kutegemea sana msaada wa wanaomzunguka isipokuwa pale inapobidi. Udadisi wake ni sawa na wenzake wa kundi la pili.

Anapofikia miaka miwili na kuendelea, shauri ya uchangamfu, ucheshi wa hapa na pale pamoja na tabia ya kupenda wengine, wakati mwingi huaminiwa kirahisi sana na watoto wenzake na kujikuta akiwa kama kiongozi wao katika kuendesha michezo hiyo. Kinachochangia kuaminiwa na wenzake pia ni kutokuwa na tabia ya ugomvi na uchoyo. Huwa ana wepesi wa kutoa alichonacho hasa anapotimiza miaka mitatu tofauti na watoto wa makundi mwengine. 

Kwa ujumla udadisi wake na shauku ya kujifunza inatokana na akili yake kuwa huru na hana wasiwasi na watu wanaomzunguka wala mazingira yake na hivyo hujikuta akielekeza nguvu zake nyingi katika kujifunza kuliko watoto wa makundi mengine wanaotumia muda mwingi kujihami.  

Nafasi ya haiba na uelewa wa mzazi
Huenda ni sawa tukisema kila mzazi angependa kuwa na mtoto wa aina hii ingawa ni kweli wapo wazazi shauri ya haiba zao wasingependa kuwa na mtoto ‘mnyenyekevu’ na 'mtulivu' kiasi hiki kama tutakavyoona kwenye makala inayofuata. Hata hivyo, tafiti zilizofanyika sehemu mbalimbali zinaonesha kwamba asilimia kati ya 55 na 65 ya watoto wa umri wa miaka 0 – 3 wanaangukia kwenye kundi hili ingawa asilimia hii hupungua kadri umri wa mtoto unavyoongezeka. Sababu kuu ni kwamba wazazi wengi huwekeza sana katika mahusiano yao na watoto wanapokuwa wachanga kuliko wanavyokuwa wakubwa. 

Kwa ujumla mtoto wa kundi hili amelelewa na mzazi anayechukulia uzazi na malezi kuwa jukumu muhimu na nyeti. Ni mzazi mwenye sifa nne kuutulizozitaja kwenye makala iliyopita, ambazo ni pamoja na 1) kupatikana kimwili na kihisia kwa mtoto, 2) kuelewa matarajio ya mtoto na kuyajibu yalivyo na 3) kushirikiana naye. 

Mzazi wa namna hii, pamoja na kuyapa uzito malezi, tafiti zinaonesha kwamba huwa ni mtu asiye na matatizo makubwa ya nafsi yanayoweza kumfanya awatumie watu wengine (pamoja na mtoto wake) kama kichaka cha kuficha udhaifu wake. Kwa lugha nyingine ni mtu aliye tayari kuona wengine wakifurahi hata ikibidi kwa gharama ya furaha na matarajio yake. 

Huyu ni mzazi anayeweka mazingira ya kumruhusu mtoto kuonesha hisia zenye matarajio na kumfanya mtoto aamini kuwa kuonesha hisia na sio kuficha ndio njia muafaka ya kufikiwa matarjio yake. Mtoto hujua, kwa mfano anapoumia, mzazi atajishughulisha kuelewa tatizo ni nini. Anapofurahi na kujisikia fahari, mzazi atakuwepo kuelewa kilichofanyika. Matokeo yake anamwamini mzazi kwa kujua yuko upande wake na kwamba kuonesha hisia nzuri au mbaya si jambo baya. Hali hii haipo kwa watoto wa makundi mengine matatu.

Ndio kusema, kadri mtoto wa kundi hili anavyokua, mzazi humwekea mazingira ya kutokuwa na hofu ya kudhihirisha hisia zake. Anapofika umri wa kati ya miaka mwili na mitatu, mtoto huyu huwa na uwezo mzuri wa kutambua hisia zake na kuzimudu hatua kwa hatua kadri anavyokua tofauti na watoto wa makundi mengine. Kwa mfano, anaweza kuanza kukiri kuogopa kulala mwenyewe, tofauti na mtoto wa kundi la pili anayeweza kuogopa lakini aogope kusema kwa hofu ya 'kupotezewa'.

Tafiti nyingi zinaonesha kwamba watoto hujifunza kuelewa hisia zao kwa kusaidiwa kutambua hisia za huzuni, furaha, hasira na woga kwa wengine. Hili linaweza kufanyika vizuri kwa njia nyingi ikiwa ni pamoja na kutumia hadithi fupi fupi zenye kuamsha hisia mbalimbali. Hisia anazoziona mtoto kwa wengine humsaidia kuelewa tofauti ya hisia halisi za ndani na namna hisia hizo zinazoweza kuoneshwa waziwazi na hivyo inakuwa rahisi kutambua hisia zake mwenye na kuzimudu hatua kwa hatua.

