Unavyoweza Kumsaidia Mtoto Kuwa Mkweli

Bila shaka umewahi kujiuliza kwa nini mtoto amekudanganya kwa jambo dogo ambalo, kwa hali ya kawaida, angeweza kukwambia ukweli na mambo yakaisha. Chukulia kwa mfano, una watoto kadhaa nyumbani. Unagundua kuna kosa limefanyika. Unapowauliza kujua nani aliyehusika, hakuna anayekuwa tayari kukubali.

Kama umekuwa ukijiuliza kwa nini watoto hudanganya, usiwe na wasiwasi.  Karibu watoto wote hudanganya katika mazingira fulani fulani. Wanapodanganya, hata hivyo, nia yao huwa ni kulinda uhusiano wao na wewe mzazi kwa kusema kile wanachojua unakitaka.  Tahadhari ni kuwa ikiwa kudanganya kwa nia njema kutaachwa kuendelee, hujenga tabia ya uongo mbeleni.
PICHA: psmforsingleparents.org


Sababu za watoto kudanganya

Umri. Mtoto mwenye miaka pungufu ya mitatu, kwa mfano, hana uwezo wa kusema uongo. Hata pale anapoonekana kudanganya, kimsingi hakusudii kudanganya kwa sababu akili yake haina uwezo wa kutunga uongo. Kinachoonekana kuwa uongo ni kusema kile anachotamani kingekuwa.

Kwa mfano, anaposema hajalamba sukari wakati anajua amelamba, hadanganyi bali anatamani ingetokea awe hajalamba sukari. Uongo ni kama matamanio ya kufanya alichopaswa kufanya.

Vile vile, mtoto hudanganya kwa lengo la kukwepa matokeo ya kusema ukweli utakaomgharimu. Kwa sababu mara nyingi matokeo hayo ni pamoja na adhabu, mtoto hutumia uongo kama namna ya kujihami awe salama.

Je, tunawezaje kumsaidia mtoto kuwa mkweli? Ingawa zipo namna nyingi, hapa nina mapendekezo makubwa matatu yanayohusiana.

Usimdanganye

Tabia ya mtoto ni sura ya kile anachokifanya mzazi wake. Ikiwa unataka mtoto wako asikudanganye, basi anza kwa kuwa mkweli kwake. Unapoahidi kumletea zawadi, kwa mfano, usiache kutekeleza ahadi yako.

Aidha, usitumie uongo kumridhisha mtoto. Anapouliza swali gumu, mpe maelezo rahisi ya kweli badala ya uongo ‘mzuri’ ambao, hata hivyo, anaweza kuugundua baadae. Anapogundua ulimdanganya, ni rahisi kuuona uongo kuwa tabia ya kawaida.


Usimwadhibu kwa kusema ukweli

Unafanyaje mtoto anapokwambia ukweli usioupenda? Je, unamwadhibu kwa sababu amekosea? Ukweli ni kwamba kumwadhibu mtoto kwa kukuambia ukweli ni sawa na kumwambia, ‘katika maisha ni hatari kuwa mkweli’. Hivyo, ni vizuri kuweka mazingira ya mtoto kujua kuwa ni afadhali kusema ukweli pale tunapokosea kuliko kufunika makosa kwa kutumia uongo.

Pia, kutokumwadhibu kwa kukiri kosa, kwa mfano, ni motisha ya kujisikia anaweza kusema ukweli na bado uhusiano wake na wewe mzazi usiathirike.  

Usiweke mazingira ya kudanganywa

Kama tayari unajua mtoto amefanya kosa, haina sababu ya kumwuuliza maswali ya mtego yanayotafuta majibu ambayo tayari unayajua. Kwa mfano, kama ulitarajia mtoto alale mchana na umegundua hajalala, usiombe kudanganywa kwa kuuliza swali kama, “hivi umelala leo?” Badala ya kumfanya alazimike kudanganya, ni vyema kushughulikia kosa moja kwa moja kwa lugha inayojenga badala ya kuuliza maswali yasiyosaidia kutatua tatizo na yanayokaribisha uongo.

Kadhalika, usimwite mtoto ‘mwongo’ hata kama amekudanganya. Majina ya ‘wewe ni mwongo’, ‘nilijua tu utanidanganya’ hujenga taswira ya kujiona uongo ni sehemu ya maisha yake. Tumia lugha yenye kuonesha matarajio chanya hata pale unapogundua umedanganywa.

Kukosea ni sehemu ya maisha

Kwa ujumla, ni vyema kumfundisha mtoto kwamba kukosea si jambo baya katika maisha. Makosa ni fursa ya kujirekebisha yanaposhughulikiwa vizuri. Hakuna sababu ya kumfanya mtoto ajifunze kufukia makosa yake kwa uongo.



christianbwaya [at] gmail [dot] com

Maoni

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Haiba ni nini?

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3

Uislamu ulianza lini?