Kuanzisha na Kuimarisha Urafiki wa Karibu
Katika zama hizi za
maendeleo ya kidijitali, ni rahisi sana kufahamiana na watu wengi ambao, hata
hivyo, wanaweza wasiwe marafiki. Unaweza, kwa mfano, kuwa na ‘marafiki’ elfu
tano kwenye mitandao ya kijamii, lakini usiwe na rafiki hata mmoja katika
maisha halisi.
Marafiki wa kweli na wa
karibu ni moja wapo ya mahitaji muhimu katika maisha. Tunaweza kuwa na sababu
nyingi kuhalalisha kwa nini hatuna (haja na) marafiki wa karibu. Hata hivyo, zipo nyakati hufika tukajikuta katika maisha yenye kujaa upweke na msongo wa mawazo kwa sababu hatukutumia
muda wetu kutengeneza urafiki wa karibu na watu tunaofahamiana nao.
Rafiki ni nani?
Rafiki wa karibu ni mtu
mnayehahamiana kwa karibu sana , mnayeminiana na kushirikiana mambo mengi binafsi
kwa uwazi bila wasiwasi wa kugeukana. Mara nyingi huyu ni mtu asiye ndugu wa damu wala mwanafamilia, hufanyika sehemu ya maamuzi
yetu, furaha yetu na hata katika hali ngumu tunazoweza kukutana nazo katika maisha. Ndio kusema, si kila mtu mnayefahamiana anaweza kuwa rafiki
wa karibu. Tunaweza kufahamiana na watu wengi, lakini tukawa na marafiki chache
wa karibu.
Marafiki tegemezi
Kwa ujumla, tunaweza
kuwagawa marafiki katika makundi mawili
makubwa; marafiki tegemezi na marafiki wainuaji. Marafiki tegemezi ni wale tunaowazidi
katika mengi na hivyo wanajifunza zaidi kwetu. Hawa ndio wale marafiki ambao
wakati mwingine tunaweza kuwaona kama wenye hali duni kiuchumi, ndoto zao nyingi hazijafikiwa na pengine
wanatutegemea sana ili kufikia ndoto zao za kimaisha.
Katika mazingira ya ‘maendeleo
ya kisasa’ yaliyotukuza ubinafsi, ni rahisi kuwaona marafiki hawa kama mizigo
tunayohitaji kuitua pale inapowezekana. Tunawaona kama watu wanaovuta mashati
kutuchelewesha kufanya mambo yetu. Hata hivyo, kadri tunavyozidi kujitambua, ndivyo
tunavyoweza kuwachukulia hawa kama sehemu ya mafanikio yetu.
Marafiki wainuaji
Marafiki wainuaji ni
wale wanaotuzidi kiroho, kuchumi, kiufahamu na kiuzoefu na hivyo tuna mengi ya
kujifunza kwao kuliko wao wanavyojifunza kwetu. Hawa ndio wale watu maarufu
katika jamii zetu kwa sababu ya mafanikio ya kazi wanazofanya.
Katika hali ya kawaida,
ni rahisi sana kuvutiwa nao na kutaka kuwa nao karibu kwa sababu tunajua wametuzidi.
Tunawatamani kutumia ujuzi wao, maarifa yao, uzoefu wao ili kufika kule
tunakotaka kwenda.
Lakini kwa kutumia kanuni
ya kuwatendea wengine vile tunavyopenda kutendewa, tunaweza kuona nafasi ya
aina zote hizi za marafiki katika kufanya maisha yawe mduara wa kutegemeana. Tunawahitaji
marafiki tegemezi ili tuwasaidie kufikia ndoto zao, na hali kadhalika,
tunawahitaji marafiki wainuaji ili na sisi tupate mwangaza wa kufikia ndoto zetu.
Kwa hakika, urafiki wa
karibu na watu hauwezi kutokea hivi hivi. Urafiki ni kama uwekezaji unaodai
gharama kubwa hasa katika hatua za mwanzo kabla ya kufikiria kupata faida.
Tuone baadhi ya gharama hizo tunazolazimika kuzilipa ili kujenga ukaribu na
marafiki zetu.
Kuwekeza muda
Muda ni gharama ya
kwanza kutuweka karibu na watu. Tunalazimika
kutoa muda wetu kuwatafuta na kuwasiliana na watu tunaotaka kujenga nao urafiki
wa karibu pasipokusubiri wao watutafute.
Kwa kawaida watu hawavutiwi na marafiki tegemezi wanaotaka watafutwe. Watu wana kawaida ya kujipenda wenyewe zaidi. Tunaposubiri wengine wafanye jitihada za kututafuta, tunaweza kungoja sana kwa sababu na wao wanasubiri tuwatafute.
Kwa kawaida watu hawavutiwi na marafiki tegemezi wanaotaka watafutwe. Watu wana kawaida ya kujipenda wenyewe zaidi. Tunaposubiri wengine wafanye jitihada za kututafuta, tunaweza kungoja sana kwa sababu na wao wanasubiri tuwatafute.
Kwa hiyo ikiwa tunataka kujenga uhusiano wa karibu na watu tunalazimika kuchukua hatua za makusudi na kufanya bidii ya kupatikana. Kupatikana ni pamoja na kuwa na muda wa kutoka pamoja, kufanya shughuli za kijamii pamoja, kutembeleana na mambo mengine yanayotufanya tuonane ana kwa ana.
Ni rahisi kuwatafuta watu pale tunakuwa na shida. Hata hivyo, kuwatafuta watu tunaowaita ‘marafiki’ wakati tunapowahitaji hujenga picha ya rafiki tegemezi na hivyo kuzorotesha
ukaribu wa kirafiki.