Ili hilo liwezekane, tafiti zinaonesha panahitajika uwezo wa kuvumilia kumwona mtoto akiwa katika mtazamo na hisia tofauti bila kumfanya ajisikie hatia. Tunaambiwa, kumwonesha mtoto kwamba unaelewa anachokifikiri na kujisikia ni hatua ya kwanza kumrekebisha kuliko kukimbilia kumrekebisha bila kuonesha kuelewa.
Maana yake ni kwamba mzazi aweze kuvumilia kuona mwanae ana hasira bila kumkasirikia au kukimbilia kumfundisha hatari ya hasira. Uwezo huu wa kumsaidia mtoto kusoma hisia zake hata zile zisizokubalika pasipokumfanya ajisikie kuhukumiwa, humsaidia mtoto kuwa mkweli wa hisia zake sifa moja kuu ya watoto wanaojiamini na kuwaamini wengine.

Kuthamini matarajio ya mtoto sio kudekeza
Kwa ujumla tunaweza kusema, ili mzazi aweze kumjenga mtoto anayejiamini na kuwathamini wengine lazima kwanza aweze kuthamini matarajio ya mtoto na kumthibitishia mtoto kadri anavyokua kwamba kinachomsibu yeye mtoto moja kwa moja kinamsibu mzazi. Kwamba anachojisikia mtoto ni jambo la maana kuliko anachojisikia mzazi. Hili hufanyika kwa 1) kuwasiliana na mtoto kwa lugha inayoonesha kuelewa yanayomsibu mtoto hata kama yanaonekana kuwa ya kipuuzi kwa kiwango gani na 2) kutambua anayoyafanya mtoto kwa kumpongeza kwa kufanikiwa kuliko kusubiri akosee na kuonesha makosa yake.

Kadhalika, tunazungumzia uwezo wa kuadhibu tabia pasipo kumwadhibu mtoto mwenyewe; uwezo wa kumwambia mtoto maneno yanayojenga tabia inayotarajiwa kuliko yanayoonesha tabia isiyotarajiwa; uwezo wa kumtia hamasa mtoto kuliko kumwonesha anavyokatisha tamaa kwa matendo fulani; uwezo wa kutenganisha matatizo binafsi ya mzazi na mahusiano yake na mtoto. 

Sasa kwa haraka, haya yote yanaweza kuonekana kuwa ni, “kumdekeza mtoto…kumlea mtoto kimayai mayai”. Hili si kweli. Kudekeza si kumwelewa ni mbinu za kujihami kwa mzazi. Wakati kumwelewa mtoto ni pamoja na kuthubutu kuadhibu tabia kwa lengo la kujenga tabia njema baada ya kuhakikisha mtoto anajua anaeleweka, kudekeza kwa upande mwingine ni kupuuza mambo ya msingi kwa hofu binafsi ya mzazi ya kuonekana hamthamini mtoto. Kwa lugha nyingine kumdekeza mtoto ni matokeo ya matatizo ya kisaikolojia anayokabiliana nayo mzazi kwa kujaribu kujenga sura ya ‘kumwelewa mtoto’ wakati katika hali halisi haonekani kuelewa kinachohitajika kwa mtoto bali ni mtu mwenye hofu. Hii si tabia inayoweza kujenga mtoto wa kundi hili.

Katika kuhitimisha tunaweza kusema, kujiamini kwa mtoto wa umri wa miaka 0-3 ni matokeo ya malezi na sio vinginevyo. Kwa kuwa, kama tulivyoona, zaidi ya nusu ya watoto wenye umri huu wanazo tabia hizi, maana yake ni kwamba wazazi wengi bila kujali matatizo yao ya kisaikolojia, msongo wa mawazo, kadhia za mahusiano yao na wenzi wao, mashinikizo ya kazi na maisha, bado wanaweza kuwawafanya watoto wakajiona wako kwenye ulimwengu unaoaminika na unaowatakia mema, hali ambayo ndio msingi wa kujiamini kwa mtoto na kuwathani wengine.

Katika makala inayofuata tunatazama makundi mengine matatu kwa kuangalia makosa yanayofanywa na wazazi ambayo ama yanatokana na matatizo yao ya nafsi au kutokuelewa matarajio ya mtoto na kusababisha watoto waangukie katika makundi hayo matatu.

Soma makala ifuatayo kujua kwa nini watoto wengine hukwepa watu na huwa na aibu kusema mbele za watu ingawa wana uwezo mzuri wa kujifunza.
Inaendelea

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Haiba ni nini?

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3

Uislamu ulianza lini?