Tabia ya Kukwepa Watu kwa Watoto wa Miezi 0 - 36

Tuliona namna malezi yanavyosababisha watoto kujiamini nakuthamini wengine. Katika makala haya tutaangalia makosa kadhaa yanayofanywa na wazazi kwa kujua au kutokujua ambayo husababisha mambo yanayoweza kuchukuliwa na wengi kama ‘matatizo ya kitabia’. Hata hivyo, kuna ukweli kwamba kinachoonekana ni tatizo chaweza kuwa fursa katika mazingira mengine. Kwa sababu ya kupunguza urefu wa makala moja katika kueleza makundi yote kwa pamoja, tutaangalia kundi moja kwa makala.


Watoto wanaojiamini lakini hawaamini watu wengine
Kwa ujumla hawa ni watoto wasiojali sana watu wengine lakini wakijijali wenyewe zaidi. Wanajiona hawana sababu ya kuhusiana na watu na muda mwingi wanakuwa wenyewe kwa ‘shughuli’ zao. Shauri ya kuwa ‘wenyewe-wenyewe’ na kufanya mambo yao kivyao-vyao, ni vyepesi kuwaweka kundi la watoto wenye dharau na kiburi ingawa ni kweli hujiona kuwa bora kuliko watu wengine.

Chanzo cha yote ni malezi yanayojaribu kudhibiti na hata kuzima hisia za mtoto kwa sababu tu (huenda) zinamfanya mzazi ajisikie vibaya.  Kwa mfano, mtoto anapolia kwa kujikwaa, haoni jitihada yoyote ya kumpooza maumivu. Sana sana, anaweza kuambulia kuambiwa ‘watoto wazuri huwa hawalii wakiumia’. Maoni kama haya kwa mtazamo wa mtoto yana maana kwamba hisia ni tabia mbaya na kwamba ni ujinga kuthamini hisia hata kama zina ukweli. 

Aidha, wakati mwingine mtoto hujikuta katika mazingira ambayo mzazi huamua ‘kuzirekebisha’ hisia zake kwa sababu anahisi zinamfanya aonekane dhaifu kwa namna fulani iwe kwa mtoto mwenyewe au kwa wanaomzunguka. Njia moja ya kurekebisha hisia hizi ni kuadhibu na 'kuhubiri' kuliko kuzielewa kwanza. 

Mtoto wa kundi hili akiwa 'bize'a shughuli zake. Picha: slightlywarped.com
Chukulia kwa mfano mtoto amekasirika kwa madai ya kuoenewa na wenzake michezoni. Anaporipoti hasira yake kwa mzazi, mzazi anaanzisha ‘mahubiri’ ya hatari ya hasira akiamini kwamba kwa kufanya hivyo anamsaidia mtoto kuachana na hasira. Kwa uelewa wa mtoto, anachokifanya mzazi ni kupuuza anachojisikia na humfanya aone kuonesha hisia zake ni kosa na kutamfanya ama aonekana ‘kituko’ au kuadhibiwa.

Hali hii huwafanya watoto wajenge tabia ya kuzuia hisia zao, huwafanya watoto wakose ujasiri wa kusema wanavyojisikia kwa hofu ya kukosolewa na matokeo yake wanajenga tabia ya kuyaona mambo katika sura moja tu na kuwa ‘wasanii’ kwa kuonesha hisia tofauti na vile wanavyojisikia ndani. Ndio kusema hujenga woga na hofu kuwasiliana na wazazi wao. Shauri ya kujiona hawatendewi haki kwa kupewa wanachokihitaji, hutumia silaha ya kuwa walalamishi hali inayowafanya wazazi waone kama vile wanabughudhiwa. 