Kuaminika
Watu hawajengi uhusiano
wa karibu na mtu wasiyemwamini. Wangependa kuwa na mtu wasiye na wasiwasi naye. Ili kuaminika, tunalazimika kujenga
tabia ya kuwa waaminifu kwa mambo yao. Uaminifu ni pamoja na kutunza ahadi zetu
na kutovunja makubaliano na watu tunaowaita marafiki.
Kadhalika, kutunza siri
za wengine ni jambo la lazima. Tunapotambulika kwa sifa ya kuongea na watu
tunaokuwa nao badala ya kuongelea watu wasiokuwepo, tunajenga kuaminika. Kusema
mambo ya watu wasiokuwepo, ni kujipunguzia imani bila kujua. Hii ni kwa sababu
watu kwa kawaida hawapendi waseng’enyaji hata kama wanaweza kuvumilia kusikiliza mambo
mabaya ya wengine. Wanajua yule anayewaambia mambo yao, huwaambia wengine mambo
yao.
Uwezo wa kusikiliza
Binadamu anapenda kusikilizwa.
Tukitaka kuishi na watu vizuri tunahitaji kuwapa nafasi ya kuwasikiliza kuliko
tunavyotaka watusikilize sisi. Kusikiliza ni kuwa na uwezo wa kufuatilia kwa
makini kile wanachojaribu kusema. Ni kujaribu kuelewa mtazamo wa
anayezungumza badala ya kufikiria kile tunachodhani kilitakiwa kusemwa.
Kadhalika, kusikiliza ni
kutokukatisha na kuingilia ingilia wengine wanapozungumza. Ni rahisi sana, kwa mfano, kumkatisha mtu pale tunapohisi anasema asichotakiwa kukisema ama tunapoamini
amepotoka. Lakini tunapoweza kuvaa viatu vyao, tunaweza kabisa kuvumilia maoni
yao hata kama wakati mwingine hatubaliani nayo.
Kukubali mapungufu ya wengine
Haiwezekani watu wakawa
vile tunavyotaka wawe. Tunatofautiana kimtazamo, kiimani, na kiuelewa. Ni
makosa kulazimisha mitazamo yetu, imani zetu na hata uelewa wetu na kuufanya
uwe wa watu wote. Tuna kawaida ya kutokupenda watu wanaojiona sahihi muda wote wenye tabia ya kukosoa wengine zaidi. Ni muhimu kuonesha kukubali mapungufu ya watu kwa upendo.
Hata hivyo, yapo
mazingira ambayo twaweza kuwa na tofauti kubwa za kimisimamo na wengine.
Mathalani, kuna masuala kama imani, itikadi na misimamo mingine muhimu ya kimaisha. Tofauti kubwa wakati mwingine zinaweza kuathiri ukaribu
wa dhati na wengine. Sababu ni kwamba watu wana tabia ya kuvutiwa na wale wanafanana nao.
Aidha, pamoja na kwamba
zipo nyakati tunalazimika kutofautiana na wengine bado tunaweza kabisa kufanya
hivyo kwa upendo bila kuwafanya wengine wajisikie kudharauliwa. Kukosoa kupita
kiasi, kudhihaki na kukejeli wengine ni tabia zinazoweza kuzorotesha urafiki.
Kushiriki
furaha, huzuni zao
Tunahitaji kufurahi wenzetu
wanapokuwa na furaha. Tunahitaji uwezo wa kuhesabu mafanikio ya rafiki zetu
kama mafanikio yetu badala ya wivu na husuda pale tunapohisi kuzidiwa.
Upo ukweli
kwamba kadri unavyofurahia mafanikio ya wengine, ndivyo unavyokuwa na furaha. Lakini
pia, watu hufurahi wanapoona tunafurahia mafanikio yao kwa dhati pasipo unafiki.
Tukitaka kuwa na marafiki wa karibu, tunalazimika kuwa na tabia ya kufurahia
mafanikio ya wengine.
Kadhalika, zipo nyakati
ngumu katika maisha. Kuna matukio mazito hutokea yanayotufanya tuwahitaji
wengine kutusaidia kubeba mizigo yetu. Mfano, kufiwa na watu wa karibu,
kupoteza kazi, changamoto za kiuchumi na kijamii na mambo kama hayo. Tunahitaji kuwa tayari kubeba mizigo ya
wenzetu na kuifanya kama yetu. Waswahili walishasema mapema, akufaae wakati wa
shida, ndiye rafiki wa kweli. Kuhesabu matatizo ya wengine kama matatizo yetu
wenyewe, ni sehemu ya kujitambua.
Jitihada za kujenga
urafiki wa karibu na watu zina gharama kubwa kama tulivyoona. Lakini faida
zinazoambatana na urafiki wa karibu sana kiasi hicho zinaweza kabisa
kuhalalisha gharama hizo za lazima. Wanasema, hakuna kizuri kisicho na gharama.
Tunaweza kutoa visingizio vingi leo kuonesha kwa nini haiwezekani kufanya
jitihada hizi, lakini ukweli ni kwamba maisha hayawezi kukamiliki bila urafiki
wa karibu sana na baadhi ya watu. Uwezo na jitihada za kujenga urafiki wa karibu na watu ni sehemu ya kujitambua.
Unaweza kufuatilia safu ya
Saikolojia kwenye Gazeti la Mtanzania kila Alhamisi kwa mijadala kama hii.
Ubarikiwe mwl wangu..
JibuFutaNi kweli kabisa.
JibuFuta