Tuyafanyayo ni Matokeo ya Tujionavyo

Ungeulizwa swali, ‘wewe ni nani’ ungejibuje? Wengi tungetaja majina yetu kwa kuamini ‘sisi’ ni majina yetu. Wengine tungetaja kazi zetu kwa sababu kwetu majukumu ndio utambulisho wetu. Sisi ni nani basi? Kwa hakika swali hili si jepesi lakini linatuwezesha kuelewa tabia zetu. Karibu kila tunachofanya ni matokeo ya vile tujionavyo. Katika makala haya, tutaangazia  mitazamo michache inayoweza kutusaidia kutafakari swali hilo. 

Imani zetu/tunayoyaamini

Mtazamo wa kwanza ni nafasi ya kile tunachokiamini chenye mizizi yake katika fahamu zetu. Kila mwanadamu anayo mambo fulani anayoyaamini. Na mambo haya anayoyaamini yana nguvu kubwa ya kuamua fikra zake, mtazamo wake na hata matendo yake wakati mwingine bila kufikiri. Kwa mfano, binadamu anayeamini anayo nguvu ndani yake ya kufanya lolote alitakalo huwa na uthubutu wa kufanya yasiyofikirika kwa binadamu wengine. Kwake, sisi maana yake ni nguvu ambayo si kila mtu anaitambua. Na anapoitumia humpa matokeo kwa sababu anaamini 'sisi' ni nguvu.



Tunavyokubalika na wengine

Kwa wengine ‘sisi’ ni hali ya kukubalika kwa wengine na hivyo hujitambulisha kwa yaliyo mema hata pale wanapojua hawanayo. Ni hivyo kwa sababu nafsi zetu hutafuta kujipambanua na sifa zinazovutia. Hata pale tunapofahamu tunazo tabia zisizokubalika na wengine, si rahisi kujitambulisha nazo.  Hatupendi kuonekana hatuna sifa nzuri. Tunatamani kujitambulisha kwa sifa njema kwa sababu tunaamini sisi ni wema wetu. Kwa hiyo utaona 'sisi' katika mazingira hayo, ni yale yaliyo mema.


Matarajio ya marafiki yana nafasi Picha: ase.org.za
Aidha, sisi yaweza kuwa vile tunavyotamani tuwe. Sisi ni matamanio na ndoto nzuri tulizonazo hata kama hazijatimia. Ni rahisi, kwa mfano, masikini kujiona ni tajiri mtarajiwa hata kama hana nauli ya daladala. Hatupendi kujitambulisha kwa hali duni/dhoofu tulizonazo na zitarajiwazo. Sisi ni ule ubora tunaoutamani.


Watumiaji wa mitandao wanaweza kulielewa jambo hili vizuri zaidi. Mara nyingi watu huweka mtandaoni ‘wasifu wa matamanio yasiyo halisi’. Ni nadra, kwa mfano, mtu mwenye kazi/ajira asiyoipenda kujitambulisha waziwazi kwa kazi yake hiyo. Ukichunguza wasifu wa watu wengi kwenye mitandao unaweza kuamini kila mmoja amemaliza Chuo Kikuu hata kama wapo wengi  wasio hata na cheti. Sababu ni kwamba ‘sisi’ ni ile hali tunayoitamani. Tunajitambulisha kwa hali bora hata zile tusizokuwa nazo.


Matarajio ya makundi yetu

Vile vile, makundi tunayojipambanua nayo yana nguvu kubwa kubeba utambulisho wetu. Ni kawaida, kwa mfano, mwanadamu kujiona sehemu ya makundi ama aliyojikuta ni sehemu yake au aliyoyachagua kwa hiyari. Dini/imani, kazi/ajira, makabila, vyama, mataifa na kadhalika ni makundi yanayotulazimisha kulipa gharama fulani ya kukidhi matarajio na misingi ya makundi hayo.

Kwa mfano, ni rahisi kujenga mtazamo chanya kwa kundi langu kiasi cha kuwa tayari kutetea msimamo wowote unaobebwa na kundi langu bila hata kufikiri. kwa hiyo usahihi/makosa ya chochote hupimwa kwa mizania ya mtazamo wa kundi langu. Katika mazingira hayo ‘sisi’ ni kundi tunalojitambulisha nalo. Utambulisho huo hutfanya tujisikie hatia kufanya kinyume na misingi ya makundi yetu.

Tunavyojilinganisha 


Kadhalika, kuna hulka ya kujilinganisha na wengine. Kwa mfano, umasikini ama utajiri, urefu au ufupi, uzuri au ubaya ni matokeo ya kujilinganisha na tunaowajua. Mathalani, ni rahisi mwanafunzi kujiona mwenye akili kwa sababu anawashinda wasio na uwezo. Mwanafunzi huyo huyo anapohamia kwenye shule yenye wengi wanaomzidi hujiona ‘kilaza’. Ndio kusema utambulisho wake hubadilika kutegemea kile anachojilinganisha nacho. 

Hata hivyo, zipo nyakati watu hujilinganisha na hali zao wenyewe walizowahi kukutana nayo nyuma. Twaweza kujichukulia wenye mafanikio kwa kutazama mabadiliko ya maisha yetu bila kujali wengine wanatuonaje. Asiye na ajira hujiona amefanikiwa kwa kupata ajira bila kujali hadhi ya ajira yake hiyo kwa sababu 'sisi' katika mazingira yake ni kujilinganisha na yaliyopita.

Kile tunachofurahia kukisikia?


Kwa ufupi tunaweza kusema, kile tunachofurahi kujihusisha nacho, kile kinachotuchangamsha kinaposikika vizuri kwa wengine, yale tunayoyapigania, ni sehemu ya jawabu la swali muhimu, ‘sisi ni nani.’ Vile tunavyojiona na kuwaona wengine, hutegemea na vile tunavyojibu swali hilo. Tuyafanyayo ni matokeo ya tujionavyo kwa sababu utambulisho wetu ndio kila kitu katika maisha yetu.

Inaendelea 


Barua pepe: bwaya@mwecau.ac.tz

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3

Uislamu ulianza lini?