Kadhalika, mazingira yanayochangia mtoto kupuuzia anavyojisikia ni wazazi kuwa ama hawana muda wa kupatikana ‘kusoma’ hisia za mtoto au hupuuzia matarajio halisi ya mtoto kwa wanachojali zaidi hisia zao wenyewe. Chukulia mfano, mtoto anapoonesha shauku ya kuwa karibu na mama, ndio kwanza mama hapatikani au anakuwa ‘bize’ na majukumu mengine ya ‘muhimu’. Lakini mtoto anapokata tamaa kwa kujua anachojisikia hakina maana na  hivyo ‘kupotezea’ hisia zake, huo ndio wakati ambao mama hupatikana. Kwa hiyo, mtoto anajikuta akiamini kuonesha hisia ni shughuli isiyolipa na kujitenga na hisia zake ndio ufumbuzi.

Matokeo yake mtoto hujifunza kuwa kuonesha hisia halisi ni kosa.  Kukiri hisia ulizonazo ni kosa. Hivyo ili kuwa karibu na mzazi wake lazima awe msanii wa kuonesha hisia zile tu ambazo wazazi wanazitarajia. Wanakuwa watoto wasio na hisia, wanaoogopa kuonesha kile wanachojisikia ndani yao na kukiri kwamba wanajisikia hali fulani ndani. Sababu kubwa ikiwa ni kukosekana kwa malezi yanayojaribu kusikiliza na kushughulikia mambo halisi anayokutana nayo mtoto na kumfanya mtoto ajione hana nguvu yoyote ya kumfanya mzazi afanye vile anavyotarajia yeye. Kwa maana nyingine, watoto hawa wanaathiriwa na malezi yanayokidhi matarajio ya mzazi pasipo kuangalia mtoto naye ana matarajio gani.

Kuelewa kuliko kuishi uhalisia
Ili kujihami na hali ya kujiona mpweke asiyeeleweka, mbinu ni kutumia akili kugundua kile hasa kinachoweza kumfanya mzazi awe karibu nae badala ya hisia. Hatma yake, hutumia muda mwingi kutumia akili kwa lengo la kujua ni wakati gani hasa ataonekana kwa mzazi. Na kwa sababu anagundua hisia si suluhu ya kuonekana kwa mzazi, anaanza kujikita zaidi katika kujifunza na utundu wa kujua mambo ili ‘kumpata’ mzazi. Hata hivyo, anaweza kuwa na bahati mbaya kwamba  hata anapofanikiwa katika kujifunza bado hampati mzazi wake. Ikiwa hivyo, mtoto huyu hukosa ujasiri kwa sababu anakuwa hana namna ya kumpata mzazi wake.

Katika mazingira ambayo mzazi anavutiwa na jitihada za kujifunza anazozionesha mtoto, kujua na kuelewa mambo kadha wa kadha ndio hubaki kuwa tiketi ya kukukubalika na watu. Matokeo yake ni kujikuta wakiyaelewa zaidi mahusiano yao na wazazi wao na watu wengine kuliko wanavyohusiana katika hali halisi. Sababu ni kwamba kuhusiana kwa akili hakuwezekani pasipo hisia. Huwezi kuwa na urafiki na mtu kama huna uwezo mzuri wa kusoma anachojisikia. Hata hivyo, kwa kuwa wanafikiri kuliko wanavyohisi, wana faida ya kufanya mambo bila kutegemea kuzungukwa na marafiki. Kwa hiyo wanafuatwa na watu shauri ya kile wanachokijua na kukiwezesha lakini sio kwa namna walivyo ‘watu wa watu’.

Tabia ya ukimya, ubunifu na kutokuwa mgomvi 
Unaweza kuwagundua watoto hawa katika umri wa miezi ya mwanzo. Anapoamwachwa na mzazi huweza kulia kama watoto wengine, lakini mzazi anaporudi anaweza asiwe na msisimko sana na kurudi kwake. Tabia hii ikikomaa, mzazi unaweza hata kuondoka na bado mtoto asilie na ukirudi wala hana habari kama umerudi. Maana yake ni kwamba ameamua kujiondolea ‘presha’ kwa ‘kukupotezea’.

Akifika miaka kati ya miwili na mitatu, huwa na shughuli nyingi zinazochukua muda wake kuliko anavyojichanganya na wenzake. Na kwa kawaida huwa mkimya kadri anavyokua ingawa kwenye umri wa maswali huuliza maswali ya hapa na pale hasa wasipokuwepo wageni. Mbele za watu ana aibu na wakija wageni nyumbani kazi kubwa anayoifanya ni kurekodi matukio atakayoyaeleza wageni wakiondoka. Uzungumzaji wake unakuwa rahisi anapokuwa na watu anaowafahamu zaidi, tabia ambayo inaweza kuendelea hata akiwa mtu mzima.

 Akiamua kucheza, hucheza bila ugomvi wala ghasia wala kulalamika kwa sababu kwake hisia ni udhaifu. Kama wewe ni mzazi wa mtoto huyu, ni nadra kusiletewa mashitaka ya ‘fulani mchokozi’. Hagombani sana kwa sababu anaficha hisia zake na kinachompa umaarufu katika michezo yake ni ubunifu unaotokana na udadisi wake ambao kwa kweli haupo kwa watoto wenzake isipokuwa wa kundi la kwanza. Udadisi, kama tulivyosema ni njia pekee ya kupata ‘attention’ asiyoipata kwa wazazi wake na watu wengine. Katika umri wa shule, watoto wa kundi hili ndio huwa mafundi wa magari, mipira, midoli, wabunifu uwezo ambao ndio unaohitajika sana kwenye michezo. Kwa hiyo tunaweza kusema wanajua kuhusiana na vitu kuliko watu.

Hawezi kuhusiana na wenzake kwa ukaribu
Tatizo kubwa anapocheza na wenzake ni kuonekana mjuaji na kiongozi wa karibu kila kitu. Changamoto ni kwamba kujua ndiyo fahari yake kuliko kutambua hisia za wenzake wanaoweza kukerwa na ujuaji wake. Katika umri mdogo, hili linaweza lisiwe tatizo isipokuwa anapofikia umri wa shule. 

Hata hivyo, ni vigumu kuachana na ujuaji wake kwa sababu jamii ikiwa ni pamoja na wazazi wake huthamini sana watoto wanaoonesha kujua. Hali hii humjengea kiburi fulani cha kujiona bora kuliko wengine. Kwa hiyo ana ujasiri kwa sababu anajua uwezo wake lakini ana aibu fulani hivi kwa sababu anajua hawezi kujichanganya na watu vizuri. 

Bahati mbaya kwake ni kwamba uhusiano na watu haujengwi katika kujua pekee bali kusoma hisia za wengine. Kwa hiyo kwa sababu hana uwezo wa ‘kucheza’ na hisia, hujihami kwa kukwepa watu hasa anapoanza shule kama tutakavyoona huko mbeleni.

Kwa muhtasari, watoto hawa hukua wakijua kwamba ili maisha yawe rahisi na wazazi wao  1) ni muhimu kukwepa hasira za mzazi kwa kukana hisia halisi na sio kujenga urafiki naye katika mazingira yoyote 2) kujua kinachotarajiwa na watu wa karibu ni muhimu kuliko unachojua unakihisi ndani yako na hivyo 3) kwa sababu ya kuwa wazuri wa kutumia akili ili kujua wazazi wanataka nini hujikuta wakiweka nguvu zote kwenye shughuli zinazotumia akili na maarifa na hiyo huongeza kujiamini kwao.

Katika makala inayofuata, tutaangalia kwa nini watoto wengine hugeuka kuwa ‘watu wa watu’ na ‘michezo mingi’ shauri ya kutumia muda mwingi kuhudumia mahusiano na watu wengine kuliko udadisi na kujifunza.
Inaendelea

Maoni

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Pay $900? I quit blogging

Heri ya mwezi mpya!